Mkutano Mkuu
Bonnie, Usiache Kamwe Nafasi ya Kushuhudia Juu ya Kristo
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Bonnie, Usiache Kamwe Nafasi ya Kushuhudia Juu ya Kristo

Furaha ya kweli ipo kwenye utayari wetu wa kuja karibu na Kristo na kumshuhudia sisi wenyewe.

Siku kama ya leo miaka mitano iliyopita, tulinyanyua mikono yetu kumkubali nabii wetu mpendwa, Rais Russell M.Nelson, kama Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho―mnenaji wa Bwana wa nyakati hizi nzuri za ukuaji na ufunuo. Kupitia yeye, tumepokea mialiko isiyohesabika na tumeahidiwa baraka za utukufu ikiwa tutaweka maisha yetu kwa Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

Mnamo 2011, wakati nikitumikia na mume wangu kama viongozi wa misheni huko Curitiba, Brazili, simu yangu iliita wakati wa mkutano. Wakati nakimbilia kuizima, niligundua ilikuwa ni simu kutoka kwa baba yangu. Haraka niliondoka kwenye mkutano na kujibu: “Halo, Baba!”

Bila kutarajia, sauti yake ilijaa hisia: “Halo, Bonnie. Nahitaji kukwambia kitu. Nimekutwa na ugonjwa kwenye seli za neva,”

Akili yangu ilikanganyikiwa, “Ngoja kidogo! Ugonjwa wa seli ni nini?

Baba alikuwa tayari akielezea, “Akili yangu itakuwa bado makini wakati mwili wangu taratibu ukiishiwa na nguvu.”

Nilihisi dunia nzima imehamishwa nilipoanza kupambana na matokeo ya habari hii nzito. Ila katika siku hiyo isiyosahaulika, ilikuwa sentensi yake ya mwisho ambayo ilipata nafasi ya kudumu katika moyo wangu. Baba yangu mpendwa alisema kwa msisitizo, “Bonnie, usiache kamwe fursa ya kumshuhudia Kristo.”

Nimetafakari na kusali juu ya ushauri wa Baba. Kila mara nimejiuliza ikiwa hakika najua kile inachomaanisha kamwe kutoacha fursa ya kumshuhudia Yesu Kristo.

Kama wewe, mara kadha wa kadha nimesimama Jumapili ya kwanza ya mwezi na kutoa ushuhuda juu ya Kristo. Mara nyingi nimeshuhudia ukweli wa injili kama sehemu ya somo. Kwa uthabiti nimefundisha ukweli na kutangaza uungu wa Kristo kama mmisionari.

Hata hivyo kusihi huku kulikuwa binafsi zaidi! Ilionekana kama vile alikuwa akisema, “Bonnie, usiache ulimwengu ukushinde! Baki mkweli kwenye maagano yako na Mwokozi. Tafuta uzoefu wa baraka Zake kila siku, na uweze kushuhudia kupitia Roho Mtakatifu juu ya nguvu Zake na uwepo Wake katika maisha yako!”

Tunaishi katika ulimwengu ulioanguka, wenye uharibifu ukivuta macho na mioyo yetu chini badala ya kuelekea juu mbinguni. Kama vile Wanefi katika 3 Nefi 11, tunamuhitaji Yesu Kristo. Je, unaweza kujifikiria ukiwa pale, kati kati ya watu waliopitia taharuki na uharibifu mkubwa? Ingekuwaje kusikia mwaliko binafsi wa Bwana:

“Inukeni na mje kwangu, ili mweke mikono yenu kwenye mbavu zangu, na kwamba muweze kuhisi alama za misumari katika mikono yangu na miguu yangu, na kwamba mjue kwamba mimi ni Mungu … Mungu wa dunia nzima, na nimeuawa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu.

