Mkutano Mkuu
Kwa Usalama Wamekusanyika Nyumbani
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Kwa Usalama Wamekusanyika Nyumbani

Tuko katika nafasi ya kipekee ya kuwakusanya Israeli pande zote mbili za pazia kuliko hapo awali chini ya mpango wa Baba.

Rais Russell M. Nelson, nabii wetu mpendwa, kwa dhati amesisitiza kwamba wajibu wetu wa kipekee ni kusaidia kukusanya Israeli waliotawanyika na kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo.1 Baba wa roho zetu anatamani watoto Wake kwa usalama wakusanyike nyumbani.

Mpango wa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili ya usalama wa kukusanyika kwa watoto wake nyumbani hautegemei mafanikio ya kiulimwengu, hali za kiuchumi, elimu, rangi au jinsia. Mpango wa Baba umejikita kwenye haki, kushika amri zake, na kupokea ibada takatifu na kuheshimu maagano tunayofanya.2

Mafundisho matakatifu yenye mwongozo wa kiungu kwamba sisi sote ni kaka na dada na “sote ni sawa kwa Mungu” ndio msingi wa kazi hii kuu ya kukusanya. Fundisho hili linakubaliana na wale wanaotamani sana kwamba watu wa hali mbalimbali za kiuchumi na rangi wapate uzoefu wa maisha bora. Tunapongeza na kujiunga katika juhudu za aina hiyo. Zaidi ya hayo, matamanio yetu ni kwa watoto wote wa Mungu waje kwake na wapokee baraka za milele Yeye anazozitoa kupitia injili Yake.3 Kwenye maneno ya utangulizi ya Bwana kwenye Mafundisho na Maagano Anatamka, “Sikilizeni enyi watu kutoka mbali; na ninyi mlio juu ya visiwa vya bahari, sikilizeni kwa pamoja.”4

Napenda kwamba mstari wa kwanza kabisa katika Mafundisho na Maagano unajumuisha watu walio juu ya “visiwa vya bahari.” Nimewahi kuwa na miito maalumu mara tatu ya kuhudumu na kuishi juu ya visiwa vya bahari. Kwanza nilihudumu kama mmisionari kijana kwenye visiwa vya Uingereza, pili kama Kiongozi Mkuu mpya mwenye Mamlaka katika visiwa vya Ufilipino na baadaye kama Rais wa Eneo katika visiwa vya Pasifiki, ambavyo vinajumuisha Visiwa vya Polinesia.

Maeneo haya yote matatu kwa mafanikio makubwa yamefanikiwa kukusanya waumini katika injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Wamisionari kwa mara ya kwanza waliwasili katika visiwa vya Uingereza mnamo mwaka 1837. Hii ilikuwa mwaka mmoja baada ya Joseph Smith kuweka wakfu Hekalu la Kirtland, mahali ambapo Musa alirejesha “funguo za kukusanyika kwa Israeli kutoka pande nne za dunia, na kuongozwa kwa makabila kumi kutoka nchi ya kaskazini.”5 Mafanikio ya mapema kabisa katika Visiwa vya Uingereza ni hadithi kuu ya kale. Kufikia mwaka 1851 zaidi ya nusu ya waumini wa Kanisa walikuwa waongofu waliokuwa wamebatizwa katika Visiwa vya Uingereza.6

Mnamo 1961, Mzee Gordon B. Hinkley alitembelea na kuanzisha juhudi za kwanza za kazi ya umisionari katika Visiwa vya Ufilipino. Kwa wakati huo kulikuwa na mwanamume mmoja tu aliyekuwa na Ukuhani wa Melkizedeki. La kushangaza, kuna waumini zaidi ya 850,000 leo katika Visiwa vya Ufilipino. Ninavutiwa na watu wa Ufilipino; wanao upendo wa kina na wa kudumu kwa Mwokozi.

Pengine isiyojulikana sana ni juhudi ya kazi ya umisionari katika visiwa vya Polinesia. Ilianza mnamo 1844 wakati Addison Pratt alipowasili kwenye kile ambacho sasa kinajulikana kama French Polinesia.7 Wengi wa Wapolinesia tayari walikuwa wakiamini katika familia za milele na kumpokea Yesu Kristo kama Mwokozi wao. Leo asilimia 25 ya Wapolinesia katika Visiwa vya Polinesia ni waumini wa Kanisa.8

Wakati fulani nilimsikiliza msichana wa miaka 17 kwenye kisiwa cha mbali cha Tahiti aliyekuwa wa kizazi cha 7 cha waumini. Alitoa heshima kwa waanzilishi wake ambao waliongoka mnamo mwaka 1845 huko Tubuai, miaka miwili kabla ya waumini wa kwanza wa Kanisa kuwasili katika Bonde la Salt Lake.9

