Maagano na Majukumu
Kanisa la Yesu Kristo linajulikana kama kanisa ambalo husisitiza kufanya maagano na Mungu.
“Ni kwa jinsi gani Kanisa lako ni tofauti na mengine?” Jibu langu kwa swali hili muhimu limekuwa tofauti kadiri ya ukomavu wangu na kadiri ambavyo Kanisa limekuwa. Nilipozaliwa Utah mwaka 1932, uumini wetu wa Kanisa ulikuwa takribani 700,000, uliojikusanya zaidi Utah na majimbo ya jirani. Wakati huo, tulikuwa na mahekalu 7 pekee. Leo waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho unafikia zaidi ya milioni 17 katika takribani mataifa 170. Na mpaka kufikia Aprili 1, tunayo mahekalu 189 yaliyowekwa wakfu katika mataifa mengi na 146 zaidi katika mipango na ujenzi. Nimejisikia kuzungumza kuhusu dhumuni la mahekalu haya na historia na jukumu la maagano katika kuabudu kwetu. Hili litakuwa nyongeza kwa mafundisho yenye mwongozo wa kiungu ya wazungumzaji walionitangulia.
I.
Agano ni ahadi ya kutimiza majukumu fulani. Ahadi binafsi ni muhimu kwa udhibiti wa maisha yetu binafsi na kwa utendaji wa jamii. Dhana hii kwa sasa inakosolewa. Wenye sauti wachache wanapinga mamlaka ya taasisi na kusisitiza kwamba watu wanapaswa kuwa huru dhidi ya vikwazo ambavyo vinaweka ukomo kwenye uhuru wao binafsi. Bado tunajua kutokana na milenia ya uzoefu kwamba watu wanaacha baadhi ya uhuru binafsi ili wapate faida za kuishi kwenye jamii zenye utaratibu. Kuachilia huko uhuru wa mtu kumejikita kimsingi kwenye ahadi au maagano, yanayooneshwa dhahiri au yasiyo dhahiri.
Hapa ni baadhi ya mifano ya majukumu ya maagano katika jamii yetu: (1) waamuzi, (2) jeshi, (3) wahudumu wa afya na (4) zima moto. Wote wanaohusika katika kazi hizi zinazojulikana wanaweka ahadi—mara nyingi ikirasimishwa na kiapo au agano—la kutimiza majukumu yao waliyopangiwa. Hilo pia ni kweli kwa wamisionari wetu. Mavazi ya kipekee au beji za majina zinakusudiwa kuashiria kwamba mvaaji yuko chini ya agano na hivyo ana wajibu wa kufundisha na kuhudumu na anapaswa kusaidia katika huduma hiyo. Lengo linalohusiana ni kuwakumbusha wavaaji juu ya majukumu yao ya agano. Hakuna “muujiza” katika mavazi yao au ishara zao zenye upekee, isipokuwa hitaji au ukumbusho wa majukumu maalumu mvaaji aliyojichukulia. Hii pia ni kweli kwa ishara za pete za uchumba na pete za ndoa na jukumu la pete hizo katika kutoa angalizo kwa watazamaji au ukumbusho kwa wavaaji juu ya majukumu ya agano.
II.
Kile nilichokisema kuhusu maagano kuwa msingi kwa ajili ya kuongoza maisha yetu binafsi kinahusika hasa kwenye maagano ya kidini. Msingi na historia ya miunganiko na vigezo vingi vya kidini vimejikita kwenye maagano. Kwa mfano, agano la Ibrahimu ni la msingi kwenye tamaduni kadhaa kubwa za kidini. linatambulisha wazo takatifu la ahadi za agano la Mungu kwa watoto Wake. Agano la Kale mara nyingi hurejelea agano la Mungu na Ibrahimu na uzao wake.
Sehemu ya kwanza ya Kitabu cha Mormoni, ambayo iliandikwa kipindi cha Agano la Kale, kwa wazi inaonesha jukumu la maagano katika historia na kuabudu kwa Waisraeli. Nefi aliambiwa kwamba maandishi ya Waisraeli ya kipindi kile yalikuwa “kumbukumbu ya Wayahudi, ambayo ina maagano ya Bwana, ambayo aliagana na nyumba ya Israeli.” Vitabu vya Nefi pia vinafanya marejeleo ya mara kwa mara kwenye agano la Ibrahimu na kwa Israeli kama “watu wa Bwana wa Agano.” Utamaduni wa kuweka agano na Mungu au kiongozi wa dini pia umerekodiwa kwenye maandishi ya Kitabu cha Mormoni kuhusu Nefi, Yusufu wa Misri, Mfalme Benjamini, Alma na Kapteni Moroni.
