Kuokoa kwa Umoja
Ili kumsaidia Mwokozi, tunapaswa kufanya kazi kwa umoja na kwa maelewano. Kila mmoja, kila nafasi, na kila wito ni muhimu.
Mara nyingi sisi humsikia Rais Thomas S. Monson akisema “Jitolee kuokoa”1 Hadithi katika Agano Jipya huja akilini mwangu. Ni mfano mzuri wa jinsi washiriki na wamisionari wanavyoweza kufanya kazi pamoja kwa umoja kupitia mabaraza ya kata ili kuwasaidia na kuokoa wengine. Hadithi inapatikana katika Marko 2:1–5. Nagundua kwamba matukio ambayo Yesu aliyatumia kutufundisha mafundisho au kanuni fulani daima huwa ni ya kuvutia zaidi na rahisi kueleweka.
Mmoja wa wahusika katika hadithi hii ni mtu mwenye kupooza, mtu ambaye hakuwa na uwezo wa kutembea bila msaada. Mtu huyu angeweza tu kukaa nyumbani, akisubiri wa kumwokoa.
Katika siku zetu, inaweza kutokea kama hivi. Watu wanne walikuwa wanatimiza jukumu kutoka kwa Askofu wao kumtembelea nyumbani kwake bwana mwenye ugonjwa wa kupooza. Katika taswira ninaweza kuona mmoja wao alitoka Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, mmoja kutoka katika jamii ya wazee, mmoja kutoka Ukuhani wa Haruni, na wa mwisho, lakini sio kwa umhimu bila shaka, ni mmisionari. Katika baraza la kata la hivi majuzi, baada ya kushauriana pamoja juu ya mahitaji ya kata, askofu alikuwa ametoa majukumu ya “kwenda kuokoa.” Hao wanne walipewa kazi ya kumsaidia mtu huyu aliyeugua kupooza. Hawakusubiri yeye aje kanisani mwenyewe. Iliwabidi wao waende kumtembelea nyumbani kwake. Walipaswa kumtafuta, na hivyo wakaenda. Mtu huyu alikuwa akiletwa kwa Yesu
“[Wakaja] watu, wakimleta mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne”Marko2:3.
Hata hivyo, chumba kilikuwa kimejaa sana. Hawakuweza kuingia kupitia mlangoni. Nina uhakika walijaribu kila kitu walichoweza kukifikira, lakini hawakuweza kupitia. Mambo hayakufanyika kwa urahisi kama yalivyopangwa. Kulikuwa na vikwazo katika njia yao ya “kuokoa.” Lakini hawakufa moyo. Hawakumwacha mtu yule aliyepooza mlangoni. Walishauriana kwa pamoja nini cha kufanya--- wangemletaje mtu yule kwa Yesu Kristo ili aponywe?. Kazi ya kusaidia Yesu Kristo katika kuokoa watu, angalau kwao, kamwe haikiwa ngumu sana. Waliunda mpango, si mpango rahisi, lakini waliutekeleza.
“Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakaliteremsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza” (Marko 2: 4).
Walimpandisha juu ya paa. Fikiria yakuwa hapakuwa na ngazi ya nje kwa ajili ya wao kupanda, ingewachukua muda mrefu kila mtu kupanda juu paa. Nadhani huenda ilifanyika hivi: kijana kutoka kata yake alipanda juu ya paa kwanza. Kwa vile yeye alikuwa kijana na mwenye wingi wa nguvu, haingekuwa vigumu mno kwake. Mwenzi wake katika ualimu wa nyumbani kutoka jamii ya wazee na Yule mrefu na mwenye nguvu mmisionari huenda walisukuma kwa nguvu kutoka chini. Dada wa Muungano wa Usaidizi wa akina Mama huenda aliwakumbusha kuchukua tahadhari na kuwapa maneno ya kutia moyo. Wanaume kisha wangefunua paa wakati dada akiendelea kumfariji mtu yule akisubiri kuponywa---ili aweze kutembea yeye mwenyewe na kuwa huru.
