Mkutano Mkuu
Baraka Yako ya Patriaki—Mwongozo wenye Uvuvio kutoka kwa Baba wa Mbinguni
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Baraka Yako ya Patriaki—Mwongozo wenye Uvuvio kutoka kwa Baba wa Mbinguni

Baraka yangu ya patriaki ilinisaidia nielewe utambulisho wangu wa kweli wa milele—nilikuwa nani hasa na ningeweza kuwa nani.

Nililelewa na wazazi wema ambao walitupenda na kutufunza sisi, watoto wao, injili kwa uaminifu. Cha kuhuzunisha, walikuwa na changamoto katika ndoa yao. Nilikuwa mtoto wa Msingi wakati nilipoambiwa kwamba wangeweza kutalikiana siku moja na mimi pamoja na ndugu zangu tungechagua mzazi yupi wa kuishi naye. Kama matokeo, kwa miaka mingi nilipitia wasiwasi mkubwa, hata hivyo, zawadi kutoka kwa Baba yangu wa Mbinguni hatimaye ilibadili kila kitu kwangu—baraka yangu ya patriaki.

Nikiwa na miaka 11, nikiwa na hofu kubwa kuhusu uhusiano wa wazazi wangu, kwa dhati nilitamani baraka yangu ya patriaki. Nilifahamu kwamba Baba yangu wa Mbinguni alinifahamu vyema na kujua hali zangu mahsusi. Na pia nilijua ningepokea mwelekeo kutoka Kwake. Mara moja baada ya kufika miaka 12, nilipokea baraka yangu ya partiaki. Hiyo ilikuwa zaidi ya nusu karne iliyopita, lakini ninakumbuka dhahiri kila kitu cha uzoefu ule mtakatifu.

Kwa shukrani, tuna mwongozo wenye uvuvio kuhusu baraka za patriaki katika Kitabu cha Maelezo ya Jumla cha Kanisa:

“Kila muumini mwenye kustahili, aliyebatizwa ana haki ya kupokea baraka ya patriaki, ambayo hutoa mwongozo wenye uvuvio kutoka kwa Baba wa Mbinguni.”

Muumini anapaswa kuwa “amepevuka vya kutosha kuelewa asili ya umuhimu na utakatifu wa baraka hii” na “kuelewa mafundisho ya msingi ya injili.”

“Kiuhalisia muumini anapaswa kuwa kijana mkubwa vya kutosha kwamba maamuzi mengi muhimu katika maisha bado yanatazamiwa.” “Viongozi wa ukuhani hawapaswi kuweka umri unaofaa kwa ajili ya muumini kupokea baraka ya patriaki.”

“Kila baraka ya patriaki ni takatifu, ya faragha na binafsi. …”

“Mtu anayepokea baraka ya patriaki anapaswa kuthamini maneno yake, kuyatafakari na kuishi kwa kustahili kupokea baraka zilizoahidiwa katika maisha haya na milele.”1

Rais wetu mpendwa Russell M. Nelson amefundisha tena na tena kuhusu umuhimu wa baraka ya patriaki,2 kwamba inampa kila mpokeaji “tamko la ukoo kurudi nyuma mpaka kwa Ibrahimu, Isaka na Yakobo”3 na kwamba “ni maandiko binafsi kwako.”4

Baraka yangu ya patriaki ilikuwa ya muhimu sana kwangu nilipokuwa mdogo kwa sababu kadhaa. Kwanza, kupitia nguvu ya Roho Mtakataifu, baraka yangu ya patriaki ilinisaidia nielewe utambulisho wangu wa kweli wa milele—nilikuwa nani hasa na ningeweza kuwa nani. Ilinisaidia nijue, kama vile Rais Nelson alivyofundisha, kwamba nilikuwa “ni mwana wa Mungu,” “ni [mtoto] wa agano,” na “ni mfuasi wa Yesu Kristo.”5 Nilijua kwamba nilijulikana na kupendwa na Baba yangu wa Mbinguni na Mwokozi wangu na kwamba Wao walijihusisha binafsi katika maisha yangu. Hii ilinisaidia nisonge karibu Nao na niongeze imani yangu na tumaini Kwao.

