2010–2019
Nguvu za Mbinguni
Aprili 2012


Nguvu za mbinguni,

Wenye ukuhani vijana na wakongwe wote wanahitaji mamlaka na uwezo---ruhusa inayohitajika na nguvu za kiroho za kumwakilisha Mungu katika kazi ya wokovu.

Ndugu zangu wapendwa, ninashukuru kuwa tunaweza kuabudu pamoja kama kikundi kikubwa cha wenye ukuhani. Ninawapenda na kuvutiwa nanyi kwa ajili ya ustahili wenu na athari yenu ya wema duniani kote.

Ninaalika kila mmoja wenu kufikiria jinsi ungejibu swali lifuatalo lililoulizwa washiriki wa Kanisa miaka mingi iliyopita na Rais David O. McKay: “Ikiwa kwa wakati huu kila mmoja wenu angeulizwa kueleza katika sentensi au kishazi sifa inayotofautisha zaidi Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, jibu lako lingekuwa lipi?” (“The Mission of the Church and Its Members,” Improvement Era, Nov. 1956, 781).

Jibu ambalo Rais McKay alilipa swali lake mwenyewe lilikuwa “mamlaka ya kiungu ya ukuhani.” Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linasimama tofauti na makanisa mengine yanayodai kuwa mamlaka yao yanatokana na urithi wa kihistoria, maandiko au mafunzo ya kidini. Tunatoa tangazo lililo tofauti kwamba mamlaka ya ukuhani yametolewa kwa kuwekelea mikono moja kwa moja kutoka kwa wajumbe wa mbinguni hadi kwake Nabii Joseph Smith.

Ujumbe wangu unaangazia huu ukuhani wa uungu na nguvu za mbinguni. Ninaomba kwa dhati usaidizi wa Roho wa Bwana tunapojifunza pamoja kuhusu kweli hizi muhimu.

Mamlaka na Nguvu za Ukuhani

Ukuhani ni mamlaka ya Mungu yaliyojukumishwa kwa watu duniani kutenda mambo yote kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. (ona Spencer W. Kimball, “The Example of Abraham,” Ensign, June 1975, 3). Ukuhani ni njia ambayo kwayo Bwana hutenda kupitia kwa watu kuokoa roho. Mojawapo ya sifa fafanuzi ya Kanisa la Yesu Kristo nyakati za kale na sasa ni mamlaka yake. Hapawezi kuwa na Kanisa la kweli bila mamlaka ya kiungu.

Watu wa kawaida hupatiwa mamlaka ya ukuhani. Ustahili na hiari – si tajiriba wala ujuzi wala elimu- ndizo sifa zinazohitajika kwa kutawazwa kwa ukuhani.

Mpangilio wa kupata mamlaka ya ukuhani unaelezwa katika makala ya tano ya imani: Tunaamini kwamba mwanadamu ni lazima aitwe na Mungu, kwa unabii, na kwa kuwekelewa mikono na wale walio katika mamlaka, ili kuhubiri Injili na kuhudumu katika ibada zake. Hivyo basi mvulana au mtu hupokea mamlaka ya ukuhani na kutawazwa kwa ofisi maalum na mmoja aliye na ukuhani na ameidhinishwa na kiongozi mwenye funguo za ukuhani zinazohitajika.

Mwenye ukuhani anatarajiwa kutumia haya mamlaka matakatifu kulingana na akili, hiari na madhumuni ya Mungu. Hapana chochote katika ukuhani kilicho na ubinafsi. Ukuhani kila mara hutumika kuhudumu, kubariki, na kuimarisha watu wengine.

Ukuhani wa juu hupokelewa kwa agano kunjufu ambalo linahusisha jukumu la kutenda katika mamlaka (ona M&M 68:8) na ofisi (ona M&M 107:99) ambazo zimepokelewa. Kama wenye mamlaka matakatifu ya Mungu, sisi ni maajenti wa kutenda na wala si vifaa vya kutendewa (ona 2 Nefi 2:26). Ukuhani kwa asili ni amilifu wala si wa kutofanya kazi.

