Uwezo wa Ukombozi
Tunaweza kukombolewa kutokana na njia za uovu na dhambi kwa kugeukia mafundisho ya maandiko matakatifu.
Ninaye rafiki mwema sana ambaye hunitumia tai nzuri ya kuvalia wakati wangu wa kunena katika kila mkutano mkuu. Hana chaguo bora, mnaonaje?
Huyu rafiki yangu kijana ana changamoto ngumu kadhaa. Zinamzuia kwa njia zingine, lakini katika njia zingine yeye ni mtu wa ajabu. Kwa mfano, ushupavu wake kama mmisionari unaweza kulinganishwa na wana wa Mosia. Uhalisi wa imani yake huifanya hii amini kuwa thabiti zaidi na imara. Naamini kwamba katika akili ya Scott haikubaliki kwamba kila mtu si mshiriki wa Kanisa La Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na kwamba si kila mtu hajakisoma Kitabu cha Mormoni na hajapokea ushuhuda wa ukweli wake.
Acha niwaambie kuhusu tukio katika maisha ya Scott, wakati wa mara yake ya kwanza kupanda ndege peke yake ili kumtembelea nduguye. Jirani aliyeketi karibu alisikia mazungumzo kati ya Scott na mtu kandoni mwake:
“Habari, jina yangu ni Scott. Na lako je?”
Yule mwenzake alimwambia jina lake..
“Unafanya kazi gani?”
“Mimi ni mhandisi.”
“Hivyo ni vizuri. Unaishi wapi?”
“Katika Las Vegas.”
“Tuna hekalu huko. Unajua mahali hekalu la Mormoni lipo?”
“Ndio. Ni jengo nzuri sana.”
“Wewe ni Mmormoni?”
“La.”
“Vema, unapaswa kuwa. Ni dhehebu la ajabu. Umewahi kusoma Kitabu cha Mormoni?”
“La.”
“Vema, unapaswa kukisoma . Ni kitabu cha ajabu.”
Nakubaliana kabisa na Scott—Kitabu cha Mormoni ni kitabu ajabu. Maneno ya Nabii Joseph Smith yaliyonukuliwa kwenye ukurasa wa utangulizi wa Kitabu cha Mormoni yamekuwa yenye maana kwangu: “Niliwaambia ndugu kwamba Kitabu cha Mormoni ndicho kitabu sahihi duniani, na ndicho jiwe la katikati la teo la dini yetu, na kuwa mwanadamu angemkaribia Mungu zaidi kwa kufuata mafunzo yake, zaidi ya kitabu kingine.”
Mwaka huu katika madarasa yetu ya Shule ya Jumapili tunajifunza kuhusu Kitabu cha Mormoni. Tunapojitayarisha kushiriki, acha tuweze kuhamasika ili kufuata mfano mwema wa Scott wa kushiriki upendo wetu wa maandiko haya maalum na wengine wasiokuwa wa imani yetu.
Dhamira kuu ya Kitabu cha Mormoni imeelezwa katika fungu la mwisho la mlango wa kwanza wa 1 Nefi. Nefi anaandika, “Lakini tazama, mimi, Nefi nitawaonyesha nyinyi kuwa Bwana ana huruma nyororo juu ya wale ambao amewachagua, kwa sababu ya imani yao, kuwatia nguvu hata kwenye uwezo wa ukombozi” (1 Nefi 1:20).
Ningependa kuongea jinsi Kitabu cha Mormoni, ambacho ni rehema ya Bwana kilichohifadhiwa kwa siku hizi za mwisho, kinatukomboa kwa kutufundisha mafundisho ya Kristo kwa njia safi na “sahihi kabisa”.
Nyingi kati ya hadithi za Kitabu cha Mormoni ni hadithi za ukombozi. Safari ya Lehi kwenda nyikani pamoja na familia yake ilikuwa inahusu ukombozi kutokana na maagamizi ya Yerusalemu. Hadithi ya Wayaredi ni hadithi ya ukombozi, kama ilivyo hadithi ya watu wa Muleki. Alma Mdogo alikombolewa kutoka kwa dhambi. Vijana mashujaa wa vita wa Helamani walikombolewa vitani. Nefi na Lehi walikombolewa kutoka kwa jela. Dhamira ya ukombozi inapatikana kote katika Kitabu cha Mormoni.
Kuna hadithi mbili katika Kitabu cha Mormoni ambazo zinafanana na zinafundisha somo muhimu sana. Ya kwanza inapatikana katika kitabu cha Mosia, kuanzia mlango wa 20. hapa tunajifunza juu ya Mfalme Limhi akiishi katika nchi ya Nefi. Walamani walipigana vita dhidi ya watu wa Limhi. Matokeo ya vita yalikuwa kwamba Walamani wangeruhusu Mfalme Limhi kutawala watu wake mwenyewe, lakini wangekuwa katika utumwa kwao. Ilikuwa ni maisha yasiokuwa na amani. (Ona Mosia 19–20.)
