Leo Hii
Nabii wetu aishiye anafanya sehemu yake kwenye kuijaza dunia na Kitabu cha Mormoni. Yatupasa kufuata mfano wake.
Kaka na dada zangu wapendwa, kwenye Kitabu cha Mormoni kirai “leo hii”1 kinarudiwa rudiwa ili kusisitiza ushauri, ahadi na mafundisho. Mfalme Benyamini, katika maneno yake ya mwisho, aliwahusia watu, “Sikilizeni maneno yangu nitakayowazungumzia leo hii; … mfungue masikio yenu ili msikie, na mioyo yenu ili mfahamu, na akili zenu ili siri za Mungu zifunguliwe machoni mwenu.”2 Mkutano Mkuu ni sehemu sawa na hiyo. Tunakuja kusikiliza ushauri kwa ajili ya “leo hii,” ili kwamba tuweze kuwa “wakweli muda wote”3 kwa Bwana na injili Yake. La muhimu mawazoni mwangu “leo hii” ni umuhimu wa kufanya upya nia zetu juu ya Kitabu cha Mormoni, ambacho Joseph Smith alikiita “kitabu sahihi duniani.”4
Nimeshikilia nakala ya Kitabu cha Mormoni. Hii ni nakala ya kale ya mwaka 1970 na ni ya thamani kwangu. Kwa mwonekano wake kimechakaa na kuchanika, lakini hakuna kitabu kingine cha muhimu katika maisha yangu na ushuhuda wangu kama hiki. Kwa kukisoma, nilipata ushahidi kupitia Roho kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu,5 kwamba Yeye ni Mwokozi wangu,6 kwamba maandiko haya ni maneno ya Mungu,7 na kwamba injili imerejeshwa.8 Kweli hizo ziko ndani yangu. Kama nabii Nefi alivyosema, “nafsi yangu hufurahia vitu vya Bwana.”9
Hii ni historia fupi. Kama mmisionari kijana, nilisikiliza ushauri wa Mzee Marion D. Hanks, ambaye alitutembelea katika Misheni ya Eastern States. Alikuwa rais wa misheni ya Uingereza hapo awali, na wawili wa wamisionari wake wako kwenye jukwaa leo hii: ndugu zangu wapendwa Mzee Jeffrey R. Holland na Mzee Quentin L. Cook.10 Kama vile wamisionari huko Uingereza, alitupatia changamoto ya kusoma nakala ya Kitabu cha Mormoni ambayo haijatiwa alama angalau mara mbili kwa mwaka. Niliukubali wajibu huo. Usomaji wangu wa kwanza ulikuwa na nia ya kuweka alama au kupigia mstari kila kitu kilichoelekeza au kushuhudia juu ya Yesu Kristo. Nilitumia penseli nyekundu, na nilipigia mstari kurasa nyingi. Usomaji wa pili, Mzee Hanks alisema ulikuwa ni kuainisha kanuni na mafundisho ya injili, na wakati huu nilitumia rangi ya bluu kuweka alama kwenye maandiko. Nilisoma Kitabu cha Mormoni mara mbili, kama ilivyopendekezwa, na kisha mara mbili zaidi nikitumia rangi ya njano na nyeusi kuweka alama kurasa ambazo zilikuwa muhimu kwangu.11 Kama muonavyo, niliweka nukuu nyingi.
Kulikuwa na cha ziada kwenye usomaji wangu kuliko kuweka alama kwenye maandiko. Kwa kila usomaji wa Kitabu cha Mormoni, mwanzo mpaka mwisho, nilijawa na upendo wa dhati kwa Bwana. Nilihisi ushahidi thabiti wa ukweli wa mafundisho Yake na jinsi yanavyotumika “leo hii.” Kitabu hiki kinaendana na kichwa chake “Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo.”12 Kwa kujifunza huko na ushahidi wa kiroho uliopokelewa, nilikuwa mmisionari wa Kitabu cha Mormoni na mfuasi wa Yesu Kristo.13
“Leo hii,” moja ya wamisonari wakuu wa Kitabu cha Mormoni ni Rais Russell M. Nelson. Wakati akiwa mtume mpya aliyeitwa, alitoa mhandara Accra Ghana.14 Kwenye mahudhurio walikuwepo viongozi wa heshima, ikijumuisha mfalme wa kikabila wa kiafrika ambaye alizungumza kupitia mkalimani. Mfalme alikuwa mwanafunzi wa Biblia mwenye ari na alimpenda Bwana. Baada ya hotuba yake, alijiwa na mfalme, ambaye aliuliza kwa Kiingereza sanifu, “Wewe ni nani?” Rais Nelson alielezea kwamba alikuwa Mtume aliyetawazwa wa Yesu Kristo.”15 Swali la mfalme lililofuata lilikuwa “Ni kipi unaweza kunifundisha kuhusu Yesu Kristo?”
