Miujiza, Malaika na Nguvu za Ukuhani
Kama unatamani baraka za ukuhani, ikijumuisha miujiza na huduma ya malaika,tembea kwenye njia ya maagano ambayo Mungu ameiweka.
Wengi leo husema miujiza imekoma, kwamba malaika ni wa kufikirika, na kwamba mbingu zimefungwa. Nashuhudia kwamba miujiza haijakoma, malaika wapo miongoni mwetu, na mbingu hakika zipo wazi.
Wakati Mwokozi wetu, Yesu Kristo alipokuwa duniani, alitoa funguo za ukuhani kwa Mtume Wake Mkuu, Petro. Kupitia funguo hizi, Petro na Mitume wengine waliliongoza Kanisa la Mwokozi. Lakini wakati Mitume hao walipofariki, funguo za ukuhani zilichukuliwa kutoka duniani.
Ninashuhudia kwamba funguo za kale za ukuhani zimerejeshwa. Petro,Yakobo na Yohana na manabii wengine wa kale walitokea kama viumbe waliofufuka, wakimpa nabii Joseph Smith kile Bwana alichokielezea kama “funguo za ufalme wangu, na kipindi maalumu cha injili.”
Funguo hizo hizo zimetolewa kutoka kwa nabii mmoja hadi mwingine mpaka hivi leo. Wanaume 15 tunaowakubali kama manabii, waonaji na wafunuzi huzitumia kuliongoza Kanisa la Mwokozi. Kama vile nyakati za kale, kuna Mtume mmoja mwandamizi anayeshikilia na kuruhusu kutumika kwa funguo zote za ukuhani. Ni Rais Russell M.Nelson, nabii na Rais wa Kanisa lililorejeshwa katika siku yetu: Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Kupitia Kanisa la Mwokozi, tunapokea baraka za ukuhani—ikiwa ni pamoja na nguvu za Mungu ili kutusaidia katika maisha yetu. Chini ya funguo za ukuhani zilizoruhusiwa, tunaweka ahadi takatifu kwa Mungu na kupokea ibada takatifu ambazo hutuandaa kuishi katika uwepo Wake. Tunaanza na ubatizo na uthibitisho na kisha katika hekalu, tunasonga mbele katika njia ya maagano ambayo hutuongoza turudi Kwake.
Mikono ikiwekwa kwenye vichwa vyetu, pia tunapokea baraka za ukuhani, ikiwa ni pamoja na mwongozo, faraja, ushauri, uponyaji, na nguvu za kumfuata Yesu Kristo Katika maisha yangu yote, nimebarikiwa kwa nguvu hii kuu. Kama ilivyofunuliwa katika maandiko, tunairejelea hii kama nguvu ya Ukuhani mtakatifu wa Melkizedeki.
Katika ujana wangu nilipata kuheshimu sana nguvu hii, hasa pale ilipojidhihirisha kupitia baraka za ukuhani. Wakati nikitumika kama mmisionari kijana huko Chile, mimi na mmisionari mwenzangu tulikamatwa na kutenganishwa. Hatukuambiwa sababu. Ulikuwa wakati wa mgogoro mkubwa wa kisiasa. Maelfu ya watu walikamatwa na jeshi la polisi na hawakusikika tena.
Baada ya kuhojiwa, nilikaa pekee yangu kwenye chumba cha gereza, bila kujua kama ningewaona tena wapendwa wangu. Nilimgeukia Baba yangu wa Mbinguni, kwa dhati nikisihi: “Baba mara zote nilifundishwa Wewe huwalinda wamisionari Wako. Tafadhali, Baba, mimi si maalumu, lakini nimekuwa mwaminifu na ninahitaji msaada Wako usiku wa leo.”
Mbegu za msaada huu zilikuwa zimekwishapandwa miaka mingi iliyopita. Baada ya ubatizo wangu, nilithibitishwa kuwa muumini wa Kanisa na kupewa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kadiri nilivyosali, peke yangu gerezani, Roho Mtakatifu mara moja alikuja na kunifariji. Alileta akilini mwangu aya maalumu kutoka kwenye baraka yangu ya kipatriaki, ambayo ni baraka nyingine ya ukuhani. Ndani ya baraka hiyo, Mungu aliniahidi kwamba kupitia uaminifu wangu ningeweza kuunganishwa kwa muda na milele yote kwa mwanamke mrembo, aliyejaa utu wema na upendo, kwamba tungekuwa wazazi wa wana na mabinti wa thamani, na kwamba ningebarikiwa na kukuzwa kama baba katika Isareli.
Maneno hayo yenye mwongozo wa kiungu kuhusu siku zangu za baadaye yaliijaza nafsi yangu kwa amani. Nilijua kwamba yalitoka kwa Baba yangu Mpendwa, ambaye mara zote hutimiza ahadi Zake. Katika wasaa ule, nilikuwa na uhakika kwamba ningeachiliwa huru na kuishi kuziona ahadi hizo zikitimizwa.