“Na … umati ulisogea mbele … mmoja mmoja … na waliweza kuona kwa macho yao na kuhisi kwa mikono yao, na walijua … na walishuhudia wao wenyewe.”1

Wanefi kwa shauku walisonga mbele na kuweka mikono yao ubavuni Mwake, na kuhisi alama za misumari katika mikono na miguu Yake, ili kwamba waweze kuwa mashahidi wao wenyewe kwamba huyu alikuwa Kristo. Kadhalika, watu wengi waaminifu ambao tumewasoma kwenye Agano Jipya mwaka huu walisubiri kwa hamu kuja kwa Kristo. Kisha walitoka mashambani mwao, sehemu zao za kazi na kwenye meza zao za chakula na kumfuata Yeye, wakimsogelea Yeye, wakikusanyika kumzunguka Yeye na kuketi Naye. Je, nasi tuna shauku ya kushuhudia sisi wenyewe kama umati kwenye maandiko? Je, baraka tunazotafuta zinahitajika kwa uchache kuliko zao?

Kristo alipowatembelea Wanefii kwenye hekalu lao, mwaliko Wake haukuwa kusimama kwa mbali na kumtizama Yeye, bali kumgusa, kuhisi wao wenyewe uhalisia wa ubinadamu wa Mwokozi. Ni kwa jinsi gani tunaweza kusonga karibu zaidi ili tupate ushahidi binafsi juu ya Yesu Kristo? Hii inaweza kuwa sehemu ya kile baba yangu alichojaribu kunifundusha. Wakati tunaweza tusifurahie ukaribu wa kimwili kama ule wa wale waliotembea na Kristo wakati wa huduma Yake duniani, kupitia Roho Mtakatifu tunaweza kupata uzoefu wa nguvu zake kila siku! Kadri tunavyohitaji!

Wasichana duniani kote wamenifunza mengi kuhusu kumtamfuta Kristo na kupata ushahidi binafsi wa kila siku kumhusu Yeye. Acha nishiriki hekima ya wawili kati yao:

Livvy ametazama mkutano mkuu maisha yake yote. Kimsingi, kwenye familia yake kama desturi wanatazama vikao vyote vitano. Hapo kabla, mkutano mkuu kwa Livvy ilimaanisha kupatwa au kushikwa na usingizi usiotarajiwa. Lakini mkutano mkuu wa Oktoba iliyopita ulikuwa tofauti. Ulikuwa wa kibinafsi.

Safari hii, Livvy aliamua kuwa mpokeaji makini. Alizima vitoa taarifa kwenye simu yake na kuandika misukumo ya Roho. Alishangazwa alipohisi vitu maalumu ambavyo Mungu alitaka yeye asikie na afanye. Uamuzi huu ulileta utofauti katika maisha yake kwa haraka.

Siku chache baadae rafiki zake walimwalika kwenye sinema isiyo na maadili mema. Alisema, “Nilikumbuka maneno na roho ya kwenye mkutano vikirejea kwenye moyo wangu, na nilijisikia nikikataa mwaliko.” Alishiriki pia alikuwa na ujasiri wa kushiriki ushuhuda wake wa Mwokozi katika kata yake.

Baada ya matukio haya alisema, “Kitu cha kushangaza ni kwamba, nilipojisikia nikishuhudia kuwa Yesu ndiye Kristo, nilihisi Roho Mtakatifu akithibitisha hilo tena kwangu.”

Livvy hakuweka juhudi kidogo kwenye wikiendi hiyo ya mkutano; aliweka juhudi kubwa, akili na roho na alimpata Mwokozi.

Na kisha kuna Maddy. Wakati familia yake ilipoacha kuhudhuria kanisani, Maddy alikanganyikiwa na hakujua nini cha kufanya. Aligundua kitu muhimu kilikua kinapungua. Kwa hiyo, katika umri wa miaka 13, Maddy alianza kwenda kanisani peke yake. Ingawa kuwa peke yake ilikuwa wakati mwingine vigumu na ya kuchosha, alijua angempata Mwokozi kanisani na alitaka kuwa Mwokozi alipo. Alisema, “kanisani moyo wangu ulihisi kama palikuwa ni nyumbani.”

Maddy alishikilia ukweli kwamba familia yake ilikuwa imeunganishwa pamoja milele. Alianza kwenda na wadogo zake kanisani na kusoma maandiko pamoja nao nyumbani. Hatimaye mama yake alianza kujumuika nao. Maddy alimweleza mama yake hamu yake ya kuhudumu misheni na kumuomba kama angeweza kuhudhuria hekaluni pamoja naye.

