“Kaa Ndani Yangu, Nami Ndani Yako; Kwa Hiyo, Tembea Pamoja Nami”
Ahadi ya Mwokozi ya kukaa ndani yetu ni ya kweli na ipo kwa kila muumini atunzaye maagano ya Kanisa Lake lililorejeshwa.
Henoko nabii wa kale, aliyeelezwa katika Agano la Kale, Mafundisho na Maagano na Lulu ya Thamani Kuu,1 alikuwa chombo muhimu katika kujenga mji wa Sayuni.
Simulizi ya kimaandiko ya wito wa Henoko wa kutumikia inaonesha kwamba “alisikia sauti kutoka mbinguni, ikisema: Henoko, mwanangu, toa unabii kwa watu hawa, na uwaambie—Tubuni, … kwa kuwa mioyo yao imekuwa migumu, na masikio yao hayasikii vyema, na macho yao hayawezi kuona mbali.”2
Na Henoko alipoyasikia maneno haya, akapiga magoti chini ya nchi … na kunena mbele za Bwana, akisema: Kwa nini nimepata upendeleo mbele za uso wako, nami ni kijana mdogo, na watu wote wanichukia; kwa maana mimi si mwepesi wa kusema; kwani mimi ni mtumishi wako?”3
Tafadhali tambua kwamba wakati wa wito wa Henoko wa kutumikia, alifahamu kwa dhati kuhusu mapungufu na madhaifu yake binafsi. Na ninahisi sote wakati mmoja au mwingine katika huduma yetu kwa Kanisa tumehisi zaidi kama Henoko. Lakini naamini jibu la Bwana kwa swali la Henoko la kutaka kujua ni la kutosheleza na hutumika kwetu sote leo.
“Naye Bwana akamwambia Henoko: Enenda zako na ukafanye kama nilivyokuamuru wewe, na hakuna mtu atakayekurarua wewe. “Fumbua kinywa chako, nacho kitajazwa, nami nitakupa maneno. …
“Tazama Roho yangu i juu yako, kwa sababu hiyo maneno yako yote nitayahesabia kuwa haki; na milima itakukimbia mbele yako, na mito itageuka kutoka uelekeo wake; nawe utakaa ndani yangu, nami ndani yako; kwa hiyo tembea pamoja nami.”4
Hatimaye Henoko alikuwa nabii mwenye nguvu na chombo katika mikono ya Bwana katika kukamilisha kazi kuu, lakini hakuanza huduma yake katika njia hiyo ya ukuu! Bali, uwezo wake ulikuzwa kadiri alivyojifunza kukaa na kutembea pamoja na Mwana wa Mungu.
Kwa dhati ninaomba msaada wa Roho Mtakatifu tunapoangazia kwa pamoja ushauri uliotolewa na Bwana kwa Henoko na kile unachoweza kumaanisha kwako na kwangu leo.
Utakaa Ndani Yangu
Bwana Yesu Kristo anatoa mwaliko kwa kila mmoja wetu wa kukaa ndani Yake.5 Lakini tunajifunzaje na hatimaye kukaa ndani Yake?
Neno kaa huashiria kubakia hapo hapo au imara na kuvumilia pasipo kushawishika. Mzee Jeffrey R. Holland alieleza kwamba “kukaa” kama kitendo humaanisha “‘[kubakia]—lakini [kubakia] milele.’ Huo ndio wito wa ujumbe wa injili kwa … kila mmoja … katika ulimwengu. Njoo, lakini njoo ubakie. Njoo kwa dhamira na uvumilivu. Njoo udumu, kwa ajili yako na kwa ajili ya vizazi vyote ambavyo lazima vikufuatie.”6 Hivyo, tunakaa ndani ya Kristo tunapokuwa imara na wasiotingishika katika ibada zetu kwa Mkombozi na malengo Yake matakatifu, nyakati zote nzuri na mbaya.7
Tunaanza kukaa ndani ya Bwana kwa kutumia uhuru wetu wa kimaadili wa kujichukulia juu yetu nira Yake8 kupitia maagano na ibada za injili ya urejesho. Muunganiko wa kimaagano tulionao pamoja na Baba yetu wa Mbinguni na Mwana Wake aliyefufuka na aliye hai ni chanzo kikuu cha mtazamo, tumaini, amani na shangwe ya kudumu; pia ni msingi imara9 ambapo juu yake tunapaswa kujenga maisha yetu.
