Kumezwa katika Furaha ya Kristo
Ninashuhudia kwamba Baba yetu wa Mbinguni husikia sala zenu za majonzi na daima hujibu kwa hekima kamili.
Tunakupenda, Mzee Kearon. Je, ninaweza kuazima lafudhi hiyo kwa dakika 10?
Kutamani Miujiza
Katika Agano Jipya tunajifunza juu ya kipofu Bartimayo, ambaye alilia kwa Yesu akitaka muujiza. “Yesu Akamwambia, Inuka enenda zako, imani yako imekuokoa. Na kisha akapata kuona.”
Katika tukio jingine, mwanamume mmoja huko Bethsaida alitamani sana uponyaji. Kinyume chake, muujiza huu haukutokea mara moja. Badala yake, Yesu alimbariki mara mbili kabla ya “kurejeshewa.”
Katika mfano wa tatu, Mtume Paulo “akamwomba Bwana mara tatu” katika mateso yake, na bado, kwa ufahamu wetu, ombi lake la dhati halikukubaliwa.
Watu watatu tofauti. Matukio matatu ya kipekee.
Hivyo, swali hili: Kwa nini baadhi hupokea miujiza waliyoitamania kwa haraka, wakati wengine kwa subira huvumilia, wakimngojea Bwana? Pengine hatuwezi kujua kwa nini, bali kwa shukrani, tunamjua Yeye ambaye “anatupenda [sisi]” na “[hufanya] mambo yote kwa ajili ya ustawi [wetu] wa milele na furaha.”
Madhumuni ya Kiungu
Mungu, ambaye huona mwisho tangu mwanzo, hutuhakikishia kwamba “Dhiki zako na mateso yako yatakuwa kwa kitambo kidogo tu” na yatawekwa wakfu “kwa faida yako.”
Kutusaidia sisi kupata maana zaidi katika majaribu yetu, Mzee Orson F. Whitney alifundisha: “Hakuna maumivu ambayo tunayapata, hakuna majaribu ambayo tunayapitia ambayo ni bure. Yanatumika katika elimu zetu. … Yote … tunayovumilia [kwa subira] … , yanajenga tabia zetu, yanatakasa mioyo yetu, yanapanua nafsi zetu, na hutufanya tuwe wapole na wenye hisani zaidi. … Ni kupitia huzuni na mateso, dhiki na masumbuko, ambapo tunapata elimu ambayo tunakuja hapa kuipata na ambayo itatufanya tufanane zaidi na [wazazi wetu wa mbinguni].”
Kuelewa kwamba “nguvu ya Kristo [ingekuwa] juu [yake]” katika dhiki yake, Mtume Paulo kwa unyenyekevu alisema, “Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.”
Majaribu ya maisha hututhibitisha sisi. Hata Mwokozi “alijifunza … utiifu kwa” na alikuwa “kamili kupitia mateso.”
Na siku moja Yeye alitamka kwa huruma, “Nimekutakasa wewe, nimekuchagua wewe katika tanuru ya mateso.”
Kufikia kutumaini katika malengo matakatifu ya Mungu hutoa tumaini ndani ya nafsi zilizochoka na huamsha ari katika nyakati za masumbuko na kuvunjika moyo.
Mitazamo Mitakatifu
Miaka iliyopita, Rais Russell M. Nelson alishiriki utambuzi huu muhimu: “Tunapotazama mambo yote kwa mtazamo wa milele, itatupunguzia mzigo wetu kwa kiasi kikubwa.”
Mimi na mke wangu, Jill, hivi karibuni tulishuhudia ukweli huu katika maisha ya uaminifu ya Holly na Rick Porter, ambao mwana wao wa miaka 12, Trey, alifariki dunia kwa majonzi yaliyoletwa na moto. Akiwa na mikono na miguu iliyoungua sana kutokana na pambano la kishujaa la kumwokoa mwanawe mpendwa, Holly baadaye alishuhudia katika mkutano wa sakramenti wa kata juu ya amani na furaha kuu ambayo Bwana alikuwa ameimimina juu ya familia yao katika uchungu wao, akitumia maneno kama vile ya ajabu, ya kustaajabisha, na ya kushangaza.
