Ushahidi wa Kile Nilichoona na Kusikia
Hakujawahi kuwa na wakati mzuri wa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kuliko leo.
Baada ya kuhitimu shule ya sheria, mimi pamoja na mke wangu, Marcia, tulichagua kujiunga na kampuni ya sheria ambayo ilikuwa imebobea katika sheria ya mashtaka. Nilipoanza mafunzo yangu ya kazi, nilitumia muda wangu mwingi kuandaa mashahidi wa kutoa ushahidi wakati wa kesi. Nilijifunza haraka kwamba jambo linaamuliwa katika chumba cha mahakama kama mashahidi, chini ya kiapo, walishuhudia ukweli wa kile walichokiona na kusikia. Mashahidi waliposhuhudia, maneno yao yalirekodiwa na kuhifadhiwa. Umuhimu wa mashahidi wa kuaminika daima ulikuwa mstari wa mbele katika maandalizi yangu.
Haikuchukua muda mrefu kwangu kutambua kwamba maneno yale yale niliyokuwa nikitumia kila siku kama wakili pia yalikuwa maneno niliyotumia katika mazungumzo yangu ya injili. “Ushahidi” na “ushuhuda” ni maneno tunayotumia tunaposhiriki maarifa na hisia zetu kuhusu ukweli wa injili ya Yesu Kristo.
Nilipokubaliwa kama Sabini wa Eneo mpya, nilifungua maandiko ili kujifunza majukumu yangu na kusoma Mafundisho na Maagano 107:25, ambayo inasema, “Wale Sabini pia wanaitwa … kuwa mashahidi maalumu kwa Wayunani na katika ulimwengu wote.” Kama unavyoweza kufikiria, macho yangu yalivutiwa na neno “mashahidi maalumu.” Ikawa wazi kwangu kwamba nilikuwa na jukumu la kutoa ushuhuda wangu—kushuhudia jina la Yesu Kristo—popote niendako ulimwenguni.
Kuna mifano mingi katika maandiko ya wale ambao walikuwa mashahidi wa kuona kwa macho na ambao walishuhudia kile walichokiona na kusikia.
Kama nabii wa kale Mormoni alipoanza kumbukumbu yake, anaandika, “Na sasa mimi, Mormoni, ninaandika maandishi ya vitu ambavyo nimeona na kusikia, na kuyaita Kitabu cha Mormoni.”
Mitume wa Mwokozi Petro na Yohana walimponya mtu kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti. Walipoamriwa kutokunena katika jina la Yesu, wao walijibu:
“Iwapo ni haki mbele ya Mungu kuwasikiliza ninyi zaidi kuliko Mungu, hukumuni ninyi.
“Kwani hatuwezi kuacha kuyanena mambo ambayo tumeyaona na kuyasikia.”
Ushuhuda mwingine wa kuvutia unatoka kwa Watakatifu wa Kitabu cha Mormoni ambao walishuhudia ziara ya Mwokozi Yesu Kristo. Sikiliza maelezo haya ya ushahidi wao: “Na kwa maneno haya walishuhudia: Jicho halijaona, wala sikio kusikia, hapo mbeleni, vitu vikubwa na vya ajabu vile tuliona na kusikia Yesu akisema kwa Baba.”
Kaka zangu na dada zangu, leo natangaza ushuhuda wangu na kuweka kumbukumbu ya yale niliyoona na kusikia wakati wa huduma yangu takatifu kama Sabini wa Bwana Yesu Kristo. Kwa kufanya hivyo ninashuhudia kwenu juu ya Baba wa Mbinguni mwenye upendo na Mwanawe mwenye huruma, Yesu Kristo, ambaye aliteseka, alikufa na kufufuka tena ili kutoa uzima wa milele kwa watoto wa Mungu. Ninashuhudia juu ya “kazi kubwa na ya ajabu” na kwamba Bwana ameweka mkono Wake tena ili kurejesha injili Yake duniani kupitia manabii na mitume Wake walio hai. Ninashuhudia kwamba kulingana na kile nilichoona na kusikia, hakujawahi kuwa na wakati mzuri wa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kuliko leo. Najua hili kwa maarifa yangu mwenyewe, bila kutegemea chanzo kingine chochote, kwa sababu ya kile nilichoona na kusikia.