Rais Ezra Taft Benson alifundisha:

“Haitoshi tu kupokea ukuhani na kukaa tu bila kufanya chochote na kungoja hadi mtu atushawishi kutenda. Tunapopokea ukuhani, tuna jukumu la kuwa watendaji na kujihusisha kikamilifu katika kuendeleza kiini cha haki ulimwenguni kwa sababu Bwana anasema:

‘Yule asiyefanya lolote mpaka ameamriwa, na kupokea amri kwa moyo wenye mashaka, na kuzishika kwa ulegevu, huyo amelaaniwa. [M&M 58:29]” (So Shall Ye Reap [1960], 21).

Rais Spencer{nbW. Kimball pia alitilia mkazo kwa kusema hasili tendaji ya ukuhani. Mtu huvunja agano la ukuhani anapovunja amri za Mungu. Pia, kuvunja agano hili, mtu anahitaji tu kutofanya chochote” (The Miracle of Forgiveness [1969], 96).

Tunapofanya tuwezavyo kutimiza majukumu yetu ya ukuhani tunaweza kubarikiwa na nguvu za ukuhani. Nguvu za ukuhani ni nguvu za Mungu zinazofanya kazi kupitia kwa wanaume na wavulana kama sisi na huhitaji utakatifu, uaminifu, bidii ya kibinafsi. Mvulana au mwanamume anaweza kupokea mamlaka ya ukuhani kwa kuwekelewa mikono lakini hatakuwa na nguvu za ukuhani ikiwa atakuwa mtovu wa utii, asiyestahili au asiye na hiari ya kuhudumu.

“Haki za ukuhani zimeungana na hazitenganishwi na nguvu za mbinguni, na ... nguvu za mbinguni haziwezi kudhibitiwa wala kutawaliwa isipokuwa tu kwa kanuni za haki.

“Kwamba zinaweza kutunukiwa juu yetu; lakini tutakapojaribu kuficha dhambi zetu, au kuridhisha kiburi chetu, tamaa yetu ya makuu, au kutumia katika udhibiti au utawala au ulazimishaji juu ya nafsi za wanadamu, katika kiwango chochote kisicho cha haki, tazama, mbingu hujitoa zenyewe; Roho wa Bwana husikitika; na mara akijitoa, Amina kwa ukuhani au mamlaka ya mtu yule” (M&M 121:36–37; mkazo umeongezewa).

Ndugu, kwa mvulana au mwanamume kupokea mamlaka ya ukuhani na kupuuza kufanya kinachihitajika ili kutimu kwa nguvu za ukuhani haikubaliki kwa Bwana. Wenye ukuhani wadogo na wakongwe wote wanahitaji mamlaka na nguvu--- ruhusa inayohitajika na uwezo wa kumwakilisha Mungu katika kazi ya wokovu.

Funzo kutoka kwa Baba Yangu

Nililelewa katika boma lililokuwa na mama mwaminifu na baba wa ajabu. Mama yangu alitoka katika ukoo wa watangulizi waliojitolea kila kitu kwa Kanisa na ufalme wa Mungu. Baba yangu hakuwa mshiriki wa kanisa letu na kama kijana alikuwa na hamu ya kuwa kasisi wa Kikatoliki. Hatimaye, alichagua kutohudhuria seminari ya mafunzo ya dini na badala yake akafuatilia kazi ya kuunda vifaa na chapa ya chuma.

Katika wakati mwingi wa ndoa yake, baba yangu alihudhuria mikutano ya Kanisa la Yesu Kristo la Wataatifu wa Siku za Mwisho na familia yetu yote. Kwa hakika, watu wengi wa tawi letu hawakuwa na habari kuwa hakuwa mshiriki wa Kanisa. Alicheza na kufunza timu ya mpira ya tawi letu, akasaidia na shughuli za uskauti, na kumsaidia mamangu katika aina tofauti za miito na majukumu. Nataka kuwaambia kuhusu mojawapo ya mafunzo niliyojifunza kutoka kwa baba yangu kuhusu mamlaka na nguvu za ukuhani.

Nikiwa mvulana nilimwuliza baba yangu mara nyingi kila wiki ni lini atabatizwa. Alijibu kwa upendo lakini kwa ithibati kila mara nilipomkera: “David, mimi sitajiunga na Kanisa kwa ajili ya mama yako, wewe, au mtu yeyote yule. Nitajiunga na Kanisa nikijua kuwa ni kitu kinachofaa kufanya.”

