Mkutano Mkuu
Hosana kwa Mungu Aliye Juu Sana
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Hosana kwa Mungu Aliye Juu Sana

Kuingia kwa Yesu Kristo kwa shangwe katika Yerusalemu na yale matukio ya wiki ambayo yalifuatia yanaonesha kwa mfano fundisho tunaloweza kutumia katika maisha yetu leo.

Leo, kama ambavyo imesemwa, tunaungana na Wakristo ulimwenguni kote kutoa heshima kwa Yesu Kristo katika Jumapili hii ya Matawi. Karibu miaka 2,000 iliyopita Jumapili ya Matawi iliashiria kuanza kwa wiki ya mwisho ya huduma ya duniani ya Yesu Kristo. Ilikuwa wiki muhimu sana katika historia ya mwanadamu.

Kile kilichoanza kama kushangiliwa kwa Yesu kama Masiya mwahidiwa katika kuingia Kwake kwa shangwe Yerusalemu kulifungwa kwa Kusulubiwa Kwake na Ufufuko Wake.1 Kwa usanifu wa kiungu, dhabihu yake ya upatanisho ilihitimisha huduma Yake duniani, ikifanya iwezekane kwetu sisi kuishi na Baba yetu wa Mbinguni milele.

Maandiko yanatuambia kwamba wiki hii ilianza kwa makutano kusimama malangoni mwa mji kumwona “Yesu yule nabii wa Nazareti ya Galilaya.”2 Walichukua “matawi ya mitende, na kwenda mbele kumlaki, na wakipiga kelele: Hosana: Mbarikiwa Mfalme wa Israeli ajaye kwa jina la Bwana.”3

Hadithi hiyo ya biblia ya siku nyingi zilizopita inanikumbusha mimi nikiwa kwenye jukumu la Kanisa huko Takoradi, Ghana. Cha kushangaza, nilikuwa huko siku ya Jumapili ya Matawi.

Picha
Mkusanyiko huko Takoradi, Ghana

Ilikuwa nikigawanye Kigingi cha Takoradi Ghana ili kutengeneza Kigingi cha Mpintsin Ghana. Leo, kuna waumini wa Kanisa zaidi ya 100,000 huko Ghana.4 (Tunamkaribisha Ga Manste, Mfalme Mtukufu Nii Tackie Tsuru II wa Accra Ghana, ambaye yuko nasi leo.) Kukutana na waumini hawa, nilihisi upendo mkubwa na kujitoa kwa Bwana. Nilielezea upendo wangu mkubwa kwao, na kwamba Rais wa Kanisa anawapenda. Nilirejelea maneno ya Mwokozi yaliyoandikwa na Yohana. “Kwamba pendaneni, kama nilivyowapenda.”5 Walichukulia kama “mkutano wa ninakupenda.”6

Picha
Mzee Rasband akisalimiana kwa mikono huko Takoradi, Ghana

Nilipokuwa natazama chini na juu ya ile mistari waliyokaa wale akina kaka na akina dada na familia zao pale Kanisani, niliweza kuona katika nyuso zao mng’aro wa ushuhuda na imani yao katika Yesu Kristo. Nilihisi hamu yao ya kutaka kuhesabiwa kama sehemu ya Kanisa Lake linalofika mbali sana. Na kwaya ilipoimba, waliimba kama malaika.

Picha
Kwaya huko Takoradi, Ghana.
Picha
Mzee Rasband na waumini huko Ghana

Kama vile katika Jumapili ya Matawi ya kale, kulikuwa na wafuasi wa Yesu Kristo waliokusanyika kutoa heshima Kwake kama walivyofanya wale waliokuwa malangoni Yerusalemu ambao, wakiwa na matawi ya mitende mikononi mwao, walipiga kelele, “Hosana … : Mbarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana.”7

Picha
Kupunga matawi ya mitende huko Ghana

Hata wale wakazi wa parokiani katika Kanisa la jirani walikuwa wakiadhimisha Jumapili ya Matawi. Nilipokuwa nikizungumza kutoka kwenye mimbari, niligundua nje ya dirisha walikuwa wakitembea mtaani kwa furaha wakipunga matawi ya mitende katika mikono yao, kama vile ilivyo katika picha hii. Ni kitu ambacho sitakisahau—sote siku hiyo tukimwabudu Mfalme wa wafalme.

