“Ndiyo, Bwana, Nitakufuata.”
Bwana anawaalika mtumie vitenzi tofauti: “Njoni kwangu,” “Nifuate,” “Tembea pamoja nami.” Katika kila hali ni mwaliko wa kutenda.
“Kwani tazama, Bwana huwakubali mataifa yote, kila taifa na lugha yake, kufundisha neno lake, ndio, kwa hekima.”1 Leo andiko hili limetimizika kwa mara nyingine tena kwa vile nimepatiwa nafasi ya kuelezea hisia zangu kwa lugha yangu ya asili.
Ilikuwa katika mwaka wa 1975, na nilikuwa nikihudumu katika misheni ya Uruguay Paraguay kama mmisionari kijana. Katika mwezi wangu wa kwanza katika misheni, viongozi wa kanda waliandaa shughuli ya kuonyesha kanuni ya injili. Kila mmisionari katika kanda alifumbwa macho, na tukaambiwa kwamba tufuate njia inayoelekea kwenye ukumbi wa utamaduni. Tulitakiwa kufuata sauti ya kiongozi mmoja mahususi, sauti tuliosikia kabla ya kuanza kutembea. Hata hivyo, tulionywa kwamba wakati wa safari tungesikia suati kadhaa ambazo zitajaribu kutuchanganya na kutufanya tuchepuke kutoka kwenye njia.
Baada ya dakika kadhaa za kusikia sauti, zikizungumza, na---katikati ya yote---sauti ambayo ilisema, “Nifuate Mimi,” Nilihisi kujiamini nilikuwa nikifuata sauti sahihi. Tulipowasili katika ukumbi wa utamaduni wa kanisa, tuliulizwa kuondoa vifumba macho vyetu. Nilipofanya hivyo, niligundua kwamba kulikuwa na makundi mawili na kwamba nilikuwa katika kundi ambalo lilikuwa linafuata sauti isiyo sahihi. “Ilisikika sana kama vile ile iliyo sahihi,” nilijisemea mwenyewe.
Tukio hili lililotokea miaka 39 iliyopita lilikuwa na athari ya kudumu kwangu. Nilijiambia mwenyewe, “Kamwe, sitafuata tena sauti isiyo sahihi.” Kisha nikajiambia, “Ndio, Bwana Nitakufuata.”
Ninataka kulinganisha tukio na mwaliko mwema wa Mwokozi kwetu:
“Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua. …
“Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.”2
Mwaliko wa “kufuata Yeye,” ni rahisi sana, wa moja kwa moja na mwaliko wa nguvu sana tunaoweza kupokea. Huja kwa sauti iliyo wazi ambayo haiwezi kukuchanganya.
Bwana hutualika sisi akitumia vitenzi tofauti: “Njoni kwangu,” “Nifuate,” “tembea pamoja nami.” Katika kila hali haikuwa mwaliko baridi; ilikuwa ni mwaliko wa kutenda. Ulilenga wanadamu wote ukitolewa na mmoja ambaye ni Nabii wa manabii, Mwalimu wa walimu, Mwana wa Mungu, Masiya.
Mwaliko wa “Njoni Kwangu”
“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”3
Ninyi ambao bado si washiriki wa Kanisa mtapokea mwaliko huu kupitia sauti za wamisionari kwa maneno haya: “Je! Utasoma Kitabu cha Mormoni? Je! Utasali? Je! Utahudhuria kanisa? Je! Utafuata mfano wa Yesu Kristo na kubatizwa na wale walio na mamlaka?”4 Je! Mtajibu vipi mwaliko huu leo?5
Nawaalikeni msikilize na mpokea ujumbe kwa kusema, “Ndio, Bwana, Nitakufuata!”
