Kushiriki Nuru Yako
Lazima tusimame imara katika imani yetu na tupaze sauti zetu ili kutangaza mafundisho ya kweli
Usiku wa leo ningetaka kuzingatia majukumu mawili muhimu tuliyonayo. Kwanza, kuongeza nuru ya injili katika maisha yetu kwa kila wakati, na pili, kushiriki nuru hio na wengine.
Kina dada, je, mnajua mlivyo muhimu? Kila mmoja wenu---hivi sasa---ana thamani na umuhimu katika mpango wa wokovu wa Baba wa Mbinguni. Tuna kazi ya kufanya. Tunajua ukweli wa injili rejesho. Je, tuko tayari kutetea ukweli? Tunahitaji kuishi kulingana na injili, tunahitaji kuishiriki. Lazima tusimame imara katika imani yetu na kupaza sauti zetu ili kutangaza mafundisho ya kweli.
Katika Ensign na Liahona, ya Septemba 2014, Mzee M. Russell Ballard anaandika: “Tunahitaji zaidi ushawishi na imani ya kipekee ya wanawake wa imani. Tunawahitaji wajifunze mafundisho na waelewe kile tunachoamini ili kwamba waweze kutoa shuhuda zao kuhusu ukweli wa mambo yote.” 1
Kina dada, ninyi huimarisha imani yangu katika Yesu Kristo. Nimetazama mifano yenu, nimesikiza shuhuda zenu, na nimehisi imani yenu kutoka Brazil hadi Botswana! Mna uwezo wa kushawishi wale walio karibu nanyi popote mweendapo. Unahisiwa na watu wa karibu nanyi ---kutoka kwa familia yenu hadi kwa watu katika orodha ya simu zenu na kutoka kwa marafiki zenu kwenye mtandao wa kijamii hadi kwa wale walioketi karibu nanyi usiku wa leo. Ninakubaliana na Dada Harriet Uchtdorf, ambaye aliandika, “Mna nguvu, na ninyi ni mfano katika dunia inayozidi kuwa ovu mnapoonesha, kwamba injili ni ujumbe wa furaha. 2
Rais Thomas S. Monson alisema, “Ikiwa unataka kuwaangaza wengine, lazima ung’ae mwenyewe.” 3 Tunawezaje kuweka nuru ya ukweli kuangaza ndani yetu?” Wakati mwingine mimi huhisi kama taa iliyo na mwangaza mdogo. Je, nitaangaza zaidi vipi?
Maandiko yanafundisha, “Kile kilicho cha Mungu ni nuru; na yule ambaye huipokea nuru, na kukaa ndani ya Mungu, hupokea nuru zaidi.” 4 Lazima tukae ndani ya Mungu kama vile andiko linavyosema. Lazima twende kwenye chanzo cha nuru---kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Tunaweza pia kwenda kwa hekalu, tukijua kwamba kila kitu ndani yake kinaelekeza kwa Kristo na dhabihu Yake kuu ya upatanisho.
Fikiria juu ya athari mahekalu huwa nayo kwenye mazingira yao. Huwa yanarembesha miji; yanang’aa kutoka milimani. Kwa nini yanarembesha na kung’aa? Kwa sababu kama vile maandiko yanavyosema, “ukweli hunga’ara” 5 na mahekalu yana ukweli na kusudi ya milele; nanyi pia.
Mnamo mwaka wa 1877, Rais George Q. Cannon alisema, “kila hekalu, hupunguza nguvu za shetani duniani.”6 Ninaamini kwamba popote hekalu hujengwa duniani, husukuma kando giza. Kusudi la hekalu ni kuhudumia wanadamu na kuwapa watoto wote wa Baba wa Mbinguni uwezo wa kurudi na kuishi Naye. Je, si kusudi letu ni sawa na majengo haya yaliyowekwa wakfu, manjumba haya ya Bwana? Kuhudumia wengine na kuwasaidia kutupa mbali giza na kurejea kwa nuru ya Baba wa Mbinguni?
Kazi takatifu ya hekalu itaongeza imani yetu katika Kristo, na kisha tutaweza kushawishi vyema zaidi imani ya wengine. Kupitia kwa roho ya kunawirisha ya hekalu, tunaweza kujifunza ukweli, uwezo, na tumaini la Upatanisho wa Mwokozi katika maisha yetu binafsi.
