Mkutano Mkuu
Wakati Sahihi wa Kupokea Baraka Yako ya Patriaki
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Wakati Sahihi wa Kupokea Baraka Yako ya Patriaki

Unapopokea baraka yako, utatambua na kuhisi jinsi Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanavyokupenda na wanavyofokasi juu yako wewe binafsi.

Jana rafiki yangu mpendwa Mzee Randall K. Bennett alizungumzia kuhusu baraka za patriaki. Ulikuwa ujumbe mkuu na ulituvutia sisi sote. Wapendwa kaka na dada zangu, je, naweza pia kuzungumzia kuhusu baraka za patriaki? Mapatriaki, kadiri maombi ya baraka za patriaki yanavyoongezeka, naomba kwamba Bwana awabariki mnapoendelea kukuza wito wenu.

Ninapokwenda katika mikutano ya kigingi, daima ninazungumza na patriaki wa kigingi na mke wake. Mapatriaki ni viongozi wapole, watiifu na wa kupendeza sana walioitwa na Mungu. Wananiambia uzoefu mwingi mzuri wa kiroho. Ninawauliza umri wa mtu aliye kijana zaidi na aliye mzee zaidi ambaye wamempatia baraka. Kijana zaidi alikuwa wa miaka 11 na mzee zaidi alikuwa miaka 93.

Nilipokea baraka zangu za patriaki kama muumini mpya wa Kanisa, katika umri wa miaka 19, miaka miwili baada ya kubatizwa. Patriaki wangu alikuwa mzee sana. Yeye alijiunga na Kanisa mnamo 1916 na alikuwa mwasisi wa Kanisa nchini Japan. Ilikuwa heshima kubwa kwangu kupokea baraka yangu ya patriaki kutoka kwa mfuasi huyu wa kusifika wa Bwana. Kijapani chake kilikuwa kigumu kwangu kuelewa, lakini kilikuwa chenye nguvu sana.

Mapatriaki niliokutana nao wameniambia kwamba watu wengi wanapokea baraka zao za patriaki muda mfupi kabla ya kuhudumu misheni. Wapendwa wavulana na wasichana, wazazi na maaskofu, baraka za patriaki siyo tu kwa maandalizi ya kwenda kuhudumu misheni. Waumini waliobatizwa wenye kustahili wanaweza kupokea baraka zao wakati muda unapokuwa sahihi kwao.1

Wapendwa waumini mlio watu wazima, baadhi yenu bado hamjapokea baraka zenu za patriaki. Kumbukeni, hakuna ukomo wa umri.

Mama mkwe wangu alikuwa muumini aliyeshiriki sana Kanisani, akihudumu kama mwalimu wa Muungano wa Usaidizi hadi alipofariki akiwa na miaka 91. Nilihuzunika kujua kwamba hakuwa amepokea baraka yake ya patriaki. Alikuwa amepitia magumu mengi katika maisha yake, na kwa sababu hakuwa na mtu mwenye ukuhani katika nyumba yake, hakuwa amepokea baraka nyingi za ukuhani. Baraka ya patriaki yawezekana ingelimpa faraja wakati alipoihitaji zaidi.

Watu wazima, kama bado hamjapokea baraka ya patriaki, tafadhali msifadhaike! Ratiba ya kiroho ya kila mtu iko toauti. Kama una umri wa miaka 35 au 85 na unayo hamu, zungumza na askofu wako kuhusu kupokea baraka yako.

Waumini wapya katika Kanisa, je, mmewahi kusikia juu ya baraka za patriaki? Sikujua kuhusu fursa ya kupokea baraka hii wakati ninajiunga na Kanisa, lakini askofu wangu mpendwa aliniambia kuhusu baraka hizi na akanihimiza nijiandae kupokea yangu baada ya kubatizwa. Wapendwa wangu waumini wapya, ninyi vile vile mnaweza kupokea baraka za patriaki. Bwana atawasaidieni mjitayarishe kwa ajili ya fursa hii takatifu.

Acha tufikirie makusudi mawili ya baraka ya patriaki:

  1. Baraka ya patriaki inayo ushauri binafsi kutoka kwa Bwana kwa ajili yako.2

  2. Baraka ya patriaki inatamka ukoo wako katika nyumba ya Israeli.

Baraka yako ya patriaki ni ujumbe kutoka kwa Baba yako wa Mbinguni na huenda ikajumuisha ahadi na ushauri wenye mwongozo wa kiungu ili ukuongoze maisha yako yote. Baraka ya patriaki haitachora ramani ya maisha yako au kujibu maswali yako yote. Kama haitaji tukio muhimu katika maisha yako, usichukulie kwamba hiyo inamaanisha hautapata fursa hiyo. Vile vile, hakuna hakikisho kwamba kila kitu kilichomo katika baraka yako kitakuja kutokea katika maisha haya. Baraka ya patriaki ni ya milele, na kama utaishi kwa kustahili, ahadi ambazo hazijatimia katika maisha haya zitatolewa katika maisha yajayo.3

Unapopokea tamko la ukoo, utakuja kujua kwamba wewe ni wa nyumba ya Israeli na uzao wa Ibrahimu.4 Ili kujua upekee wa hili, fokasi juu ya ahadi za Bwana alizozifanya kwa nyumba ya Israeli kupitia Ibrahimu.

