2010–2019
Ufunuo Endelevu
Oktoba 2014


17:30

Ufunuo Endelevu

Hukumu na fikra za kimantiki za binadamu haziwezi kutosha kupata majibu ya maswali ambayo ni muhimu sana katika maisha. Sisi tunahitaji ufunuo kutoka kwa Mungu.

Matumaini yangu kwetu ni kwamba sote tuhisi upendo na nuru kutoka kwa Mungu. Kuna wengi wanaosikiliza leo wanaohisi haja ya haraka kwa ajili ya baraka za kibinafsi kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni mpendwa.

Kwa marais wa misheni, inaweza kuwa maombi ya kutaka kujua jinsi ya kumsaidia mmisionari anayetaabika. Kwa baba au mama katika maeneo yaliyoathirika kwa vita, watahitaji kujua iwapo wanahitaji kuipeleka familia sehemu ya usalama au kubaki mahala walipo. Mamia ya marais wa vigingi na maaskofu leo wanaomba ili kujua jinsi ya kuwaokoa kondoo waliopotea. Na kwa nabii, itakuwa kujua kile Bwana angependa yeye aongee kwa Kanisa na ulimwengu wenye machafuko.

Sote tunajua kwamba hukumu na fikra za kimantiki za binadamu haziwezi kutosha kupata majibu ya maswali ambayo ni muhimu sana katika maisha. Sisi tunahitaji ufunuo kutoka kwa Mungu. Na hatutahitaji angazo moja la nuru tu na ufariji, bali tunahitaji baraka endelevu za mawasiliano na Mungu.

Uwepo wa Kanisa umetokana na mvulana mdogo akijua kwamba ilikuwa kweli. Kijana Joseph Smith alijua kwamba yeye peke yake asingeweza kujua ajiunge na kanisa gani. Hivyo akamwomba Mungu kama vile kitabu cha Yakobo kilivyomtaka afanye. Mungu Baba na Mwanae mpendwa walimtokea katika kichacha. Walijibu swali ambalo lilikuwa nje ya uwezo wa Joseph kulitatua.

Siyo tu aliitwa na Mungu kulianzisha Kanisa la Yesu Kristo la kweli, bali ndani yake palikuwa na nguvu zilizorejeshwa za Roho Mtakatifu ili kwamba ufunuo kutoka kwa Mungu uweze kuendelea.

Rais Boyd  K. Packer alielezea kwamba alama ya kutambulisha Kanisa la kweli kwa njia hii: “Ufunuo unaendelea katika Kanisa: nabii anapata ufunuo kwa ajili ya Kanisa; rais kwa kigingi chake, misheni yake, au wa jamii yake; askofu kwa kata yake; baba kwa familia yake; na mtu kwake binafsi.”1

Huu mfululizo mzuri wa ufunuo unaanza, unaishia, na unaendelea pale tunapopokea ufunuo binafsi. Acha tumwangalie Nefi, mwana wa Lehi, kama mfano wetu. Baba yake aliona ono. Wengine katika familia ya Nefi walilichukulia ono la Lehi kama ushahidi wa kuchanganyikiwa. Ono lilikuja na amri toka kwa Mungu kwenda kwa wana wa Lehi kujihatarisha sana katika kurejea Yerusalemu kwa ajili ya mabamba ambayo yalikuwa na neno la Mungu ili waweze kuyachukua katika safari yao ya nchi ya ahadi.

Mara nyingi tunayanukuu maelezo ya kishujaa ya Nefi wakati baba yake alipowaambia warudi Yerusalemu. Mnayajua hayo maneno: “Nitakwenda na kutenda mambo ambayo Bwana ameamuru.” 2

Pindi Lehi aliposikia Nefi akiongea maneno yale, maandiko yanasema kwamba alikuwa na “furaha tele.”3 Alikuwa na furaha kwa sababu alijua kwamba Nefi alibarikiwa na kuthibitisha kwamba ono lake lilikuwa ni mawasiliano ya kweli kutoka kwa Mungu. Nefi hakusema, “Nitakwenda na kutenda yale ambayo baba yangu ameniambia nitende.” Badala yake alisema, “Nitakwenda na kutenda mambo ambayo Bwana ameamuru.”

Katika ufahamu wako katika familia yako, pia unajua kwa nini Lehi alikuwa na “furaha tele.” Furaha yake ilikuja kutokana na kujua kwamba Nefi alipokea ufunuo wa uthibitisho.

