“Hapawezi Kuwa na Kitu Kizuri Hivyo na Kitamu vile Ilivyokuwa Shangwe Yangu”
Kutubu kila siku na kuja kwa Yesu Kristo ni njia ya kupata shangwe—shangwe zaidi ya fikra zetu.
Kote katika huduma yake duniani, Mwokozi alionesha huruma nyingi kwa watoto wote wa Mungu—hasa kwa wale waliokuwa wakiteseka au waliopotea. Alipokosolewa na Mafarisayo kwa kuchangamana na kula pamoja na wenye dhambi, Yesu alijibu kwa kufundisha mifano mitatu tunayoifahamu.1 Katika kila moja ya mifano hii, alisisitiza umuhimu wa kuwatafuta wale wote waliopotea, na shangwe inayohisiwa pale wanaporejea. Kwa mfano, katika mfano wa kondoo aliyepotea, Yeye alisema, “Kutakuwa na furaha [tele] mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”2
Tamanio langu leo ni kuimarisha muunganiko kati ya shangwe na toba—hususani zaidi, shangwe inayokuja tunapotubu na hisia za shangwe tunazopata tunapowaalika wengine kuja kwa Kristo na kutumia dhabihu yake ya kulipia dhambi katika maisha yao.
Tupo Ili Tupate Shangwe
Katika maandiko, neno shangwe kwa kawaida lina maana zaidi ya nyakati zipitazo za kuridhika au hata hisia za furaha. Shangwe katika muktadha huu ni sifa ya kiungu, inayopatikana katika utimilifu wake pale tunaporejea kuishi katika uwepo wa Mungu.3 Ni kuu zaidi, yenye kuinua, kustahimili na yenye kubadili maisha kuliko starehe au faraja nyingine inayoweza kutolewa na ulimwengu huu.
Tuliumbwa ili tuwe na shangwe. Ni hatma yetu iliyokusudiwa kama watoto wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Anataka kushiriki nasi shangwe Yake. Nabii Lehi alifundisha kwamba mpango wa Mungu kwa kila mmoja wetu ni kwamba “tupate shangwe.”4 Kwa sababu tunaishi katika ulimwengu ulioanguka, shangwe ya kudumu au shangwe ya milele mara nyingi huonekana kama jambo lisilofikika. Bado katika mstari unaofuata, Lehi anaendelea kufafanua kwamba “Masiya [alikuja] … ili atukomboe [sisi] kutokana na anguko.”5 Ukombozi, kwa, na kupitia Mwokozi Yesu Kristo, hufanya shangwe iwezekane.
Ujumbe wa injili ni ujumbe wa tumaini, wa “habari njema ya furaha kuu,”6 na ni njia ambayo sote tunaweza kupata amani na shangwe wakati fulani katika maisha haya na kupokea utimilifu wa shangwe katika maisha yajayo.7
Shangwe tunayoizungumzia ni zawadi kwa wale walio waaminifu, na bado inakuja kwa gharama. Shangwe si rahisi wala haitolewi kiholela. Bali, inanunuliwa “kwa damu ya thamani ya [Yesu] Kristo.”8 Ikiwa tulielewa thamani hasa ya shangwe ya kweli ya kiungu, tusingesita kutoa dhabihu mali yoyote ya ulimwenguni au kufanya mabadiliko yoyote muhimu ili kuipokea.
