Mkutano Mkuu
Ni Hekima ya Bwana Kwamba Tuwe na Kitabu cha Mormoni
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Ni Hekima ya Bwana Kwamba Tuwe na Kitabu cha Mormoni

Ni sala yangu kwamba usomaji wa kitabu cha Mormoni mwaka huu utakuwa ni shangwe na baraka kwa kila mmoja wetu.

Wapendwa akina kaka na dada, tuna shukrani kwa sababu ya juhudi zenu katika kusoma maandiko pamoja na Njoo, Unifuate. Asanteni kwa yote mfanyayo. Muunganiko wenu wa kila siku na Mungu na neno Lake una matokeo ya kustaajabisha. “Mnajenga msingi wa kazi kubwa. Na kutokana na mambo madogo huja yale yaliyo makuu.”

Kusoma mafundisho ya Mwokozi kwenye maandiko hutusaidia kubadili nyumba zetu kuwa mahali patakatifu pa imani na kitovu cha kujifunza injili. Humwaliko Roho nyumbani kwetu. Roho Mtakatifu huzijaza nafsi zetu kwa shangwe na hutuongoa kuwa wanafunzi wa maisha yote wa Yesu Kristo.

Kwa miaka hii kadhaa iliyopita, wakati tukisoma vitabu vya maandiko matakatifu, tumegundua ukubwa wa mafundisho ya Mungu kwa watoto Wake katika vipindi vyote vikuu vya injili.

Katika kila kipindi cha uwepo wa injili, tumeona mfumo sawa na huo. Mungu hurejesha au kufunua injili ya Yesu Kristo kupitia manabii Wake. Watu humfuata nabii na hubarikiwa sana. Hata hivyo, baada ya muda, baadhi ya watu huacha kutii maneno ya nabii na hujitenga kutoka kwa Bwana na injili Yake. Hiki ndicho tunakiita ukengeufu. Injili ilifunuliwa kwanza kwa Adamu, lakini baadhi ya watoto wa Adamu na Hawa waligeuka kutoka kwa Bwana kwa ukengeufu. Tunaona mfumo wa urejesho na ukengeufu ukijirudia katika kipindi cha Henoko, Nuhu, Ibrahamu, Musa na wengine.

Sasa, leo, tunaishi katika kipindi cha utimilifu wa nyakati. Hiki ndicho kipindi pekee cha uwepo wa injili ambacho hakitaishia kwenye ukengeufu. Ni kipindi hiki ambacho kitakaribisha Ujio wa Pili wa Mwokozi Yesu Kristo na utawala Wake wa milenia.

Hivyo, kipi ni tofauti kuhusu kipindi hiki? Ni kipi ambacho Bwana amekitoa kwetu leo, hasa kwa ajili ya wakati wetu, ambacho kitatusaidia kusonga karibu na Mwokozi na kamwe Kutomwacha?

Jibu moja ambalo huja akilini mwangu ni maandiko—na hususani Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo.

Wakati Mungu ameahidi kwamba hakutakuwa na ukengeufu mwingine wa jumla tunahitaji kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari kuepuka ukengeufu binafsi—tukikumbuka, kama Rais Russell M. Nelson ambavyo amefundisha, “Sote tunawajibika kwa ajili ya ukuaji wetu binafsi wa kiroho.” Kujifunza Kitabu cha Mormoni, kama tunavyofanya mwaka huu, mara zote hutusogeza karibu na Mwokozi—na hutusaidia kubakia karibu Naye.

Tunaita “kujifunza” na hii ni vizuri kwa sababu huashiria juhudi. Lakini si mara zote tunahitaji kujifunza ukweli mpya. Wakati mwingine kusoma Kitabu cha Mormoni ni kuhusu kuhisi kuunganishwa na Mungu leo—kulisha nafsi zetu, kuimarishwa kiroho kabla ya kwenda kukabiliana na ulimwengu au kutafuta uponyaji baada ya siku yenye changamoto ulimwenguni.

Tunajifunza maandiko ili kwamba Roho Mtakatifu, mwalimu mkuu, aweze kukuza uongofu wetu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na kutusaidia kuwa kama Wao.

Kwa mawazo haya akilini, tungeweza kuzingatia “Ni kipi Roho Mtakatifu alitufundisha wiki hii wakati wa usomaji wetu wa Kitabu cha Mormoni?” na “Hili linatusogeza vipi karibu na Mwokozi?”