Rais Nelson alichukua Kitabu cha Mormoni na kufungua 3 Nefi 11. Kwa pamoja Rais Nelson na mfalme walisoma mafundisho ya Mwokozi kwa Wanefi: “Tazama, Mimi ni Yesu Kristo ambaye manabii walishuhudia atakuja ndani ya ulimwengu. … Mimi ni nuru na uzima wa ulimwengu.”17
Rais Nelson alimpatia mfalme nakala ya Kitabu cha Mormoni, na mfalme akajibu, “ungeweza kunipa almasi au rubi, lakini hakuna kilicho cha thamani sana kwangu kuliko nyongeza hii ya maarifa kuhusu Bwana Yesu Kristo.”18
Huo si mfano pekee wa jinsi nabii wetu mpendwa hushiriki Kitabu cha Mormoni. Ametoa nakala za Kitabu cha Mormoni kwa mamia ya watu, mara zote akitoa ushuhuda wake wa Yesu kristo. Wakati Rais Nelson akikutana wa wageni, marais, wafalme, wakuu wa nchi, viongozi wa kibiashara na taasisi na wa imani tofauti tofauti iwe kwenye makao makuu ya Kanisa au kwenye sehemu zao wenyewe, kwa upole hushiriki kitabu hiki cha maandiko yaliyofunuliwa. Angeweza kuwapa vitu vingi ambavyo vimefungwa kwenye riboni ambavyo vingeweza kuwa mezani au dawatini au kwenye kabati kama ukumbusho wa matembezi yake. Badala yake, huwapa kilicho cha thamani zaidi, kuliko rubi na almasi, kama alivyoelezea mfalme wa kikabila.
“Kweli za Kitabu cha Mormoni” Rais Nelson amesema, “zina nguvu ya kuponya, kufariji, kurejesha, kusaidia, kuimarisha, kuliwaza, na kufurahisha nafsi zetu.”19 Nimekuwa nikiona nakala hizi za Kitabu cha Mormoni zikiwa zimeshikiliwa mikononi mwa wale ambao wamezipokea kutoka kwa nabii wetu wa Mungu. Hakungekuwa na zawadi kuu yoyote.
Hivi karibuni ofisini kwake alikutana na mke wa rais wa Gambia na kwa unyenyekevu alimpa Kitabu cha Mormoni. Hakuishia hapo. Alifunua kurasa zake ili kusoma naye, kufundisha na kushuhudia juu ya Yesu Kristo, Upatanisho Wake na upendo Wake kwa watoto Wake wote—kila mahali.
Nabii wetu aishiye anafanya sehemu yake kwenye kuijaza dunia na Kitabu cha Mormoni.20 Lakini hawezi kufungua milango peke yake. Yatupasa kufuata mfano wake.
Nikitiwa msukumo na mfano wake, nimekuwa nikijaribu kwa unyenyekevu na kwa utulivu kushiriki Kitabu cha Mormoni.