Mfalme mwenye nguvu lakini mnyenyekevu katika Kitabu cha Mormoni alilielewa hili. “Nitafanya nini,”aliuliza, “ili nizaliwe kwa Mungu, ili hii roho mbovu ingʼolewe nje ya mwili wangu, na nipokee Roho yake, ili niweze kujazwa na shangwe … ? Tazama, alisema, nitatoa umiliki wangu wote, ndio, nitaacha ufalme wangu, ili nipokee hii shangwe kuu.”9
Katika kujibu swali la mfalme, mmisionari Haruni alisema, “Ikiwa unatamani kitu hiki, … msujudie Mungu … [na] utubu dhambi zako zote.”10 Toba ni njia ya kuelekea shangwe11 kwa sababu ni njia inayoongoza kwa Mwokozi Yesu Kristo.12
Shangwe Huja kupitia Toba ya Dhati
Kwa baadhi, kufikiria toba kama njia ya kuelekea kwenye shangwe inaweza kuonekana ya kukanganya. Toba, nyakati fulani, inaweza kuwa yenye maumivu na ngumu. Inahitaji kukiri kwamba baadhi ya mawazo na matendo yetu—hata baadhi ya imani zetu— vimekuwa si sahihi. Toba pia huhitaji badiliko, ambalo, nyakati fulani, linaweza kuwa si la kuleta faraja. Lakini shangwe na faraja si kitu kimoja. Dhambi—ikijumuisha dhambi za kuridhia—huzuia shangwe yetu.
Kama ilivyoelezwa na Mtunga Zaburi, “Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha.”13 Tunapotubu dhambi zetu, tunapaswa kufokasi kwenye shangwe kuu inayofuatia. Usiku waweza kuonekana mrefu, lakini asubuhi huja, na, ee, ni nzuri jinsi gani amani na shangwe ya fahari tunayoihisi pale Upatanisho wa Mwokozi unapotuweka huru kutoka dhambi na mateso.
Hapawezi Kuwa na Kitu Kizuri Hivyo na Kitamu Vile
Zingatia uzoefu wa Alma katika Kitabu cha Mormoni. Alikuwa “akisumbuliwa na adhabu ya milele” na roho yake “iliteseka” kwa sababu ya dhambi zake. Lakini pale alipomgeukia Mwokozi kwa ajili ya rehema, “ hakukumbuka uchungu [wake] tena.”14
“Na Ee, ni shangwe gani,” alitangaza, “na ni mwangaza gani wa ajabu niliouona; ndiyo, … hapawezi kuwa na kitu kizuri hivyo na kitamu vile ilivyokuwa shangwe yangu.”15
Hii ni aina ya shangwe inayopatikana kwa wale wanaokuja kwa Yesu Kristo kupitia toba.16 Kama vile Rais Russell M. Nelson alivyofundisha:
“Toba hufungua njia yetu ya kufikia nguvu ya Upatanisho wa Yesu Kristo. …
“Tunapochagua kutubu, tunachagua kubadilika! Tunamruhusu Mwokozi atubadilishe kuwa toleo zuri zaidi la sisi wenyewe. Tunachagua kukua kiroho na kupokea shangwe—shangwe ya ukombozi katika Yeye. Tunapochagua kutubu, tunachagua kuwa zaidi kama Yesu Kristo!”17
Toba huleta shangwe kwa sababu inaandaa mioyo yetu kupokea ushawishi wa Roho Mtakatifu. Kujawa na Roho Mtakatifu, humaanisha kujawa na shangwe. Kujawa na shangwe humaanisha kujawa Roho Mtakatifu.18 Shangwe yetu huongezeka tunapofanya kazi kila siku kumleta Roho kwenye maisha yetu. Kama ilivyofundishwa na nabii Mormoni, “Walakini walifunga na kuomba kila wakati, na wakapokea nguvu zaidi na zaidi katika unyenyekevu wao, na wakawa imara zaidi na imara katika imani [yao] [katika] Kristo, hadi nafsi zao zikajazwa na shangwe na faraja.”19 Bwana anawaahidi wote wanaofanya kazi kumfuata Yeye, “Nitakupa … Roho wangu, ambaye ataiangaza akili yako, ambaye itaijaza nafsi yako kwa shangwe.”20
Shangwe ya Kuwasaidia Wengine Watubu
Baada ya kuwa tumehisi shangwe inayokuja kutokana na toba ya dhati, kwa moyo mmoja tunataka kushiriki shangwe hiyo na wengine. Tunapofanya hivyo, shangwe yetu inaongezeka. Hicho ndicho hasa kilichotokea kwa Alma.