Wazazi wengi wameweka sheria za familia pale kijana anaporudi nyumbani usiku. Lakini fikiria furaha wakati mzazi anapogundua, kama ilivyotokea kwa mmoja wa wazazi wiki chache zilizopita, kwamba mtoto ambaye hivi majuzi aliondoka nyumbani siyo tu alijiwekea amri ya kutotembea wakati wa usiku mwenyewe bali pia aliweka Sabato kama vile alivyokuwa amefundishwa nyumbani. Ufunuo wa mzazi unakuwa na matokeo mazuri katika ufunuo binafsi unaoendelea kwa mtoto.

Mama yangu lazima ameelewa kanuni ile ya ufunuo. Nikiwa kijana, nilifunga mlango wa nyuma kimya kimya nilipochelewa kurudi nyumbani jioni. Ilibidi nipite katika chumba cha mama yangu nikienda chumbani kwangu. Hata hivyo nilitembea kimya kimya, wakati nilipopita nusu ya mlango wake uliokuwa wazi, nilisikia jina langu, “Hal. Njoo kidogo.”

Nilienda na kukaa pembeni mwa kitanda chake. Chumba kilikuwa giza. Kama ungesikia, ungefikiria yalikuwa maongezi ya kirafiki kuhusu dunia. Lakini hadi siku ya leo, aliyoyasema yanarudi katika fikra zangu, kwa nguvu zilezile ninazozisikia pale ninaposoma baraka yangu ya baba mkuu.

Sijui nini alikuwa anaomba kwenye sala huku akinisubiri mimi usiku ule. Nahisi ilikuwa ni sehemu ya usalama wangu. Lakini nina uhakika kwamba aliomba kama baba mkuu aombavyo kabla ya kutoa baraka. Anaomba kwamba maneno yake yamfikie mlengwa kama maneno ya Mungu, na siyo yake. Sala ya mama yangu kwa ajili ya baraka ilikuwa imejibiwa kwa ajili yangu. Yupo katika ulimwengu wa roho na amekuwa huko kwa zaidi ya miaka 40. Nina uhakika atakuwa na furaha sana kwamba nilibarikiwa kwa sababu nilisikiliza ushauri wake wa amri za Mungu. Na nimejaribu kwenda na kutenda yale aliyotegemea ningeyafanya.

Nimeona muujiza kama huu wa muendelezo wa ufunuo kwa marais wa vigingi na maaskofu katika Kanisa. Na, ni kweli katika ufunuo kwa viongozi wa familia, thamani ya ufunuo inategemea na wale wanaoongozwa kuweza kupokea ufunuo wa uthibitisho.

Niliona muujiza huo wa ufunuo baada ya Bwawa la Teton huko Idaho kubomoka mwaka 1976. Wengi wenu mnaijua habari hii ya kile kilitokea. Lakini somo la mwendelezo wa ufunuo ambao ulipitia kwa rais wa kigingi ungeweza kutubariki sisi sote katika siku za baadaye.

Maelfu ya watu walihamishwa wakati nyumba zao ziliharibika. Juhudi za msaada zilimwangukia rais wa kigingi, mkulima. Mimi nilikuwa darasani katika Chuo cha Ricks siku chache baada ya janga kutokea. Kiongozi kutoka shirika la misaada la kitaifa alikuja. Yeye na wasaidizi wake waliingia katika chumba kikubwa ambacho rais wa kigingi alikuwa amewakusanya maaskofu na hata watumishi wengine toka madhehebu mengine. Nilikuwepo pale kwa sababu manusura wengi walikuwa wanahudumiwa na kuhifadhiwa pale chuoni ambapo mimi nilikuwa rais wa chuo.

Mkutano ulipoanza, mwakilishi toka katika shirika la misaada la taifa akasimama na akaanza kusema kwa sauti ya mamlaka kile kitafanyika. Baada ya kuorodhesha mambo matano au sita ambayo yalikuwa muhimu, rais wa kigingi alimjibu, “Hayo yote tumeyafanya.”

