Bwana ana mpango Kwetu!
Tukiendelea kuishi jinsi tunavyoishi, je, baraka zilizoahidiwa zitatimizwa?
Ni fursa iliyoje kuwa sehemu ya wakati huu wa kihistoria wakati wasemaji wa mkutano mkuu wana fursa ya kuzungumza katika lugha yao ya kwanza. Mara ya mwisho nilizungumza katika mimbari hii, nilikuwa na wasiwasi juu ya lafudhi yangu katika lugha ya Kiingereza. Sasa, nina wasiwasi kuhusu mwendo wa Kireno changu. Sitaki kusema kwa haraka zaidi kuliko vichwa vya habari.
Sisi sote tumekuwa na au bado tutakuwa na nyakati za uamuzi mkubwa katika maisha yetu. Je, napaswa kutekeleza kazi hii au kazi ile? Je, napaswa kutumikia misheni? Je, huyu ndiye ninayefaa kuoa?
Hizi ni hali katika maeneo mbalimbali ya maisha yetu ambapo mabadiliko madogo katika mwelekeo yanaweza kuwa na madhara makubwa siku zijazo. Kwa maneno ya Rais Dieter F. Uchtdorf: “Kwa miaka ya kumtumikia Bwana ..., nimejifunza kwamba tofauti kati ya furaha na taabu katika watu binafsi, katika ndoa, na familia mara nyingi hushuka chini kwa makosa ya nyusi chache tu” (“A Matter of a Few Degrees,” Ensign orLiahona, May 2008, 58).
Tunaweza kuepukana vipi na makosa haya madogo katika hesabu?
Nitatumia uzoefu wangu binafsi ili kueleza ujumbe wangu.
Wakati wa mwisho wa miaka ya 1980, familia yetu ndogo ilijumuisha mke wangu, Monica, wawili kati ya watoto wetu wanne, nami. Tuliishi katika São Paulo, Brazil, nilifanyaa kazi kampuni nzuri. Nilikuwa nimemaliza masomo yangu ya chuo kikuu na karibuni nilikuwa nimeachiliwa kama askofu wa kata ambapo tulikuwa tunaishi. Maisha yalikuwa mazuri, na kila kitu kilionekana kuwa kama ilivyopaswa kuwa---mpaka siku moja rafiki wa zamani alipokuja kututembelea.
Katika hitimisho la ziara yake, alitoa maoni na kuuliza swali lililobadilisha mawazo yangu. Alisema, “Carlos, kila kitu kinaonekana kinaendelea vizuri kwako, familia yako, kazi yako, na huduma yako katika Kanisa, lakini---”na kisha likaja swali, “ukiendelea kuishi jinsi unavyoishi, je, ahadi zilizoahidiwa katika baraka yako ya baba mkuu zitatimizwa?”
Sijawahi kamwe kufikiria kuhusu baraka yangu ya baba mkuu kwa njia hii. Naisoma mara kwa mara lakini kamwe si kwa nia ya kuangalia upande wa ahadi zilizoahidiwa katika siku zijazo na kutathmini jinsi nilivyokuwa nikiishi kwa sasa.
Baada ya ziara yake, niligeuza mtazamo wangu kwa baraka yangu ya babu, nikishangaa, “Tukiendelea kuishi jinsi tunavyoishi, je, ahadi zilizoahidiwa zitatimizwa?” Baada ya kutafakari kidogo, Nilikuwa na hisia kwamba mabadiliko kadhaa ni muhimu, hasa kuhusiana na elimu yangu na taaluma.
Haikuwa uamuzi kati ya kile kilichokuwa cha haki na makosa lakini kati ya kile kilichokuwa kizuri na kile ambacho ni bora, kama vile Mzee Dallin H Oaks alivyotufundisha aliposema: “Tunapofikiria chaguzi mbalimbali, tunapaswa kukumbuka kwamba haitoshi kwamba kitu fulani ni kizuri. Chaguzi zingine ni bora zaidi, na bado zingine ni bora” (“Good, Better, Best,” Ensign orLiahona, Nov. 2007, 104–5).
Ni kwa jinsi gani basi tunaweza kuhakikisha kwamba tunafanya uamuzi bora?
