Mkutano Mkuu
Kuunganisha Amri Mbili Kuu
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Kuunganisha Amri Mbili Kuu

Uwezo wetu wa kumfuata Yesu Kristo hutegemea juu ya nguvu na uwezo wetu wa kuishi amri ya kwanza na ya pili kwa usawa na kujitoa kuliko sawa kwenye amri zote mbili.

Utangulizi

Mimi na mke wangu Lesa, tunaposafiri kutimiza majukumu ulimwenguni kote, tunafurahia fursa ya kukutana nanyi katika mikusanyiko mikubwa na midogo. Kujitoa kwenu kwenye kazi ya Bwana hutuinua na kunasimama kama ushuhuda kwenye injili ya Yesu Kristo. Tunarejea nyumbani baada ya kila safari tukijiuliza kama tumetoa kingi kama tulivyopokea.

Picha
Daraja la Rainbow.
Picha
Daraja la Tsing Ma.
Picha
Daraja la Tower.

Tunaposafiri, tunakuwa na muda mdogo wa kuona maeneo. Hata hivyo, inapowezekana, ninatumia muda kidogo kwenye kitu nikipendacho. Ninavutiwa na ubunifu na usanifu wa majengo na mvuto maalumu kwenye madaraja. Madaraja ya juu huwa yananishangaza. Iwe Daraja la Rainbow huko Tokyo, Daraja la Tsing Ma huko Hong Kong, Daraja la Tower huko London, au mengineyo niliyoyaona, ninastaajabu kwa ustadi wa kiuhandisi uliojengwa ndani ya maumbo haya makubwa. Madaraja hutupeleka kwenye maeneo ambayo vinginevyo tusingeyafikia. (Kabla sijaendelea, ninatambua kwamba tangu ujumbe huu utayarishwe, janga la ajali ya daraja lilitokea huko Baltimore. Tunaomboleza upotevu wa maisha na kutoa rambirambi kwa familia zilizoathiriwa.)

Daraja la Juu la Kupendeza

Hivi karibuni, jukumu langu la mkutano lilinipeleka California, ambapo kwa mara nyingine tena nilivuka Daraja kuu la Golden Gate, linalozingatiwa kama uhandisi wa kustaajabisha ulimwenguni. Muundo huu mkubwa unajumuisha umbo zuri, kutimiza jukumu muhimu na uhandisi hodari. Ni daraja la juu la kisasa lenye minara kama ncha za kitabu, likisaidiwa na nguzo kubwa sana. Minara pacha mikubwa sana, yenye uwezo wa kuhimili uzito wa daraja inayoinuka juu ya bahari ndiyo ilikuwa ya kwanza kujengwa. Kwa pamoja hushikilia nyaya zinazounganisha nguzo hizi mbili na zinazotawanyika kutoka nguzo hizi, nyaya ambazo hushikilia barabara iliyo chini yake. Uwezo wa ajabu wa kuhimili—nguvu za mnara—ndio muujiza wa uhandisi wa daraja hili.

Picha
Daraja la Golden Gate likiwa katika ujenzi.

Wilaya ya Daraja la Golden Gate

Picha za mwanzo za ujenzi wa daraja zinashuhudia kanuni hii ya uhandisi. Nguzo hizi mbili za daraja hutoa msaada wa kubeba uzito kwa kila kipengele cha daraja, kila moja ikiwa imeunganika na kutegemea nyenzake.

Picha
Daraja la Golden Gate likiwa katika ujenzi.

Getty Images/Underwood Archives

Wakati daraja linapokuwa limekamilika, likiwa na minara yake miwili imewekwa kwa uimara mahali pake na nguzo zikiwa zimejengwa juu ya msingi wa mwamba, ni taswira yenye nguvu na urembo.

Picha
Daraja la Golden Gate.

Leo ninawaalika mtazame daraja hili la kitaifa—lenye minara pacha iliyojengwa juu ya msingi imara—kupitia lenzi ya injili.

Katika zama za kale za huduma ya Yesu Kristo, katika kile ambacho sasa tunakiita Wiki Takatifu, Mfarisayo ambaye pia alikuwa mwanasheria alimwuliza Mwokozi swali alilojua lilikuwa gumu kujibika: “Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika sheria?” Mwanasheria, “akimjaribu” na akitafuta jibu la kisheria, akiwa na nia dhahiri ya ulaghai, alipokea jibu halisi, takatifu, la kiungu.