III.
Muda ulipofika kwa ajili ya Urejesho wa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo, Mungu alimwita nabii, Joseph Smith. Hatujui maelezo kamili ya maelekezo ya mwanzo ya malaika Moroni kwa nabii huyu mdogo. Tunajua alimwambia Joseph Smith kwamba “Mungu alikuwa na kazi ambayo [yeye] angefanya” na kwamba “utimilifu wa injili isiyo na mwisho” lazima ungekuja, ikiwa ni pamoja na “ahadi zilizofanywa kwa mababu.” Tunajua pia kwamba maandiko ambayo Joseph mdogo aliyasoma kwa tafakuri sana—hata kabla hajaelekezwa kurejesha kanisa—yalikuwa mafundisho mengi kuhusu maagano aliyokuwa akiyatafsiri katika Kitabu cha Mormoni. Kitabu hicho ni chanzo kikuu cha Urejesho wa utimilifu wa injili, ikijumuisha mpango wa Mungu kwa ajili ya watoto Wake, na Kitabu cha Mormoni kimejaa marejeleo ya maagano.
Akiielewa vyema Biblia, Joseph lazima alijua juu ya rejeleo la kitabu cha Waebrania kwenye lengo la Mwokozi la “kuwatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya.” Waebrania pia humrejelea Yesu kama “mpatanishi wa agano jipya.” Kwa umuhimu, maelezo ya kibiblia juu ya huduma ya duniani ya Mwokozi yana kichwa cha habari ambacho kisawe chake cha karibu ni “Agano Jipya.”
Maagano yalikuwa msingi katika Urejesho wa injili. Hili ni dhahiri katika hatua za mwanzo ambazo Bwana alimwelekeza Nabii kulizingatia katika kurejesha Kanisa Lake. Punde tu baada ya Kitabu cha Mormoni kuchapishwa, Bwana alielekeza uanzishwaji wa Kanisa Lake la urejesho, ambalo punde lingeitwa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ufunuo ulioandikwa mnamo Aprili 1830 unaelekeza kwamba watu “watapokelewa kwa njia ya ubatizo katika kanisa lake” baada ya wao “kushuhudia” (ambako humaanisha kushuhudia kwa dhati) “kwamba kwa ukweli wametubu dhambi zao zote, na wako radhi kujichukulia juu yao jina la Yesu Kristo, wakiwa na dhamira ya kumtumikia Yeye hadi mwisho”
Ufunuo huu huu unaelekeza kwamba Kanisa “likutane pamoja mara kwa mara kushiriki mkate na divai [maji] kwa ukumbusho wa Bwana Yesu.” Umuhimu wa ibada hii ni dhahiri katika maneno ya maagano yaliyoainishwa kwa ajili ya mzee au kuhani anaye hudumu. Anabariki nembo za mkate kwa ajili ya “roho za wale wote watakaoula …, ili … wakushuhudie, Ee Mungu Baba wa Milele, kwamba wako radhi kujichukulia juu yao jina la Mwanao, na daima kumkumbuka na kushika amri zake ambazo amewapa.”
Jukumu kuu la maagano katika kanisa jipya lililorejeshwa lilithibitishwa tena katika utangulizi ambao Bwana aliutoa kwa ajili ya chapisho la kwanza la mafunuo Yake. Hapo Bwana alitamka kwamba Yeye amemwita Joseph Smith kwa sababu wakazi wa dunia “wamepotoka kutoka kwenye ibada zangu, na wamevunja agano langu lisilo na mwisho.” Ufunuo huu unafafanua zaidi kwamba amri Zake zinatolewa “kwamba agano langu lisilo na mwisho liweze kuanzishwa.”
Leo tunao uelewa mzuri zaidi wa jukumu la maagano katika Kanisa lililorejeshwa na kuabudu kwa waumini wake. Rais Gordon B. Hinckley alitoa ufupisho huu juu ya matokeo ya ubatizo wetu na ulaji wa sakramenti kila wiki: “Kila muumini wa Kanisa hili ambaye ameingia katika maji ya ubatizo amekuwa sehemu ya agano takatifu. Kila wakati tunapokula sakramenti ya mlo wa Bwana, tunafanya upya agano hilo.”
