Mkutano Mkuu
Hadithi Kuu ya Pasaka Iliyowahi Kusimuliwa
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Hadithi Kuu ya Pasaka Iliyowahi Kusimuliwa

Kitazame Kitabu cha Mormoni kwa nuru mpya na tafakari ushahidi wake wenye nguvu unachokitoa wa uhalisia wa Kristo aliyefufuka.

Barua ya Urais wa Kwanza kwenye Pasaka

Huenda unakumbuka kusikia barua kutoka Urais wa Kwanza ikisomwa kwenye kata au tawi lako wiki chache zilizopita. Barua hiyo ilitangaza kwamba Jumapili ijayo—Jumapili ya Pasaka—kata zote na matawi wanatakiwa kukutana kwa ajili ya mkutano wa sakramenti tu, ikitoa muda wa ziada kwa ajili ya kuabudu nyumbani kama familia ili kuadhimisha sikukuu hii takatifu.1

Barua ya Urais wa Kwanza ilivuta umakini wangu, na kunisababisha nitafakari jinsi ambavyo familia yetu imesherehekea Pasaka miaka hii yote. Kwa zaidi nilipokuwa nikifikiria kuhusu sherehe, ndipo zaidi nilipojikuta nikijiuliza kama kimakosa tumebadili maana halisi ya sikukuu hii, ambayo ni muhimu kwa wote waaminio katika Yesu Kristo.

Desturi za Krismasi na Pasaka

Mawazo hayo yalinipelekea kutafakari tofauti kati ya jinsi tulivyosherehekea Krismasi ukilinganisha na Pasaka. Wakati wa Desemba, kwa kiasi fulani tunahusisha shangwe ya “milio ya kengele,” soksi za Krismasi na zawadi pamoja na mengine, desturi za kujali zaidi—kama vile kuwajali wenye mahitaji, kuimba nyimbo zetu pendwa za Krismasi na bila shaka kufungua maandiko na kusoma hadithi za Krismasi kwenye Luka 2. Kila mwaka tunaposoma hadithi hii pendwa kutoka kwenye Biblia kubwa ya zamani, familia yetu hufanya kile ambacho huenda familia yako hufanya—kujifunga taulo vichwani na mabegani mwetu na kuvaa majoho ya kuogea kumwakilisha Yusufu, Mariamu na wengi waliokuja kumwabudu mtoto Yesu, tunasimulia upya hadithi pendwa ya Krismasi kuhusu kuzaliwa kwa Mwokozi.

Sherehe za familia yetu kwenye Pasaka, hata hivyo, zimekuwa kiasi fulani za tofauti. Nahisi familia yetu imetegemea sana kwenye “kwenda kanisani” ili kutoa kilicho muhimu cha Pasaka, kinacholenga kwa Kristo; na kisha kama familia, tunakutana kushiriki desturi zingine zihusianazo na Pasaka. Nimependa kuwaona watoto wetu na sasa wajukuu wetu wakitafuta mayai ya Pasaka na kukusanya kutoka vikapu vyao vya Pasaka.

Lakini barua ya Urais wa Kwanza ilikuwa ni wito wa ukumbusho. Sio tu kwamba walitualika sote kuhakikisha kwamba sherehe zetu za tukio muhimu lililowahi kutokea duniani—Upatanisho na Ufufuko wa Yesu Kristo—hujumuisha unyenyekevu na heshima inayotakiwa kwa Bwana, lakini pia wametupatia muda zaidi pamoja na familia na marafiki zetu katika Jumapili ya Pasaka ili tufanye hivyo.

Picha
Mwokozi Aliyefufuka

Maneno haya ya nabii Joseph Smith yanaongeza muktadha wa ziada kwenye umuhimu wa matukio yahusianayo na Pasaka: “Kanuni za msingi za dini yetu ni ushuhuda wa Mitume na Manabii, kuhusu Yesu Kristo, kwamba alikufa, akazikwa, na akafufuka tena siku ya tatu, na kupaa mbinguni; na mambo yote mengine ambayo yanahusiana na dini yetu ni viambatisho kwenye hilo.”2

Mimi pamoja na Lesa tumejadili njia ambazo familia yetu inaweza kufanya vyema wakati wa kipindi cha Pasaka. Pengine swali ambalo tumejiuliza ni ambalo sote tungeweza kutafakari: Tunapanga vipi mafundisho na sherehe za Ufufuko wa Yesu Kristo, hadithi ya Pasaka, kwa uwiano sawa, timilifu na desturi tele za kidini za kuzaliwa kwa Yesu Kristo, hadithi ya Krismasi?