Haya ni maswali mazuri kwa ajili ya kujifunza kwetu maandiko nyumbani. Pia ni maswali bora zaidi ya kuanza darasa la Jumapili kanisani. Tunaboresha ufundishaji wetu kanisani Jumapili kwa kuboresha kujifunza kwetu nyumbani katikati ya wiki. Hivyo basi, katika madarasa ya Jumapili, “yule ambaye huhubiri na yule apokeaye, huelewana, na wote hujengana na kufurahi kwa pamoja.”

Hapa kuna mistari michache ambayo Roho amesisitiza mawazoni mwangu kutoka kwenye usomaji wa Kitabu cha Mormoni wiki hii:

  • Nefi anamwamuru Yakobo “kuhifadhi bamba hizi na kupokezana … kutoka kizazi hadi kizazi. Na kama kulikuwa na mahubiri yaliyo matakatifu, au ufunuo … , au unabii,” Yakobo hana budi “kuyachora … katika bamba hizi … kwa faida ya watu [wao].”

  • Yakobo baadaye alishuhudia, “Tunachunguza [maandiko], … na pamoja na mashahidi hawa wote tunapokea tumaini, na imani yetu haiwezi kutingishwa.”

Sasa mistari hii ilinisababisha kukumbuka ambacho Nefi alikisema awali kuhusu bamba za shaba:

“Na tulikuwa tumepata yale maandishi … na kuyachunguza na tukagundua kwamba yalikuwa … yenye thamani kubwa kwetu sisi, kwani tungeweza kuhifadhi amri za Bwana na kuwapa watoto wetu.

“Kwa hivyo, ilikuwa ni hekima katika Bwana kwamba tuyabebe tulipokuwa tukisafiri nyikani tukielekea nchi ya ahadi.”

Sasa, kama ilikuwa ni hekima kwa Lehi na familia yake kuwa na maandiko, vivyo hivyo ni hekima kwetu hivi leo. Thamani kuu na nguvu za kiroho za maandiko huendelea bila kukoma katika maisha yetu leo.

Hakujawahi kuwa na watu katika historia wenye Kitabu cha Mormoni na maandiko mengine ambayo tunayafurahia kama ilivyo sasa. Ndio, Lehi na familia yake walibarikiwa kubeba mabamba ya shaba pamoja nao, lakini hawakuwa na nakala kwa ajili ya kila hema. Nakala muhimu zaidi ya Kitabu cha Mormoni ni nakala yetu. Ni nakala ambayo tunaisoma.

Katika ono la Lehi la mti wa uzima, Lehi alitufundisha umuhimu wa uzoefu binafsi wa upendo wa Mungu. Baada ya kuwa amekula tunda, Lehi aliwaona mke wake, Saria na wana wake Nefi na Samu kwa mbali.

“Walisimama wakawa kama hawajui wanapoenda.

“… Niliwapungia mkono,” Lehi anasema , “na pia kwa sauti kubwa nikawaambia wanikaribie, na wale tunda, ambalo lilikuwa la kupendeza zaidi kuliko tunda lingine.

“Na … ikawa kwamba walinikaribia na kula tunda pia.”

Ninapenda mfano wa Lehi wa mzazi mwenye kujali. Saria, Nefi na Samu walikuwa wakiishi vizuri, maisha ya haki. Lakini Bwana alikuwa na kitu kizuri zaidi, kitu kitamu zaidi kwa ajili yao. Hawakujua wapi pa kukipata, lakini Lehi alijua. Hivyo, aliwaita “kwa sauti kubwa” kwenda katika mti wa uzima na kula tunda wao wenyewe. Uelekezi wake ulikuwa dhahiri. Kusingekuwepo na kutoeleweka.

Mimi ni zao la malezi sawa na hayo. Wakati nilipokuwa mvulana, kama miaka 11 au 12, mama yangu aliniuliza “Mark, je, unajua wewe mwenyewe, kwa kupitia Roho Mtakatifu, kwamba injili ni ya kweli?”

Swali lake lilinishangaza. Mara zote nilijitahidi kuwa “mvulana mzuri,” na nilifikiri hiyo ilitosha. Lakini mama yangu, kama Lehi, alijua kwamba kitu fulani zaidi kilihitajika. Nilihitajika kutenda na kujua mimi mwenyewe.

Nilijibu kwamba sikuwa nimewahi kuwa na uzoefu huo. Hakuonekana kushangazwa kabisa na jibu langu.

Kisha alisema kitu ambacho sijawahi kukisahau. Ninakumbuka maneno yake mpaka leo: “Baba wa Mbinguni anataka wewe mwenyewe ujue. Lakini lazima uweke juhudi. Unahitaji kusoma Kitabu cha Mormoni na kusali ili kujua kupitia Roho Mtakatifu. Baba wa Mbinguni atajibu sala zako.”