Rais Russell M. Nelson ametusihi sisi tufanye Jumapili ya Matawi “hakika kuwa takatifu kwa kukumbuka, siyo tu mitende kwamba ilipungwa kwa heshima ya kuingia kwa Yesu huko Yerusalemu, bali kwa kukumbuka viganja vya mikono yake.” Kisha Rais Nelson alirejelea kwa Isaya, ambaye alizungumza juu ya Mwokozi akiahidi, “sitawasahau ninyi,” kwa maneno haya: “Tazama, nimekuchora wewe kwenye viganja vya mikono yangu.”8

Bwana anajua moja kwa moja kwamba maisha ya duniani ni magumu. Majeraha Yake yanatukumbusha kwamba Yeye “amejishusha chini yao … wote”9 ili kwamba Yeye apate kutusaidia sisi tunapoteseka na kuwa mfano wetu wa “shikilia njia yako,”10 njia Yake, kwani “Mungu atakuwa pamoja [nasi] milele na milele.”11

Jumapili ya Matawi haikuwa tu tukio, ni ukurasa mwingine katika historia wenye tarehe, muda na mahali. Kuingia kwa Yesu Kristo kwa shangwe katika Yerusalemu na yale matukio ya wiki ambayo yalifuatia yanaonesha kwa mfano fundisho tunaloweza kutumia katika maisha yetu leo.

Acha tuangalie baadhi ya mafundisho ya milele ambayo yanafumwa kupitia huduma Yake yote na kuhitimishwa huko Yerusalemu.

Kwanza, unabii. Kwa mfano, Nabii wa Agano la Kale Zekaria alitoa unabii juu ya Yesu Kristo kuingia kwa shangwe huko Yerusalemu, hata alieleza kwamba Yeye angeingia akiwa amepanda juu ya punda.12 Yesu alitabiri Ufufuko Wake alipokuwa akijiandaa kuingia mjini, akisema:

“Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe,

“Kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.”13

Pili, wenza wa Roho Mtakatifu. Joseph Smith alifundisha, “Hakuna mtu anayeweza kujua kwamba Yesu ni Bwana, isipokuwa kwa Roho Mtakatifu.”14 Mwokozi aliwaahidi wafuasi Wake15 kwenye Karamu ya Mwisho16 chumba cha orofani,17 “Sitawaacha ninyi yatima.”18 Hawangekuwa peke yao katika kuupeleka mbele ukweli wa injili bali angewapa kipawa kikamilifu cha Roho Mtakatifu ili kuwaongoza. “Amani nawaachieni, amani yangu nawapa,” Yeye aliahidi, “sivyo kama ulimwengu utoavyo.”19 Kwa kipawa cha Roho Mtakatifu tunalo hakikisho kama hilo—kwamba “tuweze daima kuwa na Roho Wake pamoja [nasi]”20 na “kwa uweza wa Roho Mtakatifu [sisi] tuweze kujua mambo yote.”21

Tatu, Ufuasi. Ufuasi wa kweli ni udhati usioshindwa, utiifu kwa sheria za milele, na upendo kwa Mungu, kwanza na zaidi ya yote. Pasipo kuyumba. Umati uliotoa heshima kwa matawi ya mitende walimshangilia Yeye kama Masiya. Ndiye hasa Yeye alikuwa. Walivutwa Kwake, kwenye miujiza Yake na kwenye mafundisho Yake. Lakini sifa hiyo kwa wengi haikudumu. Baadhi ambao awali walishangilia kwa sauti, “Hosana”22 punde waligeuka na kupaza sauti, “Msulubishe.”23

Nne, Upatanisho wa Yesu Kristo.24 Katika siku Zake za mwisho, kufuatia Jumapili ya Matawi, Yeye alitekeleza Upatanisho Wake wa ajabu, kutoka mateso ya Gethsemane hadi dhihaka ya mashtaka Yake, maumivu makali juu ya msalaba, na maziko Yake katika kaburi la kuazima. Lakini haikuishia hapo. Pamoja na ukuu wa wito Wake kama Mkombozi wa watoto wote wa Baba wa Mbinguni, siku tatu baadaye Yeye aliinuka kutoka kwenye kaburi lile, amefufuka25 kama yeye alivyotoa unabii.

