Kulisha na Kutoa Ushuhuda Wako
Ninawaalikeni mtafute fursa za kutoa ushuhuda wenu kwa maneno na vitendo.
Utangulizi
Nyakati za kutujenga katika maisha huja mara nyingi na pasipo kutegemea, hata wakati unapokuwa bado mdogo. Niruhusu nishiriki hadithi kuhusu mwanafunzi wa shule ya upili, Kevin, aliyechaguliwa kusafiri nje ya jimbo kwa ajili ya tukio la kiongozi wa mwanafunzi, kama alivyosimulia kwa maneno yake mwenyewe.
“Zamu yangu katika mstari ilifika, na karani mwandikishaji aliyepangwa aliulizia jina langu. Akaangalia orodha yake na kusema, ‘Kwa hiyo wewe ndio kijana kutoka Utah.’
“‘Unamaanisha niko peke yangu?’ Niliuliza.
“‘Ndiyo, ni wewe tu.’ Akanipatia beji yenye jina langu neno “Utah” likiwa limeandikwa chini ya jina langu. Nilipoibandika, nilihisi kama nilikuwa napigiwa chapuo.
“Niliingia kwenye kusanyiko ndani ya lifti ya hoteli pamoja na wanafunzi wengine watano wa upili wakiwa na beji za majina kama yangu. ‘Habari, wewe unatoka Utah. Wewe ni Mmormoni?’ aliuliza mwanafunzi mmoja.
“Nilihisi sikuwa sehemu sahihi pamoja na viongozi hawa wote wa wanafunzi kutoka nchini kote. ‘Ndiyo,’ Nilikubali kwa mashaka.
“‘Ninyi ni wale watu wanaoamini katika Joseph Smith, ambaye alisema aliona malaika. Kwa kweli wewe huamini hilo ama?
“Sikujua la kusema. Wanafunzi katika ile lifti wote walinitazama mimi. Ndio kwanza nimefika, na tayari kila mmoja alifikiri kuwa mimi ni wa tofauti. Nilijikingia kifua lakini nikasema, ‘Ninajua kwamba Joseph Smith alikuwa nabii wa Mungu.’
“‘Huo ushuhuda umetokea wapi?’ Nilijiuliza. Sikujua kama nilikuwa na ushuhuda ndani yangu. Lakini nilihisi maneno kuwa ya kweli.
“‘Ndiyo, nimewahi kuambiwa kwamba ninyi wote ni dini tu,’ yeye alisema.
“Pamoja na hilo, palikuwa na ukimywa usio mzuri wakati mlango wa lifti ulipofunguka. Tulipokuwa tukikusanya mizigo yetu, mvulana yule aliondoka akicheka.
“Kisha, sauti nyuma yangu iliuliza, ‘Habari, hivi Wamormoni si wana kitu kama Biblia nyingine?’
“Ah hapana. Usianze tena. Niligeuka kumwangalia mwanafunzi mwingine Christopher aliyekuwa katika ile lifti pamoja nami.”
“‘Kinaitwa Kitabu cha Mormoni,’ nilisema, nikitaka kuachana na somo hilo. Niliokota mabegi yangu na kuanza kwenye ukumbi ule.
“‘Je, hicho ndicho kile kitabu ambacho Joseph Smith alitafsiri?’ aliuliza.
“‘Ndiyo, ni chenyewe,’ nilijibu. Niliendelea kutembea, nikitumaini kuepuka aibu.
“‘Je, unajua jinsi ninavyoweza kupata kimoja?’
“Andiko nililojifunza katika seminari ghafla likanijia. ‘Siionei haya injili ya Yesu Kristo.’1 Hili lilipoingia akilini mwangu, nilihisi kuaibika kwa kuona aibu.
“Kwa muda wote uliobaki wa ile wiki, andiko lile halikuweza kuniondoka. Nilijibu maswali mengi kuhusu Kanisa kadiri nilivyoweza na nilitengeneza marafiki wengi.
Niligundua kuwa nilikuwa naionea fahari dini yangu.
“Nilimpatia Christopher Kitabu cha Mormoni. Baadaye aliniandikia, akiniamba kuwa amewaalika wamisionari nyumbani mwake.
“Nilijifunza kutoona aibu kushiriki ushuhuda wangu.”2
Ninavutiwa na ujasiri wa Kevin katika kushiriki ushuhuda wake. Ni ujasiri unaorudiwa kila siku na waumini waaminifu wa Kanisa kote ulimwenguni. Ninaposhiriki mawazo yangu, ninakualika wewe kufikiria juu ya maswali haya manne.
-
Je, mimi ninajua na kuelewa ushuhuda ni nini?
-
Je, ninajua jinsi ya kutoa ushuhuda wangu?
-
Je, vikwazo vya kushiriki ushuhuda wangu ni vipi?
-
Je, ni kwa namna gani ninatunza ushuhuda wangu?
Je, Ninajua na Kuelewa Ushuhuda ni Nini?