Kweli, sikuwa nimewahi kusoma Kitabu cha Mormoni. Nilidhani sikuwa mkubwa vya kutosha kufanya hivyo. Lakini mama yangu alijua vyema zaidi.

Swali lake liliweka hamu ndani yangu ya kujua mimi mwenyewe.

Hivyo, kila usiku, kwenye chumba ambacho mimi na kaka zangu wawili tulitumia, niliwasha taa iliyo juu ya kitanda changu na kusoma mlango mmoja kwenye Kitabu cha Mormoni. Kisha, baada ya kuzima taa, nilipiga magoti na kusali. Nilisali kwa dhati zaidi na kwa hamu kubwa kuliko nilivyowahi kufanya. Nilimuomba Baba wa Mbinguni kwamba aniwezeshe kujua ukweli wa Kitabu cha Mormoni.

Tangu nilipoanza kusoma Kitabu cha Mormoni, nilihisi kwamba Baba wa Mbinguni alikuwa akijua juhudi zangu. Na nilihisi nilikuwa wa thamani Kwake. Wakati nikisoma na kusali, hisia nzuri, za amani zilikuwa nami. Kutoka mlango mmoja hadi mwingine, mwanga wa imani ulikuwa uking’aa zaidi na zaidi ndani ya nafsi yangu. Baada ya muda, nilitambua kwamba hisia hizo zilikuwa uthibitisho wa ukweli kutoka kwa Roho Mtakatifu. Nilikuja kujua mimi mwenyewe kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli na kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wa ulimwengu. Nina shukrani jinsi gani kwa mwaliko mkunjufu wa mama yangu.

Uzoefu huu wa kusoma Kitabu cha Mormoni kama mvulana ulianzisha mfumo wa kujifunza maandiko ambao unaendelea kunibariki leo hii. Bado ninasoma Kitabu cha Mormoni na kupiga magoti kusali. Na Roho Mtakatifu huthibitisha ukweli wake tena na tena.

Nefi alisema kwa usahihi. Ilikuwa ni hekima katika Bwana kwamba sisi tubebe maandiko pamoja nasi maishani mwetu mwote. Kitabu cha Mormoni ni “jiwe la katikati la tao” ambacho hufanya wakati huu wa uwepo wa injili kuwa wa utofauti na nyakati zingine zilizopita. Wakati tunapojifunza Kitabu cha Mormoni na kumfuata nabii, hakutakuwa na ukengeufu binafsi katika maisha yetu.

Mwaliko wa kwenda kwenye mti wa uzima kwa kushikilia kwa nguvu neno la Mungu si tu mwaliko kutoka kwa Lehi kwenda kwa familia yake, na si tu mwaliko kutoka kwa mama kuja kwangu wa kusoma na kusali kuhusu Kitabu cha Mormoni. Ni mwaliko pia kutoka kwa nabii wetu, Rais Russell M. Nelson, kwenda kwa kila mmoja wetu.

“Ninaahidi” alisema “kwamba unapojifunza kwa sala Kitabu cha Mormoni kila siku, utafanya maamuzi mazuri zaidi—kila siku. Ninaahidi kwamba mnapotafakari kile mnachojifunza, madirisha ya mbinguni yatafunguka, na mtapata majibu ya maswali yenu na mwongozo kwa ajili ya maisha yenu.”

Ni sala yangu kwamba usomaji wa kitabu cha Mormoni mwaka huu utakuwa ni shangwe na baraka kwa kila mmoja wetu na utatusogeza zaidi kwa Mwokozi.

Baba wa Mbinguni anaishi. Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Kitabu cha Mormoni kinabeba maneno na upendo Wake. Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Bwana duniani leo. Ninajua vitu hivi kuwa vya kweli kwa sababu ya ushahidi wa Roho Mtakatifu, ushahidi ambao kwanza niliupokea wakati nikisoma Kitabu cha Mormoni kama mvulana. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mafundisho na Maagano 64:33.

  2. “Mtaala mpya unaolenga nyumbani, unaosaidiwa na Kanisa na uliofanywa sawa una uwezo wa kufungulia nguvu za familia, pale kila familia inapofuatilia kwa makini na uangalifu ili kubadilisha nyumba zao kuwa kimbilio la imani. Ninakuahidi ya kwamba utakapofanya bidii kupanga upya nyumba yako kuwa kituo cha kujifunza injili, baada ya muda Siku zako za Sabato zitakuwa takatifu sana. Watoto.wako watafurahia kujifunza na kuishi mafundisho ya Mwokozi, na ushawishi wa adui katika maisha yako na katika nyumba yako utapungua. Mabadiliko katika familia yako yatakuwa ya kuvutia na endelevu” (Russell M. Nelson, “Kuwa Mtakatifu wa Siku za Mwisho wa Mfano,” Liahona, Nov. 2018, 113).