Je, daima sisi tunayo shukrani kwa Upatanisho wa Yesu Kristo usiolinganishwa na chochote? Je, tunahisi uweza wake wenye kutakasa, sasa hivi? Hiyo ndiyo sababu Yesu Kristo, Mwanzilishi na Mtimizaji wa Wokovu wetu, alienda Yerusalemu, ili kutuokoa sote. Je, maneno haya katika Alma yanaleta umuhimu: “Ikiwa mmepata mabadiliko ya moyo, na ikiwa mmesikia kuimba wimbo wa upendo wa ukombozi, nitauliza, mnaweza kuhisi hivyo sasa?”26 Ninaweza hakika kusema, kwaya huko Takoradi ile Jumapili ya Matawi iliimba “wimbo wa upendo wa ukombozi.”

Wiki hiyo ya mwisho yenye matukio mengi katika huduma Yake ya duniani, Yesu Kristo alitoa mfano wa wanawali kumi.27 Alikuwa anafundisha juu ya kurudi Kwake kwa wale waliojiandaa kumpokea Yeye, pasipo matawi ya mitende mikononi mwao bali wakiwa na nuru ya injili ndani yao. Alitumia picha za taa zilizowashwa, pamoja na akiba ya mafuta ili moto usizime, kama kielelezo cha utayari wa kuishi kwa njia Yake, kukumbatia ukweli Wake na kushiriki nuru Yake.

Mnaijua hadithi. Wanawali wale kumi wanawakilisha waumini wa Kanisa, na bwana harusi anamwakilisha Yesu Kristo.

Wale wanawali kumi walizitwaa taa zao na wakaenda kumlaki bwana harusi.”28 Wanawali watano wenye hekima, walijiandaa na mafuta katika taa zao na akiba, na watano walikuwa wapumbavu, taa zilizima kwa kukosa akiba ya mafuta. Wito ulipokuja, “Tazama, bwana harusi anakuja; nendeni mkamlaki,”29 wale watano waliokuwa na “hekima na wamepokea ukweli, na wamemtwaa Roho Mtakatifu kuwa kiongozi wao,”30 walikuwa tayari kwa ajili ya “mfalme wao na mtoa sheria wao,”31 ili “utukufu wake [ungekuwa] juu yao.”32 Wale watano wengine walikuwa wakihangaika kutafuta mafuta. Lakini walikuwa wamechelewa sana. Maandamano yalisonga mbele pasipo wao. Walipobisha hodi na kusihi wafunguliwe, Bwana alijibu, “Siwajui ninyi.”33

Je, tungehisije kama Yeye angesema hivi kwetu, “ Siwajui ninyi!”

Sisi, kama wale wanawali kumi, tunazo taa; lakini je, tunayo mafuta? Nina hofu kuna baadhi ambao wanaendelea tu na mafuta kidogo sana, wana kazi nyingi sana na mashinikizo ya kidunia. Mafuta huja kutokana na kuamini na kutendea kazi unabii na maneno ya manabii walio hai, hususan Rais Nelson, Washauri wake na mitume Kumi na Wawili. Mafuta yanazijaza nafsi zetu tunaposikia na kuhisi Roho Mtakatifu na kufanyia kazi mwongozo huo wa kiungu. Mafuta yanamiminika katika mioyo yetu pale chaguzi zetu zinapoonesha tunampenda Bwana na tunapenda kile anachopenda. Mafuta huja kutokana na kutubu na kutafuta uponyaji wa Upatanisho wa Yesu Kristo.