Ninaamini kuwa nilikuwa katika miaka ya mapema ya ujana wangu wakati mazungumzo yafuatayo yaliendelea kati yangu na baba yangu. Tulikuwa tumerudi nyumbani kutoka katika kuhudhuria mikutano yetu ya Jumapili pamoja, na nilimwuliza baba lini atabatizwa. Alitabasamu na kusema, “ Wewe ndiwe wa kuniuliza kuhusu kubatizwa. Hivi leo nina swali kwako.” Mara moja na mhemko niliona kuwa tulikuwa tunafanya maendeleo!

Baba yangu aliendelea, “David, kanisa lako linafundisha kuwa ukuhani ulichukuliwa kutoka duniani hapo zamani na umerejeshwa na wajumbe kutoka mbinguni kwa Nabii Joesph Smith, au siyo?” Nilijibu kuwa tamshi lake lilikuwa sahihi. Kisha akasema, “Swali langu ni hili. Kila wiki katika mkutano wa ukuhani ninamsikiliza askofu na wale viongozi wengine wa ukuhani wakikumbusha, kuomba na kusihi wanaume kufanya ufundishaji wa nyumbani na kutimiza majukumu yao ya kikuhani. Ikiwa kanisa lenu kwa kweli lina ukuhani uliorejeshwa wa Mungu, kwa nini kuna wanaume wengi sana kanisani mwenu wasio tofauti katika kufanya majukumu yao ya kidini na watu wa kanisa langu?” Akili yangu changa mara moja ikawa tupu. Sikuwa na jibu kwa babangu.

Ninaamini babangu alikosea kuhukumu uhalisi wa madai ya Kanisa letu kuhusu mamlaka ya kiungu kwa makosa ya watu ambaye alikutana na nao katika tawi letu. Lakini lililojikita katika swali lake kwangu ilikuwa ni dhana sahihi kuwa watu walio na ukuhani mtakatifu wa Mungu ni sharti wawe tofauti na watu wengine.Watu walio na ukuhani si bora kimaumbile kuliko wengine, lakini wanapaswa kutenda tofauti. Wanaume wanaoshikilia ukuhani wanapaswa kupokea siyo tu mamlaka ya ukuhani bali pia kuwa wa kustahili na mapitio waaminifu wa nguvu ya Mungu. “Kuweni safi ninyi mnaochukua vyombo vya Bwana” (M&M 38:42).

Sijasahau kamwe mafunzo kuhusu mamlaka na nguvu ya ukuhani niliyojifunza kutoka kwa baba yangu, mtu mwema asiye wa imani yetu, ambaye alitarajia zaidi kutoka kwa wale waliodai kuwa na ukuhani wa Mungu. Mazungumzo ya Jumapili hiyo alasiri na baba yangu miaka mingi iliyopita yalizaa ndani yangu hamu ya kuwa “mvulana mwema” Sikutaka kuwa mfano mbaya wala kikwazo kwa maendeleo ya baba yangu kujifunza kuhusu injili iliyorejeshwa. Nilitaka tu kuwa mvulana mwema. Bwana anatuhitaji sote kama wenye mamlaka yake kuwa waheshimiwa, waadilifu na wavulana wema nyakati zote mahali popote.

Unaweza kuwa na haja ya kujua kuwa baada ya miaka kadhaa, baba yangu alibatizwa. Na katika nyakati zilizofaa, nilikuwa na nafasi ya kumtunukia ukuhani wa Aaroni na Melkizediki Mojawapo ya matukio makuu ni kumtazama baba yangu akipokea mamlaka na hatimaye, nguvu za ukuhani.

Ninashiriki nanyi funzo hili dhahiri kutoka kwa baba yangu ili kutia mkazo ukweli rahisi. Kupokea mamlaka ya ukuhani kwa kuwekelewa mikono ni mwanzo muhimu lakini hautoshi. Kuwekelewa mikono kunapeana mamlaka, lakini utakatifu unahitajika ili kutumia nguvu tunapojaribu kuinua mioyo, kufundisha na kushuhudia, kubariki na kushauri, na kuendeleza kazi ya wokovu.