Tunakaa ndani Yake kwa kujitahidi daima kuimarisha muunganiko wetu binafsi wa kimaagano pamoja na Baba na Mwana. Kwa mfano, kusali kwa dhati kwa Baba wa Milele katika jina la Mwanaye Mpendwa hukuza na huimarisha muunganiko wetu wa kimaagano pamoja Nao.
Tunakaa ndani yake kwa kusherehekea maneno ya Kristo. Mafundisho ya Mwokozi hutuleta sisi, kama watoto wa agano, karibu na Yeye10 na atatuambia yote yatupasayo kutenda.11
Tunakaa ndani Yake kwa kujiandaa kwa dhati kushiriki katika ibada ya Sakramenti, kurejelea na kuakisi kwenye ahadi za maagano yetu na kutubu kwa dhati. Kula sakramenti kwa kustahili ni ushahidi kwa Mungu kwamba tuko radhi kujichukula juu yetu wenyewe jina la Yesu Kristo na kujitahidi “daima kumkumbuka”12 baada ya kipindi cha muda huo mfupi unaohitajika kushiriki katika ibada hiyo takatifu.
Na tunakaa ndani Yake kwa kumtumikia Mungu pale tunapowahudumia watoto Wake na tunapowatumikia kaka na dada zetu.13
Mwokozi alisema, “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.”14
Kwa ufupi nimeelezea njia kadhaa kati ya nyingi ambazo kupitia hizo tunaweza kukaa kwa Mwokozi. Na sasa ninamwalika kila mmoja wetu kama mfuasi Wake kuomba, kutafuta, kubisha na kujifunza wenyewe kwa nguvu ya Roho Mtakatifu njia zingine bora za kumfanya Kristo kuwa kiini cha maisha yetu katika yote tufanyayo.
Na Mimi Ndani Yako
Ahadi ya Mwokozi kwa wafuasi Wake ina pande mbili: kama tukikaa ndani Yake, Yeye atakaa ndani yetu. Lakini je, ni kweli inawezekana kwa Kristo kukaa ndani yako na kwangu—binafsi? Jibu kwa swali hili ni ndiyo!
Katika Kitabu cha Mormoni, tunajifunza kuhusu Alma kufundisha na kushuhudia kwa masikini ambao mateso yao yaliwafanya wajinyenyekeze. Katika maelekezo yake, alilinganisha neno na mbegu ambayo inapaswa kupandwa na kulishwa, na akaelezea “neno” kama maisha, misheni na dhabihu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi.
Alma alisema, “Uanze kuamini katika Mwana wa Mungu, kwamba atakuja kukomboa watu wake, na kwamba atateseka na kufa ili alipie dhambi zao; na kwamba atafufuka tena kutoka kwa wafu, na kutimiza ufufuo, kwamba watu wote watasimama mbele yake, kuhukumiwa katika siku ya mwisho ya hukumu, kulingana na matendo yao.”15
Kwa maelezo haya ya “neno” kutoka kwa Alma, tafadhali tazama muuganiko wa kuvutia anaoueleza.
