Mkutano Mkuu
Baada ya Siku ya Nne
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Baada ya Siku ya Nne

Tunaposonga mbele kwa imani katika Yesu Kristo, siku ya nne daima itakuja. Yeye daima atakuja kutupatia msaada.

Kama tulivyokumbushwa asubuhi hii, leo ni Jumapili ya Matawi, ikiashiria kuingia Yerusalemu kishujaa kwa Mwokozi na mwanzo wa wiki ile takatifu ikitangulia Upatanisho Wake mkuu, ambao ungejumuisha kuteseka Kwake, Kusulubiwa na Ufufuko Wake.

Punde kabla ya kuingia Kwake mjini kulikotolewa unabii, Yesu Kristo alikuwa akijishughulisha na huduma Yake wakati alipopokea taarifa kutoka kwa rafiki Zake wapendwa Mariamu na Martha kwamba kaka yao Lazaro alikuwa mgonjwa.1

Japo ugonjwa wa Lazaro ulikuwa mzito, Bwana “bado alikaa siku mbili pale pale alipokuwapo. Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Yudea tena.”2 Kabla ya kuanza safari kuelekea nyumba ya rafiki zake huko Bethania, “Yesu akawaambia [wanafunzi wake] waziwazi, Lazaro amekufa.”3

Yesu alipofika Bethania na kukutana na Martha na kisha Mariamu—labda kwa kukosa tumaini kwa kuchelewa Kwake—kila mmoja alimsalimia akisema, “Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa.”4 Martha alieleza zaidi, “Ananuka sasa; maana amekuwa mfu kwa siku nne.”5

Siku hizi nne zilikuwa za kipekee kwa Mariamu na Martha. Kulingana na baadhi ya imani za kiyahudi, iliaminika kwamba roho ya mtu aliyekufa ingebakia na mwili kwa muda wa siku tatu, ikitoa tumaini kwamba uhai bado ungewezekana. Hata hivyo, kufikia siku ya nne tumaini hilo lilipotea, huenda kwa sababu mwili ungeanza kuoza na “kunuka.”6

Mariamu na Martha walikuwa katika hali ya kukata tamaa. “Basi Yesu alipomwona [Mariamu] analia, … aliugua rohoni, akafadhaika roho yake,

“Akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame.”7

Ni wakati huu ambapo tunaona moja ya miujiza mikuu wakati wa huduma ya Mwokozi duniani. Kwanza Bwana alisema, “Liondoeni jiwe.”8 Kisha baada ya kumshukuru Baba Yake, “alilia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje.

“Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.”9

Kama Mariamu na Martha, tunayo fursa ya kupitia yote ya duniani, hata huzuni10 na udhaifu.11 Kila mmoja wetu atapitia maumivu ya moyo yanayoambatana na kumpoteza mpendwa. Safari yetu ya duniani inaweza kujumuisha magonjwa binafsi au ugonjwa wa kudhoofisha wa mpendwa, msongo wa mawazo, wasiwasi au changamoto nyinginezo za akili; ugumu wa pesa; usaliti; dhambi. Na wakati mwingine haya huambatana na hisia za kukosa tumaini. Mimi si tofauti. Kama nyinyi, nimepitia changamoto lukuki zinazoweza kutarajiwa katika maisha haya. Nimevutiwa na simulizi hii kuhusu Mwokozi na kile inachonifundisha kuhusu uhusiano wetu pamoja Naye.

Wakati wa hofu zetu kuu, sisi, kama Mariamu na Martha, tunamtafuta Mwokozi au kumwomba Baba kwa ajili ya msaada Wake wa kiungu. Hadithi ya Lazaro inatufundisha kanuni ambazo zinaweza kutumika katika maisha yetu wenyewe tunapokabiliana na changamoto binafsi.