Huzuni isiyo stahimilika ya mama huyu wa thamani ilibadilishwa na amani ipitayo amani zote akiwa na wazo hili: “Mikono yangu si mikono iokoayo. Mikono hiyo ni ya Mwokozi! Badala ya kutazama makovu yangu kama ukumbusho wa kile ambacho sikuweza kufanya, ninakumbuka makovu ambayo Mwokozi wangu anayo.
Ushahidi wa Holly unatimiza ahadi ya nabii wetu: Unapofikiria selestia, utayatazama majaribu na upinzani katika nuru mpya.”
Mzee D. Todd Christofferson alisema: “Ninaamini kuwa changamoto ya kushinda na kukua kutokana na dhiki ilitupendeza wakati Mungu alipowasilisha mpango Wake wa ukombozi katika ulimwengu ule wa kabla ya kuzaliwa. Tunapaswa kuikabili changamoto hiyo sasa tukijua kwamba Baba yetu wa Mbinguni atatusaidia. Lakini ni muhimu sana tumgeukie Yeye. Bila Mungu, uzoefu wa kiza wa mateso na dhiki utajaribu kutuvunja moyo, kutukatisha tamaa na hata kuleta huzuni.”
Kanuni za Kiungu
Ili kuepuka giza la kutoridhika na badala yake kupata amani kuu, tumaini, na hata shangwe wakati wa changamoto ngumu za maisha, ninashiriki kanuni tatu za kiungu kama mialiko.
Moja—imani thabiti huja kwa kumweka Yesu Kristo kwanza. “Nitegemeeni katika kila wazo,” Yeye alisihi; msitie shaka, msiogope.” Rais Nelson alifundisha:
“Uzima [wetu] wa milele unategemea imani [yetu] katika [Kristo] na katika Upatanisho Wake,”
“Wakati nikipambana na maumivu makali yaliyosababishwa na jeraha la hivi karibuni, nimehisi hata zaidi shukrani kwa ajili ya Yesu Kristo na zawadi yake ya Upatanisho isiyolinganishwa. Fikiria hilo! Mwokozi aliteseka ‘maumivu na masumbuko na majaribu ya kila aina’ ili kwamba Yeye aweze kutufariji, kutuponya, [na] kutuokoa katika nyakati za shida.”
Aliendelea: “Jeraha langu limenisababisha kutafakari tena na tena juu ya “ukuu wa Yule Mtakatifu wa Israeli.” Wakati wa uponaji wangu, Bwana amedhihirisha nguvu Zake za kiungu katika njia za amani na bayana.”
“Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo,” mimi nimeushinda ulimwengu.”
Pili—tumaini angavu huja kwa kupata taswira ya kudra yetu ya milele. Katika kuzungumza juu ya nguvu asili katika “ono la baraka za Baba yetu za ajabu zilizoahidiwa … mbele ya macho yetu kila siku,” Dada Linda Reeves alishuhudia: “Sijui ni kwa nini tuna majaribu haya mengi tuliyonayo, lakini ni hisia yangu binafsi kwamba thawabu ni kubwa sana, … ya furaha na ya kupita uelewa wetu kwamba katika siku ile ya thawabu, tuweze kujisikia kusema kwa Baba yetu mpendwa, mwenye rehema, ‘Je, hayo ndiyo yote yaliyohitajika?… Je, itajalisha … kile tulichoteseka hapa, ikiwa hatimaye, majaribu hayo … yatatustahilisha kwa ajili ya uzima wa milele … katika ufalme wa Mungu?”
Rais Nelson alishiriki umaizi huu: “Fikiria mwitikio wa Bwana wa sala ya Joseph Smith wakati aliposihi kwa ajili ya unafuu akiwa jela ya Liberty. Bwana alimfundisha Nabii kwamba kutendewa kwake kusiko kwa kibinadamu kungempa yeye uzoefu na kungekuwa kwa faida yake. ‘Kama utastahimili vyema,’ Bwana aliahidi, ‘Mungu atakuinua juu.’ Bwana alikuwa akimfundisha Joseph kufikiria selestia na kuvuta taswira ya thawabu ya milele kuliko kufokasi kwenye magumu ya kutisha ya siku hiyo.”