Wakati watu wa Limhi walipochoshwa na dhuluma za Walamani, walishawishi mfalme wao kwenda vitani dhidi ya Walamani. Mara tatu watu wa Limhi walishindwa. Majukumu mengi yaliwekwa juu yao. Hatimaye wajinyenyekeza na kulia sana kwa Bwana kwamba angewakombowa. (Ona Mosia 21:1–14.) mstari wa 15 katika Mlango wa 21 unatueleza kuhusu majibu ya Bwana: “Na sasa Bwana alikuwa na upole kwa kusikia kilio chao kwa sababu ya maovu yao; haidhuru Bwana alisikia vilio vyao, na akaanza kulainisha mioyo ya Walamani kwamba wakaanza kupunguza mizigo yao; walakini Bwana hakuonelea vyema kuwakomboa kutoka utumwani.”
Mara tu baada ya Ammoni na kikosi kidogo cha wanaume kutoka Zarahemla walipowasili, na pamoja na Gideon—mmoja wa viongozi wa watu wa Limhi—walitengeneza mpango ambao ulifaulu, na wakatoroka kutokana na dhuluma za Walamani. Bwana alikuwa mpole kwa kusikia vilio vyao. Kwa nini? Kwa sababu ya dhambi zao.
Hadithi ya pili inafanana kwa njia nyingi lakini pia tofauti. Hadithi imerekodiwa katika Mosia Mosia 24.
Alma na watu wake walikuwa wameishi katika nchi ya Helamu, wakati ambapo jeshi la Walamani lilipoingia katika mpaka wa nchi. Walikutana na kutengeneza suluhu la amani. (Ona Mosia 23:25–29.) Mara tu viongozi wa Walamani walianza kulazimu matakwa yao juu ya watu wa Alma na kuweka majukumu mazito kwao. (ona Mosia 24:8). Katika kifungu cha 13 tunasoma, “Na ikawa kwamba sauti ya Bwana iliwafikia katika mateso yao, ikisema: Inueni vichwa vyenu na msherehekee, kwani ninajua agano ambalo mlinifanyia; na nitaagana na watu wangu na kuwakombowa kutoka utumwani.”
Watu wa Alma walikombolewa kutoka kwa mikono ya Walamani na kurudi kwa usalama ili kuunganishwa na watu wa Zarahemla.
Ni tofauti gani iliokuwa kati ya watu wa Alma na watu wa Mfalme Limhi? Ama kweli, kulikuwa na tofauti kadha: watu wa Alma walikuwa wenye amani na watakatifu zaidi; walikuwa tayari wamebatizwa na kuweka agano na Bwana; walijinyenyekeza mbele za Bwana hata kabla matatizo zao kuanza. Tofauti hizi zote ziliwawezesha kukombolewa kwa haraka na Bwana kwa njia ya kimiujiza kutokana na mkono uliowaweka katika utumwa. Maandiko haya yanatufundisha juu ya uwezo wa Bwana wa ukombozi.
Unabii unaotabiri maisha na misheni ya Yesu Kristo unatuahidi ukombozi ambao atapeana. Upatanisho wake na Ufufuko unatupatia sote ukombozi kutokana na kifo cha mwili na, ikiwa tutatubu, ukombozi kutokana na kifo cha kiroho, ukija pamoja na baraka za uzima wa milele. Ahadi za Upatanisho na Ufufuko, ahadi za ukombozi kutokana na kifo cha kimwili na kiroho, zilitangazwa na Mungu kwake Musa aliposema, “Kwa maana tazama, hii ndiyo kazi yangu na utukufu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.” (Moses 1:39).
Tofauti na kanuni za ajabu zilizobuniwa kwa ajili yetu katika maandiko matakatifu, tunapata nguvu za upinzani za wapinga dini wanaoshambulia kanuni za kudumu katika maandiko matakatifu—maandiko ambayo yametupatia mwongozo kwa karne hizi zote katika kuelezea maadili ya milele na kanuni za tabia zetu maishani. Wanatangaza kwamba mafundisho katika Biblia kuwa yana upotovu na mafundisho za Bwana kupitwa na wakati. Sauti zao zinadai kwamba kila mtu lazima awe na uhuru wa kuweka kanuni yake mwenyewe; wanajaribu kubadilisha haki za waaminio, tofauti na vile inavyofundishwa katika maandiko na katika maneno ya manabii.