Ushuhuda wako ni jambo la thamani zaidi, mara nyingi likihusiana na hisia nzuri za kiroho. Hisia hizi kwa kawaida huwasilishwa kwa utulivu na kuelezewa kama sauti ndogo, tulivu.3 Ni imani yako au ufahamu wako wa ukweli, unaotolewa kama ushahidi wa kiroho kupitia ushawishi wa Roho Mtakatifu. Kupata ushahidi huu kutabadilisha kile unachosema na jinsi unavyotenda. Vipengele muhimu vya ushuhuda wako, vikithibitishwa na Roho Mtakatifu, hujumuisha:
-
Mungu ni Baba yako wa Mbinguni; wewe ni mtoto Wake. Yeye anakupenda.
-
Yesu Kristo yu hai. Yeye ni Mwana wa Mungu aliye hai na ni Mwokozi na Mkombozi wako.
-
Joseph Smith ni nabii wa Mungu aliyeitwa kurejesha Kanisa la Yesu Kristo.
-
Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni Kanisa la Mungu lililorejeshwa duniani.
-
Kanisa la Yesu Kristo lililorejeshwa linaongozwa na nabii anayeishi.
Je, Ninajua Jinsi ya Kutoa Ushuhuda Wangu.
Unatoa ushuhda wako pale unaposhiriki hisia zako za kiroho pamoja na wengine. Kama muumini wa Kanisa, unazo fursa za kutoa ushuhuda wako wa maneno katika mikutano rasmi ya Kanisa au isiyo rasmi, maongezi ya mmoja kwa mwingine pamoja na familia na watu wengine.
Njia nyingine unayoshiriki ushuhuda wako ni kupitia tabia njema. Ushuhuda wako katika Yesu Kristo si tu kile unachosema—ni kile wewe ulicho.
Kila wakati unapotoa ushuhuda wako kwa sauti au unapoonyesha kupitia vitendo vyako azma yako ya kumfuata Yesu Kristo, unawaalika wengine “kuja kwa Kristo.”4
Waumini wa Kanisa wanasimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote, katika vitu vyote, na mahali pote.5 Fursa za kufanya hivi katika ulimwengu wa kidijitali kwa kutumia maudhui yetu wenyewe ya kuinua au kushiriki maudhui yenye kuinua yaliyoandaliwa na wengine hazina mwisho. Tunashuhudia tunapopenda, kushiriki na kualika hata mtandaoni. Jumbe za moja kwa moja na machapisho vitachukua lengo la juu, takatifu wakati wewe pia unapotumia mitandao ya kijamii kuonesha jinsi injili ya Yesu Kristo ilivyoyatengeneza maisha yako.
Je, Vikwazo vya Kushiriki Ushuhuda Wangu ni Vipi?
Vikwazo vya kushiriki ushuhuda wako vyaweza kujumuisha kutokuwa na uhakika kuhusu kitu cha kusema. Matthew Cowley, Mtume wa mwanzoni, alishiriki uzoefu huu alipokuwa anaondoka kwenda misheni ya miaka mitano huko New Zealand akiwa na miaka 17:
“Kamwe sitasahau sala za baba yangu siku ile niliyoondoka. Sijawahi kamwe kusikia baraka nzuri sana kama hiyo katika maisha yangu yote. Kisha maneno yake ya mwisho kwangu katika kituo cha gari moshi, ‘Mwanangu, utakwenda kwenye misheni yako hiyo; utajifunza, utajitahidi kuandaa mahubiri yako na wakati mwingine utakapoitwa, utafikiri umejiandaa vya kutosha, lakini utakaposimama, mawazo yako yatabaki tupu kabisa.’ Nimekuwa na uzoefu huo zaidi ya mara moja.
“Niliuliza, ‘Unafanya nini akili yako inapokuwa tupu?’
“Yeye alisema, ‘Unasimama hapo na kwa bidii yote ya roho yako, unatoa ushahidi kwamba Joseph Smith alikuwa nabii wa Mungu aliye hai, na mawazo yatafurika akilini mwako na maneno kwenye kinywa chako … kwenda kwenye moyo wa kila mtu anayesikiliza.’ Na hivyo akili yangu, ikiwa mara nyingi tupu wakati wa … misheni yangu … ilinipa fursa ya kutoa ushuhuda wa tukio kubwa katika historia ya ulimwengu tangu kusulubiwa kwa Bwana. Jaribuni wakati mwingine, wanaume wenzangu na wasichana. Kama hauna kitu kingine cha kusema, shuhudieni kwamba Joseph Smith alikuwa nabii wa Mungu na historia yote ya Kanisa itafurika ndani ya akili zenu.”6
Vile vile, Rais Dalin H. Oaks alishiriki, “Baadhi ya shuhuda hupokelewa vyema kwa miguu inayoubeba kuliko kwa magoti yanayopigwa kuuomba.”7 Roho hushuhudia sawa kwa mzungumzaji na msikilizaji.
