Kuwaidhinisha Manabii
Kuwaidhinisha kwetu kwa manabii ni sharti la kibinafsi ambalo tunalifanya kwa juhudi zote ili kuhimili vipaumbele vya kinabii vyao.
Rais Eyring, tunakushukuru kwa ujumbe wako wenye maelekezo na wa kuvutia. Wapendwa ndugu na dada zangu, tunawashukuru kwa imani yenu na mioyo yenu ya kujitolea. Hapo jana kila mmoja wetu alialikwa kumwidhinisha Thomas S. Monson kama nabii wa Bwana na Rais wa Kanisa la Bwana. Na mara kwa mara tunaimba, “Tunakushukuru, Ee Mungu, kwa nabii.”1 Wewe nami kwa kweli tunaelewa nini maana yake? Fikiria faida kubwa Bwana ametupa sisi ya kumwidhinisha nabii Wake, ambaye ushauri wake utakuwa msafi, usiopotosha, usiotia hamasa ya tamaa ya mtu yeyote na wa kweli kabisa!
Tunawezaje kwa kweli kumwidhinisha nabii? Zamani kabla hajawa Rais wa Kanisa, Rais Joseph F. Smith alielezea : “Ni kazi muhimu inayowategemea Watakatifu ambao… wanaidhinisha wenye mamlaka wa Kanisa, kufanya hivyo sio tu kwa kunyoosha mkono ambao ni uwakilishi wa nje tu, lakini kwa matendo na kwa kweli. ”2
Nakumbuka vizuri sana “kitendo” changu cha kipekee cha kumwidhinisha nabii. Katika wajibu wangu kama daktari wa tiba na daktari mpasuaji wa moyo, nilikuwa na wajibu wa kufanya upasuaji wa moyo kwa Rais Spencer W. Kimball mnamo mwaka wa 1972, wakati alikuwa Kaimu Rais wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili. Alihitaji hasa upasuaji changamano sana. Lakini sikuwa na uzoefu wa kufanya utaratibu kama huu kwa mgonjwa mzee wa miaka 77 katika hali ya moyo uliosita. Mimi sikupendekeza upasuaji na kwa hiyo nilimfahamisha Rais Kimball na Urais wa Kwanza. Lakini, katika imani, Rais Kimball alichagua kufanyiwa upasuaji, kwa sababu tu alishauriwa na Urais wa Kwanza. Hiyo inaonyesha jinsi alivyowaidhinisha viongozi wake! Na uamuzi huu uliniogofya!
Shukrani kwa Bwana, upasuaji ulifanikiwa, wakati moyo wa Rais Kimball ulipoanza tena kupiga, ulifanya hivyo kwa uwezo mkubwa! Kwa wakati ule, nilikuwa na ushahidi wa dhahiri kutoka kwa Roho kwamba mtu huyu siku moja atakuwa Rais wa Kanisa!3
Mnajua matokeo yake. Miezi 20 tu baadaye, Rais Kimball akawa Rais wa Kanisa. Na alitoa uongozi wa kijasiri na ushupavu kwa miaka mingi.
Tangu hapo tumewaidhinisha Marais Ezra Taft Benson, Howard W. Hunter, Gordon B. Hinckley, na sasa Thomas S. Monson kama Marais wa Kanisa---manabii halisi kwa kila hali.
Wapendwa ndugu na dada zangu, kama urejesho ulifanya chochote, ulivunjavunja dhana ambayo imedumu kwa muda mrefu kwamba Mungu ameacha kuzungumza na watoto wake. Hakuna kinachoweza kuwa mbali na ukweli. Nabii ameongoza Kanisa la Mungu katika vipindi vyote, kutoka kwa Adamu mpaka siku ya leo.4 Manabii wanashuhudia juu ya Yesu Kristo---Uungu wake na ujumbe na huduma Yake ya duniani.5 Tunamheshimu Nabii Joseph Smith kama nabii wa kipindi hiki cha mwisho. Na tunamheshimu kila mtu ambaye amemfuata yeye kama Rais wa Kanisa.
