TJS, Luka 12:9–12. Linganisha na Luka 12:9–10; ona pia TJS, Mathayo 12:37–38 na M&M 132:26–27
Yesu anaelezea kwamba kukufuru dhidi ya Roho Mtakatifu haitasamehewa.
9 Lakini mwenye kunikana mimi mbele za watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.
10 Sasa wanafunzi wake walijua kwamba amesema hiyo, kwa sababu wamenena uovu dhidi yake mbele ya watu; maana walikuwa waoga kumkiri mbele ya watu.
11 Nao wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Anajua yaliyo mioyoni mwetu, naye anasema kuhusu hukumu yetu, nasi hatutasamehewa. Lakini yeye aliwajibu, na kuwaambia,
12 Yeyote atakaye nena neno dhidi ya Mwana wa mtu, na akatubu, naye atasamehewa; bali kwa yeye atakayekufuru dhidi ya Roho Mtakatifu, hatasamehewa.
TJS, Luka 12:41–57. Linganisha na Luka 12:37–48
Yesu anafundisha kwamba watumishi Wake lazima daima wawe tayari kwa ajili ya ujio Wake.
41 Maana, tazama, yeye aja katika zamu ya kwanza ya usiku, na pia atakuja katika zamu ya pili, na tena atakuja katika zamu ya tatu.
42 Na amini ninakuambieni, Yeye tayari amekwisha kuja, kama ilivyoandikwa juu yake; na tena yeye ajapo katika zamu ya pili, au zamu ya tatu, heri watumishi wale wakati ajapo, akiwakuta wakifanya hivyo;
43 Maana Bwana wa watumishi wale atajifunga yeye mwenyewe, na kuwafanya wakae chini chakulani, na atakuja na kuwatumikia.
44 Na sasa, amini ninayasema mambo haya kwenu ninyi, ili mpate kujua hii, kwamba ujio wa Bwana ni kama mwivi usiku.
45 Na ni mfano wa mtu aliye mwenye nyumba, ambaye, kama halindi mali yake, mwivi huja katika saa asiyoijua, na kuchukua mali yake, na kuwagawia jamaa zake.
46 Nao wakasemezana wao kwa wao, Kama Bwana mwema mwenye nyumba angelijua saa ile mwivi atakayokuja, angelikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa na kupoteza mali yake.
47 Naye akawaambia, Amini, ninawaambia, nanyi jiwekeni tayari pia; maana Mwana wa mtu yuaja katika saa msiyodhania.
48 Kisha Petro akamwambia, Bwana, watuambia sisi fumbo hili, au kwa wote?
49 Naye Bwana akasema, Ninawaambia wale ambao Bwana atawafanya watawala juu ya nyumba yake, ili kuwapa watoto wake sehemu yao ya chakula katika wakati wake.
50 Nao wakasema, Ni nani huyo basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye hekima?
51 Na Bwana akawaambia. Ni mtumishi yule ambaye hukesha, ili kutoa sehemu yake ya chakula katika wakati wake.
52 Heri mtumishi yule ambaye Bwana wake ajapo, atamkuta akifanya hivyo.
53 Kweli nawaambia, kwamba atamweka kuwa mtawala juu ya vyote alivyo nanyo.
54 Lakini mtumishi mwovu ni yule ambaye hatakutwa akikesha. Na kama mtumishi wa hivyo hatakutwa akikesha, yeye atasema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja; na ataanza kuwapiga wajoli, na wanaume kwa wanawake, na kula, na kunywa, na kulewa.
55 Bwana wake mtumishi huyo atakuja katika siku asiyoitazamia, na katika saa asiyoijua, naye atamkatilia chini, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini.
56 Na mtumishi yule aliyejua mapenzi ya Bwana wake, na asijiweke tayari kwa ujio wa Bwana wake, wala kutenda kulingana na mapenzi yake, atapigwa kwa viboko vingi.
57 Lakini ambaye hajui mapenzi ya Bwana wake, na akafanya mambo yenye kustahili viboko, atapigwa kwa viboko vichache. Maana kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakiwa vingi; na kwa yule ambaye Bwana amemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watu watataka zaidi.