Katika msimu huu wa ajabu katika historia ya ulimwengu, wewe na mimi kama wenye ukuhani wa Mungu tunahitaji kuwa watu wenye haki na vyombo vifaavyo katika mikono ya Mungu. Tunahitaji kuinuka kama watu wa Mungu. Wewe na mimi tutafanya vyema kujifunza kutoka kwa na kuzingatia mfano wa Nefi, mjukuu wa Helamani na wa kwanza wa mitume kumi na wawili walioitwa na Mwokozi katika mwanzo wa huduma yake kati ya Wanefi. “Na [Nefi] aliwafundisha vitu vingi; ... Na Nefi alifundisha kwa uwezo na mamlaka.” (3 Nefi 7:17).

Tafadhali Msaidie Mme Wangu Kuelewa

Katika hitimisho la mahojiano ya sifu ya hekalu niliyofanya kama askofu na rais wa kigingi, mara nyingi niliwauliza akina dada walioolewa jinsi ningewahudumia vyema zaidi na familia zao. Usawa wa majibu niliyopokea kutoka kwa akina dada hawa waaminifu ulikuwa wa kufundisha na kuhofisha. Akina dada hawa ilikuwa nadra wao kulalamika au kukosoa, lakini walijibu hivi. “tafadhali msaidie mme wangu kuelewa jukumu lake kama kiongozi wa ukuhani nyumbani mwetu. Ninafurahia kuchukua uongozi katika kujifunza maandiko, maombi ya familia na mkutano wa jioni wa familia nyumbani, na nitaendelea kufanya hivyo. Lakini ninatamani mme wangu angekuwa mwenzi sawa na kutoa uongozi thabiti wa ukuhani alionao. Tafadhali msaidie mme wangu kujifunza jinsi ya kuwa baba mkuu na kiongozi wa kikuhani nyumbani mwetu anayesimamia na kutunza.”

Mara nyingi ninafikiria uaminifu wa kina dada hao na ombi lao. Viongozi wa kikuhani husikia hofu kama hizi hivi leo. Wake wangi wanaomba waume wao ambao hawana tu mamlaka ya ukuhani bali pia nguvu za ukuhani. Wanatamani kufungiwa nira na mme mwaminifu na mwenza wa kikuhani katika kazi ya kuunda familia iliyo na kitovu cha Kristo na nyumbani iliyolenga injili.

Kina ndugu, nawaahidi kuwa ikiwa ninyi nami tutatafakari kwa maombi maulizo ya kina dada hao, Roho Mtakatifu atatusaidia kujiona jinsi tulivyo kweli (Ona M&M 93:24), na kutusaidia kutambua yale tunayohitaji ili kubadilika na kuwa bora. Na wakati wa kutenda ni sasa!

Kuwa Mifano ya Haki

Usiku wa leo ninahimiza mafundisho ya Rais Thomas S. Monson ambaye ametualika sisi kama wenye ukuhani kuwa “mifano ya utakatifu.” Ametukumbusha mara nyingi kuwa tumo katika utumishi wa Bwana na tuna haki ya usaidizi wake juu ya ustahili wetu. (Ona “Examples of Righteousness,” Liahona and Ensign, May 2008, 65–68. Wewe na mimi tuna ukuhani ambao umerudishwa ulimwenguni katika Maongozi haya ya Mungu na wajumbe wa mbinguni, hata Petro Yakobo na Yohana. Na hivyo basi, kila mtu anayepokea ukuhani wa Melkizediki anaweza kufuatilia mstari wake binafsi wa ukuhani moja kwa moja kwa Bwana Yesu Kristo. Ninatumaini kwamba tuna shukrani kwa Baraka hii ya ajabu. Ninaomba tutakuwa wasafi na kustahili kumwakilisha Bwaba tunapotumia mamlaka yake matakatifu. Na kila mmoja wetu apate kufuzu kwa nguvu za ukuhani.

Nashuhudia kuwa ukuhani mtakatatifu kwa kweli umerejeshwa duniani katika siku hizi za mwisho na unapatikana katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ninashuhudia kuwa Rais Thomas S. Monson ni kuhani mkuu msimamizi wa ukuhani mkuu wa Kanisa (Ona M&M 107:9, 22, 65–66, 91–92) na mtu wa pekee duniani ambaye anashikilia na ameidhinishwa kutumia funguo zote za ukuhani. Juu ya mambo haya nashuhudia kwa dhati katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.