Mkutano Mkuu
Utulivu kama wa Kristo
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


11:17

Utulivu kama wa Kristo

“Na yeye aliamka, na kuukemea upepo, na kuiambia bahari, Nyamaza, utulie. Na upepo ukakoma, kukawa shwari kuu” (Marko 4:39).

Mara ya mwisho nilipozungumza kwenye mkutano mkuu, mkwe wangu Ryan alinionesha ujumbe wa twitter ambao ulisema, “Kweli? Jina la mwandishi ni Bragg”—ikimaanisha “kujivuna”—“na Bragg huwa hazungumzi kuhusu unyeyekevu? Ni hasara kiasi gani!” Kwa huzuni, kuvunjika moyo kunaendelea.

Don Bragg kama mcheza mpira wa kikapu

Baba yangu wa kupendeza alikuwa mchezaji wa mpira wa kikapu wa marekani wa UCLA chini ya Kocha mahiri John Wooden. Walibakia na ukaribu maisha yote ya baba yangu, na mara kadha wa kadha kocha na mama yangu. Wooden angekuja nyumbani kwetu kwenye chakula cha jioni. Daima alikuwa na furaha kuzungumza nami kuhusu mpira wa kikapu au kitu kingine kilichokuwa akilini mwangu. Wakati mmoja nilimuuliza ni ushauri gani alikuwa nao kwa ajili yangu nilipokuwa ninaingia katika mwaka wangu wa mwisho wa shule ya upili. Daima akiwa mwalimu alisema, “Baba yako aliniambia kwamba umejiunga na Kanisa la Yesu Kristo, kwa hiyo najua una imani katika Bwana. Kwa imani hiyo hakikisha una utulivu katika kila hali. Kuwa mtu mwema kwenye dhoruba.”

Kwa miaka mingi, mazungumzo hayo yamebaki nami. Ushauri huo wa kuwa na amani, kutulia, na kutohofu kwenye hali zote, hasa katika nyakati za dhiki na shinikizo, unatoa mwangwi kwangu. Ningeweza kuona jinsi timu za Kocha Wooden zilicheza kwa utulivu na ufanisi mkuu ambapo walipata ushindi mara 10 kwenye mashindano ya kitaifa.

Lakini utulivu hauzungumzwi sana siku hizi na hautumiwi hata kidogo katika nyakati za ghasia na za mgawanyiko. Mara nyingi hurejelewa kwenye michezo—mchezaji mwenye utulivu hapapatiki kwenye mchezo mgumu au timu yenye upinzani mkubwa kwa sababu ya kukosa utulivu. Lakini sifa hii ya njema ni zaidi ya michezo. Utulivu una matumizi mengi zaidi katika maisha na unaweza kuwabariki wazazi, viongozi, wamisionari, walimu, wanafunzi, na mtu mwingine yoyote anayekabiliana na dhoruba za maisha.

Utulivu wa kiroho hutubariki sisi kubaki watulivu na kufokasi kwenye mambo yaliyo na maana sana hasa wakati tuko chini ya shinikizo. Rais Hugh B. Brown alifundisha, “Imani katika Mungu na ushindi wa mwisho wa haki huchangia kwenye utulivu wa kiakili na kiroho katika kukabiliana na magumu.”1

Rais Russell M. Nelson ni mfano wa ajabu wa utulivu wa kiroho. Wakati fulani, akiwa daktari. Nelson alikuwa akifanya upasuaji wa mshipa wa moyo, presha ya damu ya mgonjwa ghafla ilishuka. Dkt. Nelson kwa utulivu alichunguza hali hiyo na kutambua kwamba kibanio kwa bahati mbaya kilikuwa kimeondolewa na mmoja wa wanatimu. Kilirudishwa mara moja, na Dkt. Nelson alimfariji yule mwana timu, akisema, “bado nakupenda,” kisha akaongezea kwa utani, “Wakati mwingine nakupenda zaidi kuliko nyakati zingine!” Alionesha jinsi dharura inavyopaswa kuchukuliwa—kwa utulivu, kwa kufokasi tu kwenye mambo yaliyo na maana zaidi—kushughulikia dharura. Rais Nelson alisema, “Ni jambo la nidhamu binafsi iliyo kuu sana. Mwitikio wako wa asili ni, ‘Kocha, nitoe nje! Ninataka kwenda nyumbani.’ Lakini bila shaka huwezi. Maisha yanategemea kabisa kwenye timu yote ya upasuaji. Kwa hiyo sharti ubakie mtulivu na asiye na hofu na makini kuliko ulivyokuwa hapo awali.”2

Bila shaka, Mwokozi ni mfano kamili wa utulivu.

