Mafundisho ya Yesu Kristo
Tumepewa maandiko ili kuyaelekeza maisha yetu. Ujumbe wangu leo unajumuisha uchaguzi wa maneno ya Mwokozi wetu—kile Yeye alichokisema.
Tunaamini katika Kristo. Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunamwabudu Yeye na kufuata mafundisho Yake katika maandiko.
Kabla ya Anguko, Baba yetu wa Mbinguni alizungumza moja kwa moja na Adamu na Eva. Baada ya hapo, Baba alimtambulisha Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo, awe Mwokozi na Mkombozi wetu na alitupa amri ya “kumsikiliza Yeye.”1 Kutokana na maelekezo haya tunahitimisha kwamba taarifa za maandiko yaliyotamkwa na “Mungu” au “Bwana” daima yote ni maneno ya Yehova, Bwana aliyefufuka, Yesu Kristo.2
Tumepewa maandiko ili kuyaelekeza maisha yetu. Kama nabii Nefi alivyotufundisha sisi, tunapaswa “kushiriki maneno ya Kristo; kwani tazama maneno ya Kristo yatawaelezea vitu vyote mnavyostahili kutenda.”3 Maandiko mengi ambayo hutoa taarifa ya huduma ya Yesu duniani ni maelezo ya kile ambacho Yeye alifanya. Ujumbe wangu leo unajumuisha uchaguzi wa maneno ya Mwokozi wetu—kile Yeye alichokisema. Haya ndiyo maneno yaliyorekodiwa katika Agano Jipya (ikijumuisha nyongeza za uvuvio za Joseph Smith) na katika Kitabu cha Mormoni. Mengi ya machaguzi haya yapo katika mtiririko kadiri ambavyo Mwokozi wetu aliyazungumza.
“Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuingia ufalme wa Mungu.”4
“Na heri wale … [walio] na njaa na kuwa na kiu kwa ajili ya haki, kwani watashibishwa na Roho Mtakatifu.”5
“Heri wapatanishi: maana hao wataitwa wana wa Mungu.”6
“Mmesikia kwamba imenenwa na wale wa kale, Usizini:
“Lakini mimi nawaambia, kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.”7
“Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na umchukie adui yako.
“Lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, wabarikini wanao walaani, watendeeni mema wanao wachukia, na waombeeni wale wanaowatumia kwa madharau na wanaowaudhi;
“Ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.”8
“Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia:
“Lakini kama hamtawasamehe watu makosa yao, Baba yenu hatawasamehe makosa yenu.”9
“Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake: lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, kwa hiyo ulimwengu huwachukia ninyi.”10
“Kwa hiyo, usitafute mambo ya ulimwengu huu bali kwanza tafuteni kujenga ufalme wa Mungu, na kustawisha haki zake, na mambo haya yote mtazidishiwa.”11
“Kwa hivyo vitu vyote ambavyo mngetaka kwamba watu wawafanyie, wafanyie pia wengine, kwani hii ni sheria na manabii.”12
“Jihadharini na manabii wa uwongo, ambao huwajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali.
“Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?
“Hata hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; lakini mti mwovu huzaa matunda mabaya.”13
“Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”14
“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.
“Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”15
“Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.
“Na sasa kwa mtu kuchukua msalaba wake, ni kukana mwenyewe maovu yote, na kila tamaa ya kiulimwengu, na kushika amri zangu.”16
“Kwa hiyo, achaneni na ulimwengu, na muokoe roho zenu; kwani binadamu ananufaika nini, kama atapata ulimwengu wote, na kupoteza nafsi yake? Au binadamu atatoa nini kubadilishana na nafsi yake?”17
“Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kama mimi nanena kwa nafsi yangu tu.”18
“Na ninawaambia, Ombeni, na mtapewa; tafuteni, na mtapata, bisheni, na mtafunguliwa.
“Kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.”19
“Kwamba kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili: na hao nao imenipasa kuwaleta, na watasikia sauti yangu; na kutakuwa na kundi moja, na mchungaji mmoja.”20
“Yesu alimwambia, mimi ndimi huo ufufuo, na uzima: yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi:
“Na yeyote kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele.”21
“[Amri kuu katika sheria ni:] Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.
“Hii ndiyo amri iliyo kuu tena ni ya kwanza.
“Na ya pili yafanana nayo, Mpende jirani yako kama nafsi yako.
“Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.”22
“Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye: naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda, na kujidhirihisha kwake.”23
“Amani nawaachieni, amani yangu nawapa: niwapavyo mimi, sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”24
“Hii ni amri yangu, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi.”25
“Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe: nishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo.”26
“Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu:
“Mkiwafundisha kuyashika yale yote Niliyo waamuru nyinyi: na lo, Nipo pamoja nanyi daima, hata mwisho wa ulimwengu.”27
Baada ya huduma Yake katika Nchi Takatifu, Yesu Kristo aliwatokea watakatifu katika bara la Amerika. Haya ni baadhi ya maneno aliyoyazungumza kwao:
“Tazama, Mimi ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Niliumba mbingu na dunia, na vitu vyote vilivyomo. Nilikuwa na Baba kutoka mwanzo. Niko ndani ya Baba, na Baba ndani yangu; na ndani yangu Baba ametukuza jina lake.”28
“Mimi ni nuru na uzima wa ulimwengu. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho.
“Na hamtatoa kwangu tena kumwagwa kwa damu; ndiyo, dhabihu na sadaka zenu za kuteketezwa zitakomeshwa, kwani sitakubali dhabihu na sadaka zenu zozote za kuteketezwa.
“Na mtatoa kwangu dhabihu ya moyo uliopondeka na roho iliyovunjika. Na yeyote atakayekuja kwangu na moyo uliopondeka na roho iliyovunjika, huyo nitambatiza kwa moto na Roho Mtakatifu. …
“Tazama, nimekuja duniani kuleta ukombozi katika ulimwengu, ili kuokoa dunia kutokana na dhambi.”29
“Na tena nawaambia, lazima mtubu na mbatizwe katika jina langu na muwe kama mtoto mchanga au hamtarithi ufalme wa Mungu kwa vyovyote.”30
“Kwa hivyo, ningependa kwamba mngekuwa wakamilifu hata kama vile nilivyo, au Baba yenu ambaye yuko mbinguni ambaye ni mkamilifu.”31
“Amin, amin, ninawaambia, lazima mjihadhari na kusali daima, msije mkajaribiwa na ibilisi, na mwongozwe mbali kama mateka wake.”32
“Kwa hivyo lazima msali siku zote kwa Baba katika jina langu.”33
“Kwa hivyo, chochote mtakachofanya, mfanye katika jina langu; kwa hiyo mtaita kanisa kwa jina langu.”34
“Tazama, nimewapatia injili yangu, na hii ndiyo injili ambayo nimewapatia—kwamba nilikuja kwenye ulimwengu kufanya mapenzi ya Baba, kwa sababu Baba yangu alinituma.
“Na Baba yangu alinituma ili nipate kuinuliwa juu kwenye msalaba; na baada ya kuinuliwa juu kwenye msalaba, kwamba niweza kuwaleta watu wote kwangu, … kuhukumiwa kwa vitendo vyao, ikiwa vitakuwa vizuri au ikiwa vitakuwa viovu.”35
“Sasa hii ndiyo amri: Tubuni, ninyi nyote katika sehemu zote za dunia, na mje kwangu na mbatizwe katika jina langu ili muweze kutakaswa kwa kupokea Roho Mtakatifu, ili muweze kusimama mbele yangu bila mawaa katika siku ya mwisho.”36
Tunaamini katika Kristo. Ninahitimisha na kile Yeye alichokisema kuhusu namna ya kujua na kufuata mafundisho Yake:
“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”37
Ninathibitisha ukweli wa mafundisho haya katika jina la Yesu Kristo, amina.