“Yesu akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.

“Hii ndiyo amri iliyo kuu tena ni ya kwanza. Tukirejelea analojia yetu ya daraja, mnara wa kwanza!

“Na ya pili yafanana nayo, Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Huu ni mnara wa pili!

“Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.” Vipengele vilivyobakia vya daraja!

Acha tuchunguze kila moja ya amri hizi mbili kuu, kama zilivyofunuliwa na kusemwa katika jibu la Mwokozi. Tunapofanya hivyo, ruhusu taswira ya daraja zuri la juu livume katika macho ya akili zako.

Mpende Bwana

Ya kwanza, kumpenda Bwana kwa moyo wako wote, roho na akili.

Katika jibu hili, Yesu Kristo anaweka umuhimu wa sheria uliotolewa katika mafundisho matakatifu ya Agano la Kale. Kumpenda Bwana huwa na kiini kwanza kwenye moyo wako—asili yako hasa. Bwana anakutaka kwamba upende kwa roho yako yote—umbile lako lote—na mwishowe, upende kwa akili yako yote—mawazo yako na uwezo wako wa kufikiri. Upendo kwa Mungu hauishi au hauna kikomo. Hauna mwisho na ni wa milele.

Kwangu mimi, kutekeleza amri kuu ya kwanza wakati mwingine kunaweza kuonekana kama dhahania, hata kusikowezekana. Kwa shukrani, ninapotafakari zaidi maneno yaliyotolewa na Yesu, amri hii inaonekana kutekelezeka zaidi: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Hili ninaweza kulifanya. Ninaweza kumpenda Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, ambayo kisha huongoza kwenye sala, kujifunza maandiko na kuabudu hekaluni. Tunampenda Baba na Mwana kupitia ulipaji wa zaka, kuitakasa siku ya Sabato, kuishi maisha mema na masafi na kuwa mtiifu.

Kumpenda Bwana mara nyingi hupimwa kwa matendo madogo madogo ya kila siku, hatua kwenye njia ya agano: kwa vijana, matumizi ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujenga baala ya kubomoa; kuondoka kwenye sherehe, sinema au shughuli ambapo viwango vinaweza kuhatarishwa; kuonyesha unyenyekevu kwa vitu vitakatifu.

zingatia mfano huu wa upendo. Ilikuwa Jumapili ya mfungo wakati mimi na Vancetulipobisha hodi kwenye mlango wa nyumba ndogo, tulivu. Sisi na mashemasi wengine katika akidi tulikuja tukitarajia maneno, “Karibuni ndani,” yakisemwa kwa ukunjufu katika lafudhi nzito ya Kijerumani, sauti kubwa vya kutosha kusikika upande mwingine wa mlango. Dada Muellar alikuwa mojawapo wa wajane wahamiaji katika kata. Hakuweza kufungua mlango kwa urahisi sana, kwa sababu alikuwa na changamoto ya uoni. Tulipoingia ndani ya nyumba iliyokuwa na mwanga hafifu, alitusalimia kwa maswali ya ukarimu: Majina yenu ni nani? Mnaendeleaje? Je, mnampenda Bwana? Tulijibu na kushiriki kwamba tumekuja kupokea matoleo yake ya mfungo. Hata katika umri wetu wa ujana, hali yake ya uhaba ilikuwa dhahiri, na jibu lake lililojaa imani lilikuwa la kugusa sana: “Nimeweka senti moja kwenye kabati mapema asubuhi hii. Ninashukuru sana kuweza kutoa matoleo yangu ya mfungo. Mnaweza kuwa wakarimu vya kutosha kuiweka ndani ya bahasha na kujaza risiti yangu ya matoleo ya mfungo?” Upendo wake kwa Bwana uliinua imani yetu kila mara tulipoondoka nyumbani kwake.

Mfalme Benjamini aliahidi nguvu ya ajabu kwa wale wanaofuata amri kuu ya kwanza. “Ningetamani mtafakari juu ya hali ya baraka na yenye furaha ya wale wanaotii amri za Mungu. … Wanabarikiwa katika vitu vyote, … na kama watavumilia kwa uaminifu hadi mwisho watapokelewa mbinguni … katika hali ya furaha isiyo na mwisho.”

Kumpenda Bwana huongoza kwenye furaha ya milele!