Mafundisho yetu yako wazi kwamba patakuwa na muda na majira kwa watu wote kupokea na kujibu ujumbe wa injili. Mifano hii ni sehemu tu ya picha iliyo kubwa. Rais Nelson daima amekuwa akisisitiza kwamba kukusanywa kwa Israeli ni changamoto “kubwa, … kusudi, na … kazi iliyoko duniani leo.”10

Mpaka kufikia Urejesho wa Kanisa la Yesu Kristo, ikijumuisha kuja kwa Kitabu cha Mormoni na ufunuo na funguo za ukuhani kutolewa kwa Nabii Joseph Smith, uelewa juu ya kukusanywa kwa Israeli ulikuwa wa vipande vipande na wenye ukomo.11

Jina la kipekee “Israeli” lilikuwa jina alilotunukiwa Yakobo.12 Limekuja kuwakilisha uzao wa Ibrahimu kupitia Isaka na Yakobo. Ahadi na agano halisi kwa Baba Ibrahimu vinapatikana kwenye Ibrahimu 2:9–10, ambayo inasomeka hivi kwa sehemu:

“Na nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, …

Nami nitawabariki [mataifa yote] kupitia jina lako; kwani kadiri wengi watakavyoipokea Injili hii wataitwa kwa jina lako, nao watahesabiwa kuwa uzao wako, na watainuka na kukubariki, kama baba yao.”

Wakati wa Baraza la Mbinguni katika maisha kabla ya kuja duniani, mpango wa wokovu ulijadiliwa na kukubaliwa. Ulijumuisha sheria kadhaa na ibada za injili zilizoanzishwa kabla ya kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu na kutabiriwa juu ya kukusanyika.13 Pia ulijumuisha kanuni ya msingi ya haki ya kujiamulia.

Baada ya karne nyingi kama watu wenye nguvu, ikijumuisha utawala wa Sauli, Daudi, na Solomoni, Israeli iligawanyika. Kabila la Yuda na sehemu ya kabila la Benyamini yakawa ufalme wa Yuda. Waliobaki, walijitambulisha kama makabila kumi ya Israeli.14 Baada ya miaka 200 ya kukaa katika mgawanyiko, msambaratiko wa kwanza wa Israeli ulitokea mnamo mwaka 721 K.K wakati makabila 10 ya Israeli yalipochukuliwa mbali utumwani na mfalme wa Ashuru.15 Baadae walienda nchi za kaskazini.16

Mnamo 600 K.K mwanzoni mwa Kitabu cha Mormoni, Baba Lehi aliongoza kundi la Waisraeli kwenda mabara ya Amerika. Lehi alielewa kukusanyika kwa Israeli ambapo yeye alikuwa sehemu yake. Ananukuliwa na Nefi akisema kwamba nyumba ya Israeli “inapaswa kulinganishwa na mti wa mzeituni, ambao matawi yake yanapaswa kukatwa na kutawanywa kote usoni mwa dunia.”17

Katika sehemu inayoitwa Ulimwengu Mpya, historia ya Wanefi na Walamani kama ilivyowekwa katika Kitabu cha Mormoni inamalizika karibia mwaka wa 400 B.K. Watoto wa Baba Lehi wamesambaa kote katika mabara ya Amerika.18

Hii inaelezwa kwa usahihi na Mormoni kwenye 3 Nefi 5:20, ambayo inasomeka: “Mimi ni Mormoni, na ni wa kizazi halisi cha Lehi. Ninayo sababu ya kumsifu Mungu wangu na Mwokozi wangu Yesu Kristo, kwamba aliwatoa babu zetu kutoka nchi ya Yerusalemu.”19

Ni dhahiri kwamba kilele cha historia ya matukio ya Israeli ni kuzaliwa, ujumbe, huduma, na misheni ya Bwana wetu na Mwokozi, Yesu Kristo.20

Baada ya kifo na Ufufuko wa Mwokozi vilivyosanifu umilele, kutawanywa kwa mara ya pili kwa Yuda kunakojulikana vyema kulikotokea kati ya mwaka 70 B.K na 135 B.K ambapo, kutokana na ukandamizaji na mateso ya Kirumi, Wayahudi walitawanywa kote kulikojulikana kama ulimwengu kwa wakati huo.

