Maandiko Matakatifu
Mosia 5


Mlango wa 5

Watakatifu huwa wana na mabinti wa Kristo kwa imani—Kisha wanaitwa kwa jina la Kristo—Mfalme Benjamini anawaonya wawe imara na wasiotingishika katika matendo mema. Karibia mwaka 124 K.K.

1 Na sasa, ikawa kwamba wakati mfalme Benjamini alipomaliza kuwazungumzia watu wake, alituma ujumbe miongoni mwao, akitamani kujua kama watu wake wameyaamini maneno ambayo alikuwa amewazungumzia.

2 Na wote wakalia kwa sauti moja, wakisema: Ndiyo, tunaamini maneno yote ambayo umetuzungumzia; na pia, tunajua uhakika na ukweli wao, kwa sababu ya Roho wa Bwana Mwenyezi, ambaye ameleta mabadiliko makuu ndani yetu, au mioyoni mwetu, hata kwamba hatuna tamaa ya kutenda maovu tena, lakini kutenda mema daima.

3 Na sisi, wenyewe, pia, kwa wema mkuu wa Mungu, na madhihirisho ya Roho wake, tunayo maono makuu ya yale yatakayokuja; na kama ingefaa, tungetoa unabii wa vitu vyote.

4 Na ni kwa imani katika vitu vile ambavyo mfalme wetu ametuzungumzia ambavyo vimetuletea ufahamu huu mkuu, ambayo kwayo tunasherekea kwa shangwe kuu sana.

5 Na tunataka tuagane na Mungu wetu ili tutende nia yake, na tuwe watiifu kwa amri zake kwa vitu vyote atakavyotuamuru, katika maisha yetu yaliyosalia, kwamba tusijiletee sisi wenyewe mateso yasiyo na mwisho, kama vile alivyosema malaika, kwamba tusinywe kutoka kile kikombe cha ghadhabu ya Mungu.

6 Na sasa, haya ndiyo maneno ambayo mfalme Benjamini aliwatakia; na kwa hivyo akawaambia; Mmezungumza maneno yale ambayo nilitaka; na agano ambalo mmefanya ni agano takatifu.

7 Na sasa, kwa sababu ya agano lile ambalo mmefanya mtaitwa watoto wa Kristo, wanawe, na mabinti zake; kwani tazama, siku hii amewazaa kiroho; kwani mnasema kwamba mioyo yenu inabadilishwa kwa imani katika jina lake; kwa hivyo, amewazaa na mkawa wanawe na mabinti zake.

8 Na chini ya jina hili mmefanywa huru, na hakuna jina lingine ambalo linaweza kuwafanya muwe huru. Hakuna jina lingine ambalo kwalo huleta wokovu; kwa hivyo, ningependa mjivike juu yenu jina la Kristo, nyote ambao mmeingia katika agano na Mungu kwamba mtakuwa watiifu hadi mwisho wa maisha yenu.

9 Na itakuwa kwamba yeyote atakayefanya hivi atakuwa katika mkono wa kulia wa Mungu, kwani atajua jina ambalo anaitwa; kwani ataitwa kwa jina la Kristo.

10 Na sasa itakuwa kwamba, yeyote asiyejitundika jina la Kristo lazima aitwe kwa jina lingine; kwa hivyo, anajikuta kwenye mkono wa kushoto wa Mungu.

11 Na nataka pia mkumbuke, kwamba hili ndilo jina ambalo nilisema kwamba nitawapatia ambalo kamwe halitafutwa, ila tu kwa dhambi; kwa hivyo, jichungeni kwamba msianguke dhambini, kwamba jina hilo lisifutwe kutoka mioyo yenu.

12 Ninawaambia, nataka kwamba mkumbuke kudumisha jina ambalo limeandikwa mioyoni mwenu, kwamba msipatikane kwenye mkono wa kushoto wa Mungu, lakini kwamba msikie na kujua sauti ambayo itawaita, na pia, lile jina ambalo atawaita.

13 Kwani ni vipi mtu atamjua yule bwana ambaye hajamtumikia, na aliye mgeni kwake, na yuko mbali katika mawazo na nia za moyo wake?

14 Na tena, je mtu huchukua punda wa jirani yake, na kumweka? Ninawambia, La; hatakubali hata ale miongoni mwa mifugo yake, lakini atamfukuza, nakumtupilia mbali. Nawambia, itakuwa hivyo nanyi msipojua ni kwa jina gani mtakaloitwa.

15 Kwa hivyo, nataka muwe imara na msiotingishika, daima mkitenda matendo mema, ili Kristo, Bwana Mungu Mwenyezi, awaweke muhuri wake, ili mletwe mbinguni, ili mpokee wokovu usio na mwisho na uzima wa milele, kwa hekima, na uwezo, na haki na rehema za yule aliyeumba vitu vyote, mbinguni na ardhini, ambaye ni Mungu juu ya yote. Amina.