2010–2019
Na Mtoto Mdogo Atawaongoza
Aprili 2012


Na Mtoto Mdogo Atawaongoza

Waume na wake wanapaswa kuelewa kwamba mwito wao wa kwanza—kwao ambao kamwe hawatawahi kuachiliwa—ni kwa mmoja na mwingine.

Miaka iliyopita, katika usiku wenye baridi kwenye stesheni mwa gari moshi huko Japani, nilisikia mbisho kwenye dirisha la behewa langu la kulala. Palisimama kijana aliyekuwa na baridi aliyevalia shati kuukuu na tambara chafu lililofungwa kwenye taya liliovimba. Kichwa chake kilijawa na upele. Alibeba mkebe wenye kutu na kijiko, ishara ya mtoto yatima mwombaji. Nilipong’ang’ana kufungua mlango ili kumpatia pesa, gari moshi likaondoka.

Sitawahi kusahau kijana huyo mdogo mwenye njaa aliyeachwa akisimama kwenye baridi, akibeba juu mkebe mtupu. Wala siwezi kusahau jinsi nilivyohisi mdhaifu wakati gari moshi lilipoondoka pole pole na kumwacha akisimama ulingoni.

Miaka kadha baadaye huko Cusco, mji uliojuu katika Andes ya Peru, Mzee A.  Theodore Tuttle pamoja nami tulifanya ibada ya sakramenti katika chumba kirefu na chembamba kilichotazama barabara. Kulikuwa usiku, wakati Mzee Tuttle alipokuwa anaongea, kijana mdogo, pengine miaka sita, alitokea mlangoni. Alivalia tu shati kuukuu iliyomfikia magotini.

Upande wetu wa kushoto kulikuwa meza ndogo na sahani ya mkate wa sakramenti. Huyo yatima wa mtaani mwenye njaa aliona mkate na kusogea pole pole kandoni mwa ukuta kuufikia. Alikuwa karibu na meza wakati mwanamke mmoja njiani mwa kanisa alipomwona. Kwa kutupa kichwa chake kwa ishara, kufukuza kwenye giza. Nililia ndani yangu.

Baadaye huyu kijana mdogo akarudi. Alisogea kwenye ukuta, akitupa jicho toka kwenye mkate hadi kwangu. Alipokuwa karibu na mahali ambako angeonekana na yule mama tena, nilinyorosha mikono yangu, na akaja akinikimbilia. Nilimbeba pajani mwangu.

Kisha, kama jambo la ishara, nilimwekelea kwenye kiti cha Mzee Tuttle. Baada ya maombi ya kufunga, kijana mdogo mwenye njaa akakimbia nje kwenye giza.

Niliporudi nyumbani, nilimwambia Rais Spencer W. Kimball juu ya tukio langu. Aliguswa sana na kuniambia, “Ulikuwa unabeba taifa pajani mwako.” Aliniambia zaidi ya mara moja, “Tukio hilo lina umuhimu mkuu zaidi kuliko unavyojua.”

Kama nilivyotembelea nchi za Amerika ya Latin karibu mara100, nimetafuta kijana huyo mdogo nyusoni mwa watu. Sasa najua kile Rais Kimball alichomaanisha.

Nilikutana na kijana mwengine akitetemeka kwenye barabara za Mji wa Salt. Ilikuwa ni usiku mwingine wa msimu wa baridi. Tulikuwa tukitoka makuli ya jioni ya Krismasi kwenye hoteli. Nyuma mtaani kukaja vijana sita au wanane wenye makelele. Hao wote wangepaswa kuwa nyumbani mbali na baridi.

Kijana mmoja hakuwa na koti. Alirukaruka kila mara ili kuondoa baridi. Alipotelea chini mtaani, bila shaka kwenye nyumba nzee, ndogo na kwenye kitanda kisichokuwa na matandiko yakutosha kumweka joto.

Wakati wa usiku, ninapojifunika, nikatoa maombi kwa wasiokuwa na kitanda chenye joto ya kulalia.

Kituo changu kilikuwa katika Osaka, Japani, wakati Vita vya Dunia vya II vilipokamilika. Mji ulijawa na vifusi, na barabara zimetapakaa mawe, takataka, na mashimo za bomu. Ingawa miti mingi ilikuwa imelipuliwa mbali, mingine michache ilisimama ikiwa na matawi na mashina yaliyoraruliwa na kwa ujasiri wa kutoa vijitawi vichache na majani.