Takribani mwaka mmoja baadae, Baba wa Mbinguni alinibariiki kwa kunipa mke aliyejaa uzuri na utu wema na upendo. Lynette na mimi tuliunganishwa hekaluni. Tulibarikiwa kwa wana watatu na mabinti wanne wa thamani. Nilikuwa baba, yote kulingana na ahadi za Mungu katika baraka ya kipatriaki niliyopokea kama mvulana wa miaka 17.
“Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa [na akina dada], miujiza imekoma kwa sababu Kristo amekwenda mbinguni? …
“… La; wala malaika hawajakoma kuwahudumia watoto wa watu.”
Ninashuhudia kwamba miujiza na huduma vinaendelea kutokea katika maisha yetu, mara nyingi kama matokeo ya moja kwa moja ya nguvu ya ukuhani. Baadhi ya baraka za ukuhani hutimizwa haraka, katika njia tunazoweza kuziona na kuzielewa. Zingine huja hatua kwa hatua na hatuwezi kuzitambua zote moja kwa moja katika maisha haya. Lakini Mungu hutimiza ahadi zake zote, daima, kama ilivyobainishwa kwenye tukio hili kutoka katika familia yetu:
Babu yangu, Grant Reese Bowen, alikuwa mwanaume mwenye imani kubwa. Nakumbuka wazi wazi nikimsikia alivyokuwa akisimulia jinsi alivyopokea baraka yake ya kipatriaki. Katika shajara yake aliandika: “Patriaki aliniahidi kipawa cha uponyaji. Alisema, ‘Wagonjwa wataponywa. Ndiyo, wafu watafufuliwa chini ya mikono yako.’”
Miaka kadhaa baadae, Babu alikuwa akishughulikia nyasi za kulisha ng’ombe wakati alipohisi msukumo wa kurudi nyumbani. Alikutana na baba yake akija mbele yake. “Grant, mama yako amefariki dunia sasa hivi,” Baba yake alisema
Ninanukuu tena kutoka kwenye shajara ya Babu: “Sikusimama bali nilikwenda haraka ndani na kisha kutoka nje kwenye baraza la mbele ambapo mama alikuwa amelala kwenye kitanda kidogo chembamba. Nilimwangalia na sikuona ishara yoyote ya uhai ndani yake. Nilikumbuka baraka yangu ya kipatriaki na ahadi kwamba kama ningekuwa mwaminifu, kupitia imani yangu wagonjwa wangeponywa; na wafu wangerudishiwa uhai. Niliweka mikono yangu juu ya kichwa chake, na nilimwambia Mungu kwamba kama ahadi aliyoahidi kwangu kupitia patriaki ilikuwa ya kweli, afanye idhihirike katika muda huu na amrudishie mama yangu uhai. Nilimwahidi kwamba kama angelifanya hili, kamwe nisingesita kufanya yote yaliyo ndani ya uwezo wangu kwa ajili ya kuujenga ufalme Wake. Wakati nikisali, alifungua macho yake na kusema, ‘Grant, niinue. Nilikuwa kwenye Ulimwengu wa roho, lakini wewe umeniita. Acha hili daima liwe ushuhuda kwako na kwa wanafamilia wote.’”
Rais Nelson ametufundisha tutafute na kutarajia miujiza. Ninashuhudia kwamba kwa sababu ukuhani umerejeshwa, nguvu na mamlaka ya Mungu vipo duniani. Kupitia miito na mabaraza, wanaume na wanawake, vijana na wazee, wanaweza kushiriki katika kazi za ukuhani. Ni kazi ya miujiza, ikitolewa na malaika. Ni kazi ya mbinguni, na huwabariki watoto wote wa Mungu.
Mnamo mwaka 1989, familia yetu ya watu saba ilikuwa ikirejea kutoka kwenye matembezi ya kata. Muda ulikuwa umekwenda sana. Lynette alikuwa akitarajia mtoto wetu wa sita. Alipata msukumo mkubwa wa kufunga mkanda wa kiti chake, ambapo alikuwa amesahau kufanya hivyo. Muda mfupi baadaye tulifika sehemu yenye kona kwenye barabara; gari lilivuka kuja upande wa pili wa barabara kwenye njia yetu. Spidi ya gari ikiwa maili 70 (km112) kwa saa, nilikwepesha gari ili kuepusha kuligonga gari lililokuwa likija mbele yetu. Gari letu lilipinduka na kuteleza, likitoka nje ya barabara, na hatimaye kutulia, upande wa abiria ukiwa kwenye vumbi.
