Katika Kuunga Mkono Kizazi Kinachoinukia
Ni mahusiano katika maisha ya vijana ambayo yana ushawishi mkubwa katika chaguzi zao.
Katika kujiandaa kuzungumza nanyi, nimevutwa kwenye hadithi ya Helamani na wana vijana askari wa watu wa Amoni. Nimehisi uwezo wa manabii wa Kitabu cha Mormoni wakiwafundisha wazazi, maaskofu na washiriki wa kata kupitia kujifunza tukio hili.
Helamani alikuwa mtu ambaye vijana wa Waamoni wangeweza kumwamini. Aliwasaidia wakue na wakomae katika haki. Walimjua na kumpenda na “wangetaka [awe] kiongozi wao.”
Helamani aliwapenda vijana hawa kama wana na aliona uwezekano wao. Mzee Dale G. Renlund alifundisha kwamba “Ili kuwatumikia wengine vizuri lazima tuwaone … kupitia macho ya Baba wa Mbinguni. Ni hapo tu ndipo tunaweza kuelewa thamani halisi ya nafsi. Ni hapo tu ndipo tunaweza kuhisi upendo alionao Baba wa Mbinguni kwa ajili ya watoto Wake wote.” Maaskofu leo wamebarikiwa kwa utambuzi wa kuona utambulisho wa kiungu wa vijana walio chini ya uangalizi wao.
Helamani “aliwahesabu” vijana waliokuwa chini ya uangalizi wake. Aliweka kipaumbele cha kujenga nao mahusiano thabiti.
Katika wakati mgumu ambapo maisha na kifo vilining’inia katika usawa, Helamani na askari wake vijana walipoteza mwelekeo wa jeshi lililowafuatilia. Helamani alishauriana na vijana:
“Tazama, hatujui lakini wamesimama kwa kusudi kwamba tuje dhidi yao. …
“Basi mwasema nini wanangu … ?”
Vijana hawa waaminifu walijibu, “Baba, tazama, Mungu wetu yu pamoja nasi, wala hatatuacha tuanguke; basi twende zetu.” Siku ilikuwa ya ushindi, pale Helamani alipowaunga mkono vijana hawa katika azimio lao la kutenda.
Vijana wa Waamoni walikuwa na sababu kubwa na walikuwa hodari katika “kuwasaidia watu.” “Kikosi hiki kidogo,” kilichoongozwa na Helamani, kilieneza “matumaini makuu na furaha nyingi” ndani ya mioyo ya majeshi ya Wanefi wenye uzoefu. Maaskofu leo wanaweza kuwaongoza vijana wao wenye vipawa vya kipekee katika kuibariki kata na kuikusanya Israeli. Rais Russell M. Nelson amefundisha kwamba hii ndiyo “misheni ambayo kwayo [wao] walitumwa duniani.”
Kama vijana hawa wa Waamoni ambao walikuwa “wakweli siku zote katika jambo lolote walilokabidhiwa,” Helamani aliwafuata viongozi wake kwa uaminifu. Bila kujali changamoto au vikwazo, Helamani daima alibakia “imara kwenye dhamira” ili kuendeleza kusudi lao. Alipoagizwa “aende pamoja na wanawe wadogo,” alitii.
Vijana leo wanabarikiwa pale maaskofu wanapofuata mwongozo wa viongozi wetu wa “kushauriana na [marais] wa Wasichana wa kata.” Marais wa Vigingi, wanahakikisha kwamba maaskofu na marais wa Wasichana wamefunzwa katika kutimiza majukumu yao kwa vijana.
Helamani aliheshimu maagano. Wakati Amoni alipofundisha injili kwa wazazi wa wavulana askari, waliikumbatia kwa mioyo ya utayari. Walijitolea sana kwa maisha yao mapya ya uanafunzi wa haki kiasi kwamba walifanya agano la “kuweka chini silaha za uasi wao.” Kitu pekee ambacho kiliwafanya kufikiria kuvunja agano hili, kurudi kwenye maisha yao ya zamani ya mapigano, ilikuwa ni kuwaona Wanefi wakiwa hatarini.
