Kumbuka Kile Kilicho Muhimu Zaidi
Kilicho muhimu zaidi ni uhusiano wetu na Baba wa Mbinguni na Mwana Wake Mpendwa, familia zetu na jirani zetu na kumruhusu Roho kutuongoza.
Tunapokumbuka wikiendi hii ya Mwokozi kuingia kwa shangwe Yerusalemu muda mfupi kabla ya dhabihu Yake ya kulipia dhambi, ninakumbuka maneno Yake ya tumaini na faraja: “Mimi ni ufufuo, na uzima: Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi.”1
Ninampenda. Ninamwamini. Ninashuhudia kwamba Yeye ndiye ufufuo na uzima.
Ushuhuda huu umenifariji na kuniimarisha kwa kipindi cha miaka minne na nusu iliyopita tangu mke wangu, Barbara, alipofariki. Ninamkumbuka.
Mara nyingi, nimekuwa nikitafakari kwenye ndoa yetu ya milele na maisha yetu pamoja.
Nimewahi kabla kuelezea jinsi nilivyokutana na Barbara na jinsi uzoefu huo ulivyonifunza kutumia ujuzi wa “ufuatiliaji” ambao nilijifunza kwenye misheni yangu. Ilinibidi nifuatilie kwa haraka baada ya kuwa tumekutana kwa mara ya kwanza kwa sababu alikuwa mrembo, maarufu na alikuwa na ratiba yenye mambo mengi ya kijamii. Nilivutiwa mapema kwa sababu alikuwa mcheshi na rafiki. Nilipendezwa na wema wake. Nilihisi kwamba yeye na mimi tulistahili kuwa pamoja. Ilionekana rahisi hivyo katika akili yangu.
Mimi na Barbara tulianza miadi na uhusiano wetu ulianza kukua, lakini hakuwa na uhakika kwamba kuoana na mimi ilikuwa sahihi kwake.
Haikutosha tu mimi kujua; Barbara alipaswa kujua yeye mwenyewe. Nilijua kwamba ikiwa tutatenga muda kufunga na kusali kuhusu jambo hilo, Barbara angeweza kupokea uthibitisho kutoka mbinguni.
Tulitumia wikiendi pasipo miadi ili tuweze kufunga na kusali binafsi ili tujue sisi wenyewe. Bahati nzuri kwangu, alipokea uthibitisho sawa na ule niliopokea. Mengineyo, kama wanavyosema, ni historia.
Wakati Barbara alipofariki, watoto wetu waliweka juu ya kaburi lake masomo kadhaa ambayo Barbara aliwataka wayakumbuke. Moja ya masomo hayo ni “kile kilicho muhimu zaidi ndicho kinachodumu zaidi.”
Leo nitashiriki kutoka moyoni mwangu hisia na mawazo machache juu ya kile kilicho muhimu zaidi.
Kwanza, uhusiano na Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye, Bwana Yesu Kristo, ni muhimu zaidi. Uhusiano huu ni muhimu zaidi sasa na milele.
Pili, uhusiano wa familia ni kati ya mambo yale yaliyo muhimu zaidi.
Kote katika huduma yangu, nimewatembelea watu wengi binafsi na familia zilizoathiriwa na majanga ya kutisha ya asili. Wengi walihamishwa, walikuwa na njaa na hofu. Walihitaji msaada wa tiba, chakula na malazi.
Walizihitaji pia familia zao.
Ninatambua baadhi yawezekana hawana baraka ya familia ya karibu, hivyo ninajumuisha familia zingine, marafiki na hata familia za kata kama “familia.” Uhusiano huu ni wa msingi kwa ajili ya afya ya kihisia na kimwili.
Uhusiano huu unaweza pia kutoa upendo, shangwe, furaha na hisia ya kuwa wa mahala fulani.
Kukuza uhusiano huu muhimu ni uchaguzi. Uchaguzi wa kuwa sehemu ya familia unahitaji msimamo, upendo, subira, mawasiliano na msamaha.2 Kunaweza kuwako nyakati ambapo hatukubaliani na mtu fulani, lakini tunaweza kufanya hivyo bila kuwa na kutofautiana. Katika uchumba na ndoa, hatupendani au kutokupendana kana kwamba sisi ni vitu vinavyosogezwa kwenye ubao wa chess. Tunachagua kupendana na kuimarishana. Tunafanya vivyo hivyo katika uhusiano mwingine wa familia na marafiki ambao ni sawa na familia kwetu.
Tangazo la familia linaeleza kwamba “mpango mtakatifu wa furaha unawezesha uhusiano wa familia kuendelezwa zaidi ya kaburi. Ibada na maagano matakatifu yanayopatikana katika mahekalu matakatifu yanawezesha watu binafsi kurudi katika uwepo wa Mungu na kwa familia kuunganishwa milele.”3
Kitu kingine kilicho muhimu zaidi ni kufuata msukumo wa Roho katika uhusiano wetu muhimu zaidi na katika juhudi zetu za kuwapenda jirani zetu kama tunavyojipenda, ikijumuisha katika huduma zetu za faragha na za umma. Nilijifunza somo hili mapema katika maisha yangu wakati nikihudumu kama askofu.
