Muunganiko Wenye Nguvu, Mtakatifu wa Mafundisho ya Kristo
Ninawaalika kuishi mafundisho ya Kristo kwa kurudia na kuyatumia kwa kujirudia na kwa ari na kuwasaidia wengine kwenye njia yao.
Miaka kadhaa iliyopita, mimi, mke wangu, Ruth; na binti yetu, Ashley tuliungana pamoja na watalii wengine kwenye safari ya mtumbwi huko eneo la Hawaii Marekani. Mtumbwi huwa karibu sana na maji, ni kama boti ambayo mpiga kasia hukaa akielekea mbele na hutumia kasia kusukuma kutokea mbele kuelekea nyuma kwa upande mmoja na kisha upande mwingine. Mpango ulikuwa ni kuelekea kwenye visiwa viwili vidogo kwenye ufuko wa Oahu na kisha kurudi. Nilikuwa sina wasiwasi kwa sababu, kama mvulana, nilikuwa nimeendesha mitumbwi kupita milima na maziwa. Kujiamini kupita kiasi hakuleti matokeo mazuri, sivyo?
Mwongozaji wetu alitupatia maelekezo na kutuonyesha mitumbwi ambayo tungetumia. Ilikuwa tofauti na ile ambayo niliwahi kuiendesha. Nilitakiwa kukaa juu ya mtumbwi, badala ya ndani yake. Nilipofika kwenye mtumbwi, uwiano wa msawazo wangu ulikuwa mkubwa kuliko nilivyokuwa nimezoea, na sikuwa thabiti majini.
Wakati tukianza kuondoka, nilipiga kasia kwa haraka zaidi ya Ruth na Ashley. Baada ya muda, nilikuwa mbali mbele yao. Ingawa nilikuwa na furaha kwa uharaka wangu, niliacha kupiga kasia na kuwasubiri wanifikie. Wimbi kubwa—kiasi cha sentimita 13—lilipiga upande wa mtumbwi na kunibinua kuelekea majini. Wakati nilipoweza kurudisha mtumbwi vizuri na nikihangaika kurudi juu yake, Ruth na Ashley walikuwa wameshanipita, lakini nilipata tabu kupumua ili kurudi kwenye kupiga kasia. Kabla sijaweza kupumua vizuri, wimbi lingine, hili likiwa kubwa sana—angalau sentimita 20—lilipiga mtumbwi wangu na kunibinua tena. Wakati nilipofanikisha kuuweka mtumbwi wangu sawia, nilikuwa nimeishiwa pumzi kiasi kwamba niliogopa nisingeweza kupanda juu yake.
Akiiona hali yangu, mwongozaji alipiga kasia na kuuweka mtumbwi wangu sawia, akifanya iwe rahisi kwangu kupanda juu yake. Wakati alipoona kwamba nilikuwa bado sina pumzi ya kuweza kupiga kasia mwenyewe, alifunga kamba kwenye mtumbwi wangu na kuanza kupiga kasia, akinivuta pamoja naye. Punde niliweza kupata pumzi na kuanza kupiga kasia sawasawa mimi mwenyewe. Alitoa kamba, na nilifika kwenye kisiwa cha kwanza bila msaada wa ziada. Nilipofika, nililala mchangani, nikiwa nimechoka.
Baada ya kundi kupumzika, mwongozaji taratibu aliniambia, “Bwana Renlund, kama tu utaendelea kupiga kasia, usipunguze ujongeaji, nadhani utakuwa sawa.” Nilifuata ushauri wake wakati tukipiga kasia kuelekea kisiwa cha pili na kisha wakati tukirudi sehemu tuliyoanzia. Mara mbili, mwongozaji alipiga kasia karibu nami na kuniambia nilikuwa nikifanya vyema. Hata mawimbi makubwa zaidi yalipiga upande wa mtumbwi wangu, lakini sikuangushwa.
Kwa kuendelea kupiga kasia, niliimarisha kasi na kuendelea mbele, nikishinda matokeo ya mawimbi yaliyopiga upande wangu. Kanuni sawa na hiyo hutumika kwenye maisha yetu ya kiroho. Tunakuwa kwenye hatari wakati tunapopunguza kasi na hasa wakati tunaposimama. Kama tutaendeleza kasi ya kiroho kwa kuendelea “kupiga kasia” kuelekea kwa Mwokozi, tuko salama zaidi na wenye ulinzi zaidi kwa sababu maisha yetu ya milele hutegemea imani yetu Kwake.