Mpende Jirani Yako

Yesu kisha alisema, “Na ya pili yafanana nayo, Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Huu ni mnara wa pili wa daraja.

Hapa Yesu huunganisha mtazamo wetu wa juu mbinguni, kumpenda Bwana, pamoja na mtazamo wetu wa kidunia, kuwapenda binadamu wenzetu. Amri moja hutegemea nyingine. Upendo kwa Bwana haukamiliki kama tusipowajali majirani zetu. Upendo huu wa nje huwajumuisha watoto wote wa Mungu bila kujali jinsia, daraja la kijamii, mbari, kipato, umri au kabila. Tunawatafuta wote walioumizwa na kuvunjika, waliotengwa, kwani “wote ni sawa kwa Mungu.” “Tunawasaidia wadhaifu, kunyoosha mikono iliyolegea, na kuimarisha magoti yaliyo dhaifu.”

Fikiria mfano huu: Kaka Evans alishangazwa pale aliposukumwa kusimamisha gari lake na kugonga kwenye mlango wa familia asiyoijua. Wakati mama mjane wa zaidi ya watoto 10 alipofungua mlango, hali zao ngumu na uhitaji mkuu ulionekana kwake. Kitu cha kwanza kilikuwa rahisi, kupaka rangi nyumba yao, kitu ambacho kilifuatiwa na miaka mingi ya uhudumiaji wa kimwili na kiroho kwa familia hii.

Mama huyu mwenye shukrani baadaye aliandika kuhusu rafiki yake aliyetumwa na mbingu: “Umetumia maisha yako kutufikia sisi tulio masikini. Jinsi gani ningependa kusikia vitu ambavyo Bwana anasema kwako wakati anapotoa shukrani Zake kwa wema ulioufanya kifedha na kiroho kwa watu ambao ni wewe na Yeye pekee mliwajua. Asante kwa kutubariki katika njia nyingi, … kwa wamisionari ulio waleta. … Siku zote najiuliza kama Bwana alikuchagua wewe tu au wewe ndiye uliyeamua kusikiliza tu.”

Kumpenda jirani yako hujumuisha matendo kama ya Kristo ya wema na huduma. Je, unaweza kuachana na vinyongo, kuwasamehe maadui, kuwakaribisha na kuwahudumia majirani na kuwasaidia wazee? Wote mtainuliwa kadiri mnavyojenga minara ya upendo kwa jirani.

Rais Russell M. Nelson amefundisha: “Kutoa msaada kwa wengine—kufanya bidii ya kuwajali wengine kama vile au zaidi ya sisi tunavyojijali—ni shangwe yetu. Hasa … wakati ambapo si muafaka na wakati ambapo kufanya hivyo hututoa katika eneo letu la faraja. Kuishi amri hiyo kuu ya pili ni msingi wa kuwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu kristo.”

Utegemezi

Yesu alifundisha zaidi, “Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.” Jambo hili ni la kufundisha sana Kuna utegemezi muhimu kati ya kumpenda Bwana na kupendana sisi kwa sisi. Ili Daraja la Golden Gate liweze kufanya kazi yake iliyokusudiwa, minara yote miwili inapaswa kuwa na uimara ulio sawa na nguvu sawa ili kubeba uzito wa nyaya za daraja, barabara na magari yanayovuka daraja hilo. Bila usawa huu wa kiuhandisi, daraja lingekuwa hatarini, hata kusababisha kubomoka. Ili daraja lolote la juu liweze kufanya kile lilichokusudiwa kufanya, nguzo zake lazima zifanye kazi pamoja katika upatanifu kamili. Vivyo hivyo, uwezo wetu wa kumfuata Yesu Kristo hutegemea juu ya nguvu na uwezo wetu wa kuishi amri ya kwanza na ya pili kwa usawa na kujitoa kuliko sawa kwenye amri zote mbili.

Picha
Daraja la Golden Gate.

Ongezeko la mabishano katika ulimwengu huashiria, hata hivyo, kwamba sisi wakati mwingine tunashindwa kuona au kukumbuka hili. Baadhi wamefokasi sana kwenye kushika amri kiasi kwamba wanaonyesha ustahimilivu kidogo kwa watu wale wanaowaona kama si wenye haki sana. Baadhi wanapata ugumu kuwapenda wale wanaochagua kuishi maisha yao nje ya agano au hata nje ya ushiriki wa dini yoyote.