  3. “Amini, amini ninakuambia, nitakupa Roho wangu, ambaye ataiangaza akili yako, ambayo itaijaza nafsi yako kwa shangwe” (Mafundisho na Maagano 11:13).

  4. “Wakati wa uwepo wa injili ya kweli ni Kipindi ambacho Bwana angalau ana mtumishi mmoja aliyeidhinishwa duniani mwenye mamlaka ya ukuhani mtakatifu na funguo, na mwenye jukumu tukufu la kueneza injili kwa wakazi wa dunia” (Topics and Questions, “Dispensations,” Gospel Library).

  5. Ona Musa 5:12–16.

  6. Nabii Danieli aliona siku zetu, kipindi cha uwepo wa injili ya kweli, wakati alipotoa tafsiri ya ndoto ya Nebukadneza. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu Wa Siku za Mwisho ni jiwe katika ndoto ile, likichongwa bila kazi ya mikono, likiviringika na kuijaza dunia (ona Danieli 2:34–35, 44–45; Mafundisho na Maagano 65:2).

  7. “Mungu Baba na Yesu Kristo walimwita Nabii Joseph Smith kuwa nabii wa kipindi hiki. Nguvu zote za kiungu za vipindi vilivyopita zilikuwa zirejeshwe kupitia Yeye. Kipindi hiki cha utimilifu wa nyakati hakitakuwa na kikomo katika muda au eneo. Hakitaishia katika ukengeufu, na kitaijaza dunia” (Russell M. Nelson, “The Gathering of Scattered Israel,” Liahona, Nov. 2006, 79–80).

  8. Russell M. Nelson, “Maneno ya Ufunguzi,” Liahona, Nov. 2018, 8.

  9. Ona “Uongofu Ndiyo Lengo Letu,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024, v.

  10. Mafundisho na Maagano 50:22; ona pia mistari ya 17–21.

  11. Yakobo 1:3–4.

  12. Yakobo 4:6.

  13. 1 Nefi 5:21–22.

  14. Ilitangazwa hivi karibuni kwamba nakala milioni 200 za Kitabu cha Mormoni zimesambazwa katika kipindi hiki. Hii ni ya kushangaza. Kitabu cha Mormoni sasa kimetafsiriwa katika lugha 113, kukiwa na lugha 17 za tafsiri mpya zikiwa kwenye mchakato. Ni baraka iliyoje ya kuwa na Kitabu cha Mormoni kilichochapishwa, cha kidijitali, kwa sauti, video na mifumo mingine. (Ona Ryan Jensen, “Church Distributes 200 Millionth Copy of the Book of Mormon,” Church News, Dec. 29, 2023, thechurchnews.com.)

  15. 1 Nefi 8:14–16; msisitizo umeongezwa.

  16. “Ushawishi wa kiroho wenye nguvu zaidi katika maisha ya mtoto ni mfano wa uadilifu wa wazazi na bibi na babu wenye upendo ambao kwa uaminifu hushika maagano yao matakatifu. Wazazi wenye kusudi huwafunza watoto wao imani katika Bwana Yesu Kristo ili kwamba watoto pia ‘wajue asili ya kutegemea msamaha wa dhambi zao’ [2 Nefi 25:26]. Ushikaji wa maagano wa kawaida na usio endelevu huongoza kwenye kujeruhiwa kiroho. Hasara ya kiroho mara zote ni kubwa kwa watoto na wajukuu zetu” (Kevin W. Pearson, “Are You Still Willing?,” Liahona, Nov. 2022, 69).

  17. Ona Mafundisho na Maagano 6:22 –24.

  18. Nabii Joseph Smith alisema: “Niliwaambia ndugu kwamba Kitabu cha Mormoni ndicho kitabu sahihi duniani, na ndicho jiwe la katikati la tao la dini yetu, na kuwa mwanadamu angemkaribia Mungu zaidi kwa kufuata mafunzo yake, zaidi ya kitabu kingine” (kweye dibaji ya Kitabu cha Mormoni).

  19. Russell M. Nelson, “Kitabu cha Mormoni: Maisha Yako Yangekuwaje Bila Hicho?Liahona, Nov. 2017, 62–63.

Chapisha