Katika Bustani ya Gethesmane, katika uchungu usiofikirika, “jasho lake likawa kama matone makubwa ya damu,”3 Yeye alionyesha mfano mtakatifu wa utulivu kwa kauli rahisi lakini kuu, “Si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.”4 Katika shinikizo kubwa sana ili kuwezesha wokovu wa binadamu, Yesu alionyesha masharti matatu muhimu ambayo yanatusaidia kuelewa utulivu Wake mkuu. Kwanza, Yeye alijua alikuwa nani na alikuwa mkweli kwa misheni Yake takatifu. Kisha, Yeye alijua kwamba kulikuwa na mpango mkuu wa furaha. Na mwishowe, Yeye alijua kwamba kupitia Upatanisho Wake usio na mwisho, wale wote wanaojifunga nira Kwake kwa kufanya na kushika maagano matakatifu yanayotolewa kupitia ibada za ukuhani wataokolewa, kama ilivyofundishwa vyema na Mzee Dale G. Renlund hivi leo.

Kuonyesha utofauti kati ya kuupoteza na kuudumisha utulivu, fikiria kuhusu kile kilichotokea wakati Kristo na Mitume Wake walipoondoka toka Bustani ya Gethesmane. Wakati walipokumbana na askari waliotaka kumkamata Yesu, mwitikio wa Petro ulikuwa wa kupoteza utulivu wake na kwa ukali kukata sikio la mtumishi wa kuhani mkuu, Malko. Mwitikio wa Yesu Kristo, kwa upande mwingine, ulikuwa ni kutunza utulivu Wake na kuleta hali shwari kwenye hali tete kwa kumponya Malko.5

Na kwa wale kati yetu tunaosumbuka kudumisha utulivu na pengine tumekatishwa tamaa, fikiria sehemu iliyobaki ya hadithi ya Petro. Muda mfupi baada ya tukio hili na kuvunjika moyo kwa kukana uhusiano wake na Kristo,5 alisimama mbele ya viongozi wa kidini wale wale ambao walimhukumu Mwokozi, na kwa utulivu mkuu kwenye mahojiano makali yeye alitoa ushuhuda wa kina juu ya utakatifu wa Yesu Kristo.7

Tambua Wewe ni Nani na Kuwa Mkweli kwenye Utambulisho Wako

Acha tufikirie vipengele vya utulivu kama wa Kristo. Kwa kuanza, kwa kujua sisi ni akina nani na kuwa wakweli kwenye utambulisho wetu mtakatifu huleta utulivu. Utulivu kama wa Kristo hutaka kwamba tuepukane na kujilinganisha na wengine au kujifanya kuwa mtu mwingine.8 Joseph Smith alifundisha, “Kama watu hawawezi kuelewa sifa ya Mungu, hawajielewi wao wenyewe.”(9 Haiwezekani tu kuwa na utulivu mtakatifu bila kujua kwamba sisi ni wana na mabinti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo.

Katika hotuba yake “Chaguzi kwa ajili ya Umilele,” Rais Nelson alifundisha kweli hizi za milele kuhusu sisi ni akina nani: sisi ni watoto wa Mungu, sisi ni watoto wa agano na sisi ni wanafunzi wa Kristo. Kisha Yeye aliahidi, “Unapokumbatia kweli hizi, Baba yetu wa Mbinguni atakusaidia kufikia lengo lako kuu la kuishi milele katika uwepo Wake mtakatifu.” Sisi ni viumbe vya kiroho tukiwa na uzoefu wa maisha ya kufa. Kujua sisi ni akina nani na kuwa wakweli kwenye utambulisho huo mtakatifu ni msingi kuelekea kukuza Utulivu kama wa Kristo.

Jua Kwamba Kuna Mpango Mtakatifu

Pili, kukumbuka kwamba kuna mpango mkuu unaoleta ujasiri na utulivu katika hali zenye changamoto. Nefi angeweza “kwenda na kutenda”11 kama Bwana alivyomwamuru “bila kujua kilicho mbeleni”12 vitu ambavyo alikuwa afanye kwa sababu yeye alijua kwamba angeongozwa na Roho, katika kutimiza mpango wa milele wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Utulivu huja wakati tunapoviona vitu kwa mtazamo wa umilele. Bwana amewashauri wanafunzi Wake “inuieni macho yenu”13 na “kuacha taadhima ya milele iwe akilini mwenu.”14 Kwa kuzijumuisha nyakati za changamoto ndani ya mpango wa milele, shinikizo huwa fursa ya kupenda, kutumikia, kufundisha na kubariki. Mtazamo wa umilele huwezesha utulivu kama wa Kristo.