Kama mbadala, kuna wale wanaosisitiza umuhimu wa kuwapenda wengine bila kujali kwamba sote tunawajibika kwa Mungu. Wengine hukataa kabisa dhana ya kwamba kuna kitu kiitwacho ukweli halisi au jema na baya na wanaamini kwamba kitu pekee kinachohitajika kwetu ni ustahimilivu na ukubali kamili wa chaguzi za wengine. Yoyote kati ya haya yasiyo na usawa yanaweza kusababisha daraja lako la kiroho kupinda au hata kuanguka.

Rais Dallin H. Oaks alielezea hili wakati aliposema: Tumeamriwa kumpenda kila mtu, kwani mfano wa Yesu juu ya Msamaria mwema hufundisha kwamba kila mtu ni jirani yetu. Lakini azma yetu ya kutii amri hii ya pili lazima isitusababishe tusahau ya kwanza, kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote, roho na akili.”

Hitimisho

Hivyo swali kwa kila mmoja wetu ni, Ni kwa jinsi gani tunajenga daraja letu wenyewe la imani na kujitoa—tukisimamisha minara ya daraja kubwa la kumpenda Mungu na kuwapenda majirani zetu? Ni rahisi, tunaanza tu. Jitihada zetu za awali zinaweza kuonekana kama nyuma ya kitambaa au ramani ya awali ya daraja tunalotazamia kulijenga. Zinaweza kujumuisha malengo machache ya kufikika ya kuelewa injili ya Bwana zaidi au kudhamiria kuhukumu wengine kidogo. Hakuna aliye mdogo sana au mzee sana kuanza.

Picha
Ramani ya usanifu wa daraja.

Baada ya muda, kwa sala na kwa tafakuri, mawazo butu huboreshwa. Matendo mapya huwa tabia. Miswada wa awali huwa ramani iliyoboreshwa. Tunajenga daraja letu binafsi la kiroho kwa mioyo na akili zilizoelekezwa kwa Baba wa Mbinguni na Mwana Wake Mpendwa pamoja na kwa akina kaka na akina dada tunaofanya nao kazi, tunaocheza nao, na kuishi nao.

Katika siku zijazo, upitapo katika daraja maridadi la juu au hata uonapo picha, likiwa na minara yake inayopaa, ninakualika ukumbuke amri kuu mbili, zilizoelezwa na Yesu Kristo katika Agano Jipya. Acha maelekezo ya Bwana yatuvuvie. Acha mioyo na akili zetu ziinuliwe juu kumpenda Bwana na zigeukie nje, kumpenda jirani yetu.

Na hili likaimarishe imani yetu katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake, ambao juu ya huo ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. “Katika Agano Jipya, [neno mwanasheria lilikuwa] sawa na mwandishi, mtu ambaye kwa taaluma ni mwanafunzi na mwalimu wa sheria, ikijumuisha sheria iliyoandikwa ya vitabu vya Musa, na pia ‘desturi za wazee’ (Mathayo. 22:35; Marko 12:28; Luka 10:25)” (Bible Dictionary, “Lawyer”).

  2. Zamani, wasomi wa Kiyahudi waliorodhesha amri 613 katika Torati na walijadiliana kuhusu umuhimu wa amri moja dhidi ya nyingine. Huenda mwanasheria alinuia kutumia jibu la Yesu dhidi Yake. Kama angesema amri moja ndio ya muhimu sana, ingeruhusu upenyo wa kumshitaki Yesu kwa kupuuzia kipengele kingine cha sheria. Lakini jibu la Mwokozi liliwanyamazisha wale waliokuja kumtega kwa kauli ya msingi ambayo leo ndiyo mwamba wa kile tunachokifanya Kanisani.

  3. Mathayo 22:36–40.

  4. Ona Mafundisho na Maagano 88:15.

  5. Yohana 14:15.

  6. Majina yote mawili yalibadilishwa katika hadithi hii ili kulinda faragha.

  7. Mosia 2:41.

  8. Mathayo 22:39.

  9. 2 Nefi 26:33.

  10. Mafundisho na Maagano 81:5

  11. Majina yamebadilishwa ili kulinda faragha.

  12. Russell M. Nelson, “Amri Kuu ya Pili,” Liahona, Nov. 2019, 100.

  13. Mathayo 22:40.

  14. Dallin H. Oaks, “Amri Mbili Kuu,” Liahona, Nov. 2019, 73–74.

Chapisha