Inuka! Yeye Anakuita Wewe
Injili sio njia ya kuepuka changamoto na shida bali ni suluhisho la kuongeza imani yetu na kujifunza jinsi ya kukabiliana nazo.
Wakati fulani uliopita nilimuuliza mke wangu, “Unaweza kuniambia kwa nini, kwa kadri ninavyokumbuka, sisi hatujawahi kuwa na shida yoyote kubwa katika maisha yetu?”
Aliniangalia na kusema, “Sawa! Nitakuambia kwa nini kamwe hatujawahi kuwa na shida yoyote kubwa; ni kwa sababu una kumbukumbu fupi sana!”
Jibu la haraka na la uerevu lilinifanya mimi kutambua kwa mara nyingine tena kwamba kuishi injili ya Yesu Kristo hakuondoi maumivu na majaribu, ambayo ni muhimu kwa ukuaji.
Injili sio njia ya kuepuka changamoto na shida bali ni suluhisho la kuongeza imani yetu na kujifunza jinsi ya kukabiliana nazo.
Nilipata ufahamu wa ukweli huu miezi michache iliyopita wakati nilipokuwa nikitembea siku moja, na ghafla uoni wangu ukawa na ukungu, giza na mawimbi mawimbi. Niliingiwa na uoga. Kisha madaktari waliniambia, “Kama hautaanza matibabu mara moja, unaweza kupoteza uoni wako hata ndani ya wiki chache.” Nilikuwa hata na uoga zaidi.
Na kisha walisema, “Wewe unahitaji sindano za kuchoma ndani ya mshipa—sindano ndani ya jicho—jicho likiwa wazi kabisa—kila baada ya wiki nne kwa maisha yako yote.”
Hilo lilikuwa jambo lisilo la faraja.
Kisha wazo likaja katika namna ya swali. Nikajiuliza mwenyewe, “SAWA! Uoni wangu wa kimwili sio mzuri, lakini vipi kuhusu uoni wangu wa kiroho? Je, nahitaji matibabu yoyote hapo? Na inamaanisha nini kuwa na uoni angavu wa kiroho?”
Nilitafakari kuhusu hadithi ya mtu kipofu aliyeitwa Bartimayo, aliyeelezewa katika Injili ya Marko. Maandiko husema, “Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu.”
Kwa kweli, katika macho ya wengi, Yesu alikuwa tu mwana wa Yusufu, kwa hiyo kwa nini Bartimayo alimwita Yeye “Mwana wa Daudi”? Ni kwa sababu yeye alitambua kwamba Yesu alikuwa kweli ni Masiya, ambaye alikuwa ametolewa unabii wa kuzaliwa kama wa uzao wa Daudi.
Inapendeza kwamba mtu huyu kipofu, ambaye hakuwa na uoni wa kimwili, alimtambua Yesu. Aliona kiroho kile ambacho yeye hangeweza kuona kimwili, hali wengine wengi wangeweza kumuona Yesu kimwili lakini walikuwa vipofu kabisa kiroho.
Kutokana na hadithi hii tunajifunza zaidi kuhusu uoni angavu wa kiroho.
Tunasoma, “Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu.”
Wote waliokuwa karibu naye walimwambia nyamaza, lakini alizidi kupaza sauti kwa sababu alijua Yesu alikuwa nani kweli. Alipuuza sauti zile na kupaza sauti hata zaidi sana.
Alitenda badala ya kutendewa. Licha ya hali yake yenye ufinyu, yeye alitumia imani yake kushinda mapungufu yake.
Kwa hiyo, kanuni ya kwanza tunayojifunza ni sisi kuweka uoni angavu wa kiroho tunapofokasi juu ya Yesu Kristo na kubaki wakweli kwa kile tunachojua ni kweli.