Jua Nguvu Zinazowezesha za Yesu Kristo na Upatanisho Wake.

Na mwisho, nguvu zinazowezesha za Kristo, zilizofanywa kuwezekana kupitia dhabibu Yake ya upatanisho, hutupatia nguvu za kuvumilia na kushinda. Kwa sababu ya Yesu Kristo tunaweza kufanya agano na Mungu na kuimarishwa katika kuweka agano hilo. Sote tunaweza kuunganishwa kwa Mwokozi katika shangwe na utulivu, bila kujali hali zetu.15 Alma sura ya 7 hutufundisha vizuri sana kuhusu nguvu zinazowezesha za Kristo. Katika nyongeza ya kutukomboa kutokana na dhambi, Mwokozi anaweza kutuimarisha katika udhaifu wetu, hofu na changamoto zetu.

Tunapofokasi kwa Kristo, tunaweza kutuliza hofu zetu, kama watu wa Alma walivyofanya huko Helamu.16 Wakati jeshi lililotishia lilipokusanyika, wale wanafunzi waaminifu wa Kristo walionyesha utulivu. Mzee David A. Badnar amefundisha: “Alma aliwashauri waaminio kumkumbuka Bwana na ukombozi ambao Yeye pekee angeutoa (ona 2 Nefi 2:8). Na uelewa wa ulinzi wa Mwokozi uliwawezesha watu kutuliza woga wao.”17 Hii huonyesha mfano wa utulivu.

Mtu Mkuu kwenye Dhoruba

Nuhu alitufundisha mengi kuhusu subira kwenye dhoruba, lakini Mwokozi alikuwa mwalimu mkuu wa jinsi ya kushinda dhoruba. Yeye ni mtu mkuu kwenye dhoruba. Baada ya siku ndefu ya kuwafundisha wanafunzi Wake, Mwokozi alihitaji kupumzika na alipendekeza kwamba wavuke ng’ambo nyingine ya Bahari ya Galilaya kwa chombo. Mwokozi alipokuwa akipumzika, dhoruba kali ikatokea. Upepo na mawimbi yalitishia kuzamisha chombo, Mitume walianza kuhofia maisha yao. Kumbuka, baadhi ya Mitume wale walikuwa wavuvi ambao walikuwa wamezoea dhoruba ya bahari ile! Lakini, walikuwa na wasiwasi,18 walimwamsha Bwana na kuuliza, “[Bwana], si kitu kwako kuwa tunaangamia?” Kisha, kwa mfano wa utulivu, Mwokozi “aliamka na kuukemea upepo na kuiambia bahari Nyamaza, utulie. Na upepo ukakoma, na kukawa … shwari kuu.”19

Na kisha somo kuu juu ya utulivu kwa Mitume Wake. Yeye aliuliza, “Mbona mmekuwa waoga? Ni kwa namna gani hamna imani”20 Alikuwa anawakumbusha wao kwamba Yeye ni Mwokozi wa ulimwengu, na kwamba alitumwa na Baba kuleta kutokufa na uzima wa milele kwa watoto wa Mungu. Hakika, Mwana wa Mungu hangeweza kuangamia kwenye chombo. Yeye alitoa mfano wa utulivu mtakatifu kwa sababu Yeye alijua kuhusu utakatifu Wake na kujua kwamba kulikuwa na mpango wa wokovu na kuinuliwa na jinsi Upatanisho Wake muhimu ungeweza kuwa ufanisi wa milele wa mpango huo.

Ni kupitia Kristo na Upatanisho Wake ambapo vitu vyote vizuri vinakuja katika maisha yetu. Tunapokumbuka sisi ni akina nani, tukijua kwamba kuna mpango mtakatifu wa rehema, na kuweka ujasiri katika nguvu za Bwana, tunaweza kufanya vitu vyote. Tutapata utulivu. Tutakuwa wanawake na wanaume wazuri katika dhoruba yoyote.