Kama baadhi yenu mnatazamia kujaza kile wengine wanachokiita “orodha ya mambo,” hii ndio yenyewe: jaza orodha yako mafuta katika umbo la maji ya uzima ya Yesu Kristo,34 ambayo inawakilisha maisha Yake na mafundisho Yake. Kinyume chake, kukamilisha jambo fulani lisilo muhimu hakutaacha nafsi yako ihisi ukamilifu au kuridhika; kuishi mafundisho yaliyofundishwa na Yesu Kristo kutakufanya uhisi hivyo. Nilitaja mifano mapema: kumbatia unabii na mafundisho ya kinabii, fanyia kazi misukumo ya Roho Mtakatifu, uwe mfuasi wa kweli, na tafuta nguvu ya uponyaji ya Upatanisho wa Bwana wetu. Orodha hiyo itakupeleka mahali unapotaka kwenda—kurudi kwa Baba yako wa Mbinguni.

Jumapili ile ya Matawi huko Takoradi ilikuwa uzoefu maalumu sana kwangu kwa sababu niliishiriki na mkusanyiko wa akina kaka na akina dada walio waaminifu. Ndivyo ilivyokuwa kwenye mabara na visiwa vya bahari ulimwenguni kote. Moyo wangu na nafsi yangu, kama wako unatamani kushangilia, “Hosana kwa Mungu Aliye Juu Sana.”35

Ingawa hatusimami katika malango ya Yerusalemu leo na matawi ya mitende mikononi, wakati utafika, kama ilivyotolewa unabii katika Ufunuo, “umati mkubwa, ambao hakuna mtu awezaye kuhesabu, wa mataifa yote, na koo, na watu, na ndimi, [watasimama] mbele za kiti cha enzi, na mbele ya Mwanakondoo, wakiwa wamevikwa mavazi meupe, na matawi ya mitende mikononi mwao.”36

Ninawaachieni baraka yangu kama Mtume wa Yesu Kristo kwamba kwa bidii mtajitahidi kuishi kwa haki na kuwa miongoni mwa wale ambao, wakiwa na matawi ya mitende mikononi mwao, watamshangilia Mwana wa Mungu, Mkombozi mkuu wetu sote. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Injili zote nne—Mathayo 21–28, Marko 11–16, Luka 19–24, na Yohana 12–21—zinaelezea siku za mwisho za huduma ya Yesu Kristo duniani, ambayo ilikuwa imesanifiwa kiungu ili kufanya baraka ya wokovu na kuinuliwa zipatikane kwa watoto wote wa Mungu. Wakati mwingine waandishi wanatofautiana katika kile wanachokijumuisha lakini siyo katika mafundisho na matendo ya Mwokozi.

  2. Ona Mathayo 21:10–11.

  3. Yohana 12:13.

  4. Kwa Kumbukumbu za Muumini na Takwimu, kuna waumini 102,592 nchini Ghana.

  5. Yohana 15:12.

  6. Kila wakati nilipoongea na waumini, wangeniambia, “Mzee Rasband, mpendwa Mtume wetu, ninakupenda.” Watu hawa wamejawa na Roho na wanampenda Mungu na kwamba wanashiriki upendo huo kiurahisi sana.

  7. Mathayo 21:9.

  8. Ona Russell M. Nelson, “Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho,” (video), Apr. 2021, ChurchofJesusChrist.org/media; Isaya 49:16.

  9. Mafundisho na Maagano 122:8. Mnamo Oktoba 1838 Nabii Joseph na baadhi ya viongozi wengine wa Kanisa walifungwa bila haki katika jela ya Liberty. Mazingira yalikuwa ya kuogopesha. Baada ya miezi kadhaa katika hali ya kuvunjika moyo, aliwaandikia waumini mnamo Machi ya 1839, ikijumuisha sala ambamo alimsihi Bwana kuwa na huruma kwa hali yake na “mateso ya Watakatifu.” Pia alishiriki majibu ya Bwana kwa sala hizo kama yalivyorekodiwa katika Mafundisho na Maagano 121–23.

  10. Mafundisho na Maagano 122:9. Bwana akimtia moyo Joseph Smith huko Jela ya Liberty ilimletea faraja na uelewa wa kiroho kwamba dhiki na majaribu vinaweza kutuimarisha, kufundisha subira na kujizuia. Bwana alimtaka “ashikilie njia yake,” ambayo ilikuwa njia ya Bwana, akivumilia kutendewa pasipo haki kama “Mwana wa [Mungu, ambaye] amejishusha chini yao wote. Je, wewe u mkuu kuliko yeye?” (Mafundisho na Maagano 122:8).