Rais Nelson amefundisha, “Kitabu cha Mormoni kimekuja duniani kama ishara kwamba Bwana ameanza kukusanya watoto wa agano.”21 Hivyo, Kitabu cha Mormoni kilichotafsiriwa na Nabii Joseph Smith kwa njia ya kipawa na nguvu za Mungu, kimeelekezwa kwa wazao wa Lehi, Israel waliotawanyika na Wayunani ambao wameasiliwa katika makabila ya Israeli. Kichwa cha habari katika 1 Nefi 22 kinasomeka kwa sehemu, “Israeli itatawanyishwa kote katika uso wa dunia—Wayunani watawalea na kuwalisha Israeli kwa injili katika siku za mwisho.” Ukurasa wa jina wa Kitabu cha Mormoni unasomeka kwamba moja ya madhumuni yake ni kwa ajili ya “kuwasadikisha Myahudi na Myunani kwamba Yesu ndiye Kristo.” Kwa Urejesho na Kitabu cha Mormoni, muktadha wa “kukusanywa kwa Israeli” umepanuliwa sana.22

Wale wanaoikubali injili ya Yesu Kristo bila ya kujali ukoo huwa sehemu ya kukusanywa kwa Israeli.23 Kwa kusanyiko hilo na utangazwaji na ujenzi wa mahekalu mengi, tuko katika nafasi ya kipekee ya kuwakusanya Israeli pande zote mbili za pazia kuliko hapo awali chini ya mpango wa Baba.

Rais Spencer W. Kimball, akizungumzia kusanyiko halisi la Israeli, alisema: “Sasa kukusanyika kwa Israeli kunajumuisha kujiunga na kanisa la kweli na … kupata ufahamu wa Mungu wa Kweli.… Mtu yeyote, kwa hiyo, ambaye ameikubali injili ya urejesho, na ambaye sasa anatafuta kumwabudu Bwana katika lugha yake mwenyewe na pamoja na Watakatifu katika mataifa wanakoishi, amekubaliana na sheria ya kuwakusanya Israeli na ni mrithi wa baraka zote walizoahidiwa Watakatifu katika siku hizi za mwisho.”24

“Kukusanywa kwa Israeli sasa kunajumuisha uongofu.”25

Kama ilivyotazamwa kupitia lenzi safi, waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wanayo fursa kubwa ya kupenda, kushiriki, kualika na kusaidia katika kukusanya Israeli ili wapokee utimilifu wa baraka za agano za Bwana. Hii inajumuisha Waafrika na Wazungu, Wamarekani ya Kusini na Kaskazini, Waasia, Waaustralia na wale walio juu ya Visiwa vya bahari. “Kwani amin, sauti ya Bwana i juu ya watu wote.”26 “Kukusanyika huku kutaendelea hadi wenye haki watakapokusanyika katika mkusanyiko wa Watakatifu katika mataifa ya ulimwengu.”27

Hakuna mtu aliyewahi kuzungumzia kwa upana kuhusu kukusanyika kuliko Rais Russell M. Nelson: “Wakati wowote unapofanya kitu chochote kinachomsaidia mtu yeyote—upande wowote wa pazia—ukichukua hatua ya kufanya maagano na Mungu na kupokea ibada zao muhimu za ubatizo na za hekaluni, unasaidia katika kukusanya Israeli. Ni rahisi tu kama hivyo.”28

Kanisa liko wapi leo? Katika miaka 62 tangu nianze kuhudumu misheni mwaka 1960, idadi ya wamisionari wanaohudumu chini ya wito kutoka kwa nabii imeongezeka kutoka 7,683 hadi 62,544. Idadi ya misheni imeongezeka kutoka 58 hadi 411. Idadi ya waumini imeongezeka kutoka takribani 1,700,000 hadi takribani 17,000,000.

Janga la ulimwenguni kote la Uviko-19 kwa muda limeathiri baadhi ya fursa za kushiriki injili. Pia limetoa uzoefu wa kutumia teknolojia mpya, ambayo kwa sehemu kubwa itaboresha ukusanyaji. Tunashukuru kwamba waumini na wamisionari sasa wanapanua jitihada za kukusanya Israeli. Ukuaji unaendelea kila mahali, hususani Amerika ya Kusini na Afrika. Pia tunashukuru kwamba watu wengi kote ulimwenguni wameitikia mwaliko wenye nguvu wa Rais Nelson kwa kuongeza huduma ya umisionari. Hata hivyo, ahadi yetu ya kupenda, kushiriki, na kualika inaweza kukuzwa zaidi.

Sehemu muhimu ya juhudi hii ya umisionari ni kwa waumini binafsi kuwa mfano wa bikoni ya nuru29 popote tunapoishi.30 Hatuwezi kuwa wa kubadilika badilika. Mfano wetu kama wa Kristo wa ukarimu, shangwe, na upendo wa dhati kwa watu wote unaweza kutengeneza siyo tu bikoni ya nuru kwa ajili yao bali pia uelewa kwamba kuna bandari ya usalama katika ibada za wokovu na kuinuliwa za injili ya urejesho ya Yesu Kristo.