Mwokozi alipofika Bethania, wote walikuwa wamepoteza tumaini kwamba Lazaro angeweza kuokolewa—ilikuwa ni siku nne, na alikuwa ameshakufa. Wakati mwingine katika changamoto zetu, tunaweza kuhisi kama Kristo amechelewa na tumaini na imani yetu vikajaribiwa. Ushahidi na ushuhuda wangu ni kwamba tunaposonga mbele kwa imani katika Yesu Kristo, siku ya nne daima itakuja. Daima Yeye atakuja kutusaidia au kurudisha matumaini yetu kwenye uhai. Yeye ameahidi:

“Msifadhaike mioyoni mwenu.”12

“Sitawaacha ninyi yatima: Naja kwenu.”13

Wakati mwingine inaweza kuonekana kama haji kwetu mpaka siku ya nne, baada ya tumaini lote kupotea. Lakini kwa nini achelewe? Rais Thomas S. Monson alifundisha, “Baba yetu wa Mbinguni, ambaye hutupatia sisi mengi sana ya kufurahia, pia anajua kwamba tunajifunza na kukua na kuwa imara tunapokabiliana na kushinda majaribio ambayo lazima tuyapitie.”14

Hata Nabii Joseph Smith alikutana na uzoefu huu wa siku ya nne. Je, unakumbuka kusihi kwake? “Ee Mungu, uko wapi? Na ni wapi lilipo hema lifichalo mahali pako pa kujificha?”15 Kadiri tuendeleavyo kumtumainia Yeye, tunaweza kutegemea jibu la: “Mwanangu [au binti], amani iwe katika nafsi yako; taabu yako na mateso yako yatakuwa kwa muda mfupi.”16

Ujumbe mwingine tunaoweza kujifunza kutoka katika hadithi ya Lazaro ni jukumu gani lililo letu wenyewe linaloweza kuwa kwenye msaada wa kiungu tunaouhitaji. Yesu alipolisogelea kaburi, Yeye kwanza alisema kwa wale waliokuwepo pale, “Liondoeni jiwe.”17 Kwa uwezo aliokuwa nao Mwokozi, Je, Yeye asingeweza kimiujiza kuondoa jiwe bila jitihada yo yote? Hili lingekuwa la kuvutia kuona na uzoefu usiosahaulika, lakini Yeye aliwaambia wengine, “Liondoeni jiwe.”

Pili, Bwana “alilia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje.”18 Je, isingekuwa ya kuvutia kama Bwana, Yeye mwenyewe, kimiujiza angemweka Lazaro kwenye lango la kaburi ili aonekane moja kwa moja na umati baada ya jiwe kuondolewa?

Tatu, Lazaro alipotoka, alikuwa “amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.”19 Nina uhakika Bwana alikuwa ana uwezo wa kumfanya Lazaro asimame mlangoni mwa kaburi, akiwa safi na kuweza kumwongelesha na sanda yake ikiwa imekunjwa vyema.

Je, nini dhumuni la kuangazia vitu hivi? Kila moja ya vitu hivi vitatu vina mfanano—hakuna kilichohitaji msaada wa kiungu wa Kristo. Kile ambacho wanafunzi Wake wangeweza kufanya, aliwaelekeza wao wafanye. Wafuasi kwa hakika walikuwa wanaweza kuondoa jiwe wao wenyewe; Lazaro, baada ya kurudishiwa uhai, alikuwa na uwezo wa kusimama na kusogea mlangoni mwa kaburi; na wale waliompenda Lazaro wangeweza kumsaidia kuondoa sanda yake.

Hata hivyo, ilikuwa ni Kristo pekee aliyekuwa na nguvu na mamlaka ya kumrudishia uhai Lazaro kutoka kwa wafu. Mtazamo wangu ni kwamba Mwokozi anategemea sisi tufanye yote tuwezayo, na Yeye atafanya kile ambacho Yeye pekee anaweza kufanya.20

Tunajua kwamba “imani [katika Bwana Yesu Kristo] ni kanuni ya matendo”21 na miujiza haileti imani, lakini imani imara hukuzwa kwa utiifu kwenye injili ya Yesu Kristo. Kwa maneno mengine, imani huja kwa haki.”22 Tunapojitahidi kutenda kwa haki kwa kufanya na kushika maagano matakatifu na kutumia mafundisho ya Kristo katika maisha yetu, imani yetu haitakuwa tu ya kutosha kutufikisha siku ya nne, lakini kwa msaada wa Bwana pia tutaweza kuondoa mawe katika njia zetu, kuinuka kutoka kukata tamaa, na kulegeza yote yaliyotufunga. Wakati Bwana anatarajia sisi “tufanye yote yaliyo katika uwezo wetu,”23 kumbuka kwamba atatoa msaada unaohitajika katika vyote hivi kama tutamwamini Yeye.