Rafiki mpendwa aliyejiunga na Kanisa kama kijana mkubwa alisema: “Wakati patriaki alipoweka mikono yake juu ya kichwa changu na kutaja jina langu, kila kitu kilibadilika … si tu wakati huo bali kwa maisha yangu yote. Kwa haraka nilipata hisia kwamba—kupitia nguvu ambazo patriaki alizungumza—nilijulikana kikamilifu na kwa kina. Maneno aliyoyazungumza yalipenya utu wangu wote. Nilifahamu kwamba Baba yangu wa Mbinguni alinifahamu, nje na ndani.”

Kujua mimi nilikuwa nani hasa kulinisaidia nielewe na nitamani kufanya kile Mungu alichotarajia kwangu.6

Hii iliniongoza kujifunza maagano niliyokuwa nimefanya na baraka zilizoahidiwa katika agano la Mungu kwa Ibrahimu.7 Ilinipa mtazamo wa milele ambao ulinipa msukumo wa kuyashika maagano yangu kwa ukamilifu.

Nilisoma baraka yangu ya patriaki mara kwa mara, kama kijana, mara nyingi kila siku, kitu kilichonisaidia nihisi faraja, ushawishi elekezi wa Roho Mtakatifu, ambaye alisaidia nipunguze wasiwasi wangu kadiri nilivyofuata misukumo Yake. Hii iliongeza hamu yangu ya kualika nuru, ukweli na Roho Mtakatifu kwa kujifunza maandiko yangu na kusali kila siku na kujaribu kwa bidii zaidi kujifunza na kufuata mafundisho ya nabii wa Mungu na mitume. Baraka yangu ya patriaki ilinisaidia pia nitamani kuwa mnyenyekevu zaidi kwa mapenzi ya Baba yangu wa Mbinguni, na fokasi hiyo ilinisaidia nipate shangwe kuu, licha ya hali zangu binafsi.8

Nilipokea nguvu ya kiroho kila mara niliposoma baraka yangu ya patriaki. Wazazi wangu hatimaye walipotalikiana, baraka yangu ya patriaki, kama vile Rais Thomas S. Monson alivyofundisha, ilikuwa “tunu binafsi nzuri na yenye thamani,” hata “Liahona binafsi.”9

Sasa, tafadhali msielewe vibaya. Sikuwa mkamilifu. Nilifanya makosa mengi. Mwenza wangu wa milele angethibitisha kwamba bado nakosea. Lakini baraka yangu ya patriaki ilinisaidia na huendelea kunisaidia nitamani kufanya vyema zaidi na kuwa bora zaidi.10 Kusoma baraka yangu ya patriaki mara kwa mara kuliongeza tamanio langu la kuhimili majaribu. Ilinisaidia niwe na tamanio na ujasiri wa kutubu, na toba kwa kiasi kikubwa ikawa mchakato wenye kuleta shangwe.

Ilikuwa muhimu kwangu kupokea baraka ya patriaki wakati nikiwa mdogo na wakati ambapo ushuhuda wangu ulikuwa bado unakua. Na nina shukrani daima kwamba wazazi wangu na askofu walielewa kwamba tamanio langu liliashiria kwamba nilikuwa tayari.

Nilipokuwa na miaka 12, ulimwengu haukuwa wenye kutatiza na kukanganya sana kama ulivyo leo. Rais Nelson ameielezea leo kama “wakati mgumu sana katika historia ya ulimwengu,” ulimwengu ambao “umejaa dhambi” na “ubinafsi.”11 Kwa bahati nzuri vijana wetu leo wamepevuka sana kuliko nilipokuwa na miaka 12 na wao pia wana maamuzi muhimu ya msingi ya kufanya wakiwa vijana! Wao pia wanahitaji kujua wao ni akina nani na kwamba Mungu anawapenda na anawajua kwa ukamilifu!