Hivi karibuni nilipewa jukumu huko Msumbiji. Wananchi wa nchi hii nzuri wanasumbuliwa na umaskini, afya duni, ukosefu wa ajira, tufani na machafuko ya kisiasa. Nilipata heshima ya kukutana na rais wa nchi, Filipe Nyusi. Kufuatia ombi lake, nilisali kwa ajili yake na taifa lake; nilimwambia tulikuwa tukijenga hekalu la Yesu Kristo21 nchini mwake. Mwisho wa ziara yangu, nilimpatia nakala ya Kitabu cha Mormoni ya Kireno ambayo ni lugha yake. Wakati akikubali kitabu kwa furaha, nilishuhudia kuhusu tumaini na ahadi kwa ajili ya watu wake, zipatikanazo kwenye maneno ya Bwana kwenye kurasa zake.22
Kwenye tukio lingine, mimi, pamoja na mke wangu, Melanie tulikutana na Mfalme Letsie III wa Lesotho na mke wake nyumbani kwao.23 Kwetu sisi, cha muhimu kwenye ugeni wetu ilikuwa kuwapa nakala ya Kitabu cha Mormoni na kisha kushiriki ushuhuda wangu. Wakati tukikumbuka uzoefu huo pamoja na mwingine, mstari toka maandiko ya watakatifu wa siku za mwisho hunijia mawazoni: “utimilifu wa injili yangu uweze kutangazwa na watu walio dhaifu na wa kawaida hata mwisho wa dunia, na mbele ya wafalme na watawala.”24
Nilishiriki Kitabu cha Mormoni na Balozi wa India katika Umoja wa Mataifa huko Geneva, Indra Mani Pandey25; na Mtakatifu Patriaki Bartholomew26 wa Kanisa la Eastern Orthodox; na wengine wengi. Nimemhisi Roho wa Bwana pamoja nasi wakati mimi binafsi nikiwapa wao hili “jiwe la katikati la tao la dini yetu”27 na kutoa ushuhuda wangu juu ya Yesu Kristo, jiwe kuu la pembeni la imani yetu.28
Sasa, akina kaka na akina dada, si lazima uende Msumbiji au India au kukutana na wafalme na watawala kumpa mtu kitabu hiki cha mafundisho na ahadi takatifu. Ninawaalika, leo hii, kuwapa marafiki na familia zenu Kitabu cha Mormoni, wafanyakazi wenzenu, kocha wa timu yenu ya mpira wa miguu, au mzalishaji sokoni kwenu. Wanahitaji maneno ya Bwana yapatikanayo kwenye kitabu hiki. Wanahitaji majibu ya maswali ya maisha ya kila siku na ya maisha ya milele yajayo. Wanahitaji kujua juu ya njia ya agano iliyowekwa mbele yao na upendo endelevu wa Bwana kwao. Vyote viko kwenye Kitabu cha Mormoni.
Wakati ukiwapa Kitabu cha Mormoni, unafungua mawazo na mioyo yao kwa ajili ya neno la Mungu. Huna haja ya kubeba nakala zilizochapwa za Kitabu cha Mormoni. Kiurahisi unaweza kukishiriki kutoka kwenye simu yako kutoka kwenye sehemu ya maandiko ya programu ya Maktaba ya Injili.29
Fikiria wale wote ambao wangeweza kubarikiwa na injili katika maisha yao, na kisha kuwatumia nakala ya Kitabu cha Mormoni kutoka kwa simu yako. Kumbuka kujumuisha ushuhuda wako na jinsi kitabu hiki kimebariki maisha yako.
Rafiki zangu wapendwa, kama Mtume wa Bwana, ninawaalika kumfuata nabii wetu mpendwa, Rais Nelson, katika kuijaza dunia na Kitabu cha Mormoni. Hitaji hili ni kuu; tunahitaji kufanya hivyo sasa. Ninaahidi mtakuwa mkishiriki kwenye “kazi kuu duniani,” kuikusanya Israeli,30 wakati mkipata msukumo kuwafikia wale ambao “wametengwa na ukweli kwa sababu hawajui wapi pa kuupata.”31 Wanahitaji ushuhuda wenu na ushahidi wa jinsi kitabu hiki kimebadilisha maisha yenu na kuwasogeza karibu na Mungu, amani Yake,32 na habari Yake “njema ya furaha kuu.”33
Ninashuhudia kwamba kwa mpango matakatifu Kitabu cha Mormoni kiliandaliwa huko Amerika ya kale ili kuja kutangaza neno la Mungu, kuleta nafsi kwa Yesu Kristo na injili Yake ya urejesho “leo hii.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.