Je, tunaondoshaje mawe na kujenga juu ya mwamba wake?24 Tunaweza kuishi kwa ushauri wa manabii.

Kwa mfano, Oktoba iliyopita Rais Russell M. Nelson alituomba tushughulikie shuhuda zetu wenyewe juu ya Mwokozi na injili Yake, kuzifanyia kazi na kuzilea, kuzilisha kweli na kuepuka kuzichafua kwa falsafa za uongo za wasioamini. Alimwahidi kila mmoja wetu, “Unapofanya uimarishaji ushuhuda wako juu ya Yesu Kristo kuwa kipaumbele chako endelevu kwa hali ya juu zaidi, tazamia miujiza kutokea katika maisha yako.”25

Tunaweza kufanya hili!

Je, tunawezaje kifikira kuinuka na kusonga mbele? Tunaweza kwa shangwe kutubu na kuchagua kutii amri. Bwana alisema, “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye: naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda, na kujidhirihisha kwake.”26 Tunaweza kujitahidi kutubu kila siku na kwa shangwe kusonga mbele kwa moyo wa dhati uliojaa upendo kwa Bwana.

Tunaweza kufanya hili!

Je, tunawezaje, kwa msaada wa Bwana, kujiondoa kwenye yote yatufungayo? Kwa makusudi tunaweza kujifunga kwanza kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye, Yesu Kristo, kupitia maagano. Mzee D. Todd Christofferson alifundisha, “Ni kipi chanzo cha nguvu [zetu] za kimaadili na kiroho na tunakipataje? Chanzo ni Mungu. Njia yetu ya kufikia nguvu hiyo ni kwa njia ya maagano yetu na Yeye. … Katika makubaliano haya ya kiungu, Mungu hujifunga katika kutusaidia, kututakasa na kutuinua kama malipo kwa dhamira yetu ya kumtumikia na kushika amri Zake.”27 Tunaweza kufanya na kushika maagano matakatifu.

Tunaweza kufanya hili!

“Liondoeni hilo jiwe.” “Njoo huku nje.” “Mfungueni na mkamwache aende zake.”

Ushauri, amri na maagano. Tunaweza kufanya hili!

Mzee Jeffrey R. Holland aliahidi, “Baraka nyingine huja haraka, nyingine huchelewa, na nyingine haziji hadi tufikapo mbinguni; lakini kwa wale wanaoikubali injili ya Yesu Kristo, zinakuja.”28

Na hatimaye, “Kwa hiyo, changamkeni, na msiogope kwani mimi Bwana nipo pamoja nanyi, na nitasimama karibu yenu.”29

Huu ni ushahidi na ushuhuda wangu, katika jina takatifu la Yeye ambaye daima atakuja, hata Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Yohana 11:3.

  2. Yohana 11:6–7.

  3. Yohana 11:14.

  4. Yohana 11:21, 32.

  5. Yohana 11:39.

  6. “Nafsi, kulingana na imani za Kiyahudi, iliranda randa ndani ya mwili siku tatu baada ya umauti. Kulingana na imani ya Kiyahudi, hatimaye, kurudisha pumzi kwa mtu aliyekufa haukuwezekana katika siku ya nne, kwani roho haitaingia tena kwenye mwili ambao hali yake imebadilika. Ilikuwa ya kuvutia sana kama ushahidi wa kimuujiza kwamba Yesu Kristo alimfufua Lazaro siku ya nne. Kwa hiyo siku ya nne ilikuwa na maana maalumu hapa na huchukuliwa na msimuliaji kwa matumizi yahusianayo na muujiza mkubwa kuliko miujiza yote iwezekanayo ya ufufuko” (Ernst Haenchen, John 2: A Commentary on the Gospel of John, Chapters 7–21, ed. Robert W. Funk and Ulrich Busse, trans. Robert W. Funk [1984], 60–61).