Carlos Badiola na familia yake, wa Minas, Uruguay, walikuwa wanakutana na wamisionari. Kwa vile wazee wale waliuliza maswali mengi wakati wa masomo, waliamua kumwalika jirani asiye mshiriki---msichana mrembo wa miaka 14 aliyeitwa Norma---kuwasaidia wao kujibu. Norma alikuwa wanafunzi wa shule ya upili mwenye bidii ambaye alikuwa anajifunza Biblia huko shuleni mwaka huo. Alikuwa mchunguzi bora sana, kwa hivyo wamisionari walipouliza swali, Norma alijibu mara moja.
Aliporudi nyumbani baada ya somo na wamisionari, Norma alijua kile alichokuwa anapaswa kufanya. Alimwambia mama yake, “Mama, kutoka sasa sitokunywa kahawa na maziwa tena. Ni maziwa tu.” Jibu hilo lilikuwa onyesho la wazi la hamu yake ya kukubali mwaliko wa kumfuata Kristo, kama ulivyotolewa na wamisionari.
Wote Carlos Badiola na Norma walibatizwa. Na baadaye, wakifuata mfano wa Norma, mama yake, baba, na nduguze pia walibatizwa. Norma nami tulikua pamoja katika lile tawi dogo lakini lenye nguvu sana katika Minas. Baadaye, niliporudi kutoka kuhudumu misheni, tulioana. Mimi daima nilijua kwamba ingekuwa rahisi kumfuata Mwokozi yeye akiwa kando yangu.
Mtu ambaye ni mshiriki wa Kanisa na tayari ameshapokea mwaliko huu na huufanya upya kila wiki kwa kupokea sakramenti.6 Sehemu ya sharti hilo inajumuisha kuziweka amri, na tunapofanya hivyo, tunasema, “Ndio, Bwana, Nitakufuata!”7
Mwaliko wa “Nifuate”
“Nifuate” ulikuwa mwaliko wa Bwana kwa mwanamfalme tajiri. Kijana huyo alikuwa ameshika amri katika maisha yake yote. Alipouliza ni nini zaidi afanye, alipokea jibu kwa mwaliko wazi: “Njoo, … unifuate.”8 Hata hivyo, ingawa mwaliko ulikuwa rahisi, haukuwa bila dhabihu. Ulihitaji juhudi---zikiandamana na maamuzi na vitendo.
Nabii Nefi alialika tafakari ya kibinafsi wakati alipouliza: “Na [Yesu] akawaambia watoto wa watu: Nifuateni mimi. Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, je, tunaweza kumfuata Yesu tusipokubali kushika amri za Baba?”9
Mwaliko wa “njoni Kwake,” msikilize sauti Yake, na kuifuata umekuwa ujumbe wa wamisionari kutoka mwanzoni, ukiwasaidia wengi kubadilisha maisha yao kabisa.
Miaka hamsini iliyopita wamisionari waliingia katika duka la baba yangu la kutengeneza saa katika Minas, Uruguay, wakiacha saa itengenezwe. Kama vile wamisionari wema wafanyavyo, walichukuwa fursa hiyo kuongea na baba na mama yangu kuhusu injili. Baba yangu aliwakubali wamisionari, na mama yangu alikubali ujumbe na mwaliko wa kumfuata Kristo. Kutoka siku hiyo mpaka leo, yeye amebakia mhudhuriaji kamili katika Kanisa. Alisema, “Ndio, Bwana, Nitakufuata!”
Mnapojitahidi kuja Kwake, mtapata nguvu za kupunguza mizigo ya maisha, iwe ya kimwili au ya kiroho, na mtapata nguvu za kubadilika moyoni ambako kutawasaidia kuwa na furaha zaidi.