Tunapowaidhinisha manabii na viongozi wengine,6 tunatumia sheria ya kauli ya pamoja katika Kanisa, kwani Bwana alisema: “Haitatolewa kwa yeyote kwenda mbele kuhubiri injili yangu au kulijenga Kanisa langu, isipokuwa awe ametawazwa na mtu fulani ambaye ana mamlaka na inajulikana kwenye Kanisa, kwamba ana mamlaka na amekuwa kwa kawaida ametawazwa na viongozi wa Kanisa.”7
Hii inatupa sisi kama washiriki wa Kanisa la Bwana matumaini na imani wakati tunapojitahidi kuweka amri ya kisheria ya maandiko kutii sauti ya Bwana8 kama inavyokuja kupitia sauti ya watumishi Wake, manabii.9 Viongozi wote katika Kanisa la Bwana wameitwa na mamlaka stahiki. Hakuna Nabii au kiongozi yeyote katika Kanisa kwa mintarafu hiyo amejiita mwenyewe. Hakuna nabii aliyewahi kuchaguliwa kwa kura. Bwana aliweka hilo wazi wakati aliposema, “Hamkunichagua mimi, bali nimewachagueni nyinyi, na kuwatawaza.”10 Nyinyi nami hatupigi “kura” kwa viongozi wa Kanisa, kwenye ngazi yoyote. Hata hivyo, tunapata kuwa na heshima ya kuwaidhinisha.
Njia za Bwana ni tofauti na njia za binadamu. Njia za binadamu zinawatoa watu kutoka ofisini au biashara wanapokuwa wazee au wanapokuwa hawajiwezi. Lakini njia za binadamu siyo na kamwe haziwezi kuwa njia za Bwana. Kuwaidhinisha kwetu manabii ni ahadi binafsi kwamba tutafanya kwa kadri ya uwezo wetu kuunga mkono vipaumbele vya kinabii vyao. Kuidhinisha kwetu ni kama onyesho la kiapo kwamba tunatambua wito wao katika wajibu wao kama nabii kuwa halali na kutambua kuwa ni wa kutufunganisha pamoja.
Miaka ishirini na sita kabla hajawa Rais wa Kanisa, George Albert Smith, alisema: “Wajibu ambao tunafanya wakati tunapoinua mikono yetu… ni mtakatifu kweli. Haimaanishi kwamba tutakwenda kimya kimya kwenye njia zetu na kuwa radhi kwamba nabii wa Bwana ataongoza kazi yake, lakini inamaanisha… kwamba tutasimama nyuma yake; tutasali kwa ajili yake; tutalinda sifa yake halisi, na tutajitahidi kutimiza maelekezo yake kama Bwana atakavyoelekeza.”11
Bwana anayeishi anaongoza Kanisa Lake lililo hai!12 Bwana anafunua mapenzi Yake kwa Kanisa kwa nabii Wake. Jana, baada ya kualikwa kumwidhinisha Thomas S. Monson kama Rais wa Kanisa, pia tulikuwa na heshima ya kumwidhinisha yeye, washauri katika Urais wa Kwanza, na Washiriki wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili kama manabii, waonaji na wafunuaji. Fikiria hayo! Tunawaidhinisha wanaume 15 kama manabii wa Mungu! Wanashikilia funguo zote za ukuhani ambazo daima zimewahi kutolewa kwa mwanaume katika kipindi hiki.
Kuitwa kwa Wanaume 15 kwenye Utume Mtakatifu kunatoa ulinzi mkubwa kwetu kama washiriki wa Kanisa. Kwa nini? Kwa sababu maamuzi ya viongozi hawa lazima yawe ya kauli moja.13 Unaweza kufikiria jinsi Roho anavyohitaji kuvutia wanaume 15 kuleta umoja? Wanaume hawa 15 wana usuli wa kielimu na kiweledi uliotofautiana, pamoja na maoni tofauti kuhusu mambo mengi. Mniamini! Wanaume hawa 15—manabii, waonaji, na wafunuaji---wanajua mapenzi ya Bwana ni nini wakati umoja unapofikiwa! Wameweka sharti kuona kwamba mapenzi ya Bwana kiukweli yatatendeka. Sala ya Bwana inatoa mpangilio kwa kila mmoja wa hawa 15 wakati wanaposali: “Mapenzi yako yafanyike duniani kama Mbinguni.”14
Mtume mwenye ukubwa wa muda mrefu katika ofisi ya Mtume anasimamia.15 Mfumo huo wa ukubwa kwa kawaida utaleta wanaume wenye umri mkubwa kwenye ofisi ya Rais wa Kanisa.16 Inatoa mwendelezo, ukomavu unaotokana na uzoefu, na matayarisho ya muda mrefu, kama inavyoongozwa na Bwana.