Leo Maddy yupo kituo cha mafunzo ya umisionari. Anahudumu. Anamshuhudia Kristo. Mfano wake ulisaidia kuwaongoza wazazi wake wote kurudi hekaluni na kurudi kwa Kristo.

Kama Livvy na Maddy, tunapochagua kumtafuta Kristo, Roho atamshuhudia Yeye katika hali nyingi tofauti. Shuhuda hizi za Roho hujitokeza tunapofunga, kusali, kusubiri, na kusonga mbele. Ukaribu wetu kwa Kristo hukua kupitia kuabudu mara kwa mara hekaluni, kutubu kila siku, kujifunza maandiko, kuhudhuria kanisani na seminari, kutafakari baraka zetu za patriaki, kupokea ibada tukiwa wenye kustahiki, na kuheshimu maagano matakatifu. Yote haya humwalika Roho kuangazia akili zetu, na huleta nyongeza ya amani na ulinzi. Lakini je, tunaziheshimu kama fursa takatifu za kushuhudia juu ya Kristo?

Nimehudhuria hekaluni mara nyingi, lakini ninapoabudu katika nyumba ya Bwana, inanibadilisha. Wakati mwingine nikiwa ninafunga, ninajikuta nashinda tu njaa, lakini wakati mwingine ninasherehekea kwa Roho nikiwa na lengo. Wakati mwingine nimekuwa na sala za kujirudiarudia zisizo na mpangilio, lakini pia nimekuja kwa shauku kupokea ushauri kutoka kwa Bwana kupitia sala.

Kuna nguvu katika kufanya mazoea haya matakatifu kutokuwa kama orodha bali zaidi kama ushuhuda. Mchakato utakuwa wa taratibu lakini utakuzwa kwa utendaji makini wa kila siku na uzoefu wenye malengo kwa Kristo. Kadiri daima tunavyotenda juu ya mafundisho Yake, tunapata ushuhuda kumhusu Yeye; tunajenga uhusiano na Yeye na Baba yetu wa Mbinguni. Tunaanza kuwa kama Wao.

Adui hutengeneza kelele nyingi kiasi kwamba inakuwa vigumu kusikiliza sauti ya Bwana. Dunia yetu, changamoto zetu, hali zetu hazitakuwa kimya, lakini sisi tunaweza na tunapaswa kuwa na njaa na kiu ya mambo ya Kristo “kumsikiliza Yeye” kwa usahihi.2 Tunataka kutengeneza misuli ya kumbukumbu ya ufuasi na ushuhuda ambayo italeta kwenye fokasi utegemezi wetu kwa Mwokozi kila siku.

Baba yangu amefariki kwa zaidi ya miaka 11 sasa, lakini maneno yake bado yapo hai ndani yangu. “Bonnie, usiache kamwe nafasi ya kushuhudia juu ya Kristo.” Ninawaalika muungane nami katika kukubali mwaliko wake. Mtafute Kristo kila mahala―nina waahidi Yupo!3 Furaha ya kweli ipo kwenye utayari wetu wa kwenda karibu na Kristo na kumshuhudia sisi wenyewe.

Tunajua kwamba katika siku za mwisho, “kila goti litapigwa, na kila ulimi utakiri” kuwa Yesu ndiye Kristo.4 Ninaomba kwamba ushahidi huu utakuwa jambo la kawaida na la asili kwetu sasa—kwamba tutachukua kila fursa kwa shangwe tukishuhudia: Yesu Kristo yu hai!

Oh, ni jinsi gani ninampenda. Jinsi gani tuna shukrani kwa ajili ya Upatanisho Wake usio na mwisho ambao “umefanya uwezekano wa uzima wa milele na kutokufa kuwa uhalisia [kwetu] sote.”5 Ninashuhudia juu ya wema wa Mwokozi wetu na utukufu Wake mkuu katika jina Lake takatifu, hata Yesu Kristo, amina.

Chapisha