Kitu ninachokumbuka kusikia baada ya hapo ilikuwa ni sauti ya Lynette: “Shayne tunahitaji kutoka kupitia mlango wako.” Nilikuwa nikining’inia hewani kwa mkanda wa kiti changu. Ilinichukua sekunde kadhaa kujua mazingira ya pale tulipo Tulianza kuwanyanyua na kuwatoa watoto nje ya gari kupita dirisha langu, ambalo sasa lilikuwa ni dari ya gari. Walikuwa wakilia, wakijiuliza nini kilichokuwa kimetokea.
Punde tuligundua kwamba mtoto wetu wa miaka 10, Emily, hakuwepo. Tulimwita kwa sauti, lakini hapakuwa na mwitikio. Waumini wa kata, ambao pia walikuwa wakirudi nyumbani, walikuwa kwenye eneo la tukio wakihangaika kumtafuta. Kulikuwa na giza totoro. Niliangalia tena kwenye gari kwa tochi na, kwa hofu, niliuona mwili mdogo wa Emilly umebanwa chini ya gari. Nipiga kelele kwa taharuki, “Tunatakiwa tulinyanyue gari kumtoa Emily.” Nilishika dari ya gari na kunyanyua na kuirudisha. Walikuwepo wengine wachache wakinyanyua, lakini kimiujiza gari ilijigeuza na kusimamia matairi, likiuleta juu mwili wa Emily usio na uhai.
Emily alikuwa hapumui. Uso wake ulikuwa wa rangi ya zambarau. Nilisema, “Tunahitaji kumpa baraka.” Rafiki mpendwa na muumini wa kata walipiga magoti pamoja nami na kwa mamlaka ya Ukuhani wa Melkizedeki, katika jina la Yesu Kristo tulimwamuru aishi. Katika wasaa ule, Emily alivuta pumzi ndefu.
Baada ya kile kilichoonekana kama masaa mengi, hatimaye gari la kubeba wagonjwa lilifika. Emily alikimbizwa hospitali. Alikuwa na pafu lililoharibika na madhara makubwa kwenye kano ya goti lake. Uharibifu wa ubongo ulikuwa ni hofu yetu kwa sababu ya muda aliokuwa amekaa bila hewa ya oksijeni. Emily alikuwa mahututi kwa siku moja na nusu. Tuliendelea kusali na kufunga kwa ajili yake. Alibarikiwa kwa kupona kabisa. Leo hii, Emily na Kevin mume wake, ni wazazi wa watoto sita wa kike.
Kimiujiza, kila mmoja aliweza kuondoka. Mtoto ambaye Lynette alikuwa na ujauzito wake ni Tyson. Naye pia aliepushwa na alizaliwa Februari iliyofuata. Miezi minane baadaye, baada ya kupokea mwili wake wa duniani, Tyson alirudi nyumbani kwa Baba yetu wa Mbinguni. Yeye ni mwana wetu malaika mlinzi. Tunauhisi uwepo wake katika familia yetu na tunatarajia kuwa naye tena.
Wale waliolinyanyua gari kumtoa Emily waligundua kwamba gari lilionekana kutokuwa na uzito. Nilijua kwamba malaika wa mbinguni waliungana na malaika wa duniani kunyanyua gari lililokuwa juu ya mwili wa Emily. Pia ninajua kwamba, Emily alirudishiwa uhai kupitia nguvu ya ukuhani mtakatifu.
Bwana alifunua ukweli huu kwa watumishi Wake: “Kwani nitakwenda mbele ya uso wenu. Nitakuwa mkono wenu wa kuume na wa kushoto, na Roho wangu atakuwa mioyoni mwenu, na malaika wangu watawazingira, ili kuwabeba juu.”
Ninashuhudia kwamba “Ukuhani Mtakatifu, kwa Mfano wa Mwana wa Mungu”—Ukuhani wa Melkizedeki—pamoja na funguo zake, mamlaka, na nguvu vimerejeshwa duniani katika hizi, siku za mwisho. Ninajua kwamba wakati si hali zote zinaweza kuwa kama tunavyosali ziwe na kama tunavyotarajia ziwe, miujiza ya Mungu daima itakuja kulingana na mapenzi Yake, muda Wake na kwa mpango Wake kwa ajili yetu.
Kama unatamani baraka za ukuhani, ikijumuisha miujiza na huduma ya malaika, ninakualika utembee kwenye njia ya maagano ambayo Mungu ameiweka kwa ajili ya kila mmoja wetu. Waumini na viongozi wa Kanisa ambao wanakupenda watakusaidia upige hatua inayofuata.
Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, yu hai na analiongoza Kanisa kupitia manabii walio hai wanaoshikilia na kutumia funguo za ukuhani. Roho Mtakatifu yupo. Mwokozi alitoa maisha Yake ili kutuponya, kutukomboa na kuturudisha nyumbani.
Ninashuhudia kwamba miujiza haijakoma, malaika wapo miongoni mwetu, na mbingu hakika zipo wazi. Na, Ee, ni jinsi gani zilivyo wazi! Katika jina la Yesu Kristo, amina.