Karibuni kwenye Mkutano
Tunaposikiliza, mioyo yetu na iguswe, na imani yetu ikapate kuongezeka
Kaka zangu na dada zangu, ni furaha kwangu kuwakaribisheni kwenye mkutano mkuu huu wa dunia. Tumekusanyika pamoja katika maeneo mengi duniani kote kusikiliza na kujifunza kutoka kwa kina kaka na dada ambao tumewakubali kama Viongozi Wakuu na maafisa wakuu wa Kanisa. Wametafuta usaidizi wa mbinguni kuhusu ujumbe ambao watautoa, na wamepata maongozi kuhusu yale yatakayosemwa.
Mkutano huu unaadhimisha miaka 90- ya matangazo ya redio ya mkutano mkuu. Wakati wa mkutano mkuu wa Oktoba 1924, vikao vilitangazwa kwenye redio kwa mara ya kwanza kupitia KSL inayomilikiwa na Kanisa. Mkutano huu pia unaadhimisha miaka 65- ya matangazo ya televisheni ya mkutano mkuu. Katika mkutano mkuu uliofanyika mwezi Oktoba 1949, vikao vilionyeshwa katika televisheni kwa mara ya kwanza kote katika eneo la Salt Lake kupitia televisheni ya KSL.
Tunatambua baraka za vyombo vya habari vya kisasa katika kuwezesha mamilioni ya washiriki wa Kanisa kutazama na kusikiliza mkutano mkuu. Vikao hivi vya mwisho wa wiki hii vinapeperushwa kupitia televisheni, radio, televisheni ya kidigitali, mapeperusho ya setilaiti, na Intaneti, ikiwa ni pamoja na vifaa vya mkononi.
Katika miezi sita iliyopita tangu wakati tulipokutana kwa mara ya mwisho, hekalu moja jipya limewekwa wakfu na moja kuwekwa wakfu upya. Mnamo Mei Rais Dieter F. Uchtdorf aliweka wakfu Hekalu la Fort Lauderdale Florida. Sherehe nzuri ya kitamaduni ilionyeshwa na vijana ilifanyika siku iliyotangulia uwekaji wakfu. Siku iliyofuata, Jumapili, Mei 4, hekalu liliwekwa wakfu katika vikao vitatu.
Wiki mbili tu zilizopita ilikuwa ni fursa yangu kuweka wakfu upya Hekalu la Ogden Utah, lililowekwa wakfu awali mnamo mwaka 1972 na Rais Joseph Fielding Smith. Sherehe kubwa ya utamaduni ilitendeka kabla ya uwekaji wakfu upya, na vijana wengi wakishiriki na maonyesho mawili tofauti yalionyeshwa, na waonyeshaji tofauti kwa kila moja. Kwa ujumla, vijana 16,000 walishiriki. Ibada ya uwekaji wakfu upya ilitendeka siku iliyofuata, na wengi wa viongozi wa ukuhani walishiriki, pamoja na viongozi wa makundi saidizi, rais wa hekalu, washauri wake na wake zao.
Kujenga kwetu mahekalu kunaendelea vyema. Mwezi ujao Hekalu jipya la Phoenix Arizona litawekwa wakfu, na mwaka ujao, 2015, tunatarajia kuweka wakfu ama kuweka wakfu upya mahekalu yapatayo matano, na mengine ikiwezekana, itategemea kukamilika kwake .
Kama nilivyoeleza mwezi Aprili, wakati mahekalu yote yaliyotangazwa hapo awali yatakapokuwa yamejengwa na kuwekwa wakfu, tutakuwa na mahekalu 170 yanayotumika kote duniani. Kwa sababu tunaongeza juhudi zetu katika kukamilisha mahekalu yaliyotangazwa awali, hatutangazi kwa wakati huu mahekalu yoyote mapya. Hata hivyo, katika siku zijazo, tutakapoona kuna mahitaji na upatikanaji wa ardhi, matangazo ya mahekalu zaidi yatatolewa.
Kanisa linazidi kukua. Sasa tuko zaidi ya milioni 15 imara na tunaongezeka katika idadi. Jitihada zetu za umisionari zinaendelea mbele bila kuzuiwa. Tuna zaidi ya wamisionari 88,000 wakihudumu, wakifundisha ujumbe wa injili duniani kote . Tunasisitiza kwamba kazi ya umisionari ni jukumu la ukuhani, na tunawahimiza wavulana wote wanaostahili na wenye uwezo kuhudumu. Tunashukuru sana kwa wasichana ambao pia wanahudumu. Wanatoa mchango muhimu, ingawa hawana ulazima sawa na ule wa wavulana katika kuhudumu.
Sasa ninawaalikeni muwasikilize kwa makini akina kaka na akina dada ambao watashiriki leo na kesho katika vikao vyetu vya mkutano mkuu. Wote ambao wameombwa wazungumze wanatambua kuwa ni jukumu kubwa kwa wao kufanya hivyo. Tunapowasikiliza, mioyo yetu na iguswe na imani yetu ikapate kuongezeka, ninaomba katika jina la Yesu Kristo, amina.