Kizuizi kingine, kama hadithi ya Kevin ilivyotilia mkazo ni woga. Kama Paulo alivyoandika kwa Timotheo:
“Maana Mungu hakutupa Roho ya uwoga; bali ya nguvu, na ya upendo. …
“Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu.”8
Hisia za woga hazitoki kwa Bwana bali mara nyingi hutoka kwa adui. Kuwa na imani, kama ilivyokuwa kwa Kevin, kutakuruhusu wewe kushinda hisia hizi na kushiriki kwa uhuru kile kilicho ndani ya moyo wako.
Je, Ninawezaje Kuutunza Ushuhuda Wangu?
Ninaamini ushuhuda ni wa asili ndani yetu, lakini, ili kuutunza na kuukuza kikamilifu, Alma alifundisha kwamba ni lazima tuulishe ushuhuda wetu kwa uangalifu mwingi.9 Tufanyapo hivyo, “utaota mizizi, na kukua, na kuzaa matunda.”10 Pasipo hili “ utanyauka.”11
Kila mshiriki mpendwa wa Urais wa Kwanza ametupatia maelekezo juu ya jinsi ya kutunza ushuhuda.
Rais Henry B. Eyring kwa upendo alitufunza kwamba “kusherekea juu ya neno la Mungu, sala ya dhati na utiifu kwa amri za Bwana sharti zitumiwe vyema na kwa uendelevu ili ushuhuda wako ukue na kustawi.”12
Rais Dallin H. Oaks alitukumbusha kuwa ili kutunza ushuhuda wetu, “tunapaswa kushiriki sakramenti kila wiki (ona M&M 59:9) ili kustahili kwa ajili ya ahadi ya thamani kwamba ‘daima Roho wake atakuwa [nasi]’ (M&M 20:77).”13
Na Rais Russell M. Nelson aliashauri kwa upendo hivi karibuni:
“Ulishe [ushuhuda wako] ukweli. …
“… Jilishe mwenyewe katika neno la manabii wa kale na wa sasa. Mwombe Bwana akufundishe jinsi ya kumsikiliza Yeye vyema. Tumia muda zaidi hekaluni na katika historia ya familia.
“… Fanya ushuhuda wako uwe kipaumbele chako.”14
Hitimisho
Wapendwa kaka na dada zangu, ninawaahidi kwamba kadiri unavyoelewa kiukamilifu ushuhuda ni kitu gani, na unapoushiriki, utashinda vizuizi vya mashaka na woga, kukupelekea wewe kuulea na kutunza hazina hii ya thamani zaidi, ushuhuda wako.
Tumebarikiwa kuwa na mifano isiyo na idadi ya manabii wa kale na wa sasa ambao kwa ujasiri wametoa shuhuda zao.
Kufuatia kifo cha Kristo, Petro alisimama na kushuhudia:
“Na ifahamike kwenu nyote, … kwa jina la Yesu Kristo Mnazareti, ambaye mlimsulubisha, ambaye Mungu amemfufua kutoka kwa wafu, … mtu huyu anasimama hapa mbele yenu. …
“… Kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu, ambalo kwalo twapaswa kuokolewa.”15
Amuleki, kufuatia mahubiri juu ya imani, alieleza kwa ujasiri: “Nitawashuhudia mimi mwenyewe kwamba vitu hivi ni vya kweli. Tazama, nawaambia, kwamba najua kwamba Kristo atakuja miongoni mwa watoto wa watu, … na kwamba atalipia dhambi za ulimwengu; kwani Bwana Mungu amesema.”16
Joseph Smith na Sidney Rigdon, baada ya kushuhudia ono tukufu la Mwokozi aliyefufuka, walishuhudia:
“Na sasa, baada ya shuhuda nyingi zilizotolewa juu yake, huu ni ushuhuda, wa mwisho, ambao tunautoa juu yake: Kwamba yu hai!
Kwani tulimwona, hata mkono wa kuume wa Mungu; na tukasikia sauti ikitushuhudia kuwa yeye ndiye Mzaliwa Pekee wa Baba.”17
Akina kaka na dada, ninawaalikeni kutafuta fursa za kutoa ushuhuda wenu kwa maneno na vitendo. Fursa kama hiyo ilinijia mimi hivi karibuni, mwishoni mwa mkutano na meya wa mji mkuu huko Amerika ya Kusini, katika kumbi zake pamoja na idadi kadhaa ya maafisa wake. Tulipokuwa tunahitimisha kwa hisia za huruma, kwa kusita nilifikiria ninapaswa kushiriki ushuhuda wangu. Kufuatia msukumo huo, nilitoa ushahidi kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu Aliye Hai na Mwokozi wa ulimwengu. Kila kitu kilibadilika wakati ule ule. Roho katika chumba kile alikuwa dhahiri. Ilionekana kwamba kila mtu aliguswa. “Mfariji … hushuhudia juu ya Baba na Mwana.”18 Ninashukuru sana nilipata ujasiri wa kutoa ushuhuda wangu.
Wakati kama huu unapokuja, unyakue na kuukumbatia. Utahisi mwako wa mfariji ndani yako unapofanya hivyo.
Ninatoa ushuhuda na ushahidi wangu kwenu—Mungu ni Baba yetu wa Mbinguni, Yesu Kristo yu hai na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni Kanisa la Mungu duniani leo linaloongozwa na nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.