Yesu Kristo Ni Faraja
Tunaweza kushirikiana na Mwokozi ili kusaidia kutoa faraja ya kimwili na kiroho kwa wale walio na mahitaji—na katika mchakato huo kupata faraja yetu wenyewe.
Wakiwa na imani katika Yesu Kristo na kutumaini yale waliyokuwa wamesikia kuhusu miujiza Yake, waliomhudumia mtu aliyepooza walimleta kwa Yesu. Walikuwa wabunifu katika kumfikisha pale—kufunua dari na kumshusha mtu huyo, akiwa kitandani kwake, hadi mahali ambapo Yesu alikuwa akifundisha. Yesu “alipoiona imani yao, akamwambia [yule mwenye kupooza], umesamehewa dhambi zako.”1 Kisha, “Ondoka, ujitwike godoro lako, uende zako nyumbani kwako.”2 Na mara yule mtu aliyepooza akasimama, akachukua kitanda chake, akaenda zake nyumbani, “akimtukuza Mungu.”3
Je, tunajua nini zaidi kuhusu marafiki waliotoa huduma kwa mtu aliyepooza? Tunajua kwamba Yesu alitambua imani yao. Na baada ya kumwona na kumsikia Mwokozi na kuwa mashahidi wa miujiza Yake, “walishangazwa” na “wakamtukuza Mungu.”4
Yesu Kristo alikuwa ametoa uponyaji uliotumainiwa—faraja ya kimwili kutokana na matokeo yenye kulemaza ya ugonjwa sugu. Cha muhimu, Mwokozi pia alitoa faraja ya kiroho katika kumwondolea mtu huyu dhambi.
Na marafiki—katika jitihada zao za kumtunza mwenye uhitaji, walipata chanzo cha faraja; walimpata Yesu Kristo.
Ninashuhudua kwamba Yesu Kristo ni faraja. Kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, tunaweza kuondolewa mzigo na matokeo ya dhambi na kusaidiwa katika udhaifu wetu.
Na kwa sababu tunampenda Mungu, na tumefanya agano la kumtumikia Yeye, tunaweza kushirikiana na Mwokozi kusaidia kutoa faraja ya kimwili na kiroho kwa wale walio na mahitaji—na katika mchakato huo kupata faraja yetu wenyewe katika Yesu Kristo.5
Nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, alitualika tuushinde ulimwengu na tupate pumziko.6 Alifafanua “pumziko la kweli” kama “faraja na amani.” Rais Nelson alisema, “Kwa sababu Mwokozi, kupitia Upatanisho Wake usio na kikomo, alimkomboa kila mmoja wetu kutokana na udhaifu, makosa, na dhambi, na kwa sababu Yeye alipitia kila maumivu, wasiwasi, na mzigo ambao umewahi kuwa nao, basi unapotubu kwa dhati na kutafuta msaada Wake, unaweza kuinuka juu ya ulimwengu huu hatari wa sasa.”7 Hii ndiyo faraja ambayo Yesu Kristo hutupatia!
Kila mmoja wetu amebeba begi la mgongoni la kisitiari. Inaweza kuwa kikapu juu ya kichwa chako au mkoba au rundo la vitu vilivyofungwa kwa kitambaa na kuwekwa juu ya bega lako. Lakini kwa mawazo yetu, hebu tuliite begi la mgongoni.
Begi hili la kisitiari ni ambalo ndani yake tunabeba mizigo ya kuishi katika ulimwengu ulioanguka. Mizigo yetu ni kama mawe kwenye begi. Kwa ujumla, kuna aina tatu:
-
Mawe yatokanayo na matendo yetu kwa sababu ya dhambi.
-
Mawe kwenye mabegi yetu kwa sababu ya chaguzi zetu duni, tabia isiyofaa au udhalimu wa wengine.
-
Na mawe tunayoyabeba kwa sababu tunaishi katika hali ya kuanguka. Hii hujumuisha mawe ya ugonjwa, maumivu, magonjwa sugu, huzuni, kukata tamaa, upweke na matokeo ya majanga ya asili.
Ninatamka kwa shangwe kwamba mizigo yetu ya kimwili, mawe haya kwenye mabegi yetu ya mgongoni ya kisitiari hayahitajiki kuhisiwa kuwa ni mazito.
Yesu Kristo anaweza kufanya mzigo wetu uwe mwepesi.
Yesu Kristo anaweza kuinua mizigo yetu.
Yesu Kristo anatupatia njia ya kutuondolea uzito wa dhambi.
Yesu Kristo ndiye faraja yetu.
Yeye alisema:
“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha [yaani, faraja na amani].
“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.
“Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”8
Kwamba nira ni laini na mzigo ni mwepesi hudhaniwa kwamba tunaingia kwenye nira pamoja na Mwokozi, kwamba tunashiriki mizigo yetu pamoja Naye, kwamba tunamwacha Yeye aubebe mzigo wetu. Hiyo inamaanisha kuingia katika uhusiano wa agano na Mungu na kushika agano hilo, ambalo, kama Rais Nelson ambavyo ameeleza, “hufanya kila kitu kuhusu maisha kuwa rahisi.” Alisema, “Kujifunga nira na Mwokozi humaanisha kwamba unaweza kutumia nguvu Zake na uwezo Wake wa kukomboa.”9
Basi kwa nini sisi tunakuwa wachoyo kwa mawe yetu? Kwa nini mchezaji wa besiboli aliyechoka atakataa kuondoka kwenye kilima wakati msaidizi yuko pale tayari kumalizia mchezo? Kwa nini ning’ang’anie kuendelea na hali yangu nikiwa peke yangu wakati Msaidizi anasimama akiwa tayari kunisaidia?