Mwaliko wa “Tembea pamoja Nami”
Henoko aliitwa kuhubiri injili kwa watu wabishi, wenye mioyo migumu. Alijiona kuwa hastahili. Alikuwa na shaka kama angeweza kufanya hivyo. Bwana alituliza shaka yake na kuimarisha imani yake kupitia mwaliko “Tembea pamoja nami”---mwaliko ambao, kama vile fimbo ya kipofu au mkono wa rafiki unavyoweza kuongoza hatua za mtu ambaye hatua zake hazina uhakika. Kwa kutwaa mkono wa Mwokozi na kutembea pamoja Naye, Henoko aligundua kwamba hatua zake zilikuwa thabiti na akawa mmisionari hodari na nabii.10
Maamuzi ya “njoni kwangu” na “nifuate” ni ya kibinafsi. Tunapoupokea mwaliko huu, kiwango cha msimamo wetu kiimani kinainuliwa, na ndipo basi tunapoweza “kutembea pamoja Naye.” Kiwango hiki kinaanzisha uhusiano wa karibu na Mwokozi, kama tunda la kupokea kwetu mwaliko wa kwanza.
Norma na mimi kila mmoja tulipokea mwaliko wa “njoni kwangu” na “nifuate.” Kisha kwa pamoja, tukisaidiana, tumejifunza kutembea pamoja Naye.
Juhudi na azimio la kumtafuta Yeye na kumfuata Yeye vitatuzwa kwa baraka tunazotafuta.
Hivyo ndivyo ilivyo kuwa kwa mwanamke ambaye, kwa juhudi kubwa, aliweza kugusa vazi la Mwokozi 11 au ilivyokuwa kwa Bartimayo kipofu, ambaye azimio lake lilikuwa jambo muhimu katika muujiza ambao ulitokea katika maisha yake.12 Katika hali zote za uponyaji wa mwili na roho ulitolewa.
Nyoosha mkono wako, kitaswira gusa vazi Lake, pokea mwaliko Wake, tembea pamoja Naye, na sema, “Ndio, Bwana, Nitakufuata!”
“Njoni kwangu,” “Nifuate,” na “Tembea pamoja nami” ni mialiko iliyo na nguvu za asili---kwa wale ambao mnapokea---kubadilisha maisha yenu na kuanzisha mabadiliko ndani yenu ambayo yatawaongoza ninyi kusema, “[Mimi] sina tamaa tena ya kutenda maovu, lakini kutenda mema daima.”13
Kama onyesho la nje la mabadiliko hayo, utaona hamu kubwa ya “kuwasaidia wadhaifu, kuinyoosha mikono iliyolegea, na kuyaimarisha magoti yaliyo dhaifu.”14
Ni hatua gani tunazoweza kuchukua ili “kutembea pamoja Naye”?
-
Pata hamu ya kuwa mwanafunzi bora wa Kristo.15
-
Ombea hamu hii ili imani yako katika Yeye iweze kukua.16
-
Pata elimu kutoka kwenye maandiko, yakiangaza njia na kuimarisha hamu yako ya kubadilika.17
-
Fanya maamuzi leo kutenda na kusema, “Ndio, Bwana, Nitakufuata!” Kujua ukweli tu hakutabadilisha ulimwengu wako usipoigeuza elimu kuwa kitendo.18
-
Stahamili katika uamuzi uliofanya kwa kutumia hizi kanuni kila siku.19
Na maneno ya nabii wetu mpendwa, Rais Thomas S. Monson, yatuhamasishe hata kwenye matendo katika hamu zetu kupokea mwaliko wa Mwokozi. Rais Monson alisema: “Ni nani Mfalme wa utukufu, huyu Bwana wa majeshi? Yeye ndiye Bwana wetu. Yeye ni Mwokozi wetu. Yeye ni Mwana wa Mungu. Yeye ndiye mtunzi wa Wokovu wetu. Anatuita ‘Nifuate.’ Anaelekeza, ‘Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.’ Anasihi, ‘Mtazishika amri zangu.’”20
Na tufanye uamuzi leo wa kuongeza kiwango chetu cha kumwabudu na kuweka sharti kwa Mungu, na jibu letu kwa mwaliko Wake lisikike kwa sauti na wazi: “Ndio, Bwana, Nitakufuta!” 21 Katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.