Inaonekana kwamba sote tunajaribu. Ninaona ongezeko la juhudi miongoni mwa Watakatifu wa Siku za Mwisho kuelekea Pasaka inayolenga kwa Kristo. Hii hujumuisha utambuzi mkuu na wa kina wa Jumapili ya Matawi na Ijumaa Kuu kama inavyoadhimishwa na baadhi ya Wakristo wenzetu wa madhehebu mengine. Pia tunaweza kuasili desturi nzuri za Pasaka zinazolenga kwa Kristo zinazopatikana katika tamaduni na desturi za nchi ulimwenguni kote.

Msomi wa Agano Jipya N. T. Wright alipendekeza: “Tunapaswa kupiga hatua kwenye kusherehekea Pasaka katika njia yenye ubunifu mpya: katika sanaa, vitabu, michezo ya watoto, ushairi, muziki, dansi, sherehe, kengele, matamasha maalumu. … Hii ndiyo sherehe yetu kuu. Ondoa Krismasi, na katika lugha ya kibiblia utapoteza sura mbili mwanzoni mwa Mathayo na Luka, sio zaidi. Ondoa Pasaka, na hutakuwa na Agano Jipya; huna Ukristo.”3

Pasaka, Biblia na Kitabu cha Mormoni

Tunaithamini Biblia kwa yote inayotufundisha kuhusu kuzaliwa, huduma, Kusulubishwa na Ufufuko wa Yesu Kristo. Hakuna maneno ambayo hubeba tumaini zaidi na matokeo ya milele kwa wanadamu wote kuliko yale yaliyotolewa na malaika wa mbinguni kwenye asubuhi ya Pasaka katika Bustani ya Kaburi: “Amefufuka.”4 Tuna shukrani za dhati kwa andiko la Agano Jipya ambalo hutunza hadithi ya Pasaka na huduma ya Pasaka ya Mwokozi huko Yuda na Galilaya.

Kadiri mimi na Lesa tulivyoendelea kutafakari na kutafuta njia za kukuza sherehe za Pasaka ya familia yetu ziwe zimelenga kwa Kristo, tulijadili ni desturi ipi ya kusoma maandiko tungeweza kuianzisha kwenye familia yetu—iwianayo na Luka 2 kwa ajili ya Pasaka.

Kisha tulipokea dhihirisho hili la kimbingu: Kama nyongeza ya mistari muhimu kuhusu Pasaka katika Agano Jipya, sisi kama Watakatifu wa Siku za Mwisho tumejaliwa zawadi kuu ya Pasaka! Zawadi ya ushahidi wa kipekee, ushuhuda mwingine wa muujiza wa Pasaka ambao hujumuisha, pengine, maandiko ya kuvutia sana ya Pasaka katika Ukristo wote. Ninarejea bila shaka kuhusu Kitabu cha Mormoni, na hususani zaidi, kwenye masimulizi ya Yesu Kristo akiwatokea wakaazi kwenye Ulimwengu Mpya, akiwa kwenye utukufu Wake wa ufufuko.

Nabii Joseph Smith alikielezea Kitabu cha Mormoni kama “kitabu sahihi duniani,”5 na ukianza na 3 Nefi 11, husimulia hadithi ya kuvutia ya matembezi ya Kristo aliyefufuka kwa Wanefi, huduma ya Pasaka ya Mwokozi. Maandiko haya ya Pasaka hushuhudia juu ya Ufufuko wa Bwana Yesu Kristo.