Miaka michache iliyopita familia yetu ilikumbana na changamoto kuu. Nilienda hekaluni na huko niliomba kwa dhati kwa ajili ya usaidizi. Nilipewa muda wa ukweli. Nilipokea uvuvio wazi wa upungufu wangu, na nilishituka. Katika muda huo wa mafunzo ya kiroho, nilimuona mwanamke mwenye kiburi akifanya vitu kwa njia yake mwenyewe, si hasa kwa njia ya Bwana, na kuchukua sifa kwa siri kwa yale yaliyoonekana kuwa mafanikio. Nilijua nilikuwa nakijitazama mwenyewe. Niliomba moyoni mwangu kwa Baba wa Mbinguni, nikisema, “Sitaki kuwa mwanamke huyo, lakini nawezaje kubadilika?”
Kupitia kwa roho safi ya ufunuo katika hekalu, nilifundishwa juu ya mahitaji yangu makubwa ya Mkombozi. Nilimgeukia mara moja Mwokozi Yesu Kristo na kuhisi dhiki yangu ikiyeyuka na tumaini kubwa likinijaza moyoni wangu. Alikuwa ndiye tumaini langu la pekee, na nilitamani kumshikilia Yeye. Ilikuwa wazi kwangu kwamba ---mwanamke anayejipenda, mwanamke wa asili “ni adui kwa Mungu” 7 na kwa watu katika nyanja yake ya ushawishi. Katika hekalu siku hiyo nilijifunza ilikuwa tu kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo kwamba asili yangu ya kiburi ingeweza kubadilika na kwamba ningewezeshwa kutenda mema. Nilihisi upendo wake sana, na nilijua angenifundisha kwa Roho na kunibadilisha kama ningetoa moyo wangu Kwake, bila kuzuia chochote.
Bado ninapambana na upungufu wangu, lakini naamini katika msaada wa uungu wa Upatanisho. Maelekezo haya safi yalikuja kwa sababu niliingia katika hekalu takatifu, nikitafuta msaada na majibu. Niliingia hekaluni na mizigo, na nilitoka nikijua kwamba nilikuwa na Mwokozi mwenye nguvu zote. Nilikuwa mwepesi na wa furaha kwa sababu nilikuwa nimepokea nuru yake na kukubali mpango Wake kwa ajili yangu.
Yakiwa yamewekwa duniani kote, mahekalu yana mfano wao wa kipekee na mtindo wa kujengwa nje, lakini ndani yote yana nuru ya milele, kusudi, na ukweli. Katika 1 Wakorintho 3:16 tunasoma, “e, hamjui kwamba ninyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?”Sisi pia kama mabinti wa Mungu tumewekwa duniani kote, na kila mmoja wetu ana mfanano na mtindo wa kipekee wa nje, kama mahekalu. Pia tuna nuru ya kiroho ndani yetu. Nuru hii ya kiroho ni onyesho la nuru ya Mwokozi. Wengine watavutiwa kwa nuru hii.
Tuna majukumu yetu wenyewe duniani---kuanzia binti, mama, kiongozi, na mwalimu hadi kwa dada, mpokea mshahara, mke, na wengineo. Kila moja ni muhimu. Kila jukumu litakuwa na nguvu ya kimadili ---tunapoonyesha kweli za injili na maagano ya hekalu maishani mwetu.
Mzee D. Todd Christofferson alisema, “Kwa hali zote, mama anaweza kushawishi kwa kiwango kisichofikiwa mtu yeyote mwingine katika uhusiano wowote mwingine.” 8
Wakati watoto wetu walipokuwa wachanga, nilihisi kama nahodha msaidizi wa meli, pamoja na mume wangu, David, na niliwatazamia watoto wetu 11 kama mashua ndogo kando yetu kwenye bandari, tukijitayarisha kuelekea baharini mwa dunia. David nami tulihisi haja ya kuangalia dira ya Bwana kila siku kwa ajili ya mwelekezo bora wa kusafiri baharini na meli yetu ndogo.