Wakati wa mwaka wangu wa mwisho wa shule ya upili, ili kuhitimu kutoka seminari, ilibidi nitambue mahekalu yote 15 ya Kanisa. Picha ya kila hekalu ilikuwa mbele ya darasa letu, na ilibidi nijue kila moja lilikuwa wapi. Sasa, miaka kadhaa baadaye, itakuwa changamoto kubwa—kukiwa na mahekalu 335 yanayofanya kazi au yaliyotangazwa—kulitambua kila moja. Binafsi nimeona nyumba hizi nyingi za Bwana na kushuhudia kwamba Bwana anatoa baraka na ibada Zake kwa watoto Wake zaidi na zaidi ulimwenguni kote.
Marafiki zangu wa FamilySearch wamenifundisha kwamba zaidi ya majina mapya milioni moja yanaongezwa kila siku kwenye FamilySearch. Kama hukupata babu yako jana, ninakualika uangalie tena kesho. Linapokuja suala la kukusanya Israeli upande mwingine wa pazia, haijawahi kuwa wakati mzuri wa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kuliko leo.
Tukiwalea watoto wetu huko Twin Falls, Idaho, mtazamo wangu wa Kanisa la ulimwenguni kote ulikuwa finyu sana. Nilipoitwa kuwa Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka, mimi na Marcia tulipangiwa kuhudumu katika Eneo la Pasifiki, mahali ambapo hatukuwahi kufika. Tulifurahi kukuta vigingi kutoka juu ya New Zealand hadi chini, na hekalu ambalo liliwekwa wakfu mnamo 1958. Iilikuwa moja ya yale 15 niliyolazimika kukariri katika seminari. Tuliyaona mahekalu katika kila mji mkuu wa Australia na vigingi kote katika bara hilo. Tulikuwa na majukumu huko Samoa, ambapo kuna vigingi 25, na Tonga, mahali ambapo karibu nusu ya idadi ya watu ni waumini wa Kanisa. Tulikuwa na jukumu katika kisiwa cha Kiribati, ambako tulikuta vigingi viwili. Tulikuwa na kazi za kutembelea vigingi huko Ebeye katika Visiwa vya Marshall na Daru huko Papua New Guinea.
Baada ya huduma yetu katika Visiwa vya Pasifiki, tulipewa jukumu la kuhudumu huko Ufilipino. Kwa mshangao wangu, Kanisa la Yesu Kristo nchini Ufilipino linakua zaidi ya cho chote nilichokijua. Sasa kuna vigingi 125, misioni 23 na mahekalu 13 yanayofanya kazi au yaliyotangazwa. Nilishuhudia kanisa lenye waumini zaidi ya 850,000 katika nchi hiyo. Ni kwa jinsi gani nililikosa kujua ukuaji wa Kanisa la Kristo ulimwenguni kote?
Baada ya miaka mitatu huko Ufilipino, mimi niliombwa kuhudumu katika Idara ya Umisionari. Jukumu langu lilitupeleka kwenye misioni zote ulimwenguni. Mtazamo wangu juu ya Kanisa la Mwokozi ulimwenguni pote ulipanuka kwa kiasi kikubwa. Mimi na Marcia tulipangiwa kazi ya kutembelea misioni za huko Asia. Tulikuta kituo kizuri cha kigingi huko Singapore, pamoja na washiriki waaminifu, wa kushangaza. Tuliwatembelea waumini na wamisionari katika jengo la kanisa huko Kota Kinabalu, Malaysia. Tulikutana na wamisionari huko Hong Kong na kushiriki katika mkutano wakipekee wa kigingi na Watakatifu waaminifu, wanaojitolea kwa dhati.
Uzoefu huu ulijirudia tulipokutana na wamisionari na waumini kote Ulaya, Amerika ya Kilatini, Karibea na Afrika. Kanisa la Yesu Kristo linapitia ukuaji mkubwa barani Afrika.
Mimi ni shahidi wa kuona kwa macho juu ya urejesho unaoendelea wa injili ya Yesu Kristo na kutimia kwa unabii wa Joseph Smith kwamba “ukweli wa Mungu utaendelea kwa ujasiri, kwa uadilifu, na kwa uhuru, hadi utakapopenya kila bara, ufike kwenye kila tabia ya nchi, ufagie kila nchi, na kusikika katika kila sikio.”