Kazi hii ya kuokoa waliyopangiwa ilihitaji kila mtu afanye kazi kwa pamoja. Katika wakati ule muhimu sana, ingelichukua uratibu makini ili kumteremsha mtu mwenye kupooza kutoka juu ya paa. Watu wale wanne wangelazimika kufanya kazi kwa umoja na kwa maelewano. Hakungekuwa na kutoelewana ko kote miongoni mwa wale wane. Wangelazimika kumteremshe mtu mwenye kupooza kwa kasi sawa. Mtu akiachilia kamba kwa kasi zaidi kuliko wale wengine watatu, mtu angeanguka kutoka kwenye kitanda chake. Hangeweza kujishikilia yeye mwenyewe kutokana na hali yake dhaifu.
Ili kumsaidia Mwokozi, tunapaswa kufanya kazi kwa umoja na kwa maelewano. Kila mmoja, kila nafasi, na kila wito ni muhimu.. Lazima tuwe na umoja katika Bwana wetu, Yesu Kristo.
Hatimaye, mgonjwa mwenye kupooza alilazwa mbele ya Yesu. “Naye Yesu, alipoona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.” (Marko 2:5)Yesu alionyesha huruma kwake na akamponya---si tu kimwili lakini pia kiroho: “Mwanangu, umesamehewa dhambi zako” . Je hivyo si vizuri? Je, sisi tusingetaka itokee hivyo kwetu sote pia? Bila shaka mimi ningetaka.
Je, tunamjua mtu yeyote katika maisha yetu ambaye anateseka kwa kupooza kiroho, mtu ambaye hawezi kurudi Kanisani yeye mwenyewe? Yeye anaweza kuwa mmoja wa watoto wetu, mmoja wa wazazi wetu, mke, ama rafiki.
Na idadi kubwa zaidi ya wamisionari inayopatikana sasa katika kila kitengo cha Kanisa, itakuwa busara kwa Maaskofu na marais wa matawi kutumia vyema zaidi mabaraza yao ya kata na tawi. Askofu anaweza kualika kila mshiriki wa baraza la kata kuja na orodha ya majina ya wale ambao wanaweza kuhitaji msaada. Washiriki wa baraza la kata watashauriana pamoja kwa makini jinsi watakavyoweza kusaidia. Maaskofu watasikiliza kwa makini mawazo na kugawa majukumu.
Wamisionari ni rasilimali kubwa kwa kata katika juhudi hizi za kuokoa. Wao ni vijana na wana nguvu nyingi. Wanapenda kuwa na orodha maalum ya majina ya watu wa kuwasaidia. Wanafurahia kufanya kazi pamoja na washiriki wa kata. Wanajua hii ni fursa kubwa kwao ya kutafuta. Wamejitolea katika kuimarisha ufalme wa Bwana. Wana ushuhuda dhabiti kwamba watakuwa kama Kristo zaidi wanaposhiriki katika juhudi hii ya kuokoa.
Kwa kumalizia, naomba kushiriki nanyi hazina nyingine moja iliyofichika inayopatikana katika hadithi hii ya maandiko. Iko katika mstari wa 5: “Naye Yesu, alipoiona yao imani” (himizo kuongezwa). Sikuwa nimegundua jambo hili katika siku za nyuma---yaoimani. Imani yetu iliyoungana inaweza pia kuathiri ustawi wa wengine.
Watu hao ambao Yesu aliwataja walikuwa kina nani? Wangeweza kujumuisha wale wanne ambao walimbeba mtu mwenye kupooza, mtu mwenyewe, watu ambao walikuwa wamemuombea, na wale wote ambao walikuwa pale wakisikiliza mahubiri ya Yesu na kushangilia kwa kimya kimya katika mioyo yao kwa ajili ya muujiza uliosalia kuja hivi punde. Wangeweza kujumuisha pia mwenzi, mzazi, mwana au binti, mmisionari, rais wa jamii, rais wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, askofu, na rafiki aliye mbali. Sote tunaweza kusaidiana. Tunapaswa daima tujishughulishe kwa shauku katika kutafuta kuwaokoa wale wanaohitaji.
Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mungu wa miujiza. Yesu Kristo anatupenda sote na ana uwezo wa kuokoa na kuponya, kimwili na kiroho. Tunapomsaidia katika misheni Yake ya kuokoa watu, sisi pia tutaokolewa katika yale tunayopitia. Ninashuhudia hayo katika jina Lake tukufu, hata Yesu Kristo, amina.