Katika sura hizi, Kristo anawaita Mitume Kumi na Wawili, anafundisha kama Alivyofundisha katika Mahubiri Yake ya Mlimani, anatangaza kwamba ametimiza sheria ya Musa na kutoa unabii kuhusu kusanyiko la Israeli katika siku za mwisho. Anawaponya wagonjwa na kuwaombea watu katika hali takatifu kwamba “hakuna ulimi unaoweza kusema, wala haiwezi kuandikwa na mtu yeyote, wala mioyo ya watu haiwezi kufikiria vitu vikubwa na vya ajabu kama tulivyoona na kusikia Yesu akisema; na hakuna yeyote ambaye anaweza kuona shangwe iliyojaza nafsi zetu wakati tulipomsikia akituombea kwa Baba.”6

Picha
Yesu Kristo Akiwatembelea Wanefi

Pasaka hii, familia yetu itafokasi kwenye mistari 17 ya mwanzo ya 3 Nefi 11, ambayo wote mnaifahamu. Mnakumbuka umati mkubwa kuzunguka hekalu katika nchi ya Neema ambao walisikia sauti ya Mungu Baba na kumwona Yesu Kristo akishuka kutoka mbinguni kutoa mwaliko mzuri sana wa Pasaka:

“Inukeni na mje kwangu, … kwamba mguse alama za misumari katika mikono yangu na katika miguu yangu, ili mjue mimi ni … Mungu wa ulimwengu wote, na nimeuawa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu.

“Na … umati ulienda mbele, … mmoja mmoja … na waliona na macho yao na kupapasa kwa mikono yao, … na walishuhudia wenyewe, kwamba ni yeye …

“Na … walipaza sauti kwa toleo moja wakisema:

“Hosana! Li heri jina la Mungu Aliye Juu Sana! Na waliinama chini miguuni mwa Yesu na kumwabudu.”7

Fikiria: Wanefi kwenye Hekaluni waligusa mikono ya Bwana aliyefufuka! Tunatumainia kufanya sura hizi kwenye Nefi wa 3 kama sehemu muhimu ya desturi yetu ya Paska kama ilivyo Luka 2 kwenye tamaduni yetu ya Krismasi. Kiuhalisia, Kitabu cha Mormoni hushiriki hadithi kuu ya Pasaka ambayo imewahi kusimuliwa. Na isiwe hadithi kuu ya Pasaka ambayo haikuwahi kusimuliwa.

Lakini nawaalika kukitazama Kitabu cha Mormoni kwa nuru mpya na kutafakari ushahidi wake wenye nguvu unachokitoa wa uhalisia wa Kristo aliyefufuka pamoja na wingi na kina juu ya mafundisho ya Kristo.

Kitabu cha Mormoni Kinashuhudia juu ya Yesu Kristo

Tunaweza kuuliza, Ni kwa namna ipi kusoma maandiko ya Kitabu cha Mormoni katika Pasaka kutabariki maisha yetu na ya wapendwa wetu katika njia ya kufaa? Unaweza kutambua jambo zaidi ya moja. Muda wowote tusomapo na kujifunza kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni, tunaweza kutarajia matokeo makubwa.

Hivi karibuni, mimi pamoja na Lesa tulihudhuria mazishi ya rafiki kipenzi, mwanamke wa imani ambaye maisha yake yalifupishwa na ugonjwa. Tulikusanyika pamoja na familia yake na marafiki wa karibu, tukibadilishana kumbukumbu nzuri za nafsi hii nzuri zilizobariki maisha yetu.

Tukiwa tumesimama mbali na jeneza tukiongea na wengine, niliwaona wasichana wawili wa umri wa Msingi wakisogelea jeneza na kusimama kwa kuchuchumia—macho yao yakifikia tu ukingo wa jeneza—ili kutoa salamu zao za mwisho kwa shangazi yao mpendwa. Kwa kutokuwepo na mtu karibu, Lesa alisogea na kuinama pembeni yao ili kutoa faraja na somo. Aliwauliza wanaendeleaje na kama walijua alipokuwa shangazi yao wakati huo. Walishiriki majonzi yao, lakini kisha watoto hawa wa thamani wa Mungu, kwa ujasiri machoni mwao, walisema kwamba walijua shangazi yao alikuwa sasa na furaha, na angeweza kuwa pamoja na Yesu.

Katika umri huu mdogo, walipata amani katika mpango mkuu wa furaha na, katika njia yao ya kitoto, walishuhudia uhalisia mkuu na uzuri rahisi wa Ufufuko wa Mwokozi. Walilijua hili katika mioyo yao kwa sababu ya mafundisho ya wazazi wema, familia na viongozi wa Msingi wakipanda mbegu ya imani katika Yesu Kristo na uzima wa milele. Wakiwa na busara kupita umri wao, wasichana hawa walielewa kweli ambazo huja kwetu kupitia ujumbe wa Pasaka na huduma ya Mwokozi aliyefufuka na maneno ya manabii kama yalivyosemwa katika Kitabu cha Mormoni.