Baada ya dakika chache, mtu toka shirika lala misaada alisema, “Nafikiri nitakaa chini na niwasikilize kwa muda.” Yeye na wasaidizi wake walikuwa wakiwasikiliza maaskofu na marais wa jamii ya wazee wakitoa taarifa za yale wameyafanya. Walielezea yale maelekezo waliyokuwa wamepokea na kufuata kutoka kwa viongozi wao. Pia waliongea kuhusu waliyoongozwa kufanya walipokuwa wakifuata maelekezo kutafuta familia ambazo nyumba zao ziliharibika. Muda ulipita. Wote walichoka kuonyesha hisia zao ila upendo kwa watu.

Rais wa kigingi alitoa mwongozo wa mwisho kwa maaskofu, na alitangaza muda kwa ajili ya mkutano mwingine wa kutoa taarifa mapema asubuhi iliyofuata.

Asubuhi iliyofuata kiongozi toka kitengo cha misaada cha kitaifa aliwasili dakika 20 kabla ya mkutano wa ripoti kuanza. Nilisimama karibu. Nikamsikia akisema na rais wa kigingi kwa sauti ya chini, “Rais, ungependa mimi na washiriki wa timu yangu tufanye nini?”

Alichokiona yule mtu nimewahi kukiona katika nyakati za shida na kutoa mtihani kwa ulimwengu wote. Rais Packer alikuwa sahihi. Mwendelezo wa ufunuo unapitia kwa marais wa vigingi ili kuwaongezea hekima na uwezo wao wenyewe. Na, zaidi ya hayo, Bwana huwapa wale ambao rais huongoza ushahidi kamilifu kwamba amri zinatoka kwa Mungu kupitia Roho Mtakatifu na mtu aliyedhaifu.

Nimebarikiwa kuitwa kuwafuata viongozi kwa muda mwingi wa maisha yangu. Nikiwa kijana niliitwa kuwa mshauri wa rais wa jamii ya wazee. Nimekuwa mshauri kwa marais wawili wa vigingi, na Askofu Msimamizi wa Kanisa, mshiriki wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili, na mshauri kwa Marais wawili wa Kanisa. Nimebarikiwa kuona ufunuo ukitolewa kwao na kisha kwa wafuasi wao.

Kupokelewa kwa ufunuo wa kibinafsi huku, ambako wote tunataka, hakuji kirahisi, wala hakuji kwa kuomba tu. Bwana hutoa mwongozo ufuatao ili kutusaidia kupata ushahidi kutoka kwa Mungu. Ni mwongozo kwa yeyote anayehitaji ufunuo wa kibinafsi kama vile wote watakavyo.

“Na moyo wako pia uwe umejaa hisani kwa wanadamu wote, na kwa jamaa ya waaminio, na wema uyapambe mawazo yako bila kukoma; ndipo kujiamini kwako kutakuwa imara katika uwepo wa Mungu; na mafundisho ya ukuhani yatatonatona juu ya roho yako kama umande utokao mbinguni.

“Roho Mtakatifu atakuwa mwenzi wako daima.”4

Kutoka kwa haya ninapata ushauri kwa ajili yetu sote. Usizichukulie kijuujuu hisia unazozipata za upendo kwa ajili ya nabii wa Mungu. Popote niendapo katika Kanisa, nabii yeyote aliyopo kwa wakati huo, washiriki watauliza, “Utakaporudi Makao Makuu ya Kanisa, tafadhali utamwambia nabii jinsi gani tunavyompenda?

Hiyo si kama kuabudu mtu au mawazo ambayo wakati mwingine tunakuwa nayo ya kumtamani shujaa. Ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kwa sababu hiyo mtapokea zawadi zaidi za uhakikisho wa ufunuo pale anapoongea katika nafasi yake kama nabii wa Bwana. Upendo unaohisi ni upendo wa Bwana kwa awaye mwongeaji Wake.

Hii si rahisi kuhisi kila mara kwa sababu Bwana mara nyingi anawataka manabii wake kutoa ushauri ambao ni mgumu kwa watu kukubali. Adui wa nafsi zetu atajaribu kutuongoza ili tuchukizwe na tushuku wito wa nabii kama kweli unatoka kwa Mungu.

Nimeona jinsi Roho Mtakatifu anaweza kugusa mioyo iliyolainika ili kuwalinda wafuasi wanyenyekevu wa Yesu Kristo katika kudhihirisha ufunuo.