Badiliko la Joseph la kimtazamo lilileta utakaso wa kina, kama inavyoonyeshwa katika barua hii: “Baada ya kufungwa katika kuta za gereza kwa muda wa miezi mitano, inaonekana kwangu kwamba moyo wangu daima utakuwa mwororo zaidi baada ya hili kuliko hapo awali. … Ninafikiri kamwe sikuweza kuhisi kama ninavyohisi sasa, kama nisingetendwa uovu nilioteseka.”
Tatu—nguvu kuu huja kwa fokasi juu ya furaha. Wakati muhimu sana wa milele, masaa ya dhiki, Mwokozi wetu hakusita bali alikinywa kikombe kichungu. Alilifanyaje hili? Tunajifunza, “Kwa shangwe ambayo ilikuwa imewekwa mbele yake [Kristo] alivumilia msalaba,” mapenzi Yake “kumezwa katika mapenzi ya Baba.”
Kirai hiki “kumezwa” hunivutia sana. Kupendezwa kwangu kuliongezeka nilipojifunza kwamba katika Kihispania, “kumezwa” hutafsiriwa kuwa “kuteketezwa” katika Kijerumani, kama “kuliwa”; na katika Kichina, kama “mavimbi yamezavyo.” Kwa hiyo, wakati changamoto za kimaisha zina maumivu na kulemea, ninakumbuka ahadi ya Bwana—kwamba “hatupaswi kupatwa na dhiki yoyote, isipokuwa imemezwa [kumezwa, kumezwa, na kumezwa] katika furaha ya Kristo.”
Ninaona katika wengi wenu shangwe hii, ambayo “[hushinda] … uelewa wa binadamu,” ingawa vikombe vyenu vichungu bado havijaondolewa. Asanteni kwa kushika maagano yenu na kusimama kama mashahidi wa Mungu. Asanteni kwa kufikia ili kutubariki sote, huku “katika moyo [wako] uliyo kimya huficha masononeko mengi yasiyoonekana kwa macho.” Kwani wakati unapoleta faraja ya Mwokozi kwa wengine, utaipata kwa ajili yako mwenyewe, Rais Camille N. Johnson alifundisha.
Ahadi za Kiungu
Sasa, rudi pamoja nami kwenye mkutano wa sakramenti ambapo tulishuhudia muujiza wa familia ya Holly Porter ikisaidiwa na Bwana. Jukwaani huku nikitafakari kile ambacho ningeweza kusema ili kutoa faraja kwa familia hii ya kupendeza na marafiki zao, wazo hili lilinijia: “Tumia maneno ya Mwokozi.” Kwa hiyo, nafunga leo kama nilivyofanya siku ile ya Sabato, kwa maneno Yake, “ambayo huponya nafsi iliyojeruhiwa.”
“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”
“Na pia nitawapunguzia mizigo ambayo imewekwa mabegani mwenu, hata kwamba hamtaisikia kamwe migongoni mwenu, hata mkiwa utumwani; … na kwamba mjue kwa hakika kwamba mimi, Bwana Mungu, huwatembelea watu wangu katika mateso yao.”
Ushahidi Wangu
Kwa shangwe ya staha, ninashuhudia kwamba Mwokozi wetu yu hai na ahadi Zake ni za hakika” Kwa ajili yenu ambao mnateseka au “mnaosumbuka kwa njia yoyote,” ninashuhudia kwamba Baba yetu wa Mbinguni husikia kusihi kwenu kwa machozi na daima atajibu kwa hekima kamili. “Na Bwana awape,” kama Alivyofanya kwa familia yetu kwenye nyakati za uhitaji mkuu, “kwamba mizigo yenu ifanywe miepesi,” hata “kumwezwa kwenye shangwe ya Kristo.” Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.