Rais Nelson amefundisha, “Yesu Kristo … anasimama na mikono iliyonyooshwa, akitumaini na kuwa tayari kutuponya, kutusamehe, kutusafisha, kutuimarisha na kututakasa.”10
Basi kwa nini tunang’ang’ania kubeba mawe yetu peke yetu?
Hili limekusudiwa kama swali binafsi, kwa kila mmoja wenu kujiuliza.
Kwangu mimi, ni tabia mbaya ya kiburi kilichopitwa na wakati. “Nimepata hiki,” ninasema. “Hakuna wasiwasi; nitakikamilisha.” Ni yule mdanganyifu mkuu ambaye hutaka nijifiche mbali na Mungu, nigeuke mbali na uwepo Wake, na nifanye mimi mwenyewe.
Akina kaka na akina dada, siwezi kufanya peke yangu, na sihitaji iwe hivyo, na sitaki kufanya hivyo. Kuchagua kuunganishwa kwa Mwokozi wangu, Yesu Kristo, kupitia maagano niliyofanya na Mungu, “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.”11
Washika maagano wanabarikiwa kwa faraja ya Mwokozi.
Tafakari mfano huu katika Kitabu cha Mormoni: Watu wa Alma waliteswa kwa kupewa “kazi juu yao, na … wasimamizi kuwasimamia.”12 Wakiwa wamekatazwa kusali kwa sauti, “walimimina mioyo yao kwa [Mungu]; na alijua mawazo ya mioyo yao.”13
Na “sauti ya Bwana iliwafikia katika mateso yao, ikisema: lnueni vichwa vyenu na msherehekee, kwani ninajua agano ambalo mlinifanyia; na nitafanya agano na watu wangu na kuwakomboa kutoka utumwani.
“Na nitawapunguzia mizigo ambayo imewekwa mabegani mwenu, hata kwamba hamtaisikia kamwe migongoni mwenu.”14
Na mizigo yao “ilifanywa kuwa miepesi,” na “Bwana aliwatia nguvu ili waweze kubeba mizigo yao kwa urahisi, na walinyenyekea kwa furaha na subira kwa mapenzi yote ya Bwana.”15
Wale washika maagano walipokea msaada kwa njia ya faraja, kuongezeka kwa uvumilivu na uchangamfu, urahisi wa mizigo yao kwamba walihisi wepesi, na hatimaye ukombozi.16
Sasa hebu turudi kwenye mabegi yetu ya kisitiari.
Toba, kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, ndiyo hutuondolea uzito wa mawe ya dhambi. Na kwa zawadi hii adhimu, rehema ya Mungu hutusaidia sisi kutokana na uzito na madai mengine ya haki yasiyoweza kuondolewa.17
Upatanisho wa Yesu Kristo pia hutuwezesha sisi kupokea nguvu ya kusamehe, ambayo huturuhusu kutua mzigo tunaobeba kwa sababu ya kutendewa vibaya na wengine.18
Basi Mwokozi hutuondolea vipi mizigo ya maisha katika ulimwengu ulioanguka tukiwa wenye miili itakayokufa yenye kupata huzuni na maumivu?
Mara nyingi, Yeye huleta aina hiyo ya faraja kupitia sisi! Kama waumini wa agano wa Kanisa Lake, tunaahidi “kuomboleza pamoja na wale wanaoomboleza” na “kuwafariji wale wanaohitaji faraja.”19 Kwa sababu “tumekuja katika zizi la Mungu” na “tunaitwa watu wake,” ‘tuko tayari kubebeana mizigo, ili iwe miepesi.”20
Baraka yetu ya agano ni kushirikiana na Yesu Kristo katika kutoa faraja, ya kimwili na ya kiroho, kwa watoto wote wa Mungu. Sisi ni njia ambayo kupitia hiyo Yeye hutoa faraja.21
Na kwa hivyo, kama marafiki wa mtu aliyepooza, “tunawasaidia walio dhaifu, kuinua mikono iliyolegea, na kuimarisha magoti dhaifu.”22 “Tunabebeana … mizigo, na hivyo kuitimiza sheria ya Kristo.”23 Tunapofanya hivyo, tunakuja kumjua Yeye, na kuwa kama Yeye, na kupata faraja Yake.24
Faraja ni nini?
Ni kuondolewa au kufanywa wepesi kwa kitu chenye kuleta maumivu, kusumbua, au kulemea, au nguvu ya kustahimili. Humaanisha mtu ambaye huchukua nafasi ya mwingine. Ni marekebisho ya kosa kisheria.25 Neno la kifaransa lenye asili ya Kingereza kutoka Kifaransa cha Kale, neno relever, au “kuinua,” na kutoka Kilatini relevare, au “kuinua tena .”26
Akina kaka na akina dada, Yesu Kristo ni faraja. Ninashuhudia kwamba Yeye alifufuka tena katika siku ya tatu na, akiwa ametimiza upendo na Upatanisho usio na mwisho, anasimama mikono ikiwa wazi, akitupatia fursa ya kufufuka tena, kuokolewa, na kuinuliwa na kuwa kama Yeye. Faraja ambayo Yeye hutupatia ni ya milele.
Kama wanawake waliotembelewa na malaika asubuhi ile ya kwanza ya Pasaka, natamani “kwenda upesi” na kwa “furaha kuu” kutoa taarifa kwamba Yeye amefufuka.27 Katika jina la Mwokozi wetu, Yesu Kristo, amina.