Nabii alinituma kuja kutunuku nguvu takatifu za kuunganisha kwa mwanaume katika mji mdogo mbali sana. Ni nabii wa Mungu pekee aliye na funguo za kuamua nani apewe nguvu takatifu ambazo zilitolewa na Bwana kwa Petro, Mtume mkuu. Nimepokea uwezo wa muunganisho kama huo, lakini ni kwa mwongozo wa Rais wa Kanisa nami naweza kumpa mwingine.

Hivyo, katika chumba kwenye kanisa mbali na Salt Lake, niliweka mikono yangu juu ya mtu aliyechaguliwa na nabii ili kupokea uwezo wa kuunganisha. Mikono yake ilionyesha alama ya kudumu ya kutifua udongo kwa maisha ya chini. Mke wake mwenye umbo dogo alikaa karibu yake. Naye pia alionyesha alama ya maisha ya kudumu ya kazi ngumu pamoja na mumewe.

Niliongea maneno niliyopewa na nabii. “Kwa kupewa mamlaka na majukumu kutoka,” na kisha jina la nabii, “ambaye anayeshikilia funguo zote za ukuhani hapa duniani kwa wakati huu, ninatoa nguvu za kuunganisha,” na nikataja jina la mtu na kisha jina la hekalu ambalo angetumikia kama muunganishaji.

Machozi yakatiririka kwenye mashavu yake. Nikamwona mke wake akilia. Niliwasubiri watulie. Alisimama na kunijia mimi. Aliangalia juu na kisha akasema kwamba alikuwa na furaha lakini huzuni pia. Alisema kwamba alipenda sana kwenda hekaluni pamoja na mumewe, lakini kwa sasa anajisikia kwamba siyo lazima aende pamoja naye kwa sababu Mungu amemchagua yeye kwa utukufu na uaminifu mtakatifu. Kisha akasema kwamba hisia zake za kujisikia kwamba hakustahili kuwa mwenza wa hekalu zikaja kwa sababu hakuweza kusoma wala kuandika.

Nikamhakikishia kwamba mume wake atashukuru kwa kuwa naye hekaluni kwa sababu ya uwezo wake wa kiroho. Vilevile kwa uelewa wangu mdogo wa lugha yake, nilimwambia Mungu amefunua vitu kwake zaidi ya elimu ya dunia.

Alijua kwa kipawa cha Roho kwamba Mungu alitoa, kupitia nabii Wake, uaminifu mkubwa kwa mume aliyempenda. Alijua mwenyewe kwamba funguo za kutoa uwezo huo wa kuunganisha ulishikiliwa na mtu ambaye hajawahi kumwona na alijua kwamba alikuwa nabii wa Mungu. Alijua, bila ya kuambiwa na shahidi yeyote, kwamba nabii aliomba juu ya jina la mume wake. Alijua mwenyewe kwamba Mungu alikuwa ametoa huu wito.

Pia alijua kwamba ibada ambazo mume wake angezifanya zingewaunganisha watu milele katika ufalme wa selestia. Alijithibitishia katika akili na moyo wake kwamba ahadi aliyoitoa Bwana kwa Petro bado inaendelea katika Kanisa: “Chochote utakachokifunga duniani kitakuwa kimefungwa mbinguni.”5 Aliyajua hayo yeye mwenyewe, kwa ufunuo, kutoka kwa Mungu.

Acheni turudi kule tulikotoka. “Ufunuo unaendelea katika Kanisa: nabii anaupokea kwa ajili ya Kanisa; rais kwa ajili ya kigingi chake, misheni yake, au jamii yake; askofu kwa ajili ya kata yake; baba kwa ajili ya familia yake; na mtu binafsi kwa ajili yake mwenyewe.”6

Ninatoa ushahidi wangu ambao ni wakweli. Baba wa Mbinguni anasikia maombi yako, Anakupenda, Analijua jina lako. Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu, na Mkombozi wetu anakupenda zaidi ya unavyofahamu.

Mungu humwaga ufunuo, kupitia Roho Mtakatifu, kwa watoto Wake. Anaongea na nabii Wake hapa duniani, ambaye leo ni Thomas S. Monson. Ninashuhudia kwamba yeye ana funguo zote za ukuhani hapa duniani.

Mnaposikiliza katika mkutano huu maneno ya wale ambao Mungu amewaita kuongea kwa niaba Yake, ninaomba mpate uhakikisho wa ufunuo mnaouhitaji ili kupata njia ya kurudi nyumbani, kuishi pamoja Naye katika familia iliyounganishwa milele. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.