Nimegundua kwamba wakati Rais Russell M. Nelson akitoa zawadi ya Kitabu cha Mormoni kwa mtu asiye wa imani yetu, ikijumuisha viongozi wa ulimwengu, mara nyingi hufungua Nefi wa 3 na kusoma kuhusu kutokea kwa Kristo aliyefufuka kwa Wanefi. Kwa kufanya hivyo, nabii anayeishi kimsingi anashuhudia kuhusu Kristo anayeishi.

Hatuwezi kusimama kama mashahidi wa Yesu Kristo mpaka tutakapoweza kutoa ushuhuda kumhusu Yeye. Kitabu cha Mormoni ni ushahidi mwingine wa Yesu Kristo kwa sababu kote katika kurasa zake takatifu, nabii mmoja baada ya mwingine hushuhudia sio tu kwamba Kristo angekuja, lakini kwamba Alikuja.

Kwa Sababu Yake

Ninashikilia mkononi mwangu nakala ya toleo la kwanza la Kitabu cha Mormoni. Kufanya hivyo daima hunigusa. Kwani mengi ya maisha yangu ya ukubwa, nimependezwa, kuvutiwa na kushangazwa na kile kijana Joseph Smith alikifanya ili kuhakikisha kitabu hiki kitakatifu cha maandiko kinatafsiriwa na kuchapishwa. Miujiza iliyotokea ni ya kuchochea tafakuri.

Lakini hiyo siyo sababu ya kwa nini kitabu hiki hunigusa. Ni kwa sababu kitabu hiki, zaidi ya chochote kile kilichowahi kuchapishwa hapa duniani, hushuhudia juu ya maisha, huduma, mafundisho, Upatanisho na Ufufuko wa Yesu Kristo. Wapendwa akina kaka na dada zangu, kujifunza mara kwa mara kutoka kitabu hiki kumhusu Yesu Kristo kutabadili maisha yako. Kitafumbua macho yako kwenye uwezekano wa fursa mpya. Kitakuza tumaini lako na kukujaza na hisani. Zaidi ya yote, kitajenga na kuimarisha imani yako katika Yesu Kristo na kukubariki kwa ufahamu kamili kwamba Yesu na Baba yetu wanakufahamu, kukupenda na kukutaka utafute njia ya kurejea nyumbani, kunakoanzia na herufi kubwa N.

Wapendwa kaka na dada, muda umefika, uliotabiriwa na manabii wa kale, “wakati ufahamu wa Mwokozi utapenya kila taifa, kabila, lugha, na watu.”8 Tunaona utimilifu wa unabii huu mbele ya macho yetu, kupitia ushahidi juu ya Yesu Kristo upatikanao kwenye Kitabu cha Mormoni.

Picha
Bwana Yesu Kristo

Hakuna kitabu kinachofanya zaidi kuonyesha hilo:

  • Kwa sababu ya Yesu Kristo, kila kitu kilibadilika.

  • Kwa sababu Yake, kila kitu ni kizuri zaidi.

  • Kwa sababu Yake, maisha huhimilika—hasa nyakati za uchungu.

  • Kwa sababu Yake, kila kitu kinawezekana.

Matembezi Yake kama Mwokozi aliyefufuka, yaliyotambulishwa na Mungu Baba, ni ujumbe mtakatifu na wa kishujaa wa Pasaka. Utawasaidia wanafamilia wetu kupata ushuhuda binafsi wa Yesu kristo kama Mwokozi na Mkombozi wetu, aliyevunja vifungo vya kifo.

Ninahitimisha kwa ushuhuda wangu wa ukweli wa Kitabu cha Mormoni na wa Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu aliye hai. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona barua ya Urais wa Kwanza, Feb. 15, 2023.

  2. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 49; emphasis added.

  3. N. T. Wright, Surprised by Hope: Rethinking Heaven, the Resurrection, and the Mission of the Church (2008), 256.

  4. Mathayo 28:6.

  5. Teachings: Joseph Smith, 64.

  6. 3 Nefi 17:17.

  7. Ona 3 Nefi 11:1–17.

  8. Mosia 3:20.

Chapisha