Kanisa leo limeratibiwa na Bwana Mwenyewe. Ameweka mfumo wa ajabu wa utawala ambao unatoa uziada na visaidizi. Mfumo huo unatoa nafasi kwa uongozi wa kinabii hata wakati magonjwa yasiyoepukika na kutojiweza kunakotokana na umri unaozidi.17 Usawazisho na ulinzi ni mwingi ili mtu asije kamwe akapotosha Kanisa. Viongozi wakuu daima wanafundishwa ili kwamba siku moja watakuwa tayari kuketi katika mabaraza makuu zaidi. Wanajifunza jinsi ya kusikiliza sauti ya Bwana kupitia kwa minong’ono ya Roho.
Akihudumu kama Mshauri wa Kwanza kwa Rais Ezra Taft Benson, ambaye alikuwa anakaribia mwisho wa maisha yake duniani, Rais Gordon B. Hinckley alielezea:
“Kanuni na taratibu ambazo Bwana ameziweka kwa ajili ya utawala wa Kanisa Lake zinatayarisha kwa ajili mazingira … yoyote. Ni muhimu… kwamba pasiwe na wasiwasi au shaka kuhusu utawala wa Kanisa na matumizi ya vipawa vya unabii, ikijumuisha haki ya mwongozo, na ufunuo katika kusimamia mambo na utaratibu wa Kanisa, wakati Rais anaweza kuwa anaugua au hawezi kufanya kazi kikamilifu.
“Urais wa Kwanza na Baraza la Mitume Kumi na Wawili, walioitwa na kutawazwa kushikilia funguo za ukuhani, wana mamlaka na majukumu ya kuongoza Kanisa, kusimamia maagizo yake, kufafanua mafundisho yake, na kuasisi na kudumisha desturi zake.”
Rais Hinckley aliendelea:
“ Wakati Rais anaugua au hana uwezo wa kufanya kazi kikamilifu katika kazi zake zote za ofisi yake, Washauri wake wawili pamoja wanaunda Jamii ya Urais wa Kwanza. Wanaendelea na kazi za kila siku za Urais. …
“… Lakini maswali yote makubwa kuhusu sera, utaratibu, mipango, au mafundisho yanatazamwa kwa mpangilio na kwa maombi na Urais wa Kwanza na Wale Kumi na Wawili pamoja.”18
Mwaka jana, wakati Rais Monson alipofikisha miaka 5 ya kihistoria ya huduma kama Rais wa Kanisa, alitafakari kuhusu miaka yake 50 ya huduma ya kitume na akatoa kauli hii: “Umri hatimaye unatulemea sisi sote. Hata hivyo, tunaunganisha sauti zetu pamoja na Mfalme Benjamini, ambaye alisema… ‘Mimi niko kama nyinyi, kwa unyonge wa kila aina mwilini na akilini; walakini nimechaguliwa … na kutakaswa na baba yangu, … na nimelindwa na kuhifadhiwa kwa uwezo wake usio na kipimo, ili niwatumikie kwa uwezo wote, na nguvu ambazo Bwana amenipatia’ (Mosia 2:11).”
Rais Monson aliendelea: “Licha ya changamoto za kiafya zozote ambazo zinaweza kutujia, licha ya unyonge wowote katika mwili au akili, tunahudumu kwa uwezo wetu mkubwa. Ninawahakikishieni kwamba Kanisa linaongozwa kwa uwezo na vyema. Mfumo uliowekwa kwa Baraza la Urais wa Kwanza na Jamii ya wale Mitume Kumi na Wawili wanatuhakikishia [sisi] kwamba litakuwa siku zote salama na kwamba licha ya chochote kitakachotokea hakuna haja ya kuwa na wasiwasi au kuogopa. Mwokozi wetu,Yesu Kristo, ambaye tunamfuata, ambaye tunamwabudu, na ambaye tunamtumikia siku zote analiongoza Kanisa hili daima.”19
Rais Monson, tunakushukuru kwa kweli hizo! Na tunakushukuru kwa maisha yako ya huduma ya kujitolea ya mfano bora. Ningependa kusema kwa niaba ya washiriki wa Kanisa ulimwenguni kote katika muungano wetu na onyesho letu shukrani za dhati kwa ajili yako. Tunakuheshimu! Tunakupenda! Tunakuidhinisha sio tu kwa mikono yetu iliyoinuliwa juu lakini kwa mioyo yetu yote na bidii zilizowekwa wakfu. Kwa unyenyekevu na kwa hamasa, “Siku zote tunakuombea, nabii wetu mpendwa”!20 Katika jina la Yesu Kristo, amina.