Maandiko Matakatifu
Ibrahimu 3


Mlango wa 3

Ibrahimu ajifunza juu ya jua, mwezi, na nyota kwa njia ya Urimu na Thumimu—Bwana anamfunulia asili ya umilele wa roho—Anajifunza juu ya maisha kabla, kuteuliwa kabla, Uumbaji, kuteuliwa kwa Mkombozi, na hali ya pili ya mwanadamu.

1 Na mimi, Ibrahimu, nilikuwa na Urimu na Thumimu, ambavyo Bwana Mungu wangu alinipatia, katika Uru ya Wakaldayo;

2 Nami nikaziona nyota, kwamba zilikuwa kubwa sana, na kwamba mojawapo ilikuwa karibu zaidi na kiti cha enzi cha Mungu; na zilikuwa nyingi kubwa, ambazo zilikuwa karibu nayo;

3 Na Bwana akaniambia: Hizi ndizo zinazotawala; na jina la ile kubwa ni Kolobu, kwa sababu iko karibu nami, kwani Mimi ndimi Bwana Mungu wako: Nimeiweka hii izitawale zile zote zilizo katika mpangilio huo huo kama wa huo ambao juu yake wewe umesimama.

4 Na Bwana akaniambia, kwa Urimu na Thumimu, kwamba Kolobu ilikuwa mfano wa Bwana, kulingana na nyakati zake na majira katika mizunguko yake; kwamba mzunguko mmoja ni sawa na siku moja kwa Bwana, kwa jinsi ya kuhesabu kwake, ikiwa ni miaka elfu moja kulingana na wakati uliopangwa kwa hapo uliposimama wewe. Huku ndiko kuhesabu kwa wakati wa Bwana, kulingana na kuhesabu kwa Kolobo.

5 Na Bwana akaniambia: Sayari ambayo ni mwanga mdogo, ndogo kuliko ile itawalayo mchana, hata usiku, ni ya juu au ni kubwa kuliko hiyo ambayo wewe juu yake umesimama kwa kuhusu kuhesabu kwake wakati, kwa maana inatembea kwa mpangilio na pole pole zaidi; huu ni utaratibu kwa sababu inasimama juu ya dunia ambayo juu yake wewe umesimama, kwa hiyo kuhesabu wakati wake siyo mara nyingi sana kama vile idadi ya siku zake, na miezi, na miaka.

6 Na Bwana akaniambia: Sasa, Ibrahimu, kweli hizo mbili zipo, tazama na macho yako yanaziona; umejaliwa kujua nyakati za kuhesabu, na wakati uliopangwa, ndiyo, wakati uliopangwa wa dunia ambayo juu yake wewe umesimama, na wakati uliopangwa wa mwanga mkubwa uliowekwa kutawala mchana, na wakati uliopangwa wa mwanga mdogo ambao umewekwa kutawala usiku.

7 Sasa muda uliopangwa wa mwanga mdogo ni muda mrefu kwa kuhesabu kwa muda wa dunia ambayo juu yake wewe umesimama.

8 Na mahali zilipo kweli hizi mbili, hapo patakuwa na kweli nyingine juu yake, hii ni kusema, patakuwepo na sayari nyingine ambayo kuhesabu wakati wake utakuwa mrefu zaidi;

9 Na hivyo kutakuwa na kuhesabiwa kwa wakati wa sayari moja juu ya nyingine, hadi utakapofika karibu na Kolobo, Kolobo ambayo ni kwa mfano wa kuhesabu kwa wakati wa Bwana; Kolobo ambayo imewekwa karibu na kiti cha enzi cha Mungu, ili kuzitawala sayari zile zote ambazo ni za utaratibu huo huo kama wa hiyo ambayo juu yake wewe umesimama.

10 Na imetolewa kwako wewe ili kujua muda uliopangwa wa nyota zote zile zilizowekwa ili kutoa nuru, hadi wewe ufike karibu na kiti cha enzi cha Mungu.

11 Hivyo mimi, Ibrahimu, nikaongea na Bwana, uso kwa uso, kama mtu aongeavyo na mtu mwingine; naye akanieleza juu ya kazi ambazo mikono yake imezifanya;

12 Na akaniambia: Mwanangu, mwanangu (na mkono wake akiwa ameunyoosha), tazama nitakuonyesha haya yote. Naye akaweka mkono wake juu ya macho yangu, nami nikaona vitu hivyo ambavyo mikono yake ilivifanya, ambavyo vilikuwa vingi; navyo viliongezeka mbele ya macho yangu, nami sikuweza kuuona mwisho wake.