“Na sasa … natamani kwamba mtapanda hili neno kwenye mioyo yenu, na litakapoanza kuvimba endelea kulistawisha kwa imani yako. Na tazama, itakuwa mti, ukikua ndani yako kwenye maisha yasiyo na mwisho. Na kisha Mungu akubali kwamba mizigo yenu iwe miepesi, kupitia kwa shangwe inayotokana na Mwana wake. Na hata haya yote mnaweza mkafanya mkipenda.”16
Mbegu tunayopaswa kujitahidi kuipanda katika mioyo yetu ni neno—hata maisha, misheni na mafundisho ya Yesu Kristo. Na kama neno litalishwa kwa imani, litaweza kuwa mti ukichipua ndani yetu kwenye maisha yasiyo na mwisho.17
Ni nini ilikuwa ishara ya mti katika ono la Lehi? Mti unaweza kuchukuliwa kama uwakilisho wa Yesu Kristo.18
Wapendwa kaka zangu na dada zangu, je, Neno liko ndani yetu? Je, kweli za injili ya Mwokozi zimeandikwa katika vibao vya nyama za mioyo yetu?19 Je, tunakuja Kwake na hatua kwa hatua tunakuwa zaidi kama Yeye? Je, mti wa Kristo unakua ndani yetu? Je, tunajitahidi kuwa “viumbe [vipya]”20 ndani Yake?21
Pengine uwezekano huu wa kimiujiza ulimsukuma Alma kuuliza, “Je, mmezaliwa kiroho katika Mungu? Mmepokea mfano wake katika nyuso zenu? Mmeshuhudia mabadiliko haya makuu katika mioyo yenu?”22
Tunapaswa daima kukumbuka maelekezo ya Bwana kwa Henoko, “Wewe utakaa ndani Yangu, Nami ndani yako.”23 Na ninashuhudia ahadi ya Mwokozi ya kukaa ndani yetu ni ya kweli na ipo kwa kila muumini atunzaye maagano ya Kanisa Lake lililorejeshwa.
Kwa hiyo, Tembea pamoja Nami
Mtume Paulo aliwasihi waaminio waliompokea Bwana: “enendeni vivyo hivyo katika yeye.”24
Kutembea ndani ya, na pamoja na Mwokozi kunaashiria mambo mawili muhimu ya ufuasi: (1) kutii amri za Mungu, na (2) kukumbuka na kuheshimu maagano matakatifu ambayo hutuunganisha kwa Baba na Mwana.
Yohana alitangaza:
“Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake.
“Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.
“Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli: katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake.
“Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.”25
Yesu anamwita kila mmoja wetu, “Njoo Unifuate”26 na “tembea pamoja Nami.”27
Ninashuhudia kwamba tunaposonga mbele kwa imani na kutembea kwa unyenyekevu wa roho ya Bwana,28 tunabarikiwa kwa nguvu, ulinzi, mwongozo na amani.
Ushuhuda na Ahadi
Alma anaelezea kujali kwa upendo kutoka kwa Bwana kwa nafsi zote hai:
“Tazama, yeye hutoa mwaliko kwa wanadamu wote, kwani mikono ya huruma imenyoshwa kwao, na anasema: Tubuni, na nitawapokea.
“… Njooni kwangu na mtakula matunda ya mti wa uzima; ndiyo, mtakula na kunywa mkate na maji ya uhai bure.”29
Ninasisitiza udhati wa ombi la Mwokozi. Anatamani kumbariki kwa rehema na neema Zake kila mtu anayeishi sasa, aliyewahi kuishi na yule atakayeishi juu ya dunia hii.
Baadhi ya waumini wa Kanisa wanakubali mafundisho, kanuni na shuhuda zitolewazo mara kwa mara kutoka mimbari hii katika Ukumbi wa Mikutano na mikusayiko katika maeneo yote ulimwenguni kuwa ni kweli—na bado wanahangaika kuamini kweli hizi za milele kwamba hutumika katika maisha yao na katika hali zao. Wanaamini kwa dhati na kutumikia kwa dhati, lakini muunganiko wao kimaagano kwa Baba na Mwanaye Mkombozi bado havijawa uhalisia hai na wenye kubadilisha katika maisha yao.
Ninaahidi kwamba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, unaweza kujua na kuhisi kwamba kweli za injili nilizojaribu kuzieleza ni kwa ajili yako—kwa ajili yako kama mtu binafsi.
Kwa shangwe ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wetu anayetupenda na aliye hai. Kama tutakaa ndani Yake, Yeye atakaa ndani yetu.30 Na tukitembea ndani Yake na pamoja Naye, tutabarikiwa kuzaa matunda mengi mazuri. Ninashuhudia hivyo katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.