Nguzo na Miale
Sisi pia tunaweza kuwa na nguzo yetu wenyewe ya mwanga—mwale mmoja kwa wakati.
Ujumbe wangu ni kwa wale wanaohofia shuhuda zao kwa sababu hawajapata tukio kubwa la kiroho lenye kuwalemea. Ninaomba kwamba niweze kuwapa baadhi ya amani na hakikisho.
Urejesho wa injili ya Yesu Kristo ulianza kwa mlipuko wa nuru na kweli! Mvulana huko kaskazini mwa New York, akiwa na jina la kawaida kabisa la Joseph Smith, aliingia kwenye kisitu cha miti ili kusali. Alikuwa na wasiwasi kuhusu nafsi yake na msimamo wake mbele za Mungu. Anatafuta msamaha kwa ajili ya dhambi zake. Na alikanganyikiwa kuhusu kanisa lipi ajiunge nalo. Anahitaji uwazi na amani—anahitaji nuru na maarifa.
Joseph anapopiga magoti kusali na “kutoa matakwa ya moyo [wake] kwa Mungu,” giza totoro linamfunika. Kitu fulani kiovu, chenye kutaabisha na chenye uhalisia kinajaribu kumzuia—kuufunga ulimi wake ili asiweze kusema chochote. Nguvu za giza zinakuwa kali sana kiasi kwamba Joseph anadhani atakufa. Lakini “anatumia nguvu [zake] zote kumlingana Mungu ili amkomboe [yeye] kutoka kwenye nguvu za adui huyu ambaye alikuwa amemshikilia [yeye].” Na kisha, “muda huo huo ambao [yeye] alikuwa tayari kuzama katika kukata tamaa na kujiachilia [mwenyewe] ili aangamizwe,”wakati hajui kama anaweza kung’ang’ana zaidi, mng’aro mtukufu ulijaa kichakani, ukatawanya giza na yule adui wa nafsi yake.
“Nguzo ya mwanga” iliyong’aa kuliko jua pole pole inashuka juu Yake. Mtu mmoja anatokea, na kisha mwingine. “Mng’aro na utukufu wao wapita maelezo yote.” Wa kwanza, Baba yetu wa Mbinguni, anamwita jina lake, “akionyesha mkono kwa yule mwingine—[Joseph!]. Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!”
Na kwa kujitokeza huko ghafla kwa mwangaza na ukweli, Urejesho ulikuwa umeanza. Mafuriko ya kweli ya ufunuo mtakatifu na baraka vilifuata: maandiko mapya, urejesho wa funguo za ukuhani, mitume na manabii, ibada na maagano na kuanzishwa tena kwa Kanisa la Bwana la kweli na lililo hai, ambalo siku moja litaujaza ulimwengu kwa nuru na ushahidi juu ya Yesu Kristo na injili Yake iliyorejeshwa.
Hayo yote, na mengine mengi zaidi, yalianza kwa sala ya hitaji kuu na nguzo ya mwanga.
Sisi pia tunayo mahitaji yetu wenyewe. Sisi pia tunahitaji uhuru kutokana na mkanganyiko wa kiroho na giza la kiulimwengu. Sisi wenyewe pia tunahitaji kujua. Hiyo ndiyo sababu moja Rais Russell M. Nelson ametualika “kujizamisha [wenyewe] ndani ya nuru tukufu ya Urejesho.”
Mojawapo ya kweli kuu za Urejesho ni kwamba mbingu ziko wazi—kwamba sisi pia tunaweza kupokea nuru na maarifa kutoka juu. Ninashuhudia kwamba hilo ni kweli.
Lakini ni lazima tujihadhari na mtego wa kiroho. Wakati mwingine waumini waaminifu wa Kanisa wanakuwa wamevunjika moyo na hata kwenda bila mwelekeo kwa sababu hawajapata uzoefu mkubwa wa kiroho—kwa sababu hawajapata uzoefu wa nguzo yao wenyewe ya mwanga. Rais Spencer W. Kimball alionya “Siku zote kutegemea jambo la kustaajabisha, wengi watakosa kabisa ule mtirirko thabiti wa mawasiliano yaliyofunuliwa.
Rais Joseph F. Smith vile vile alikumbuka, “Bwana alizuia maajabu kutoka kwangu [nilipokuwa kijana], na kunionyesha ukweli, mstari juu ya mstari, amri juu ya amri, hapa kidogo na pale kidogo.”
