Uhudumiaji
Acha tufikie na kujali jinsi ambavyo Mwokozi wetu angefikia na kujali, hususani kwa wale ambao tumepata fursa kwa upendo na kwa jukumu kuwahudumia.
Akina kaka na dada, marafiki, karibuni kwenye mkutano mkuu!
Baada ya mkutano mkuu Oktoba iliyopita, mimi na Dada Gong tulitembea kwenye Kituo cha Mikutano ili kusalimia na kusikia uzoefu wenu wa injili.
Waumini wetu kutoka Mexico walisema, “Hoy es el tiempo de Mexico.”
Tuligundua Gilly na Mary ni marafiki kutoka Uingereza. Wakati Mary alipojiunga na Kanisa, alipoteza makazi yake. Gilly kwa ukarimu alimkaribisha Mary aishi naye. Akiwa amejawa imani, Gilly anasema, “sijawahi kuwa na mashaka Bwana yu pamoja nami.” Kwenye mkutano, Gilly pia alikutana kwa furaha na dada mmisionari aliyemfundisha miaka 47 iliyopita.
Jeff na mkewe, Melissa, walikuwa wakihudhuria mkutano mkuu na ni kwa mara ya kwanza kwake. Jeff alicheza besiboli ya kulipwa (alikuwa mdakaji) na sasa ni daktari wa dawa za maumivu ya upasuaji. Aliniambia, “Kwa mshangao mkubwa, ninasonga kuelekea ubatizo kwa sababu ni kama njia halisi na ya kweli ya kuishi.”
Mwanzoni, Melissa aliomba radhi kwa kaka mhudumiaji wa Jeff, “Jeff hataki ‘mashati meupe’ katika nyumba yetu.” Kaka mhudumiaji alisema, “nitatafuta njia.” Sasa yeye na Jeff ni marafiki wazuri. Kwenye ubatizo wa Jeff, nilikutana na mkusanyiko wa Watakatifu wa Siku za Mwisho ambao Jeff, Melissa na binti yao, Charlotte, waliupenda.
Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tunatafuta kuwahudumia wengine kama Yeye ambavyo angefanya kwa sababu maisha yanasubiri kubadilishwa.
Wakati Peggy aliponiambia mumewe, John, baada ya miaka 31 ya ndoa, alikuwa akienda kubatizwa, nilimuuliza nini kilikuwa kimebadilika.
Peggy alisema, “mimi na John tulikuwa tukijifunza Njoo Unifuate ya Agano Jipya na John akauliza kuhusu mafundisho ya Kanisa.”
Peggy alisema, “Acha tuwaalike wamisionari.”
John alisema, “Sitaki wamisionari—labda rafiki yangu awepo.” Kwa zaidi ya miaka 10, kaka mhudumiaji wa John amekuwa rafiki yake wa kuaminika. (Niliwaza, ingekuwaje kama kaka mhudumiaji wa John angeacha kuja baada ya mwaka mmoja, miwili au tisa?)
John alisikiliza. Alisoma Kitabu cha Mormoni kwa kusudi halisi. Wamisionari walipomwalika John abatizwe, alisema ndiyo. Peggy alisema, “nilidondoka kutoka kwenye kiti changu na kuanza kulia.”
John alisema, “Nilibadilika kadiri nilivyosonga karibu zaidi na Bwana.” Baadaye, John na Peggy waliunganishwa ndani ya hekalu takatifu. Desemba iliyopita, John alifariki akiwa na miaka 92. Peggy anasema, “John daima alikuwa mtu mwema, lakini alikuwa tofauti katika njia ya kupendeza baada ya kubatizwa.”
Mimi na dada Gong tulikutana na Meb na Jenny kwa video wakati wa janga la ulimwenguni kote la UVIKO. (Tulikutana na wanandoa wengi na watu binafsi wazuri kwa video wakati wa UVIKO, kila mmoja wao akitambulishwa baada ya sala ya dhati ya marais wao wa vigingi.)
Meb na Jenny walisema wasiwasi katika maisha yao uliwafanya wajiulize ikiwa ndoa yao ya hekaluni ingeweza kunusurika, na kama ndivyo, kwa namna ipi. Waliamini Upatanisho wa Yesu Kristo na uthabiti kwenye maagano yao vingeweza kusaidia.
Pata taswira ya shangwe yangu wakati Meb na Jenny walipopokea vibali vipya vya hekaluni na kurejea pamoja kwenye nyumba ya Bwana. Baadaye Meb alikaribia kufa. Ni baraka iliyoje Meb na Jenny wamerejesha uhusiano wa agano na Bwana na kwa kila mmoja na wanahisi upendo wa uhudumiaji wa wengi wanaowazunguka.
Kila mahali ninapoenda, kwa shukrani ninajifunza kutoka kwa wale wanaotumikia na kujali jinsi ambavyo Mwokozi wetu angefanya.