Akina Kaka na akina dada, ili kuweka uoni wetu wa kiroho bila waa, tunahitaji kuamua kutosikiliza sauti za ulimwengu unaotuzunguka. Katika ulimwengu huu unaokanganya na uliokanganyikiwa, lazima tubaki waaminifu kwa kile tunachojua, waaminifu kwa maagano yetu, waaminifu katika kushika amri na kuthibitisha tena imani yetu hata kwa nguvu, kama mtu huyu alivyofanya. Tunahitaji hata kupaza sauti sana kuhusu ushuhuda wetu juu ya Bwana kwa ulimwengu. Mtu huyu alimjua Yesu, alibakia mwaminifu kwa kile ambacho yeye aliamini, na hakuvutwa mawazo na sauti zilizomzunguka.
Kuna sauti nyingi leo zinazojaribu kuzima sauti zetu kama wanafunzi wa Yesu Kristo. Sauti za ulimwengu zinajaribu kutuzima sisi, lakini hiyo hasa ndiyo kwa nini lazima tutangaze ushuhuda wetu juu ya Mwokozi kwa sauti na kwa nguvu. Miongoni mwa sauti zote za ulimwengu, Bwana ananitegemea mimi na wewe kutangaza ushuhuda wetu, kupaza sauti zetu na kuwa sauti Yake. Kama hatutofanya hivyo, ni nani atakayeshuhudia juu ya Yesu Kristo? Ni nani atakaye sema jina Lake na kutangaza misheni Yake takatifu?
Tuna jukumu la kiroho ambalo hutokana na maarifa yetu juu ya Yesu Kristo.
Basi ni nini Bartimayo alifanya baada ya hapo?
Kwa amri ya Bwana ya inuka, yeye alitenda tena kwa imani.
Maandiko yanasema, “Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu.”
Huyu mtu mnyenyekevu na mwaminifu alielewa kwamba yeye angeweza kuinuka kwenye maisha bora kwa amri ya Yesu. Alijua kwamba yeye alikuwa bora kuliko hali yake, na kitu cha kwanza kabisa alichofanya wakati alipomsikia Yesu akimwita ilikuwa ni kutupa koti lake la ombaomba.
Tena yeye alitenda badala ya kutendewa.
Angeweza kufikiria, “Sihitaji hili tena, sasa kwamba Yesu amekuja katika maisha yangu. Hii ni siku mpya. Ninaachana na maisha haya ya dhiki. Nikiwa na Yesu ninaweza kuanza maisha mapya ya furaha na shangwe katika Yeye, pamoja Naye na kupitia Yeye. Sijali kile ulimwengu unafikiria juu yangu. Yesu ananiita, na Yeye atanisaidia kuishi maisha mapya
Ni badiliko la ajabu jinsi gani!
Alipotupa koti lake la ombaomba, yeye aliondoa visingizio vyote.
Na hii ni kanuni ya pili: sisi huweka uoni angavu wa kiroho wakati tunapomwacha mtu wa asili nyuma, kutubu na kuanza maisha mapya katika Kristo.
Njia ya kufanya hivyo ni kwa kufanya na kuyashika maagano ya kuinuka hadi kwenye maisha bora kupitia Yesu Kristo.
Kadiri tunavyotoa visingizio vya kujionea huruma wenyewe, kujihurumia kwa ajili ya hali zetu na shida zetu na kwa ajili ya mambo yote mabaya yanayotendeka katika maisha yetu na hata watu wote wabaya ambao tunafikiria wanatufanya tusiwe na furaha, tunaendelea kuyavika mabega yetu na koti la ombaomba. Ni kweli kwamba katika nyakati fulani watu, kwa kujua au bila kujua, wanatuumiza. Lakini tunahitaji kuamua kutenda kwa imani katika Kristo kwa kuvua koti la kiakili na kihisia ambalo tungeweza kuwa tunalibeba ili kuficha visingizo au dhambi na kulitupilia mbali, tukijua kwamba Yeye anaweza na atatuponya.
Hakuna kamwe kisingizio kizuri cha kusema, “Niko vile nilivyo kwa sababu ya hali za bahati mbaya na hali zisizo nzuri. Na siwezi kubadilika, hivyo nastahili haki.”