  11. Mafundisho na Maagano 122:9. Ahadi kwamba Mungu “atakuwa nawe” ni ahadi ya uhakika kwa wale ambao hushikilia kwa nguvu kwenye imani yao na kumtumainia Bwana.

  12. Ona Zekaria 9:9.

  13. Mathayo 20:18–19 James E. Talmage anaandika katika Jesus the Christ: “Ni … ukweli wa kustaajabisha kwamba Kumi na Wawili walishindwa kufahamu maana Yake. … Kwao kulikuwa na mlingano wa kutia hofu, baadhi ya utofauti mkubwa au mkanganyiko usiofafanulika katika misemo ya Bwana wao mpendwa. Walimjua Yeye kuwa ni Kristo, Mwana wa Mungu Aliye hai; na ni kwa jinsi gani Mtu kama huyu anaweza kuwekwa chini ya hatia ya kuuawa?” ([1916], 502–3).

  14. Joseph Smith alitoa tamko hili kwa Wanawake wa Muungano wa Usaidizi Nauvoo, Aprili 28, 1842, kama ilivyonukuliwa katika “History of Joseph Smith,” Deseret News, Sept. 19, 1855, 218. Kurejelea mlango wa kumi na mbili wa 1 Wakorintho, alifafanua katika mstari wa tatu, “Hakuna mtu anayeweza kusema kwamba Yesu ni Bwana, ila kwa Roho Mtakatifu,” akiubadili kuwa, “Hakuna mtu anayeweza kujua kwamba Yesu ni Bwana ila kwa Roho Mtakatifu.” (Ona The First Fifty Years of Relief Society: Key Documents in Latter-day Saint Women’s History [2016], 2.2, churchhistorianspress.org.)

  15. Yesu alishiriki Karamu ya Mwisho pamoja na wanafunzi Wake (ona Marko 14:12–18). Wale kumi na wawili walikuwa ni pamoja na Petro, Andrea, Yakobo, Yohana, Mathayo, Filipo, Tomaso, Bartholomeo, Yakobo, Yuda Iskarioti, Yuda (kaka wa Yakobo), na Simoni (ona Luka 6:13–16).

  16. Yesu alianzisha sakramenti miongoni mwa wanafunzi Wake katika Karamu ya Mwisho (ona Mathayo 26:26–29; Marko 14:22–25; Luka 22:19–20).

  17. Mchana/usiku maalumu ambapo Yesu alianzisha sakramenti kwenye “chumba cha orofani” una utata kwa sababu ya tofauti kati ya Mathayo, Marko, Luka na Yohana. Mathayo, Marko na Luka wanapendekeza kwamba Karamu ya Mwisho ilifanyika “siku ya kwanza ya karamu ya mikate isiyotiwa chachu,” au mlo wa Pasaka (ona Mathayo 26:17; Marko 14:12; Luka 22:1, 7). Yohana, hata hivyo, anapendekeza kwamba Yesu alikamatwa kabla ya mlo wa Pasaka (ona Yohana 18:28), ikimaanisha kwamba Karamu ya Mwisho ingefanyika siku moja mapema zaidi kuliko mlo wa Pasaka. Nyenzo za mtaala wa Kanisa na wanazuoni Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaonekana kukubali kwamba Yesu alifanya Karamu ya Mwisho pamoja na wafuasi katika Chumba cha Juu jioni ya siku kabla ya Kusulubiwa. Wakristo wanaosherehekea Wiki Takatifu wanaitambua Alhamisi kama siku ya Karamu ya Mwisho, Ijumaa kama siku ya Kusulubiwa, na Jumapili kama siku ya Ufufuko—kulingana na kalenda ya Gregori.

  18. Yohana 14:18.

  19. Yohana 14:27.

  20. Mafundisho na Maagano 20:77.

  21. Moroni 10:5.

  22. Kamusi ya Biblia inaeleza, hosana maana yake “okoa sasa.” Neno hili limechukuliwa kutoka katika Zaburi 118:25. “Uimbaji wa zaburi hii uliunganishwa na Karamu ya Tabenako pamoja na kupunga matawi ya mitende; hivyo matumizi ya neno kwa umati wa watu wakati wa kuingia kwa Bwana mjini Yerusalemu kwa shangwe” (Bible Dictionary, “Hosanna”). (Ona Mathayo 21:9, 15; Marko 11:9–10; Yohana 12:13.)