Kasi ya kiroho hujengwa “kwa maisha yote wakati kwa kurudia tunakumbatia mafundisho ya Kristo.” Kufanya hivyo, Rais Russell M. Nelson alifundisha, hutengeneza “Muunganiko wenye nguvu.” Ndio, yaliyomo kwenye mafundisho ya Kristo—kama vile imani katika Bwana Yesu Kristo, toba, kuingia kwenye uhusiano wa kimaagano na Bwana kupitia ubatizo, kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu na kuvumilia hadi mwisho—havikusudiwi kutoa uzoefu wa mara moja, kama matukio ya kuweka alma kwenye visanduku. Hususan, “kuvumilia hadi mwisho” kiuhalisia si hatua ya peke yake kwenye mafundisho ya Kristo—kwamba tunamaliza hatua nne za awali na kisha kuchuchumaa chini, kuuma meno yetu na kusubiri kufa. Hapana, kuvumilia hadi mwisho ni ya kujirudia na hutumika kwa kujirudia kwenye vipengele vingine vya mafundisho ya Kristo, hutengeneza “muunganiko wenye nguvu” ambao Rais Nelson aliufafanua.
Kwa kujirudia humaanisha kwamba tunapitia vipengele vya mafundisho ya Kristo tena na tena maishani mwetu. Kwa kurudia humaanisha kwamba tunajenga juu ya, na kuimarisha kila urudiaji. Ingawa tunarudia vipengele, hatuzunguki tu katika duara bila kuwa na mwelekeo wa mbele. Badala yake, tunasonga karibu zaidi na Yesu Kristo kila mara kupitia mzunguko huo.
Kasi hujumuisha vyote spidi na mwelekeo. Kama ningepiga kasia kwa ari kuelekea upande usio sahihi, ningeweza kutengeneza Kasi, lakini nisingefika sehemu iliyokusudiwa. Vivyo hivyo, katika maisha, tunahitaji “kupiga kasia” kuelekea kwa Mwokozi ili twende Kwake.
Imani yetu katika Yesu Kristo inahitaji kulishwa kila siku. Hulishwa wakati tunaposali kila siku, kusoma maandiko kila siku, kutafakari juu ya utakatifu wa Mungu kila siku, kutubu kila siku na kufuata misukumo ya Roho Mtakatifu kila siku. Kama ambavyo si vizuri kiafya kuahirisha kula chakula chetu chote mpaka Jumapili halafu kuleta mkusanyiko wote wa virutubisho vya wiki nzima, si vizuri kiroho kuwa na tabia ya kulisha ushuhuda kwa siku moja ndani ya wiki.
Wakati tunapowajibika kwa ajili ya shuhuda zetu wenyewe, tunapata kasi ya kiroho na taratibu kutengeneza mwamba wa imani katika Yesu Kristo, na mafundisho ya Kristo huwa kiini cha dhumuni la maisha. Kasi pia hujengeka wakati tunapojitahidi kutii sheria za Mungu na kutubu. Toba ni furaha na huturuhusu kujifunza kutokana na makosa yetu, ambapo ndivyo tunavyopata ukuaji wa milele. Bila shaka tutakuwa na nyakati ambapo tutadondoka kutoka kwenye mtumbwi na kujikuta kwenye maji ya kina kirefu. Kupitia toba, tunaweza kurudi kwenye mtumbwi na kuendelea, bila kujali ni mara ngapi tumedondoka. Cha muhimu ni kwamba hatukati tamaa.
kipengele kinachofuata katika mafundisho ya Kristo ni ubatizo, ambao unajumuisha ubatizo kwa maji na, kupitia uthibitisho, ubatizo wa Roho Mtakatifu. Wakati ubatizo ni tukio moja, tunafanya upya kwa kurudia agano la ubatizo wakati tunaposhiriki sakramenti. Sakramenti haichukui nafasi ya ubatizo, lakini huunganisha vipengele vya awali vya mafundisho ya Kristo—imani na toba—kwenye upokeaji wa Roho Mtakatifu Wakati kwa uendelevu tunashiriki sakramanti, tunamwalika Roho Mtakatifu maishani mwetu, sawa na vile wakati tulipobatizwa na kuthibitishwa. Wakati tunaposhika agano linaloelezewa kwenye sala ya sakramenti, Roho Mtakatifu huwa mwenza wetu.
Wakati Roho Mtakatifu akitumia ushawishi mkubwa kwenye maisha yetu, kwa ukuaji na urudiaji tunatengeneza tabia kama za Kristo. Mioyo yetu hubadilika. Hamu yetu ya kutenda uovu hupungua. Hamu yetu ya kutenda wema huongezeka mpaka “kutaka kutenda mema daima.” Na kisha tunafikia nguvu za mbinguni zinazohitajika ili kuvumilia hadi mwisho. Imani yetu imeongezeka, na tuko tayari kurudia tena muunganiko wenye nguvu.