Na tutafute baraka za utulivu kama wa Kristo, sio tu kujisaidia wenyewe katika nyakati zenye changamoto, bali kuwabariki wengine na kuwasaidia wao wapitiapo dhoruba katika maisha yao. Katika Jumapili hii ya Matawi, kwa shangwe ninashuhudia juu ya Yesu Kristo. Amefufuka. Nashuhudia juu ya amani, hali shwari na utulivu wa mbinguni ambao Yeye pekee huuleta kwenye maisha yetu na ninafanya hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Hugh B. Brown,” katika Conference Report, Oct. 1969, 105.

  2. Ona Sheri Dew, Insights from a Prophet’s Life: Russell M. Nelson (2019), 66–67.

  3. Tafsiri ya Joseph Smith, Luka 22:44 (katika Luka 22:44, tanbihib).

  4. Luka 22:42.

  5. Ona Luka 22:50–51; Yohana 18:10–11.

  6. (Soma Mathayo 26:34–35, 69–75.)

  7. Ona Matendo ya Mitume 4:8–10; Neal A. Maxwell, “Kuridhika kwa Vitu Tulivyopewa,” Ensign, Mei 2000, 74; Liahona, Julai 2000, 89: “Wakati tunapokuwa na uwiano kiroho, utulivu unaweza kuja, hata wakati hatujui ‘maana ya vitu vyote’ [1 Nefi 11:17].”

  8. Ona John R. Wooden, Wooden on Leadership (2005), 50: “Ninaelezea utulivu kama kuwa mkweli kwako mwenyewe, sio kuterereka, kutupwa nje, au kukosa usawa bila kujali mazingira au hali. Hii inaweza kuonekana rahisi, lakini utulivu unaweza kuwa sifa isiyopatikana katika nyakati za changamoto. Viongozi wanaokosa Utulivu wanatishika na shinikizo.

    “Utulivu humaanisha kushikilia kabisa imani zako na kutenda kulingana nazo, bila kujali jinsi hali vile inavyoweza kuwa mbaya au nzuri. Utulivu humaanisha kuepukana na mkao au kujifanya, kujilinganisha na wengine, na kuigiza mtu ambaye sio wewe. Utulivu humaanisha kuwa na moyo jasiri katika hali zote.”

  9. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 40.

  10. Russell M. Nelson, “Choices for Eternity” (worldwide devotional for young adults, May 15, 2022), broadcasts.ChurchofJesusChrist.org.

  11. 1 Nefi 3:7.

  12. 1 Nefi 4:6.

  13. Yohana 4:35.

  14. Mafundisho na Maagano 43:34; ona pia James E. Faust, “The Dignity of Self,” Ensign, May 1981, 10: “Heshima ya mtu inaongezeka kwa kiasi kikubwa kwa kutazama juu katika kutafuta utakatifu. Kama mti mkuu, tunapaswa kufikia nuru. Chanzo muhimu sana cha nuru tunachoweza kujua ni kipawa cha Roho Mtakatifu. Ni chanzo cha nguvu za ndani na amani.”

  15. Ona Russell M. Nelson, “Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona, Nov. 2016: “Wapendwa akina kaka na akina dada, furaha tuliyonayo inahusiana kidogo sana na hali ya maisha yetu na inahusiana na kila kitu kwenye fokasi ya maisha yetu.”

  16. Ona Mosia 23:27–28.

  17. David A. Bednar, “Kwa Hivyo Walituliza Woga Wao,” Liahona, Mei 2015, 46–47.

  18. Ona Jeffrey R. Holland, Our Day Star Rising: Exploring the New Testament with Jeffrey R. Holland (2022), 61–62: “Zaidi ya hayo, hawa walikuwa wanaume wenye ujuzi chomboni pamoja Naye—kumi na mmoja kati ya Kumi na Wawili wa asili walikuwa Wagalilaya (Yuda-Iskariote pekee ndiye alikuwa Myudea). Na sita kati ya wale kumi na wawili walikuwa wavuvi. Waliishi ziwani. Walipata kipato kutokana na uvuvi. Walikuwa wamekuwa hivyo tangu utotoni. Baba zao waliwafanya wao warekebishe nyavu na kufanya marekebisho ya chombo walipokuwa vijana wadogo. Wao waliijua bahari hii; walijua upepo na mawimbi. Walikuwa wanaume wenye ujuzi—lakini walikuwa na uoga. Na kama wao walikuwa na uoga, hii ilikuwa dhoruba kweli.”

  19. Ona Marko 4:35–39.

  20. Marko 4:40.