Siku zangu zilijazwa na mambo ya kusahaulika kama vile kukunja nguo, kusoma vitabu vya watoto, na kupika chakula cha jioni. Wakati mwingine katika bandari ya nyumba yetu, hatuwezi kuona kwamba kupitia vitendo hivi vidogo, vya kila mara, vikiwemo sala ya familia, kujifunza maandiko, na jioni ya familia nyumbani, mambo makubwa hufanyika. Lakini ninashuhudia kwamba vitendo hivi vina umuhimu wa milele. Shangwe kubwa huja wakati mashua hayo madogo---watoto wetu---wanakuwa wakubwa na kuwa meli zilizojazwa na nuru injili na tayari “kuingia katika utumishi wa Mungu”9Vitendo vyetu vidogo vya imani na huduma ni vile wengi wetu tunaweza kuendelea katika Mungu na hatimaye kuleta nuru ya milele na utukufu kwa familia yetu, marafiki zetu, na wenzi wetu. Hakika unaweza kuwa na uwezo wa kuwashawishi wengine!
Fikiria juu ya ushawishi ambao imani ya msichana wa umri wa Msingi anaweza kuwa nayo kwa familia yake. Imani ya binti yetu ilibariki familia yetu tulipompoteza mwana wetu mdogo kwa Uwanja wa Burudani. Familia ilikimbia kote kwa wasiwasi tukimtafuta. Mwishowe, binti yetu wa miaka tisa alinigusa mkononi na kusema, “Mama, si tuombe?” Alijua! Familia ilikusanyika katikati mwa umati wa watu na kuomba kumpata mtoto wetu. Tulimpata. Kwa wasichana wote wa Msingi ninasema, “ Tafadhali endeleeni kuwakumbusha wazazi wenu kuomba!”
Msimu huu wa jua nilikuwa na fursa ya kuhudhuria kambi ya wasichana 900 huko Alaska. Ushawishi wao kwangu ulikuwa mkubwa. Walikuja kwa kambi wakiwa wamejiandaa kiroho, wakiwa wamesoma Kitabu cha Mormoni na wakiwa wamekariri “Kristo Aliye Hai: Ushuhuda wa Mitume.” Usiku wa tatu wa kambi, wasichana wote 900 walisimama pamoja na kukariri waraka wote neno kwa neno.
Roho ilijaza ukumbi mkubwa na nikatamani kuungana nao, lakini sikuweza. Sikuwa nimelipa gharama ya kukariri.
Nimeanza kujifunza maneno ya “Kristo Aliye Hai” kama vile kina dada hawa walivyofanya, na kwa sababu ya ushawishi wao ninafurahia zaidi agano la sakramenti kumkumbuka daima Mwokozi, ninaporudia tena na tena ushuhuda wa Mitume wa Kristo. Sakramenti inaanza kuwa na maana ya kina zaidi kwangu.
Tumanini langu ni kumpa Mwokozi zawadi ya Krismasi mwaka huu kwa kukariri “Kristo Aliye Hai” na kuthaminiwa kwa dhati moyoni mwangu Desemba 25. Ninatumaini ninaweza kuwa na ushawishi wa wema---kama kina dada wa Alaska walivyokuwa kwangu.
Unaweza kujipata katika maneno yafuatayo ya waraka huu “Kristo Aliye Hai?” “Aliwahimiza wote wafuate mfano Wake. Alitembea barabara za Palestina, akiponya wagonjwa, akiwafanya vipofu waone, na kufufua wafu.”10
Sisi, kina dada wa Kanisa, hatutembei barabara ya Palestina tukiwaponya wagonjwa, lakini tunaweza kuombea na kutumia upendo wa kuponya wa Upatanisho kwa uhusiano uliogonjeka na kuvunjika.
Ingawa hatutawafanya vipofu waone kwa njia kama ya Mwokozi, tunaweza kushuhudia mpango wa wokovu kwa wale walio vipofu kiroho.Tunaweza kufungua macho ya ufahamu wao kwa umuhimu wa nguvu ya ukuhani katika maagano ya milele.
Hatutakuwa tukiwafufua wafu kama vile Mwokozi, lakini tunaweza kuwabariki wafu kwa kupatiana majina yao kwa ajili ya kazi ya hekalu. Kisha hakika tutawainua kutoka kwa jela yao ya kiroho na kuwapa njia ya uzima wa milele.
Ninashuhudia kuwa tuna Mwokozi aliye hai, Yesu Kristo, na pamoja na nguvu Yake na nuru Yake tutawezeshwa kuzuia giza ya dunia, kupaza sauti kwa ukweli tunaojua, kuwashawishi wengine kumjia Yeye. Katika jina la Yesu Kristo, amina.