Jioni moja ya baridi, yenye theluji, nilikuwa nikitoka kwenye ofisi yangu ya askofu wakati niliposikia msukumo wenye nguvu wa kumtembelea mjane mzee katika kata. Nilitazama saa yangu—ilikuwa saa 4:00 usiku. Nilijishauri kwamba muda ulikuwa umeenda sana kufanya matembezi yale. Na zaidi, theluji ilikuwa ikidondoka. Niliamua kumtembelea dada huyu mpendwa asubuhi sana badala ya kumsumbua usiku ule. Niliendesha gari kurudi nyumbani na nikaenda kulala lakini nilijirusha na kujigeuza usiku kucha kwa sababu Roho alikuwa akinitikisa.
Mapema asubuhi iliyofuata, niliendesha moja kwa moja mpaka kwenye nyumba ya mjane. Binti yake alifungua mlango na kwa machozi alisema, “Oo, Askofu, asante kwa kuja. Mama amefariki masaa mawili yaliyopita”—Nilishtushwa. Sitasahau kamwe hisia za moyo wangu. Nililia. Nani zaidi ya mjane huyu mpendwa alistahili kushikwa mkono na askofu wake, kumfariji na pengine kumpa baraka ya mwisho? Niliikosa fursa ile kwa sababu nilitupilia mbali msukumo huu wenye nguvu kutoka kwa Roho.4
Akina kaka na akina dada, wavulana na wasichana na watoto wa msingi, ninashuhudia kwamba kufuata msukumo wa Roho ni moja ya mambo yenye umuhimu zaidi katika mahusiano yetu yote.
Mwisho, kwenye Jumapili hii ya Matawi ya mitende, ninashuhudia kwamba kuongoka kwa Bwana, kushuhudia juu Yake na kumtumikia pia ni kati ya mambo yaliyo muhimu zaidi.
Imani katika Yesu Kristo ni msingi wa shuhuda zetu. Ushuhuda ni ushahidi au uthibitisho wa ukweli wa milele uliowekwa kwenye mioyo na nafsi za watu kupitia Roho Mtakatifu. Ushuhuda wa Yesu Kristo, uliotolewa na Roho na kuimarishwa na Roho, hubadili maisha—hubadili jinsi tunavyofikiri na jinsi tunavyoishi. Ushuhuda hutuongoza kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye mtakatifu.
Alma alifundisha:
“Tazama, nawashuhudia kwamba mimi najua kuwa vitu hivi ambavyo nimezungumza ni vya kweli. Na mnadhaniaje kwamba ninajua ukweli wake?
“Tazama, ninawaambia kwamba yamesababishwa kujulikana kwangu na Roho Mtakatifu wa Mungu. Tazama, nimefunga na kusali siku nyingi ili nivijue vitu hivi mimi mwenyewe. Na sasa ninavijua mwenyewe kuwa ni vya kweli; kwani Bwana Mungu amevidhihirisha kwangu kwa Roho wake Mtakatifu.”5
Kuwa na ushuhuda pekee haitoshi. Kadiri uongofu wetu kwa Yesu Kristo unavyokua, kiuasilia tunataka kumshuhudia Yeye—wema Wake, upendo na ukarimu.
Mara nyingi kwenye mikutano yetu ya ushuhuda Jumapili ya mfungo, tunasikia vifungu vya maneno “ninashukuru” na “ninapenda” kuliko tunavyosikia vifungu vya maneno “ninajua” na “ninaamini.”
Ninakualika utoe ushuhuda wako juu ya Yesu Kristo mara kwa mara. Toa ushuhuda juu ya kile unachokijua na unachokiamini na kile unachokihisi, si tu kile ulicho na shukrani nacho. Shuhudia juu ya uzoefu wako mwenyewe wa kufikia kujua na kumpenda Mwokozi, juu ya kuishi mafundisho Yake na juu ya nguvu yake ya kukomboa na kuwezesha katika maisha yako. Unapotoa ushuhuda wako juu ya kile unachokijua, unachokiamini, na unachokihisi, Roho Mtakatifu atathibitisha ukweli kwa wale wanaosikiliza kwa dhati ushuhuda wako. Watafanya hivyo kwa sababu wamekutazama ukiwa mfuasi mwenye amani wa Yesu Kristo. Wataona kile inachomaanisha kuwa mfuasi Wake. Watahisi pia jambo fulani ambalo yawezekana hawakuwahi kulihisi kabla. Ushuhuda safi huja kutoka kwenye moyo uliobadilishwa na unaweza kupelekwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kwenye mioyo ya wengine ambayo imefunguliwa kuupokea.
Wale wanaohisi kitu kama matokeo ya ushuhuda wako wanaweza kumwomba Bwana katika sala athibitishe ukweli wa ushuhuda wako. Kisha wanaweza kujua wao wenyewe.
Akina kaka na akina dada, ninashuhudia na kutoa ushahidi kwamba ninajua Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wa ulimwengu. Yu hai. Yeye ni Mwana aliyefufuka wa Mungu, na hili ni Kanisa Lake, linaloongozwa na nabii na mitume Wake. Ninaomba kwamba siku moja nitakapoenda kwenye ulimwengu mwingine, niweze kwenda nikiwa na ushuhuda wangu ukiwaka kwa mng’aro.
Katika huduma yangu, nimejifunza kile kilicho muhimu zaidi ni uhusiano wetu na Baba wa Mbinguni na Mwana Wake Mpendwa, familia zetu na jirani zetu na kumruhusu Roho wa Bwana atuongoze katika uhusiano huo ili tuweze kushuhudia juu ya vitu vilivyo muhimu zaidi na vinavyodumu zaidi. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.