Kasi ya kiroho ya kusonga mbele pia hutusukuma kufanya maagano ya ziada na Mungu ndani ya nyumba ya Bwana. Maagano mengi hutusogeza karibu na Kristo na kutuunganisha kwa nguvu zaidi na Yeye. Kupitia maagano haya, tuna ufikiaji mkubwa wa nguvu Zake. Ili kuwa wazi, maagano ya ubatizo na ya hekaluni, siyo ndani yake au kwa yenyewe, chanzo cha nguvu. Chanzo cha nguvu ni Bwana Yesu Kristo na Baba yetu wa Mbinguni. Kufanya na kushika maagano hujenga njia kwa ajili ya nguvu Zao katika maisha yetu. Kadiri tunavyoishi kulingana na maagano haya, hatimaye tunakuwa warithi wa vyote ambavyo Baba wa Mbinguni anavyo. Kasi inayozalishwa kwa kuishi mafundisho ya Kristo si tu hutoa nguvu kwa ajili ya badiliko la asili yetu ya kiungu kuwa hatma yetu ya milele, bali pia hutuhamasisha kuwasaidia wengine katika njia zifaazo.
Fikiria kuhusu muongozaji alivyonisaidia wakati nilipodondoka kutoka kwenye mtumbwi wangu. Hakupaza sauti kutokea mbali kwa swali lisilo la msaada kama vile, “Bwana Renlund, unafanya nini majini?” Hakupiga kasia na kunikaripia, akisema, “bwana Renlund, usingekuwa kwenye hali hii kama ungekuwa uko sawa kimwili.” Hakuanza kuvuta mtumbwi wangu wakati nikijaribu kukaa juu ya mtumbwi. Na hakunisahihisha mbele ya kundi la watu. Badala yake, alinipa usaidizi niliouhitaji wakati nilipouhitaji. Alinipa ushauri wakati nilipokuwa mpokeaji. Na alienda mbali zaidi kwa kunitia moyo.
Wakati tunapowahudumia wengine, hatuhitaji kuuliza maswali yasiyo ya msaada au kunena mambo ambayo ni ya kawaida. Watu wengi ambao wana changamoto wanajua kwamba wana changamoto. Hutupaswi kuwahukumu; hukumu yetu haisaidii au kukaribisha na mara nyingi huwa yenye madhara.
Kujilinganisha na wengine kunaweza kutusababishia kufanya makosa yenye madhara, hasa pale tunapohitimisha kwamba sisi tu wastahili sana kuliko wale wanaopitia changamoto. Ulinganishaji huu ni kama kuzama bila kuwa na tumaini kwenye kina cha mita tatu majini, huku ukimuona mtu mwingine akizama kwenye kina cha mita nne maji, ukimhukumu yeye kuwa mtenda dhambi mkubwa, na wewe kujihisi vizuri kuhusu nafsi yako. Zaidi ya yote, sisi sote tunahangaika katika njia zetu wenyewe. Hakuna yoyote kati yetu anayepata wokovu kwa matendo tu. Kamwe hatuwezi. Yakobo, kwenye Kitabu cha Mormoni, alifundisha, “kumbukeni, baada ya [sisi] kupatanishwa na Mungu, kwamba ni kwa kupitia neema ya Mungu pekee [sisi] tunaokolewa.” Sote tunahitaji Upatanisho usio na mwisho wa Mwokozi, na si sehemu tu.
Tunahitaji huruma yetu yote, faraja na upendo wakati tukichangamana na wale wanaotuzunguka. Wale wanaopitia changamoto “wanahitaji kupata upendo msafi wa Yesu Kristo unaoakisiwa katika maneno na matendo [yetu].” Wakati tunapohudumu, tuwatie moyo wengine mara kwa mara na kutoa msaada. Hata kama mtu fulani si mpokeaji, tunaendelea kuwahudumia kadiri wanavyoruhusu. Bwana alifundisha “kwani kwa hawa mtaendelea kuwahudumia; kwani hamjui kama watarudi na kutubu, na kuja kwangu kwa moyo wa lengo moja, na nitawaponya; na ndipo mtakuwa njia ya kuwaletea wokovu.” Kazi ya Mwokozi ni kuponya. Kazi yetu ni kupenda—kupenda na kuhudumia katika njia ambayo wengine wanavutwa karibu na Yesu Kristo. Hii ni mojawapo ya matunda yenye nguvu, muunganiko wenye nguvu wa mafundisho ya Kristo.
Ninawaalika kuyaishi kwa kurudia mafundisho ya Kristo na kuyatumia kwa kujirudia na kuwasaidia wengine kwenye njia yao. Ninashuhudia kwamba mafundisho ya Kristo ni kiini cha mpango wa Baba wa Mbinguni; hata hivyo, ni mafundisho Yake. Tunapotumia imani katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake, tunapata nguvu kwenye njia ya agano na kutiwa moyo kuwasaidia wengine wawe wafuasi waaminifu wa Yesu Kristo. Tunaweza kuwa warithi katika ufalme wa Baba wa Mbinguni, ambapo ni kilele cha kuishi mafundisho ya Kristo. Katika jina la Yesu Kristo, amina.