13 Na akaniambia: Hili ni Shineha, ambalo ni jua. Naye akaniambia: Kokobo, ambayo ni nyota. Naye akaniambia: Olea, ambao ni mwezi, Na akaniambia: Kokaubimu, ambayo humaanisha nyota, au mianga yote mikuu, ambayo ilikuwapo katika anga la mbingu

14 Na ilikuwa katika nyakati za usiku Bwana alipoyasema maneno haya kwangu: Nitakuzidisha, na uzao wako baada yako, kama hizi; na kama wewe usivyoweza kuhesabu idadi ya mchanga, hivyo ndivyo itakavyokuwa idadi ya wazao wako.

15 Na Bwana akaniambia: Ibrahimu, ninakuonyesha mambo haya kabla wewe hujaenda Misri, ili upate kuyatangaza maneno haya yote.

16 Kama vitu viwili vipo, na hapo pakiwa na kimoja juu ya kingine, hapo patakuwa na vitu vikubwa zaidi juu yao; kwa hiyo Kolobu ndiyo kubwa kupita Kokaubimu zote zile ambazo wewe umeziona, kwa sababu hiyo iko karibu zaidi na mimi.

17 Sasa, kama kuna vitu viwili, kimoja juu ya kingine, na mwezi ukawa juu ya dunia, halafu yawezekana ikawa kwamba sayari au nyota yaweza kuwa juu yake; na hakuna kitu Bwana Mungu wako atakachokichukua moyoni mwake ili akifanye isipokuwa kile atakachokikamilisha.

18 Hata hivyo yeye akazifanya nyota kubwa zaidi; vile vile, pia, kama patakuwa na roho mbili, na moja itakuwa na akili zaidi kuliko nyingine, hata hivyo roho hizi mbili, licha ya kuwa moja ina akili zaidi kuliko nyingine, zote hazina mwanzo; zilikuwepo kabla, nazo hazitakuwa na mwisho, nazo zitaishi baada ya hapa, kwa kuwa hizo ni ginolaumu, au milele.

19 Na Bwana akaniambia: Kweli hizi mbili zipo, kwamba zipo roho mbili, moja ikiwa na akili nyingi zaidi ya nyingine; na itakuweko nyingine yenye akili zaidi yao; Mimi ndimi Bwana Mungu wako, nina akili nyingi kuliko wao wote.

20 Bwana Mungu wako alimtuma malaika wake ili kukukomboa wewe kutoka mikono ya kuhani wa Elkena.

21 Mimi naishi katikati yao wote; kwa hiyo, Mimi, sasa nimeshuka chini kwako wewe ili kukutangazia kazi ambazo mikono yangu imezifanya, ambamo ndani yake hekima yangu huzipita zote, kwa maana ninatawala juu mbinguni, na chini duniani, kwa hekima yote na busara, juu ya viumbe-akili-asilia vyote ambavyo macho yako yalivyoviona kutoka mwanzo; nalishuka chini mwanzoni katikati ya viumbe-akili-asilia wote ambao wewe umewaona.

22 Sasa Bwana akanionyesha mimi, Ibrahimu, viumbe-akili-asilia ambavyo vilivyokuwepo kabla ya ulimwengu kuwako; na miongoni mwa hivi vyote vilikuwako vingi vilivyo mashuhuri na vikuu;

23 Na Mungu akaziona roho hizi kwamba zilikuwa njema, naye alisimama katikati yao, na kusema: Hawa nitawafanya watawala wangu; kwani alikuwa amesimama miongoni mwa wale ambao walikuwa roho, naye aliziona kuwa zilikuwa njema; naye akaniambia: Ibrahimu, wewe ulikuwa mmoja wao; wewe ulichaguliwa kabla hujazaliwa.

24 Na hapo akasimama mmoja miongoni mwao ambaye alifanana na Mungu, naye akasema kwa wale waliokuwa pamoja naye: Sisi tutakwenda chini, kwani kuna nafasi huko, nasi tutachukua vifaa hivi, nasi tutaifanya dunia mahali ambapo hawa watapata kukaa;

25 Nasi tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru;

26 Na wao ambao watatunza hali yao ya kwanza wataongezewa; na wao ambao hawatatunza hali yao ya kwanza hawatapata utukufu katika ufalme ule ule pamoja na wale walioitunza hali yao ya kwanza; nao wale watakaoitunza hali yao ya pili watapata kuongezewa utukufu juu ya vichwa vyao kwa milele na milele.

27 Na Bwana akasema: Nimtume nani? Na mmoja aliyekuwa mfano wa Mwana wa Mtu akajibu: Niko hapa, nitume mimi. Na mwingine akajibu na kusema: Niko hapa, nitume mimi, Naye Bwana akasema: Nitamtuma wa kwanza.

28 Na wa pili akakasirika, na hakuitunza hali yake ya kwanza; na, katika siku ile, wengi wakamfuata.