Hapa kuna baadhi ya kanuni ambazo nimejifunza:
Kanuni Nambari Moja: Tunahitaji Kufikiria Chaguzi Zetu kwa Lengo Akilini
Kutoa maamuzi ambayo yanaweza kuathiri maisha yetu na wale tunaowapenda bila kuwa na maono mapana ya matokeo yake kunaweza kuleta hatari kadha. Hata hivyo, tukifikiria kuhusu matokeo yanayowezekana ya maamuzi haya katika siku zijazo, tunaweza kuona kwa uwazi mkuu njia bora ya kufuata wakati huu.
Kuelewa uhalisi wetu, ni kwa nini tuko hapa, na kile Bwana anatarajia kutoka kwetu katika maisha haya kutasaidia kutupa maono mapana tunayohitaji.
Tunaweza kupata mifano katika maandiko ambapo kuwa na maono mapana kulitoa ufafanuzi kuhusu njia ya kwenda.
Musa alizungumza na Bwana uso kwa uso, kujifunza kuhusu mpango wa wokovu, na hivyo kuelewa vyema jukumu lake kama nabii wa kukusanyika kwa Israeli.
“Na Mungu akamwambia Musa, akisema: Tazama, mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi. …
“ … Na nitakuonyesha wewe kazi za mikono yangu. …
“Na ninayo kazi kwa ajili yako, Musa, mwanangu”(Moses 1:3–4, 6).
Kwa uelewa huu, Musa alikuwa na uwezo wa kuvumilia miaka mingi ya dhiki katika jangwa na kuongoza Israeli kurudi nyumbani.
Lehi, nabii mkuu wa Kitabu cha Mormoni, aliota ndoto, katika maono yake alijifunza juu ya huduma yake ya kuongoza familia yake hata nchi ya ahadi.
“Na ikawa kuwa akamwamrisha baba yangu, hata kwenye ndoto, kuwa aichukue jamii yake aelekee nyikani.
“… Na akaacha nyumba yake, na nchi yake ya urithi, na dhahabu yake, na fedha yake, na vitu vyake vya thamani” (1 Nefi 2:2, 4).
Lehi alibaki mwaminifu kwa maono haya licha ya matatizo ya usafiri na kuweza kuacha nyuma maisha ya starehe katika Yerusalemu.
Nabii Joseph Smith ni mfano mwingine wa ajabu. Kupitia kwa funuo nyingi, kuanzia na Ono la Kwanza, aliweza kukamilisha kazi yake ya kurejesha vitu vyote (ona Joseph Smith—Historia 1:1–26).
Na kuhusu sisi je? Bwana anatarajia nini kutoka kila mmoja wetu?
Hatuhitaji kuona malaika ili kupata uelewa. Tuna maandiko, hekalu, manabii walio hai, baraka zetu za baba mkuu, viongozi wenye maongozi, na zaidi ya yote, haki ya kupata ufunuo wa kibinafsi ili kuongoza maamuzi yetu.
Kanuni Nambari Mbili: Tunapaswa Kuwa Tayari kwa Changamoto ambazo Zitakuja
Njia bora maishani kwa nadra huwa rahisi. Mara nyingi, hasa ni kinyume. Tunaweza kuangalia mifano ya manabii niliowataja.
Musa, Lehi, na Joseph Smith hawakuwa na safari rahisi, licha ya kweli kwamba maamuzi yao yalikuwa sahihi.
Je, tuko tayari kulipa dhamana ya maamuzi yetu? Je, tuko tayari kuacha sehemu zetu za faraja ili kufikia mahali bora zaidi?
Kwa kurejelea tukio langu la baraka ya baba mkuu, nilifikia hitimisho wakati huo kwamba napaswa kutafuta elimu zaidi na kuomba udhamini kutoka chuo kikuu cha Marekani. Kama ningechaguliwa, ingebidi niache kazi yangu, kuuza kila kitu tulichokuwa nacho, na kuja kuishi nchini Marekani kama mwanafuzi mdhaminiwa kwa miaka miwili.
Mitihani kama vile TOEFL na GMAT ilikuwa changamoto za kwanza za kushinda. Ilichukua miaka mitatu mirefu ya maandalizi, kukataliwa kwingi, na majibu ya “pengine” kabla ya kukubaliwa katika chuo kikuu. Bado nakumbuka mwito wa simu mwishoni mwa mwaka wa tatu kutoka kwa mtu anayesimamia udhamini.