Msichana mdogo akivalia kimono kizee kilichochakaa, chenye rangi alikuwa akikusanya majani ya jano ya mkuyu kuunda shada la maua. Mtoto mdogo alionekana kutojua kuhusu maangamizi yaliomzunguka alipokuwa akipekua vifusi ili kuongeza matawi mengine kwenye shada lake. Alikuwa amepata kitu kimoja kizuri kilichobakia katika ulimwengu wake. Pengine inapaswa niseme alikuwa ndiye kitu kizuri cha ulimwengu wake. Vinginevyo kufikiria juu yake kunaongeza imani yangu. Kilichokua hai ndani mtoto huyu ilikuwa ni matumaini.

Mormoni alifundisha kwamba “watoto wachanga ni wazima katika Kristo”1 na hawahitaji kutubu.

Karibu mwisho wa karne iliyopita, wamisionari wawili walikuwa wakihudumu katika milima ya Marekani kusini. Siku moja, kutoka juu ya kilima waliona watu wakikusanyika kwa umbali chini. Kila mara wamisionari hawakuwa na watu wengi wa kuhubiria, kwa hivyo waliteremka chini.

Kijana mdogo alikuwa amezama majini, na kulikuwa na matanga. Wazazi wake walikuwa wameita mchungaji “kusema maneno” juu ya mwana wao. Wamisionari walisimama mbali wakati mchungaji mtembeleaji alipowaangalia baba na mama waliohuzunika na kuanza mahubiri yake. Ikiwa wazazi walitarajia kupokea ufariji kutoka kwa mtu huyu wa joho, basi walivunjika moyo.

Aliwakashifu sana kwa kutomwezesha kijana mdogo kubatizwa. Walikuwa wamehairisha kwa sababu moja au nyingine, na sasa ilikuwa imechelewa sana. Aliwaambia wazi kwamba kijana wao mdogo alienda jehanamu. Ilikuwa ni kosa lao. Ilikuwa ni wao wakulaumiwa kwa mateso yake ya milele.

Baada ya mahubiri kumalizika na kaburi kufungwa, wamisionari walikutana na wazazi waliohuzunika. “Sisi ni watumishi wa Bwana,” walimwambia mama, “na tumekuja na ujumbe kwako.” Wakati wazazi wenye huzuni wakisikiliza, wamisionari wawili walisoma kutoka kwa ufunuo na kutoa ushuhuda wao wa urejesho wa funguo za ukombozi wa walio hai na wafu.

Namhurumia mhubiri huyo. Alikuwa akifanya vyema awezavyo kwa nuru na ujuzi kama alivyonao. Lakini kuna mengi ambayo angeweza kupeana. Kuna ujalivu wa injili.

Wazee walikuja kama wafariji, kama waalimu, kama watumishi wa Bwana, kama wachungaji halali wa injili ya Yesu Kristo.

Watoto hawa ninaoongea juu yao wanawakilisha watoto wa Baba yetu wa Mbinguni. “Wana ndio urithi wa Bwana: na … heri mtu yule aliyelijaza pondo lake.”2

Uumbaji wa maisha ni jukumu kubwa kwa wenzi waliooana. Ni changamoto ya maisha ya duniani kuwa mzazi mstahiki na mwajibikaji. Sio mwanamume wala mwanamke anayeweza kuzaa mtoto peke yake. Ilikusudiwa kwamba watoto wawe na wazazi wawili—wote baba na mama. Hakuna taratibu ama njia nyingine inayoweza kubadili haya.

Zamani zilizopita mwanamke mmoja aliniambia kwa machozi kwamba kama mwanafunzi wa chuo alifanya kosa baya pamoja na mpenziwe wa kiume. Alikuwa amepanga kutoa mimba. Baada ya muda walihitimu masomo kisha wakaona na walipata watoto kadha. Aliniambia jinsi alivyofedheheka sasa kwa kuiangalia familia yake, watoto wake warembo, na kuona akilini mwake pengo ambako mtoto huyo mmoja alikuwa anakosekana.

Ikiwa wachumba hawa wanaelewa na kutumia Upatanisho, watajua kwamba mazoea hayo na uchungu wanaohusishwa nayo unaweza kufutwa. Hakuna uchungu unaweza kudumu milele. Sio rahisi, lakini maisha hayakunuiwa kuwa rahisi wala wastani. Toba na matumaini ya kudumu ambayo huletwa na msamaha yatakuwa yanastahili hizo juhudi daima.