Waamoni walitaka kuwasaidia watu hawa ambao walikuwa wamewapa makazi salama. Helamani, pamoja na wengine, waliwashawishi kutunza agano lao la kutopigana kamwe. Alitumaini zaidi katika nguvu ambazo Mungu angetoa kuliko nguvu ambazo Waamoni hawa wangeweza kutoa kwa panga na mishale yao.
Wakati Helamani na askari wake vijana walipokabiliwa na changamoto za kutisha, Helamani alibakia thabiti. “Tazama, haijalishi—tunaamini Mungu atatukomboa.” Katika tukio moja, wakiwa kwenye hatari ya kufa kwa njaa, jibu lao lilikuwa “kuzimimina nafsi [zao] katika maombi kwa Mungu, ili awatie nguvu na kuwakomboa … [na] Bwana … aliwatembelea [wao] kwa uhakikisho kwamba angewakomboa [wao]” “kwa sababu ya imani yao kuu katika yale ambayo walikuwa wamefundishwa kuamini.”
Tunajifunza kutoka kwa Helamani kwamba vijana hawa walisaidiwa na wazazi wao. Wazazi hao waaminifu walijua kwamba walikuwa na jukumu la msingi la kuwafundisha watoto wao. Waliwafundisha watoto wao kushika amri na “kuenenda kwa unyoofu” mbele za Mungu. Walikuwa wamefundishwa na mama zao kwamba kama wasingekuwa na shaka, Mungu angewaokoa.” Baba zao waliweka mifano mizuri ya kuingia kwenye maagano. Hawa askari wa zamani walijua mambo ya kutisha ya vita. Waliwakabidhi wana wao wasio na uzoefu kwenye uangalizi wa Helamani na kuwaunga mkono kwa kutuma “vyakula vingi.”
Helamani hakuwa peke yake alipotumikia jeshi lake la vijana. Alikuwa na watu karibu naye ambao aliwageukia kwa msaada na mwongozo. Alimfikia Kapteni Moroni kwa ajili ya msaada, na ulikuja.
Hakuna anayetumikia katika ufalme wa Bwana anayetumikia peke yake. Bwana ametubariki kwa kata na vigingi. Kupitia muundo Wake uliorejeshwa, tuna nyenzo, hekima na maongozi ya Mungu kukabiliana na changamoto yoyote.
Askofu husimamia kata kupitia mabaraza. Anahimiza usaili wa kila robo ya mwaka wa uhudumiaji na kisha kuwahimiza akidi ya wazee na Muungano wa Usaidizi kutimiza wajibu wao wa kuzihudumia familia. Urais huu huongoza katika kutathmini mahitaji na kutafuta suluhu zenye uvuvio. Marais wa vigingi wanatoa usaidizi kwa kuwaelekeza akidi ya wazee na urais wa Muungano wa Usaidizi katika majukumu haya.
Mwongozo unaohitajika kwa viongozi na wazazi unapatikana katika aplikesheni za Gospel Library na Gospel Living. Katika nyenzo hizi zenye uvuvio, tunaweza kupata maandiko, mafundisho ya manabii wa leo na Kitabu cha Maelezo ya Jumla. Kipengele cha vijana katika Gospel Library kina nyenzo nyingi za urais wa akidi na wa darasa na Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi. Washiriki wote wa kata wanapojifunza vyanzo hivi vyenye uvuvio na kutafuta mwongozo kutoka kwa Roho, kila mtu ataelekezwa na Bwana katika kuwaimarisha vijana.
Kata nzima itabarikiwa na kuimarishwa kadiri waumini wanavyofokasi kwenye kizazi kinachoinukia. Licha ya kutokamilika na mapungufu yetu, Baba wa Mbinguni anamwalika kila mmoja wetu, kupitia ushirika wa Roho Wake, kuwafikia wengine. Anajua kwamba tunakua na kutakaswa tunapofuata maongozi ya Roho Mtakatifu. Haijalishi kwamba juhudi zetu si kamilifu. Tunapokuwa na ubia na Bwana, tunaweza kuamini kwamba juhudi zetu zitakuwa sawa na kile ambacho Yeye angewafanyia vijana.