Wamisionari wetu maridadi ambao wametapakaa ulimwenguni sasa ni 74,000. Wakifanya kazi pamoja na waumini, wanabatiza zaidi ya watu 20,000 kila mwezi. Hivi karibuni imekuwa ni vijana waume kwa wake wa miaka 18, 19 na 20 ambao, kwa msaada wa Bwana, wamezalisha muujiza huu mkubwa wa kukusanya. Tunawakuta vijana hawa wa kike na kiume katika vijiji vidogo vya Vanuatu na katika miji mikubwa ya New York, Paris na London. Nimewatazama wakifundisha kuhusu Mwokozi katika mikusanyiko ya mbali huko Fiji na mikusanyiko mikubwa katika maeneo kama Texas, California na Florida huko Marekani.
Utawakuta wamisionari katika kila pembe ya dunia wakizungumza lugha 60 tofauti na kutimiza agizo kuu la Mwokozi katika Mathayo 28: “Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu.” Ninawaheshimu wamisionari wa zamani na wa sasa wa Kanisa na kuwakumbusha kizazi chetu kinachoinukia juu ya mwaliko wa Rais Russell M. Nelson kuja na kuwakusanya Israeli.
Ninashuhudia leo kwamba nimeona urejesho huu wa kina wa injili ya Mwokozi kwa macho yangu mwenyewe na kuisikia kwa masikio yangu mwenyewe. Mimi ni shahidi wa kazi ya Mungu duniani kote. Hakujawahi kuwa na wakati mzuri wa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za mwisho kuliko leo.
Labda muujiza wa kuvutia zaidi wa urejesho ambao nimeshuhudia ni ninyi, waumini waaminifu wa Kanisa katika kila nchi. Ninyi, Watakatifu wa Siku za Mwisho, mnaelezewa na Nefi katika Kitabu cha Mormoni, kama alivyoona siku yetu na kushuhudia, “Na ikawa kwamba mimi, Nefi, niliona nguvu za Mwanakondoo wa Mungu, kwamba ziliwashukia watakatifu wa kanisa la Mwanakondoo, na juu ya watu wa agano wa Bwana, ambao walitawanyika kote usoni mwa dunia; na walikuwa wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu.”
Ninashuhudia kwamba nimeona kwa macho yangu mwenyewe kile ambacho Nefi alikiona—ninyi, Watakatifu wa agano katika kila nchi, mkiwa mmejihami kwa haki na nguvu za Mungu. Nilipokuwa kwenye mimbari katika moja ya mataifa haya makubwa ya ulimwengu, Bwana alisisitiza akilini mwangu jambo ambalo Mfalme Benjamini alifundisha katika Mosia 2 katika Kitabu cha Mormoni. Brent, “ningetamani mtafakari juu ya hali ya baraka na yenye furaha ya wale wanaotii amri za Mungu. Kwani tazama, wanabarikiwa katika vitu vyote, vya kimwili na vya kiroho.”
Ninashuhudia kwenu kwamba nimeona hili kwa macho yangu mwenyewe na kusikia kwa masikio yangu mwenyewe kama nilivyokutana nanyi, Watakatifu waaminifu wa Mungu duniani kote ambao mnazishika amri. Ninyi ni wana wa agano wa Baba. Ninyi ni wanafunzi wa Yesu Kristo. Ninyi pia mnajua kile ninachokijua kwa sababu mmepokea ushuhuda wenu binafsi wa ukweli juu ya injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Mwokozi alifundisha, “Heri macho yenu, kwa kuwa yanaona: na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.”
Chini ya maelekezo ya Bwana na uongozi wa manabii na mitume Wake tutaendelea kuwaandaa wamisionari, kufanya na kushika maagano matakatifu, kulikuza Kanisa la Kristo ulimwenguni kote na kupokea baraka ambazo zinakuja tunaposhika amri za Mungu. Sisi tumeungana. Sisi ni watoto wa Mungu. Tunamjua na Tunampenda.
Ninaungana nanyi nyote, marafiki zangu, tunaposhuhudia kwa umoja kwamba mambo haya ni ya kweli. Tunaweka ushahidi wa yale ambayo sote tumeona na kusikia. Mimi na wewe ni mashahidi tunao shuhudia. Ni kwa nguvu ya ushuhuda huu wa umoja kwamba tunaendelea kusonga mbele kwa imani katika Bwana Yesu Kristo na injili Yake. Ninatangaza ushahidi wangu kwamba Yesu Kristo yu hai. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.