Wakati tunafikiria kwa njia hiyo, tunaamua kutendewa.
Tunabakia na koti la ombaomba.
Kutenda kwa imani humaanisha kumtegemea Mwokozi wetu, kuamini kwamba kupitia Upatanisho Wake, tunaweza kuinuka juu ya kila kitu kwa amri Yake.
Kanuni ya tatu iko katika maneno manne ya mwisho: “[yeye] alikuja kwa Yesu.”
Ni kwa jinsi gani yeye alienda kwa Yesu hali akiwa kipofu? Njia moja ilikuwa ni kutembea kumwelekea Yesu kwa kusikia sauti Yake.
Na hii ni ile kanuni ya tatu: sisi kuweka uoni angavu wa kiroho tunaposikia sauti ya Bwana na kumruhusu Yeye atuongoze.
Kama vile mtu huyu alivyopaza sauti yake juu ya sauti zilizomzunguka, aliweza kusikia sauti ya Bwana katikati ya sauti nyingine zote.
Hii ni imani sawa na ile iliyomruhusu Petro kutembea juu ya maji kwa kadiri alivyoweka fokasi yake ya kiroho juu ya Bwana na hakuvutwa mawazo na upepo uliomzunguka.
Kisha hadithi ya mtu kipofu inaishia na maneno “akapata kuona; akamfuata Yesu njiani.”
Mojawapo ya masomo muhimu sana katika hadithi hii ni kwamba mtu huyu alionyesha imani yake katika Yesu Kristo na alipokea muujiza kwa sababu aliomba kwa nia halisi, na kwa nia halisi kumfuata Yeye.
Na hii ndiyo sababu ya msingi kwa ajili ya baraka tunazopokea katika maisha yetu, ambako ni kumfuata Yesu Kristo. Ni kuhusu kumtambua Yeye, kufanya na kushika maagano na Mungu kwa sababu Yeye, anabadilisha asili yetu hasa kupitia Kwake, na kuvumilia hadi mwisho kwa kumfuata Yeye.
Kwangu mimi, kuweka uoni angavu wa kiroho ni kuhusu kufokasi kwa Yesu Kristo.
Je, uoni wangu wa kiroho ni angavu ninapochomwa sindano kwenye macho yangu? Mimi ni nani kusema? Lakini ninashukuru kwa kile ninachokiona.
Kwa uwazi ninaona mkono wa Bwana katika maisha yangu.
Ninaona imani ya wengi kokote ninakokwenda ambao wanaimarisha imani yangu.
Ninaona malaika wamenizunguka kila upande.
Ninaona imani ya wengi ambao hawawezi kumwona Bwana kimwili lakini wanamtambua kiroho, kwa sababu wanamjua Yeye kwa karibu.
Ninashuhudia kwamba injili hii ni jibu kwa kila kitu, kwa sababu Yesu Kristo ni jibu kwa kila mtu. Nina shukrani kwa kile ninachokiona ninapomfuata Mwokozi wangu.
Ninaahidi kwamba tunaposikia sauti ya Bwana na kumruhusu Yeye kutuongoza kwenye njia ya Mwokozi ya agano, tutabarikiwa na uoni angavu, uelewa wa kiroho, na amani ya moyo na akili maishani mwetu mwote.
Na tupaze sauti za ushuhuda juu Yake kwa sauti zaidi kuliko sauti zinazotuzunguka katika ulimwengu ambao unahitaji kusikia zaidi kuhusu Yesu Kristo na wala si kidogo. Na tulivue koti la ombaomba ambalo yawezekana kuwa bado tumelivaa, na kuinuka juu ya ulimwengu hadi kwenye maisha bora katika na kupitia Kristo. Na tuondoe visingizio vyote vya kutomfuata Yesu Kristo na kupata sababu zote nzuri za kumfuata Yeye tunaposikia sauti Yake. Haya ndiyo maombi yangu katika jina la Yesu Kristo, amina.