Nchini Peru, mimi na Dada Gong tulikutana na Salvador na ndugu zake.1 Salvador na ndugu zake ni mayatima. Ilikuwa kumbukizi ya siku ya kuzaliwa Salvador. Viongozi wa Kanisa na waumini wanaoihudumia familia hii kwa uaminifu walinivutia. “Dini iliyo safi, isiyo na mawaa … ni hii, kwenda kuwatazama yatima na wajane,”2 “kuwasaidia wadhaifu, kuinyoosha mikono iliyolegea, … kuimarisha magoti yaliyo dhaifu.”3
Huko Hong Kong, rais wa akidi ya wazee kwa staha anashiriki jinsi ambavyo akidi yao kwa uendelevu inafanya asilimia 100 ya mahojiano ya uhudumiaji. “Kwa sala tunapanga mtu na mwenzi wake ili kwamba kila mmoja aweze kutunza na kutunzwa,” anasema. “Mara kwa mara tunawauliza kila mtu na mwenzi wake kuhusu wale wanaowahudumia. Hatuweki tu alama kuonyesha tumekamilisha; tunawahudumia wahudumu ambao wanawatunza watu wetu.”
Huko Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rais Bokolo anashiriki jinsi yeye na familia yake walivyojiunga na Kanisa nchini Ufaransa. Siku moja, alipokuwa akisoma baraka yake ya patriaki, Roho alimwongoza Kaka Bokolo arejee na familia yake nchini Kongo. Kaka Bokolo alijua wangepata changamoto nyingi sana ikiwa wangerejea. Na Kanisa lao, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, lilikuwa bado halijaanzishwa Kinshasa.
Lakini, kwa imani, kama walivyofanya wengine wengi, akina Bokolo walimfuata Roho wa Bwana. Huko Kinshasa, waliwahudumia na kuwabariki wengi waliowazunguka, walishinda changamoto, walipokea baraka za kiroho na kimwili. Leo, wanashangilia katika kuwa na nyumba ya Bwana katika nchi yao.4
Mwongofu alihudumiwa kwa mfano binafsi. Akiwa kijana mdogo, anasema alitumia siku zake kubarizi ufukoni. Siku moja, alisema, “nilimwona msichana mrembo akiwa kwenye vazi la kuogelea.” Kwa mshangao, alikwenda kuuliza kwa nini msichana yule mrembo alivaa vazi la staha. Alikuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na aliuliza kwa tabasamu, “Je, ungependa kuja kanisani Jumapili?” Alisema ndiyo.
Miaka kadhaa iliyopita, wakati tuko kwenye jukumu pamoja, Mzee L. Tom Perry alishiriki jinsi yeye na mhudumiaji mwenzake walivyomhudumia dada aliyeishi peke yake katika ujirani hatari wa Boston. Mzee Perry na mwenzake walipowasili, dada yule kwa tahadhari alielekeza, “Pitisheni vibali vyenu vya hekaluni chini ya mlango.” Ilikuwa baada tu ya kuona vibali vya hekaluni ndipo alipolegeza makufuli kadhaa na kufungua mlango.5 Hakika, sisemi kwamba wenza katika kuhudumu wanahitaji vibali vya hekaluni. Lakini ninapenda wazo kwamba, kadiri wale wanaoheshimu maagano wanavyohudumu, nyumba hufunguliwa na mioyo hufunguka.
Mzee Perry pia alitoa ushauri wa busara. Alisema, “Wapeni wenza idadi inayofaa ya majukumu, yaliyochaguliwa kwa sala, yaliyopangwa vyema kijiografia ili muda wa kusafiri utumike vyema.” Angeshauri, “Anzeni na wale wanaohitaji sana kutembelewa. Imarisheni kuanzia kwa wale ambao wana uwezekano wa kukaribisha na kuitikia vyema matembezi. Alihitimisha, “Uendelevu wa uaminifu huleta miujiza.”
Uhudumiaji wa hali ya juu na mtakatifu6 huja tunaposali kwa ajili ya “upendo msafi wa Kristo”7 na kumfuata Roho. Unakuja pia wakati urais wa akidi za wazee na urais wa Muungano wa Usaidizi, chini ya maelekezo ya askofu, wanaposimamia juhudi za uhudumiaji, ikijumuisha kupanga wahudumu wenza. Tafadhali wapeni wavulana na wasichana wetu fursa zinazohitajika za kusindikiza na kufunzwa na akina kaka na dada wahudumiaji wenye uzoefu. Na tafadhali waruhusuni kizazi chetu kinachoinukia kuwavutia akina kaka na dada wahudumiaji wenza.
Katika baadhi ya maeneo Kanisani, tuna pengo la uhudumiaji. Wengi husema wanahudumu kuliko wanavyohudumiwa. Hatuhitaji hofu ya mambo ya kuwekea vema. Lakini mara nyingi tunahitaji zaidi ya salamu ya dhati ukumbini au neno “Naweza kukusaidia?” katika maegesho ya gari. Katika maeneo mengi, tunaweza kuwafikia, kuwaelewa wengine mahali walipo na kujenga uhusiano wakati tunapowatembelea waumini mara kwa mara katika nyumba zao. Mialiko yenye mwongozo wa kiungu hubadili maisha. Wakati mialiko inapotusaidia kufanya na kushika maagano matakatifu, tunasonga karibu zaidi na Bwana na kila mmoja wetu.