Wachumba wengine waliniambia kwa majonzi kwamba walikuwa wametoka kwa daktari ambako waliambiwa kwamba hawataweza kupata watoto wao binafsi. Walivunjwa moyo na habari hizo. Walishangaa nilipowaambia kwamba walikuwa na bahati sana. Walishangaa ni kwa nini ningesema jambo kama hilo. Niliwaambia kwamba hali yao ilikuwa bora zaidi kuliko ya wale wachumba wengine ambao walikuwa na uwezo wakuwa wazazi bali walipuuza na kuepukana na majukumu kwa uchoyo.

Niliwambia wao, “Angalau ninyi mnataka watoto, na hio hamu itaangusha ratili kwa niaba yenu katika maisha ya ulimwenguni na zaidi kwa sababu itawapatia uthabiti wa kiroho na mhemuko. Hatimaye, ninyi mtafanikiwa sana kwa sababu ninyi mlitaka watoto na hamkuweza kuwapata, ikilinganishwa na wale ambao wangeweza kupata lakini hawakupata.”

Bado wengine wamebakia bila kuoana na hivyo kukosa watoto. Wengine, kwa ajili ya hali zaidi ya uwezo wao, wanalea watoto kama kina mama na baba wasioolewa. Hizi ni hali za muda mfupi. Katika mpango wa milele wa vitu—sio kila mara katika maisha—upendeleo wa haki na matumaini yatimizwa.

“Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote.” 3

Dhamira muhimu ya shughuli zote Kanisani ni kuona mume na mkewe na watoto wakiwa na furaha nyumbani, wakilindwa na kanuni na amri za injili, kufunganishwa kwa usalama katika maagano ya ukuhani wa milele. Waume na wake wanapaswa kuelewa kwamba mwito wao wa kwanza—kwao ambao hawatawahi kuachiliwa—ni kwa mmoja na mwingine halafu kwa watoto wao..

Mojawapo wa ugunduzi mkubwa wa uzazi ni kwamba tunajifunza mengi zaidi kuhusu kilicho muhimu zaidi kutoka kwa watoto wetu kuliko tunavyojifunza kutoka kwa wazazi wetu. Tunapata kujua ukweli katika unabii wa Isaya kwamba “na mtoto mdogo atawaongoza.” 4

Katika Yerusalemu, “Yesu aliita mtoto mmoja na akamweka katikati yao,

“Akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

“Basi ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.”5

“Yesu akasema, waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao.

“Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko.” 6

Tunasoma katika Kitabu cha Mormoni juu ya matembezi ya Yesu Kristo kwa ulimwengu mpya. Aliwaponya na kuwabariki watu na kuamuru kwamba watoto wachanga waletwe kwake.

Mormoni ameandika, “Walileta watoto wao wachanga na kuwapanga chini juu ya ardhi kumzunguka na Yesu kusimama katikati; na umati ulitoa nafasi mpaka wote walipoletwa kwake.” 7

Kisha aliamuru umati kwamba hupige magoti chini. Akizungukwa na watoto, Mwokozi alipiga magoti ardhini na kutoa maombi kwa Baba yetu wa Mbinguni. Baada ya kuomba Mwokozi alilia, “na akachukua watoto wao wachanga, mmoja mmoja, na kuwabariki, na kuomba kwa Baba juu yao.

“Na baada ya kufanya hivi alilia tena.”8

Naweza kuelewa hisia zilizodhihirishwa na Mwokozi kwa watoto. Kuna mengi ya kujifunza kwa kufuata mfano Wake katika kutaka kuomba kwa, kubariki, na kufundisha “wao wachanga.” 9

Nilikuwa nambari 10 katika familia ya watoto 11, ninavyojua kufikia sasa. Sio baba yangu wala mama yangu alihudumu katika mwito mkubwa Kanisani.

Wazazi wetu walihudumu kwa haki katika mwito wao muhimu zaidi kama---wazazi. Baba yetu aliongoza nyumba yetu katika haki, bila hasira ama uwoga. Na mfano wa ajabu wa baba yangu uliboreshwa kwa ushauri mwema wa mama yetu. Injili ni mwongozo wa ajabu katika maisha ya kila mmoja wetu katika familia ya Packer na katika kizazi kijacho na kijacho na kijacho, kama vile tulivyoona.