Ni baraka iliyoje kwa maelezo ya misheni ya Bwana wetu na Mwokozi kutangazwa katika Kitabu cha Mormoni ili kuongezea ushahidi wa pili kwa mafundisho yaliyotangazwa katika Biblia. Kwa nini ni muhimu kwa ulimwengu kuwa na Biblia na Kitabu cha Mormoni? Naamini jibu linapatikana katika mlango wa 13 wa 1 Nefi. Nefi anaandika: “Na malaika akanizungumzia, akisema: Haya maandishi ya mwisho, ambayo umeona miongoni mwa Wayunani [Kitabu cha Mormoni], yatadhibitisha juu ya kweli, kwa yale ya kwanza[Biblia], ambayo ni ya wale mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo, na yatafahamisha vitu vilivyo wazi na vyenye thamani vilivyotolewa kutoka kwao; na yatafahamisha makabila yote, lugha zote, na watu wote, kwamba Mwanakondoo wa Mungu ndiye Mwana wa Baba wa Milele, na Mwokozi wa Ulimwengu; na kwamba lazima watu wote wamkubali yeye, kama sivyo, hawezi kuokolewa.” (mstari wa 40).
Sio Biblia wala Kitabu cha Mormoni peke yake kinatosha. Vyote ni muhimu kwetu ili kufundisha na kujifunza juu ya ukamilifu wa mafundisho ya Kristo. Haja ya moja haipunguzi thamani ya nyingine. Vyote Biblia na Kitabu cha Mormoni ni muhimu kwa wokovu wetu na furaha. Kama vile Rais Ezra Taft Benson alivyofunza kwa nguvu: “Vinapotumika pamoja, Biblia na Kitabu cha Mormoni hushinda mafundisho potovu (“A New Witness for Christ,” Christ,” Ensign, Nov. 1984, 8).
Nataka kumalizia kwa kujadili hadithi mbili—moja kutoka kwa Agano la Kale, na nyingine kutoka Kitabu cha Mormoni—ili kuonyesha jinsi vitabu hivi vinavyotumika kwa pamoja.
Hadithi ya Ibrahimu inaanza kwa ukombozi wake kutokana na Wakaldayo waabuduo sanamu (ona Mwanzo 11:27–31; Ibrahimu 2:1–4). Yeye na mkewe, Sarai, baadaye walikombolewa kutokana na huzuni yao na kuahidiwa kwamba kupitia kwa uzao wao mataifa yote ya dunia yatabarikiwa (ona Mwanzo 18:18).
Agano la Kale lina maelezo ya Ibrahimu akimchukua Lutu mwana wa nduguye, pamoja naye kutoka Misri. Katika chaguo la ardhi, Lutu alichagua bonde la Yordani, na kutengeneza hema kuangalia Sodoma, mji wa dhambi nyingi sana. (Ona Mwanzo 13:1–12.) Nyingi za shida ambazo Lutu alipitia baadaye maishani, na zilikuwa nyingi, zinaweza kufuatiliwa nyuma kwa uamuzi wake wa kuweka mlango wa hema yake kutazama Sodoma.
Ibrahimu, baba wa waaminifu, aliishi maisha tofauti. Hakika kulikuwa na changamoto nyingi, lakini ilikuwa ni maisha yenye baraka. Hatujui ni upande gani mlango wa Ibrahimu uliangalia, lakini kuna kidokezo halisi katika kifungu cha mwisho cha mlango wa 13 wa Mwanzo. Kina ripoti, “Basi Abramu [ama Ibrahimu] akajongeza hema yake, akaja akakaa kwenye mialoni ya Mamre, nayo ni miti iliyoko Hebroni,akamjegea Bwana madhabahu huko” (Genesis 13:18).
Ingawa sijui, binafsi naamini mlango wa hema wa Ibrahimu ulitazama madhabahu aliyomjengea Bwana. Nafikiaje uamuzi huu? Ni kwa sababu najua hadithi ya Kitabu cha Mormoni kuhusu maagizo ya Mfalme Benyamini kwa watu wake walipokusanyika ili kusikia hotuba yake ya mwisho. Mfalme Benyamini aliwaagiza kuweka milango ya hema zao zikitazama hekalu (ona Mosia 2:1–6).
Tunaweza kukombolewa kutokana na njia za uovu na dhambi kwa kugeukia mafundisho ya maandiko matakatifu. Mwokozi ndiye Mkombozi Mkuu, kwani hutukomboa kutokana na kifo na kutokana na dhambi. (ona Warumi 11:26; 2 Nefi 9:12).
Natangaza kwamba Yesu ndiye Kristo na tunaweza kusogea karibu Naye kwa kusoma Kitabu cha Mormoni. Kitabu cha Mormoni ni ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo. Shuhuda za kwanza za Mwokozi wetu ni Agano la Kale na Agano Jipya—ama Biblia.
Tena, tuweze kukumbuka maelezo ya rafiki yangu Scott ya Kitabu cha Mormoni: “Ni kitabu cha ajabu.” Na ninawashuhudia kwamba ukuu wa Kitabu cha Mormoni unapatikana kutoka kwa upatanifu wake na Biblia takatifu, katika jina la Yesu Kristo, amina.