Tumekumbushwa na wazungumzaji wengi kwenye mkutano huu kwamba Rais Russel M. Nelson mara nyingi anaurejelea mpango wa wokovu kama “njia ya agano” ambayo “hutuongoza turudi kwa [Mungu]” na “yote ni kuhusu uhusiano wetu na Mungu.” Anafundisha kuhusu umuhimu wa maagano katika ibada zetu za hekaluni na kutusihi tuuone mwisho kutokea mwanzo na “kufikiria selestia.”
IV.
Sasa ninazungumza zaidi juu ya maagano ya hekaluni. Katika kutimiza jukumu lake la kurejesha utimilifu wa injili ya Yesu Kristo, Nabii Joseph Smith alitumia miaka yake mingi ya mwishoni kuelekeza ujenzi wa hekalu huko Nauvoo, Illinois. Kupitia yeye Bwana alifunua mafundisho, injili, na maagano matakatifu kwa watakao mfuatia ili kusimamia katika mahekalu. Huko watu ambao walipokea endaumenti wangefundishwa mpango wa Mungu wa wokovu na kualikwa kufanya maagano matakatifu. Wale ambao waliishi kwa uaminifu kwenye maagano hayo waliahidiwa uzima wa milele, ambapo “vitu vyote ni mali yao” nao “watakaa katika uwepo wa Mungu na Kristo milele na milele.”
Ibada za endaumenti ndani ya Hekalu la Nauvoo zilitolewa kabla ya waanzilishi wetu wa mwanzo kufukuzwa na kuanza safari yao ya kihistoria kuelekea milima ya mbali huko Magharibi. Tunazo shuhuda nyingi kutoka kwa waanzilishi hao kwamba nguvu waliyopokea kutokana na kuunganishwa na Kristo katika endaumenti zao ndani ya Hekalu la Nauvoo iliwapa uwezo wa kufanya safari yao kuu na kujiimarisha huko Magharibi.
Watu ambao wamepokea endaumenti ndani ya hekalu takatifu wanawajibika kuvaa gamenti ya hekaluni, nguo isiyoonekana kwa sababu inavaliwa ndani ya nguo za nje. Inawakumbusha waumini waliopokea endaumenti juu ya maagano matakatifu waliyoyafanya na baraka walizoahidiwa ndani ya hekalu takatifu. Ili kufikia malengo hayo matakatifu, tumeelekezwa kuvaa gamenti za hekaluni daima, isipokuwa tu pale ambapo sababu za wazi zipo. Kwa sababu maagano hayana “siku ya mapumziko,” kuondoa gamenti inaweza kueleweka kama kanusho la majukumu na baraka ambazo zinahusiana nayo. Kinyume chake, watu wanaovaa gamenti zao kwa uaminifu na kutii maagano yao ya hekaluni wanathibitisha wajibu wao kama wanafunzi wa Bwana Yesu Kristo.
Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linajenga mahekalu ulimwenguni kote. Lengo la mahekalu ni kuwabariki watoto wa agano wa Mungu kwa ibada ya hekaluni na kwa majukumu matakatifu na nguvu na baraka za kipekee za kuunganishwa kwa Kristo kwa agano.
Kanisa la Yesu Kristo linajulikana kama kanisa ambalo husisitiza kufanya maagano na Mungu. Maagano ni ya kiasili katika kila ibada za wokovu na kuinuliwa ambazo Kanisa hili husimamia. Ibada ya ubatizo na maagano yake husika ni vigezo vinavyohitajika ili kuingia katika ufalme wa selestia. Ibada na maagano ya hekaluni yanayohusiana nayo ni vigezo vinavyohitajika kwa ajili ya kuinuliwa katika ufalme wa selestia, ambao ni uzima wa milele, “zawadi iliyo kuu katika zawadi zote za Mungu.” Hiyo ndiyo fokasi ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Ninashuhudia juu ya Yesu Kristo, ambaye ndiye kiongozi wa Kanisa hilo, na ninatamka baraka Zake juu ya wale wote wanao tafuta kushika maagano yao matakatifu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.