Huu ndiyo mpangilio wa kawaida wa Bwana, akina kaka na akina dada. Badala ya kututumia nguzo ya mwanga, Bwana anatutumia mwale wa mwanga, na kisha mwingine, na mwingine.
Miale hiyo ya mwanga inaendelea kumwagwa juu yetu. Maandiko yanafundisha kwamba Yesu Kristo “ni nuru na … uzima wa ulimwengu,” kwamba “Roho Yake hutoa nuru kwa kila mwanaume na [mwanamke] wanaokuja ulimwenguni,” na kwamba nuru Yake “inajaza sehemu kubwa,” ikitoa “uhai kwa vitu vyote.” Nuru ya Kristo kiuhalisia inatuzunguka kote.
Kama tukipokea kipawa cha Roho Mtakatifu na kujitahidi kutumia imani, kutubu, na kuheshimu maagano yetu, ndipo tunakuwa wastahiki kupokea hii miale mitakatifu kila mara. Katika kirai cha kukumbukwa cha David A. Bednar, “tunaishi katika ufunuo.”
Na hali, kila mmoja wetu ni tofauti. Hakuna watu wawili wanaopokea nuru na ukweli wa Mungu katika njia sawa kabisa. Chukua muda kufikiria kuhusu jinsi wewe unavyopata uzoefu wa nuru na Roho wa Bwana.
Yawezekana umekwisha kupata uzoefu wa mfumuko wa nuru ya ushuhuda kama “amani [iliyozungumzwa] akilini mwako kuhusiana na jambo” ambalo limekuwa likikutia wasiwasi.
Au kama msukumo—sauti ndogo, tulivu—ambayo ilitulia “akilini mwako na moyoni mwako” na kukuhimiza ufanye kitu fulani kizuri, kama vile kumsaidia mtu.
Pengine umeshawahi kuwa darasani ndani ya kanisa—au kwenye kambi ya vijana—na kuhisi hamu kubwa ya kumfuata Yesu Kristo na kubaki mwaminifu. Labda wewe hata umeshasimama na kutoa ushuhuda ambao ulitumainia ilikuwa ni kweli na kisha ulihisi ulikuwa ni kweli.
Au Labda umekuwa ukiomba na kuhisi hakikisho la shangwe kwamba Mungu anakupenda.
Unaweza kuwa umemsikia mtu akitoa ushuhuda juu ya Yesu Kristo, na ukagusa moyo wako na kukujaza tumaini.
Pengine ulikuwa unasoma katika Kitabu cha Mormoni na aya ikanena na nafsi yako, kama vile Mungu alikuwa ameiweka kwa ajili yako pekee na kisha ukagundua kwamba kweli Yeye alifanya hivyo.
Unaweza kuwa ulihisi upendo wa Mungu kwa ajili ya wengine wakati ulipowatumikia.
Au pengine ulihangaika katika kumhisi Roho kwa muda kwa sababu ya msongo wa mawazo au wasiwasi lakini ukawa na kipawa cha thamani na imani ya kutazama nyuma na kutambua “rehema nyororo za Bwana.”
Hoja yangu ni kwamba kuna njia nyingi za kupokea miale ya mbinguni ya ushuhuda. Hata hivyo, hizi ni chache tu. Zinaweza kuwa si za ajabu, lakini zote zinajenga sehemu ya shuhuda zetu.
Akina kaka na akina dada, mimi sijaona nguzo ya mwanga, lakini kama wewe nimeshapata uzoefu wa miale mingi mitakatifu. Kwa miaka mingi, nimejaribu kuthamini uzoefu kama huo. Ninaona kwamba ninapofanya hivyo, ninatambua na kukumbuka hata mingine zaidi ya hiyo. Hapa kuna baadhi ya mifano kutoka kwenye maisha yangu mwenyewe. Yawezekana isiwe ya kuvutia sana kwa baadhi ya watu, lakini ni ya thamani kwangu mimi.
Nakumbuka kuwa kijana mtundu kwenye ubatizo. Mkutano huo ulipokuwa karibu kuanza, nilihisi Roho akinisihi niketi chini na niwe mwenye staha. Niliketi chini na nikabaki mkimya kwa kipindi chote cha mkutano.