Kwa kufuata mwongozo wa Roho Mtakatifu katika kuwafikia vijana, tunakuwa mashahidi wa upendo wa Baba wa Mbinguni katika maisha yao. Kutendea kazi maongozi kutoka kwa Bwana hujenga mahusiano ya upendo na uaminifu. Ni mahusiano katika maisha ya vijana ambayo yana ushawishi mkubwa katika uchaguzi wao.
Vijana watajifunza mpangilio wa ufunuo wakati wanaposhiriki nasi katika mchakato wa kutafuta na kutenda kulingana na misukumo ya kuwatumikia wengine. Vijana wanapomgeukia Bwana kwa ajili ya mwongozo huu wenye uvuvio, mahusiano yao Kwake na tumaini lao Kwake vitaongezeka.
Tunadhihirisha imani yetu kwa vijana kwa kutoa msaada na mwongozo, bila kuchukua nafasi yao. Tunaporudi nyuma na kuwaruhusu vijana wajifunze kupitia kushauriana pamoja, kuchagua kozi kwa uvuvio na kuweka mpango wao katika vitendo, watapata furaha na ukuaji wa kweli.
Rais Henry B. Eyring alifundisha kwamba “kitakachokuwa muhimu zaidi ni kile wanachojifunza kutoka [kwenu] kuhusu wao ni akina nani hasa na kile hasa wanachoweza kuwa. Makisio yangu ni kwamba hawatajifunza mengi kuhusu hilo kutoka kwenye mihadhara. Watayapata kutokana na hisia za ninyi ni nani, mnadhani wao ni akina nani na vile mnavyodhani wanaweza kuwa.”
Vijana wetu wanatushangaza kwa ujasiri wao, imani yao na uwezo wao. Wanapochagua kuwa wanafunzi wanaoshiriki kikamilifu wa Yesu Kristo, injili Yake itawekwa kwenye mioyo yao. Kumfuata Yeye kutakuwa sehemu ya wao ni nani, siyo tu kile wanachokifanya.
Helamani aliwasaidia Waamoni vijana kuona jinsi mfuasi shujaa wa Yesu Kristo huishi. Tunaweza kuwa mifano yenye nguvu kwa vijana ya jinsi wanafunzi wa Kristo wanavyoishi leo. Wazazi waaminifu wanasali kwa ajili ya mifano hii katika maisha ya watoto wao. Hakuna programu inayoweza kuchukua nafasi ya ushawishi wa watu wazima wenye upendo, wanaoshika maagano.
Kama rais wa akidi ya makuhani, askofu anaweza kuweka mfano kwa vijana wa jinsi ya kuwa mume mwaminifu na baba mwenye upendo kwa kulinda, kutoa mahitaji na kuongoza kwa njia za haki. Maaskofu, wenye “fokasi imara [kwa] vijana,” watakuwa na ushawishi utakaodumu kwa vizazi.
Vijana leo ni miongoni mwa roho za thamani zaidi za Baba wa Mbinguni. Walikuwa miongoni mwa watetezi hodari wa ukweli na haki ya kujiamulia katika ulimwengu wa kabla ya kuja duniani. Walizaliwa katika siku hizi kuikusanya Israeli kupitia ushuhuda wao wenye nguvu wa Bwana Yesu Kristo. Yeye anamjua kila mmoja wao na anajua uwezekano wao mkubwa. Yeye ni mvumilivu kadiri wanavyokua. Yeye atawakomboa na kuwalinda. Yeye atawaponya na kuwaongoza. Yeye atawatia moyo. Sisi, wazazi na viongozi wao, tumejitayarisha kuwaunga mkono. Tunalo Kanisa la Mwokozi la kutusaidia tunapokilea kizazi kijacho.
Ninatoa ushahidi kwamba Kanisa la Kristo, lililorejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith na kuongozwa leo na Rais Russell M. Nelson, limepangwa ili kuwasaidia vijana watimize kusudi lao kuu katika siku hizi za mwisho. Katika jina la Yesu Kristo, amina.