  7. Yohana 11:33–34.

  8. Yohana 11:39.

  9. Yohana 11:43–44.

  10. Ona Musa 4:22–25.

  11. Ona Etheri 12:27.

  12. Yohana 14:1.

  13. Yohana 14:18.

  14. Thomas S. Monson, “Sitakupungukia Wala Sitakuacha,” Liahona, Nov. 2013, 87. Rais Monson alieleza zaidi kwamba: “Tunajua kwamba kuna nyakati ambapo tutapata huzuni ya kuvunja moyo, wakati ambapo tutaomboleza, na wakati ambapo tunaweza kujaribiwa kupita ukomo wetu. Hata hivyo, shida kama hizo zinaturuhusu sisi kubadilika na kuwa bora, kujenga upya maisha yetu katika njia ambayo Baba yetu wa Mbinguni anatufundisha, na kuwa kitu tofauti kuliko vile tulivyokuwa—bora kushinda tulivyokuwa, wenye uelewa zaidi kushinda tulivyokuwa, wenye huruma kuliko tulivyokuwa, na wenye ushuhuda thabiti kuliko tuliokuwa nao awali” (“Sitakupungukia Wala Sitakuacha,” 87). Ona pia Mafundisho na Maagano 84:119: “Kwani Mimi, Bwana, nimeunyosha mkono wangu ili kuzitakasa nguvu za mbinguni; hamwezi kuona hili sasa, bado kipindi kifupi nanyi mtaona, na kujua kuwa Mimi ndiye, na kwamba nitakuja.”

    Ona pia Mosia 23:21–24:

    “Walakini Bwana anaonelea vyema kuwarekebisha watu wake; ndiyo, anajaribu subira na imani yao.

    “Walakini—yeyote atakayeweka imani yake kwake, yeye atainuliwa juu siku ya mwisho. Ndiyo, na hivi ndivyo ilivyokuwa na watu hawa.

    “Kwani tazama, nitakuonyesha kwamba walitiwa utumwani, na hakuna yeyote ambaye angewakomboa ila tu Bwana Mungu wao, ndiyo, hata Mungu wa Ibrahimu na Isaka na wa Yakobo.

    “Na ikawa kwamba aliwakomboa, na akawaonyesha uwezo wake mkuu, na walifurahi sana.”

  15. Mafundisho na Maagano 121:1.

  16. Mafundisho na Maagano 121:7.

  17. Yohana 11:39.

  18. Yohana 11:43.

  19. Yohana 11:44.

  20. Rais Russell M. Nelson alisema: “Mara nyingi, mimi pamoja na washauri wangu tumetazama kupitia macho yaliyojaa machozi pale Yeye alipoingilia kati hali zenye changamoto baada ya kuwa tumefanya kadiri ya uwezo wetu na hatuwezi kufanya zaidi. Hakika tunashangazwa” (“Ujumbe wa Makaribisho,” Liahona, Mei 2021, 6).

  21. Bible Dictionary, “Faith.”

  22. Mwongozo wa Maandiko, “ImaniFaith,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org.

  23. Mafundisho na Maagano 123:17.

  24. Ona 3 Nefi 11:32–39.

  25. Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” Liahona, Nov. 2022, 97.

  26. Yohana 14:21.

  27. D. Todd Christofferson, “Nguvu ya Maagano,” Liahona, Mei 2009, 20.

  28. Jeffrey R. Holland, “Kuhani Mkuu wa Mambo Mema Yajayo,” Liahona,, Jan. 2000, 45.

  29. Mafundisho na Maagano 68:6.

Chapisha