Si kila mtu atatamani baraka ya patriaki katika umri sawa na mimi. Lakini ninasali kwamba waumini ambao hawajapokea baraka yao ya patriaki watatafuta kwa sala kujua wakati ambapo wapo tayari. Ninaahidi kwamba ikiwa utajiandaa kiroho, uzoefu wako, kama vile wangu, utakuwa mtakatifu kwako. Ninasali pia kwamba wale ambao tayari wamepokea baraka yao ya patriaki wataisoma na kuithamini. Kuthamini baraka yangu ya patriaki nikiwa bado mdogo kulinibariki kwa ujasiri wakati nilipokata tamaa, faraja nilipopata hofu, amani nilipohisi wasiwasi, tumaini nilipokosa tumaini na shangwe pale nilipoihitaji zaidi. Baraka yangu ya patriaki ilisaidia nikuze imani yangu na tumaini kwa Baba yangu wa Mbinguni na Mwokozi wangu. Pia iliongeza upendo wangu Kwao—na bado hufanya hivyo.12

Ninashuhudia kwamba baraka za patriaki hutoa mwongozo wenye uvuvio kutoka kwa Baba wa Mbinguni. Ninatoa ushahidi wangu juu ya uhalisia hai wa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye—Mwokozi wetu, Yesu Kristo—wanaotujua, kutupenda na kutamani kutubariki. Ninajua pia bila shaka kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Mungu duniani leo. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. General Handbook: Serving in The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints, 18.17, 18.17.1, ChurchofJesusChrist.org.

  2. Ona Russell M. Nelson, “Thanks for the Covenant” (Brigham Young University devotional, Nov. 22, 1988), speeches.byu.edu; “A More Excellent Hope” (Brigham Young University devotional, Jan. 8, 1995), speeches.byu.edu; “Identity, Priority, and Blessings” (Brigham Young University devotional, Sept. 10, 2000), speeches.byu.edu; “Roots and Branches,” Liahona, May 2004, 27–29; “Covenants,” Liahona, Nov. 2011, 86–89; “Youth of the Noble Birthright: What Will You Choose?” (Brigham Young University–Hawaii devotional, Sept. 6, 2013), broadcasts.ChurchofJesusChrist.org; “The Book of Mormon, the Gathering of Israel, and the Second Coming,” Ensign, July 2014, 26–31; Liahona, July 2014, 24–29; “Acha Mungu Ashinde,” Liahona, Nov. 2020, 92–95; “Agano la Milele,” Liahona, Okt. 2022, 1–6.

  3. Russell M. Nelson, “Maagano,” 88.

  4. Russell M. Nelson, “Thanks for the Covenant,” speeches.byu.edu.

  5. Russell M. Nelson, “Choices for Eternity” (worldwide devotional for young adults, May 12, 2022), ChurchofJesusChrist.org; emphasis added.

  6. Ona Russell M. Nelson, “Maagano,” 86–89.

  7. Ona Mwanzo 17:1–10; ona pia Russell M. Nelson, “Children of the Covenant,” Ensign, May 1995, 32–34.

  8. Ona Russell M. Nelson, “Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona, Nov. 2016, 81–84.

  9. Thomas S. Monson, “Your Patriarchal Blessing: A Liahona of Light,” Ensign, Nov. 1986, 65–66.

  10. Russell M. Nelson, “Tunaweza Kufanya Vizuri Zaidi na Kuwa Bora Zaidi,” Liahona, Mei 2019, 67–69.

  11. Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” Liahona, Nov. 2022, 95–96.

  12. Inspired by James E. Faust, “Priesthood Blessings,” Ensign, Nov. 1995, 62–64.

Chapisha