  23. Marko 15:14; Luka 23:21.

  24. Kitovu cha mpango wa wokovu wa Baba yetu wa Mbinguni ilikuwa Upatanisho usio na mwisho ambao ungeleta kutokufa kwa watoto Wake wote na kuinuliwa kwa wale wote wenye kustahili kupokea baraka hiyo. Pale Baba aliposema, “Nimtume nani?” Yesu Kristo alijitokeza mbele, “Niko hapa, nitume mimi”(Abrahamu 3:27). Rais Russell M. Nelson amefundisha: “Misheni ya [Yesu Kristo] ilikuwa ni Upatanisho. Wito huo ulikuwa ni Wake wa kipekee. Akiwa amezaliwa na mama wa duniani na Baba wa mbinguni, alikuwa ndiye pekee ambaye angeweza kwa hiari kuyatoa maisha yake na kuyachukua tena (ona Yohana 10:14–18). Matokeo matakatifu ya Upatanisho Wake yalikuwa ya daima na milele. Alichukua uchungu wa kifo na akafanya dhiki ya kaburi kuwa ya muda (ona 1 Wakorintho 15:54–55). Jukumu Lake la Upatanisho lilijulikana hata kabla ya Uumbaji na Anguko. Upatanisho haukuwa tu wa kuleta ufufuo na kutokufa kwa kila mwanadamu, lakini ilikuwa pia kutuwezesha kusamehewa dhambi zetu—kulingana na vigezo vilivyowekwa na Yeye. Hivyo Upatanisho Wake ulifungua njia ambayo tungeweza kuunganishwa na Yeye na familia zetu milele” (“The Mission and Ministry of Jesus Christ,” Liahona, Apr. 2013, 20).

  25. Ufufuko unajuimuisha kuunganika tena kwa mwili na roho katika hali ya kutokufa tena, mwili na roho zikiwa haziwezi kutenganishwa tena na haziguswi tena na maradhi ya kidunia au mauti (ona Alma 11:45; 40:23).

  26. Alma 5:26; ona pia Alma 5:14.

  27. Mfano wa wanawali kumi unapatikana katika Mathayo 25:1–12; Mafundisho na Maagano 45:56–59. Milango inayozunguka Mathayo 25 inapendekeza kwamba Yesu alifundisha mfano huu wakati wa wiki yake ya mwisho, baada ya kuingia Yerusalemu katika Mathayo 21 na kabla tu ya Karamu ya Mwisho na kukamatwa Kwake katika Mathayo 26. Kwa kuongezea kwenye mfano wa wale wanawali kumi uliotolewa wiki ile ya mwisho, Yesu alitoa mfano wa mti wa mtini (ona Mathayo 21:17–21; 24:32–33), mfano wa wana wawili (ona Mathayo 21:28–32), mwenye nyumba mwovu (ona Mathayo 21:33–46).

  28. Mathayo 25:1.

  29. Mathayo 25:6.

  30. Mafundisho na Maagano 45:57.

  31. Mafundisho na Maagano 45:59.

  32. Mafundisho na Maagano 45:59.

  33. Mathayo 25:12. Katika Mahubiri ya Mlimani, Bwana anawarejelea wale wanaojifikiria kuwa wamefanya “matendo mengi ya kushangaza,” akisema, kama ilivyopendekezwa katika maelezo ya wanawali watano wapumbavu, “sikuwajua kamwe” (ona Mathayo 7:22–23).

  34. Kama vile maji yalivyo muhimu kwa maisha ya duniani, Yesu Kristo na mafundisho Yake (maji ya uzima) ni muhimu kwa uzima wa milele (ona Mwongozo wa Maandiko, “Maji ya Uzima,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org; see also Isaya 12:3; Yeremia 2:13; Yohana 4:6–15; 7:37; 1 Nefi 11:25; Mafundisho na Maagano 10:66; 63:23).

  35. 3 Nefi 4:32.

  36. Ufunuo wa Yohana 7:9.

Chapisha