Alisema, “Carlos, nina habari njema na habari mbaya kadha kwako. Habari njema ni kwamba wewe ni miongoni mwa watu watatu waliofuzu mwaka huu.” Kulikuwa tu na nafasi moja wakati huo. “Habari mbaya ni kwamba mmoja wa wagombeaji ni mwana wa mtu mashuhuri, na mwingine ni mwana wa mtu mwingine muhimu, na kisha kuna wewe.”
Nilijibu kwa haraka, “Na mimi ... Mimi ni mwana wa Mungu.”
Shukrani, uzazi wa kidunia, haikuwa sababu ya kuamua, na nilikubaliwa mwaka huo, mwaka 1992.
Sisi ni watoto wa Mwenyezi Mungu. Yeye ni Baba yetu, Yeye anatupenda, na Yeye ana mpango kwetu. Hatuko hapa katika maisha haya kupoteza muda wetu tu, kuzeeka, na kufa. Mungu anataka tuwe na kufikia kilele cha uwezo wetu.
Kwa maneno ya Rais Thomas S. Monson: “Kila mmoja wenu, mseja au aliyeoleka, bila kujali umri, ana nafasi ya kujifunza na kukua. Panua maarifa yako, yote ya kiakili na kiroho, kwa kimo kamili ya uwezo wako wa Mungu” (“The Mighty Strength of the Relief Society,” Ensign, Nov. 1997, 95).
Kanuni nambari Tatu: Tunahitaji Kushirikisha Ono Hili na Watu Tunaowapenda
Lehi alifanya zaidi ya majaribio machache ili kusaidia Lamani na Lemueli kuelewa umuhimu wa mabadiliko waliokuwa wakifanya. Ukweli kwamba hawakushiriki maono ya baba yao iliwafanya kunung’unika wakati wa safari. Nefi, kwa upande mwingine, alimtafuta Bwana ili kuona kile baba yake alikuwa ameona.
“Na ikawa kwamba mimi Nefi baada ya kusikia maneno yote ya baba yangu kuhusu vile vitu ambavyo alikuwa ameona, … mimi …nikatamani nione pia na kusikia na kuvijua vitu hivi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu” (1 Nefi 10:17).
Kwa maono haya, Nefi alikuwa na uwezo si tu kukabiliana na changamoto ya safari lakini pia kuongoza familia yake wakati inapohitajika.
Kuna uwezekano mkubwa sana kwamba tunapoamua kufuata njia fulani, watu ambao tunawapenda wataathirika, na baadhi hata watashiriki nasi matokeo ya uchaguzi huu. Kimsingi, wapaswa kuwa na uwezo wa kuona kile tunachokiona na kushiriki imani yetu sawa. Hii mara nyingi haiwezekani, lakini inapotokea, safari ni rahisi sana.
Katika uzoefu binafsi niliotumia kama mfano, bila shaka nilihitaji msaada wa mke wangu. Watoto bado walikuwa wadogo na hawakuwa na mengi ya kusema, lakini msaada wa mke wangu ulikuwa muhimu. Nakumbuka kwamba, mara ya kwanza, Monica nami tulihitajika kujadili kwa makini mabadiliko katika mipango hadi alipojisikia vizuri na pia kuwajibika. Maono haya ya pamoja yalimsababisha siyo tu kuunga mkono mabadiliko lakini pia kuwa sehemu muhimu katika mafanikio yake.
Mimi najua kuwa Bwana ana mpango kwa ajili yetu katika maisha haya. Yeye anatujua. Anajua kilicho bora kwetu. Kwa sababu mambo yanakwenda vyema haimaanishi kwamba hatupaswi mara kwa mara kufikiria kama kuna kitu kizuri zaidi. Tukiendelea kuishi kama tunavyoishi, je, baraka zilizoahidiwa zitatimizwa?
Mungu yu hai. Yeye ni Baba yetu. Mwokozi Yesu Kristo yu hai, na najua kwamba kupitia kwa dhabihu Yake ya upatanisho tunaweza kupata nguvu ili kushinda changamoto zetu za kila siku. Kwa jina la Yesu Kristo, amina.