Sababu ya Tumaini Letu
Ushuhuda wa tumaini la ukombozi ni kitu ambacho hakiwezi kupimika au kuhesabika. Yesu Kristo ndiye kiini cha tumaini hilo.
Miaka michache iliyopita, Dada Packer na mimi tulienda katika Chuo Kikuu cha Oxford. Tulikuwa tukitafuta rekodi za babu yangu wa kizazi cha saba nyuma. Mkuu wa Chuo cha Christ’s kule Oxford, Dkt. Poppelwell, alitusaidia sana kwa kumuuliza mtunza rekodi wa chuo alete rekodi. Hapo katika rekodi za mwaka wa 1583 tulilipata jina la babu yangu, John Packer.
Mwaka uliofuata tulirudi Oxford ili kukabidhi maandiko matakatifu ya Kanisa yaliyofungwa vizuri kwa ajili ya maktaba ya Chuo cha Christ. Kwake Dkt. Poppelwell hakupendezwa na jambo hilo. Pengine alifikiria sisi hatukuwa Wakristo. Basi akamwita kasisi wa chuo kupokea vitabu hivyo.
Kabla ya kumpa kasisi maandiko, nilifungua Mwongozo wa Maandiko na kumuonyesha mada moja: yenye kurasa 18, iliyochapishwa kwa maandiko madogo mazuri, upana mdogo kati, ukiorodhesha marejeo kwa mada ya “Yesu Kristo.” Ni moja ya mkusanyiko kamili wa marejeo ya maandiko juu ya mada kuhusu Mwokozi ambayo haijawahi kukusanywa katika historia ya dunia -ushuhuda kutoka katika Agano la Kale na Jipya, Kitabu cha Mormoni, Mafundisho na Maagano, na Lulu ya Thamani Kuu.
”Kwa njia yoyote ufuatiliayo marejeo haya,” nilimwambia, “upande kwa upande, juu na chini, kitabu baada ya kitabu, mada baada ya mada –utaona kwamba ni ushuhuda unafanana, unakubaliana na utukufu wa misheni ya Bwana Yesu Kristo -kuzaliwa Kwake, maisha Yake, mafundisho Yake, Kusulubiwa Kwake, Ufufuo Wake, na Upatanisho Wake”.
Baada ya maongezi yangu na kasisi juu ya baadhi ya mafundisho ya Mwokozi, hisia zake juu yetu zilibadilika na akaanza kututembeza kwenye chuo, ikiwa ni pamoja na uchimbuaji uliofanywa hivi karibuni ambao ulifunua sanamu ambayo iliundwa wakati wa siku za Warumi.
Miongoni mwa marejeo yaliyoorodheshwa katika Mwongozo wa Maandiko ni moja kutoka katika Kitabu cha Mormoni: Ushahidi Mwingine wa Yesu Kristo: “Tunahubiri kuhusu Kristo, tunatoa unabii kumhusu Kristo, na tunaandika kulingana na unabii wetu, ili watoto wetu wajue asili ya kutegemea msamaha wa dhambi zao.” (2 Nefi 25:26).
Kwa maneno Yake mwenyewe, Mwokozi alitamka, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi” (Yohana 14:6).
Na kutoka katika Kitabu cha Mormoni alitamka, “Tazama, ni mimi yule aliyetayarishwa kutoka mwanzo wa dunia kuokoa watu wangu. Tazama, mimi ni Yesu Kristo ...Ndani yangu binadamu wote watapata uzima, na kwamba milele, hata wale watakaoamini katika jina langu; na watakuwa wana na mabinti zangu” (Etheri 3:14).
Yako marejeo mengi, mengi mengine kote katika maandiko ya Kanisa letu yanayotangaza nafasi tukufu ya Yesu Kristo kama Mkombozi wa wote ambao wamewahi kuzaliwa ama watakaozaliwa katika maisha hapa duniani.
Kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo sote tunakombolewa kutoka Anguko la mwanadamu, lililotendeka wakati Adamu na Hawa walipolila tunda lililokatazwa katika Bustani ya Edeni, kama ilivyoelezwa katika Wakorintho, “Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa” (1 Wakorintho 15:22).