Kabla ya misheni yangu, nilikuwa mwoga kwamba ushuhuda wangu haukuwa imara vya kutosha. Hakuna mtu yeyote katika familia yangu aliyewahi kuhudumu misheni, na mimi sikujua kama ningeweza kufanya hivyo. Ninakumbuka kujifunza na kusali sana ili nipokee ushahidi wa uhakika zaidi juu ya Yesu Kristo. Kisha siku moja, nilimsihi Baba wa Mbinguni, nilihisi hali yenye nguvu ya nuru na upendo. Na nilijua. Nilijua tu hivyo.
Ninakumbuka kuamshwa usiku mmoja miaka kadhaa baadaye na hisia ya “akili safi” zikiniambia ningeitwa kuhudumu katika akidi ya wazee. Wiki mbili baadaye niliitwa.
Ninakumbuka mkutano mkuu ambapo mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili akizungumza maneno hasa ya ushuhuda niliyokuwa nimemwambia rafiki kwamba nilitumaini kuyasikia.
Ninakumbuka kupiga magoti pamoja na mamia ya ndugu wa ukuhani ili kumuombea rafiki mpendwa ambaye alilala mahututi kwenye mashine ya kupumulia katika hospitali ndogo, ya mbali baada ya moyo wake kusimama. Tulipounganisha mioyo yetu ili kusihi kwa ajili ya maisha yake, aliamka na kuondoa mashine ya kupumulia kutoka ndani ya koo lake. Leo anahudumu kama rais wa kigingi.
Na ninakumbuka kuamka nikiwa na hisia yenye nguvu ya kiroho baada ya ndoto dhahiri ya rafiki mpendwa na mnasihi ambaye alifariki mapema sana, akiacha pengo kubwa katika maisha yangu. Alikuwa akitabasamu na mwenye shangwe. Nilijua alikuwa SAWA.
Hii ni baadhi ya miale yangu. Umekuwa na uzoefu wako mwenyewe—miale yako mwenyewe iliyojaa mifumuko ya nuru ya ushuhuda. Tunapotambua, kukumbuka na kukusanya miale hii “pamoja katika kitu kimoja,” kitu fulani cha kupendeza kinaanza kutendeka. “Nuru huambatana na nuru”—“kweli huikumbatia kweli.” Uhalisia na nguvu ya mwale mmoja wa ushuhuda huimarisha na kuunganika na mwingine, na kisha mwingine na mwingine. Mstari juu ya mstari na kanuni juu ya kanuni, hapa mwale na pale mwale—mmoja mdogo, muda wa kiroho unaothaminiwa kwa wakati fulani—hapo hukua ndani yetu kiini cha uzoefu wa kiroho uliojaa nuru. Pengine hakuna mwale mmoja ulio na nguvu za kutosha au kuangaza vya kutosha kujenga ushuhuda kamili, lakini kwa pamoja inaweza kuwa nuru ambayo giza la shaka halitashinda.
“Ee basi, hili si kweli?” Alma anauliza. “Nawaambia, Ndiyo, kwa sababu ni nuru,”
“Kile kilicho cha Mungu ni nuru” Bwana anatufundisha, “na yule ambaye huipokea nuru, na kukaa ndani ya Mungu, hupokea nuru zaidi; na nuru hiyo huzidi kungʼara hata mchana mkamilifu.”
Hiyo inamaanisha, akina kaka na akina dada, kwamba baada ya muda na kupitia “bidii kubwa,” sisi pia tunaweza kuwa na nguzo yetu wenyewe ya mwanga—mwale mmoja kwa wakati. Na katikati ya nguzo hiyo, sisi pia tutampata Baba wa Mbinguni mwenye upendo, akituita sisi kwa jina, akituelekeza kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo na kutualika “Tumsikilize Yeye!”
Ninatoa ushahidi juu ya Yesu Kristo, kwamba Yeye ndiye nuru na uzima wa ulimwengu wote—na ulimwengu wako binafsi na wangu.
Ninashuhudia kwamba Yeye kweli ni Mwana aliye hai wa Mungu aliye hai, na kwamba Yeye anasimama juu ya kichwa cha hili Kanisa la kweli lililo hai, akiliongoza na kulielekeza kupitia manabii na mitume Wake walio hai
Na tutambue na kupokea nuru Yake takatifu na kisha kumchagua Yeye badala ya giza la ulimwengu—daima na milele. Katika jina la Yesu Kristo, amina.