Ahadi hizo zinajumuisha:

  • “Wazao wake wangekuwa wengi (ona Mwanzo 17:5–6; Ibrahimu 2:9; 3:14).

  • “Wazao, au watoto wake, wangepokea injili na kuwa na ukuhani (ona Ibrahimu 2:9).

  • “Kupitia huduma ya uzao wake, ‘familia zote duniani [zingebarikiwa], hata kwa baraka za Injili, ambazo ni baraka za wokovu, hata za uzima wa milele’ (Ibrahimu 2:11).”5

Kama waumini wa Kanisa, sisi ni watoto wa agano.6 Tunapokea baraka za agano la Ibrahimu tunapotii sheria na ibada za injili.

Maandalizi kwa ajili ya baraka yako ya patriaki yatakusadia kuongeza imani yako katika Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Na unapopokea baraka yako ya patriaki na kuisoma na kuitafakari, unaweza kufokasi juu Yao zaidi mara kwa mara.

Rais Thomas S. Monson alieleza, “Bwana yule yule aliyetoa Liahona kwa ajili ya Lehi anatoa kwa ajili yako na mimi leo zawadi adhimu na yenye thamani ili kutoa mwongozo kwenye maisha yetu, ili kuweka alama za hatari kwa usalama wetu, na kuonyesha njia, hata njia salama—siyo kwenda nchi ya ahadi, bali nyumbani mbinguni.”7

Wapendwa wangu maaskofu, wazazi, marais wa akidi za wazee na marais wa Muungano wa Usaidizi, viongozi wa misheni wa kata, akina kaka na akina dada wahudumiaji, tafadhalini wahimizeni wale wavulana na wasichana, waumini watu wazima na waumini wapya ambao bado hawajapokea baraka zao za patriaki watafute mwongozo wa Bwana na msaada katika kujitayarisha wenyewe kufanya hivyo.

Mara kwa mara na kwa sala nasoma baraka yangu ya patriaki; daima inanitia moyo. Ninatambua kile Bwana anachokitarajia kutoka kwangu, na imenisaidia mimi kutubu na kuwa mnyenyekevu. Ninapoisoma na kutafakari, ninatamani kuishi nikiwa mwenye kustahili ahadi nilizoahidiwa.

Kama vile maandiko ambayo tumeyasoma mara nyingi yanavyokuwa na maana mpya kwetu baadaye, baraka yetu ya patriaki itakuwa na maana tofauti katika nyakati tofauti. Yangu ina maana tofauti sasa kuliko ilivyokuwa wakati nikiwa na miaka 30 na wakati nilipokuwa na miaka 50. Siyo kwamba maneno yanabadilika, bali tunayaona katika njia tofauti.

Rais Dallin H. Oaks alitamka kwamba baraka ya patriaki “inatolewa chini ya mwongozo wa kiungu wa Roho Mtakatifu na inapaswa isomwe na itafsiriwe chini ya ushawishi wa Roho yule yule. Maana na upekee wa baraka ya patriaki vitafundishwa mstari juu ya mstari katika maisha kwa nguvu za Roho yule yule ambaye aliiongoza [baraka hiyo].”8

Akina kaka na dada, ninatoa ushahidi wangu kwamba Baba wa Mbinguni na Mwanawe Mpendwa na Mzaliwa wa Pekee, Bwana Yesu Kristo, wako hai. Wanatupenda. Baraka za patriaki ni zawadi takatifu kutoka Kwao. Unapopokea baraka yako, utatambua na kuhisi jinsi Wao wanavyokupenda wewe na jinsi wanavyofokasi juu yako wewe binafsi.

Kitabu cha Mormoni ni ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo. Na nina shukrani kuongozwa na nabii aliye hai, Rais Russell M. Nelson.

Ninashukuru kwa ajili ya Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Jumapili hii ya Pasaka nitafokasi kwake Yeye na Ufufuko Wake, na kumwabudu Yeye na kutoa shukrani kwa dhabihu Yake. Ninajua Yeye aliteseka kwa kina kwa sababu Yeye anatupenda kwa kina sana. Ninajua Yeye alifufuka kwa sababu ya upendo Wake kwetu. Yeye yu halisi. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kutumikia katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 18.17, ChurchofJesusChrist.org.)

  2. Ona “Baraka za Patriaki,” katika True to the Faith (2004), 112.

  3. Ona “Patriarchal Blessings,” katika True to the Faith, 113.

  4. Ona Ibrahimu 2:10.

  5. Abrahamic Covenant,” katika True to the Faith, 5.

  6. Ona 3 Nefi 20:25–26.

  7. Thomas S. Monson, “Your Patriarchal Blessing: A Liahona of Light,” Ensign, Nov. 1986, 65.

  8. Dallin H. Oaks, “Patriarchal Blessings,” Worldwide Leadership Training Meeting: The Patriarch, Jan. 8, 2005, 10.

Chapisha