Natumaini kuhukumiwa kama mtu mwema kama vile baba yangu. Kabla ya kusikia maneno hayo “vyema sana” kutoka kwa Baba yangu wa Mbinguni, natumaini kuyasikia kutoka kwa baba yangu wa duniani.

Mara nyingi nimekanganyika kwa sababu gani napaswa kuitwa kama Mtume na kisha kama Rais wa Jamii ya Wale Mitume Kumi na Wawili kuzingatia kwamba natoka katika familia ambako baba anaweza kujulikana kama asiyeshiriki kikamilifu. Mimi siye tu mshiriki pekee wa Wale Kumi na Wawili anayestahili cheo hiki.

Hatimaye, naweza kuona na kuelewa kwamba inaweza kuwa ni kwa sababu ya hali hiyo kwamba niliitwa. Pia naweza kuelewa kwa sababu gani kwa yote tunayofanya Kanisani tunapaswa kuonyesha njia kama viongozi kwa wazazi na watoto ili kupata fursa pamoja kama familia. Viongozi wa Ukuhani lazima wawe makini kwa kufanya familia ya Kanisa kuwa na upendo.

Kuna mambo mengi kuhusu kuishi injili ya Yesu Kristo ambayo hayawezi kupimwa na kile kinacho hesabiwa au kuandikwa katika rekodi ya mahudhurio. Tunajishughulisha na majengo na bajeti na mipangilio na utaratibu. Katika kufanya hivyo, ni rahisi kutotambua dhamira halisi ya injili ya Yesu Kristo.

Kila mara mtu huja kwangu nakusema, “Rais Packer, si ingekuwa vyema kama  … ?”

Kila mara mimi huwakomesha na kusema, “La,” kwa sababu nashuku kwamba kitakachofuatia itakuwa shughuli geni au mpangilio utakaoongezea gharama ya muda na uwezo wa kifedha kwa familia yangu.

Muda wa familia ni mtakatifu na unapaswa kulindwa na kuheshimiwa. Tunahimiza washiriki wetu kuonyesha kujitolea kwao kwa familia zao.

Tulipooana mwanzoni, mke wangu pamoja nami tuliamua kwamba tutakubali watoto watakaozaliwa kwetu kwa jukumu la kusimamia kuzaliwa kwao na ukuaji wao. Kwa muda ufaao, wametengeza familia zao wenyewe.

Mara mbili katika ndoa yetu, wakati wakuzaliwa kwa wawili wa wavulana wetu, tumesikia daktari akisema, “Si dhani kama mtalea huyu.”

Nyakati zote, swala hili limeleta majibu kutoka kwetu kwamba tunapeana uhai wetu wote ikiwa mwana wetu mdogo angeweza kuhifadhi uhai wake. Katika kujitolea huku, tulifahamu kwamba kujitolea kule kunafanana na fikira alizonazo Baba wa Mbinguni kwa kila mmoja wetu. Ni fikira aina gani ya kiungu.

Sasa katika upeo wa maisha yetu, Dada Packer pamoja nami tunaelewa na tunao ushahidi kwamba familia zinaweza kuwa pamoja milele. Tunapotii sheria na kuishi injili kikamilifu, tutalindwa na kubarikiwa. Pamoja na watoto wetu na wajukuu wetu na sasa vitukuu vyetu, maombi yetu ni kwamba kila moja ya familia yetu inayokua itakuwa ya kijitolea vivyo hivyo kwa watoto hao wachanga.

Kina baba na mama, mara nyingine mkibeba mtoto mchanga mikononi mwenu, mnaweza kuwa na maono ya kindani ya siri na dhamira ya maisha. Mtaweza kuelewa vyema kwa nini Kanisa liko vile lilivyo na kwa nini familia ni kitengo cha msingi kwa wakati na milele yote. Nashuhudia kwamba injili ya Yesu Kristo ni ya kweli, kwamba mpango wa ukombozi, ambao unaitwa mpango wa furaha, ni mpango wa familia. Naomba Bwana kwamba familia za Kanisa zitabarikiwa, wazazi na watoto, kwamba hii kazi itasonga mbele vile Baba anavyodhamiria. Natoa ushuhuda huu katika Jina la Yesu Kristo, amina.