Kitabu cha Mormoni kinafundisha, “Kwani ni lazima kwamba upatanisho ufanywe ...,la sivyo wanadamu wote ni lazima bila kuepuka wapotee; ndio, wote wamekuwa wagumu; ndio, wote wameanguka, na wamepotea, na ni lazima wapotee isipokuwa wapitie kwa upatanisho,...dhabihu kuu na ya mwisho” (Alma 34:9–10).
Huenda tusiishi maisha makamilifu, na kuna malipo ya makosa yetu, lakini kabla ya kuja duniani, tulikubali kuwa chini ya sheria Zake na kukubali adhabu ya kuvunja sheria hizo.
“Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;
Wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu” (Warumi 3:23–24).
Mwokozi alitekeleza Upatanisho, unaotoa njia kwetu kuwa wasafi. Yesu Kristo ndiye Kristo mfufuka. Tunamuabudu na kumtambua Yeye kwa sababu ya uchungu aliopitia kwa ajili yetu sisi kwa pamoja na kwa uchungu aliostahimili kwa ajili ya kila mmoja wetu, katika Bustani ya Gethsemane na msalabani. Alipitia yote kwa unyenyekevu mkuu na akiwa na ufahamu wa milele wa jukumu na kusudi Lake tukufu.
Wale watakaotubu na kuacha dhambi watauona mkono Wake wa rehema ukiwa bado umenyooshwa. Wale wanaosikiliza na kutii maneno Yake na maneno ya watumishi Wake wateule watapata amani na ufahamu hata wakiwa katikati ya mapigo ya moyo na huzuni. Matokeo ya dhabihu yake ni kutuweka huru kutokana na madhara ya dhambi ili kwamba wote wapate kuondolewa hatia na kuwa na tumaini.
Kama asingetekeleza Upatanisho, hakungekuwa na ukombozi. Ungekuwa ulimwengu mgumu kuishi kama hatungeweza kamwe kusamehewa makosa yetu, kama hatungeweza kamwe kujisafisha wenyewe na kuendelea mbele.
Rehema na neema za Yesu Kristo mipaka yake si tu kwa wale wanaotenda dhambi ya kutenda au dhambi ya kuto kutenda yatusayo kutenda, lakini zina jumuisha ahadi ya amani ya milele kwa wote ambao watamkubali na kumfuata Yeye na mafundisho Yake. Rehema Yake ni mponyaji mkuu, hata kwa yule mjeruhiwa asiye na hatia.
Hivi karibuni nilipokea barua kutoka kwa mwanamke ambaye aliripoti kuwa alipitia mateso makuu katika maisha yake. Kosa la kutisha ambalo hakubainisha lakini alikuwa akilisema sema, lilikuwa limetendwa dhidi yake. Alikiri kwamba alipambana na hisia za uchungu mwingi. Katika hasira yake, alilia moyoni, “Mtu lazima alipie kosa hili,” Katika wakati huu wa huzuni kuu na maswali, aliandika kwamba kulikuja moyoni mwake jibu la moja kwa moja kwamba, “Mtu tayari ameshalipa.”
Kama hatuna ufahamu wa kile dhabihu ya Mwokozi kinachoweza kutufanyia, tunaweza kupitia maisha tukiwa tumebeba majuto kwamba tumefanya kitu ambacho hakikuwa sahihi ama tumemkosea mtu fulani. Hatia inayoambatana na makosa inaweza kutolewa. Tukitafuta kuelewa Upatanisho Wake, tutakuja kuheshimu kwa kina Bwana Yesu Kristo, utumishi Wake duniani, na huduma yake tukufu kama Mwokozi wetu.
Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho lilirejeshwa ili kueneza duniani kote ufahamu wa maisha na mafunzo ya Mwokozi. Mkutano huu mkuu unapeperushwa katika lugha 94 kupitia setilaiti kwa nchi 102 lakini pia unapatikana kwenye intaneti kwa kila nchi ambapo Kanisa lipo. Tuna zaidi ya vigingi 3,000. Jeshi letu la wamisionari lina zaidi ya wamisionari 88,000 na idadi ya wanachama wa Kanisa imepita milioni 15. Nambari hizi zinasimama kama ushahidi kwamba “jiwe lililochongwa mlimani bila kazi ya mikono litabiringika, hadi litaijaza dunia yote”(M&M 65:2).
Lakini cha muhimu si ukubwa Kanisa kama taasisi inavyokua ama mamilioni mangapi ya washiriki wanajiunga nasi, wala si idadi ya mabara na nchi ambamo wamisionari wetu wanaingia ama lugha ngapi tofauti tunazungumza, mafanikio ya kweli ya injili ya Yesu Kristo yatapimwa kwa nguvu ya kiroho ya mshiriki wake mmoja mmoja. Tunahitaji nguvu ya usadiki inayopatikana katika moyo wa kila mfuasi mwaminifu wa Kristo.
Ushuhuda wa tumaini la ukombozi ni kitu ambacho hakiwezi kupimika ama kuhesabika. Yesu Kristo ndiye chanzo cha tumaini hilo.
Tunakusudia kuimarisha shuhuda za wachanga na wazee, waliooa kwa wasiooa. Tunahitaji kufundisha injili ya Yesu Kristo kwa wanaume, wanawake, na watoto, wale wa kila kabila na nchi, tajiri na masikini. Tunawahitaji waliojiunga na kanisa hivi majuzi na wale miongoni mwetu ambao ni uzao wa waasisi wa kanisa. Tunahitaji kuwatafuta wale ambao wamepotea na tuwasaidie kurejea kundini. Tunahitaji hekima,umaizi, na nguvu za kiroho za kila mmoja..Kila mshiriki wa Kanisa kama mtu binafsi ni kiungo muhimu cha mwili wa Kanisa.
“Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo.
“Kwa maana katika Roho moja sisi sote tulibatizwa....
“Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi” (1 Wakorinitho 12:12–14).
Kila mshiriki hutumika kama ushuhuda wa maisha na mafundisho ya Yesu Kristo. Tuko vitani na nguvu za adui, na tunamhitaji kila mmoja wetu ikiwa tutaka kufanikiwa katika kazi ambayo Mwokozi anatutaka tuifanye.
Unaweza kufikiria, “Mimi ninaweza kufanya nini? Mimi ni mtu mmoja tu.”
Bila shaka Joseph Smith alijiona kuwa hakika alikuwa pekee yake mara nyingine. Yeye ameibuka na ukuu, lakini alianza kama mvulana mwenye umri wa miaka 14 ambaye alikuwa na swali: “Kati ya makanisa yote haya lipi nijiunge nalo?” (onaJoseph Smith -Historia 1:10). Imani na ushuhuda wa Joseph kwa Mwokozi ulikua kama vile wetu nao lazima ukue, “mstari juu ya mstari, kanuni juu ya kanuni, hapa kidogo na kule kidogo” (2 Nefi 28:30; ona pia M&M 128:21). Joseph alipiga magoti kuomba, na vitu vya ajabu jinsi gani vimekuja kwa sababu ya ombi hilo na Ono la Kwanza.
Kama mmoja wa Mitume Kumi na Wawili, ninatoa ushuhuda wa Yesu Kristo. Yu hai. Yeye ndiye Mkombozi na Mwokozi wetu. “Kwa njia ya Upatanisho wa Kristo, wanadamu wote wanaweza kuokolewa” (Makala ya Imani 1:3). Yeye Analiongoza Kanisa hili. Yeye si mgeni kwa watumishi Wake. Tunapotembea kuingia katika siku za usoni kwa kujiamini moyoni, Roho Wake atakuwa pamoja nasi. Hakuna kikomo kwa nguvu Zake katika kubariki na kuongoza maisha ya wale wanaotafuta ukweli na wema Wake. Ninatoa ushuhuda juu Yake katika jina la Yesu Kristo, amina.