Inasemwa kwamba wale wanaoelewa roho wa kweli wa kuhudumu hufanya zaidi ya mwanzo, wakati wale ambao hawaelewi hufanya kidogo. Acha tufanye zaidi, jinsi ambavyo Mwokozi wetu angefanya. Kama vile wimbo wetu unavyosema, ni “baraka ya wajibu na upendo.”8
Mabaraza ya kata, akidi za wazee na Muungano wa Usaidizi, tafadhalini msikilizeni Mchungaji Mwema na mumsaidie “kuwatafuta waliopotea, … kuwarudisha waliofukuzwa, … kuwafunga waliovunjika, … kuwatia nguvu wagonjwa.”9 Tunaweza kuwakaribisha “malaika bila kujua”10 tunapotengeneza nafasi katika nyumba Yake kwa ajili ya wote.11
Uhudumiaji wenye mwongozo wa kiungu hubariki familia na watu binafsi; huimarisha pia kata na matawi. Ifikirie kata au tawi lako kama mfumo wa ikolojia wa kiroho. Katika roho ya fumbo la Kitabu cha Mormoni la miti ya mizeituni, Bwana wa shamba na watumishi wake huleta matunda ya thamani na kuimarisha kila mti kwa kuunganisha pamoja nguvu na udhaifu wa miti yote.12 Bwana wa Shamba na watumishi Wake huuliza kwa kurudia, “Je, naweza kufaya kipi zaidi?”13 Kwa pamoja, wanabariki mioyo na nyumba, kata na matawi, kupitia uhudumiaji endelevu wenye mwongozo wa kiungu.14
Uhudumiaji—uchungaji—hufanya shamba letu kuwa “kitu kimoja”15—kijisitu kitakatifu. Kila mti katika kijisitu ni mti hai wa familia. Mizizi na matawi husokotana. Uhudumiaji hubariki vizazi. Wakati huduma inapohitajika, maaskofu wenye busara na urais wa akidi ya wazee na Muungano wa Usaidizi huuliza, “Nani ni akina kaka na dada wahudumiaji?” Mabaraza ya kata na mahojiano ya uhudumiaji huuliza si tu kuhusu changamoto au matatizo bali pia hutazama kwa macho ili kuona na kushangilia katika huruma nyingi nyororo za Bwana katika maisha yetu pale tunapohudumu kama ambavyo Yeye angehudumu.
Mwokozi ndiye mfano wetu mkamilifu.16 Kwa sababu ni mwema, anaenda akitenda wema.17 Humbariki mmoja na wale 99. Yeye ni mfano binafsi wa utumishi. Tunakuwa zaidi kama Yesu Kristo tunapowatendea “mmojawapo … wa hao walio wadogo” kama ambavyo tungemtendea Yeye,18 tunapompenda jirani yetu kama nafsi yetu,19 “tunapopendana kama vile alivyotupenda,”20 na wakati “anayekuwa mkubwa kwetu, anapokuwa mtumishi wetu.”21
Yesu Kristo anahudumia. Malaika wanahudumia.22 Wafuasi wa Yesu Kristo “wanahudumiana,”23 “hufurahi pamoja nao wafurahio na kulia pamoja nao waliao,”24 “huwalinda [na] … kuwalisha [watu] kwa vitu vinavyohusu utakatifu,”25 “huwakumbuka … masikini na wenye shida, wagonjwa na walioteseka,”26 hufanya jina Lake lijulikane kote katika huduma yetu.27 Tunapohudumu jinsi ambavyo Yeye angehudumu, tunashuhudia miujiza, baraka Zake.28 Tunapata “huduma bora zaidi.”29
Tunaweza kuchoka kimwili. Lakini katika huduma Yake “hatukati tamaa katika kutenda mema.”30 Kwa bidii tunafanya kadiri ya uwezo wetu, hatukimbii kuliko uwezo wetu,31 bali tunatumaini, kama vile Mtume Paulo anavyofundisha kwamba “Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.”32 Kwani Mungu ambaye “humpa mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atazizidisha.”33 Kwa maneno mengine, Mungu hutajirisha “vitu vyote kuwa na ukarimu wote.”34 Wale “wapandao kwa ukarimu watavuna kwa ukarimu.”35
Popote tulipo wakati huu wa Pasaka, acha tufikie na kujali kama ambavyo Mwokozi wetu angefanya, hususani kwa wale ambao tumepata fursa kwa upendo na kwa jukumu kuwahudumia. Kwa kufanya hivyo, na tusonge karibu zaidi na Yesu Kristo na kila mmoja wetu, tukiwa zaidi kama Yeye na wafuasi wa Yesu Kristo ambao Yeye angetaka kila mmoja wetu tuwe. Katika jina lake takatifu, Yesu Kristo, amina.