“Hii ni furaha yangu,” alisema, “kwamba labda niwe chombo kwenye mikono ya Mungu kuleta roho moja kwenye toba; na hii ndiyo shangwe yangu.
“Na tazama, ninapoona wengi wa ndugu zangu wametubu kweli, na kumkubali Bwana Mungu wao, ndipo nafsi yangu hujawa na shangwe; ndipo ninapokumbuka yale ambayo Bwana amenifanyia mimi, … ndiyo, ndipo ninapokumbuka mkono wake wa huruma ambao aliunyosha kwangu.”21
Kuwasaidia wengine watubu ni dhihirisho asilia la shukrani yetu kwa Mwokozi; na ni chanzo cha shangwe kuu. Bwana ameahidi:
“Na kama itakuwa kwamba … utaleta, japo iwe nafsi moja kwangu, shangwe yako itakuwa kubwa jinsi gani pamoja naye katika ufalme wa Baba yangu!
“Na sasa, kama shangwe yako itakuwa kubwa kwa hiyo nafsi moja ambayo umeileta kwangu … , itakuwa shangwe kubwa namna gani kwako kama utazileta nafsi nyingi kwangu!”22
Ni Shangwe Kubwa Kiasi Gani Kwake Katika Nafsi Ambayo Hutubu
Ninaona kuwa inasaidia ninapojaribu kupata taswira ya shangwe ambayo Mwokozi analazimika kuihisi kila wakati tunapopokea baraka za dhabihu Yake ya kulipia dhambi katika maisha yetu.23 Kama ilivyonukuliwa na Rais Nelson ,24 Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Waebrania alishiriki umaizi huu mwororo: “Na tuweke kando kila … dhambi ile ituzingayo kwa upesi; … tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba … na ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.”25 Mara nyingi tunazungumza juu ya maumivu na mateso ya Gethsemane na Kalvari, lakini mara chache tunazungumzia shangwe kuu ambayo Mwokozi aliitazamia pale alipoyatoa maisha Yake kwa ajili yetu. Kwa dhahiri, mateso na maumivu Yake vilikuwa kwa ajili yetu, kwamba tupate uzoefu wa shangwe ya kurejea pamoja Naye kwenye uwepo wa Mungu.
Baada ya kuwafundisha watu katika Amerika ya kale, Mwokozi alionesha upendo Wake mkuu kwao kwa kusema:
“Na sasa tazama, shangwe yangu ni kubwa, hata kwenye utimilifu, kwa sababu yenu … ; ndio, na hata Baba hufurahi, na pia malaika watakatifu. …
“… Ndani [yenu], nina utimilifu wa shangwe.”26
Njoo kwa Kristo na Upokee Shangwe Yake
Akina kaka na akina dada, ninahitimisha kwa kushiriki ushahidi wangu binafsi, ambao ninauchukulia kama zawadi takatifu. Ninashuhudia kwamba Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wa ulimwengu. Ninajua kwamba anampenda kila mmoja wetu. Fokasi Yake moja, “kazi Yake na utukufu [Wake],”27 ni kutusaidia tupokee utimilifu wa shangwe katika Yeye. Mimi ni shahidi binafsi kwamba kutubu kila siku na kuja kwa Yesu Kristo ni njia ya kupata shangwe—shangwe zaidi ya fikra zetu.28 Hiyo ndiyo sababu tupo hapa duniani. Hiyo ndiyo sababu Mungu aliandaa mpango Wake mkuu wa furaha kwa ajili yetu. Yesu Kristo hakika ndiye “njia, kweli na uzima”29 na “jina pekee lililotolewa chini ya mbingu ambalo mwanadamu anaweza kuokolewa katika ufalme wa Mungu.”30 Ninashuhudia hivyo katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.