Tafadhali eleweni kwamba kuna baraka za kipekee sana katika kushiriki injili ya Yesu Kristo. Maandiko yanazungumzia shangwe na amani, msamaha wa dhambi, ulinzi kutokana na majaribu na nguvu ya kuimarisha kutoka kwa Mungu.31 Tukitazama zaidi ya maisha haya ya duniani, tutakuwa tumetayarishwa kushiriki injili pamoja na wale “walio gizani na chini ya kifungo cha dhambi katika ulimwengu mkuu wa roho za wafu.”32

Sala yangu maalumu leo ni kwa kila mtoto, kila mvulana, kila msichana, kila familia, akidi, Muungano wa Usaidizi, na darasa kurejelea jinsi sisi watu binafsi na kwa pamoja tunavyopokea ushauri huu wa dharura wa kusaidia kukusanya Israeli ambao umetolewa na Bwana na nabii wetu mpendwa.

Tunaheshimu haki ya kujiamulia. Katika maisha haya ulimwenguni, wengi hawataitikia na kushiriki katika kukusanya Israeli. Lakini wengi watajitahidi, na Bwana anawategemea wale ambao wamepokea injili yake kwa haraka wajitahidi kuwa mfano wa bikoni ya nuru ambayo itawasaidia wengine waje kwa Mungu. Hii inaruhusu akina dada na kaka kote duniani kufurahia baraka kutoka mbinguni na ibada za injili ya urejesho ya Yesu Kristo na kwa usalama kukusanyika nyumbani.

Ninatoa ushahidi wangu wa uhakika na wa kitume juu ya uungu wa Yesu Kristo na mpango wa Baba Yetu wa Mbinguni kwa ajili yetu katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Ujumbe wa Ufunguzi,” Liahona, Mei 2021, 7.

  2. Ona Mafundisho na Maagano 20:37.

  3. Ona 2 Nefi 26:33.

  4. Mafundisho na Maagano 1:1. Katika Mafundisho na Maagano 1:4, Bwana anaendelea, “Na sauti ya onyo itakwa kwa watu wote, kwa kinywa cha wafuasi wangu, ambao nimewachagua katika siku hizi za mwisho.”

  5. Mafundisho na Maagano 110:11.

  6. Mnamo 1851 kulikuwa na jumla ya idadi ya waumini wa Kanisa wapatao 52,165. Kulingana na kumbukumbu za Kanisa na “Sensa ya Dini ya 1851” huko Uingereza na Wales, kulikuwa na zaidi ya waumini 28,000 katika maeneo hayo (ona Robert L. Lively Jr., “Some Sociological Reflections on the Nineteenth-Century British Mission,” in Mormons in Early Victorian Britain, ed. Richard L. Jensen na Malcolm R. Thorp [1989], 19–20).

  7. Ona Watakatifu: Hadithi ya Kanisa la Yesu Kristo katika Siku za Mwisho, juzuu ya 1, The Standard of Truth, 1815–1846 (2018), 494–95, 514–15, 573.

  8. Tonga—asilimia 45; Samoa: asilimia 31; Samoa ya Amerika: asilimia 22.5; na French Polynesia: asilimia 7.

  9. Ona Watakatifu, 573–74.

  10. Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli” (mkutano wa ibada wa vijana ulimwenguni kote, Juni 3, 2018), HopeofIsrael.ChurchofJesusChrist.org.

  11. Fundisho hili la kipekee na lenye nguvu liko katika Kitabu cha Mormoni na mahususi katika makala ya kumi ya imani, ambayo inaanza, “Tunaamini katika kukusanyika kiuhalisia kwa Israeli, na katika urejesho wa Makabila Kumi.” (ona James E. Talmage, The Articles of Faith, 12th ed. [1924], 314–44).

  12. Kama ilivyorekodiwa katika Mwanzo 32:28, maandiko yanasomeka, “Jina lako halitaitwa tena Yakobo, bali Israeli: kwani kama mfalme umeshindana na Mungu na wanadamu.”

  13. Ona Joseph Smith, katika “History, 1838–1856, volume D-1,” 1572, josephsmithpapers.org; ona pia Joseph Smith, “Discourse, 11 June 1843–A, as Reported by Wilford Woodruff,” [42–43], josephsmithpapers.org; Joseph Smith, “Discourse, 11 June 1843–A, as Reported by Willard Richards,” [241], josephsmithpapers.org.

  14. Ona Bible Dictionary, “Israel, Kingdom of”; James E. Talmage, The Articles of Faith, 315. Rehoboamu na watu wake walijulikana kama Ufalme wa Yuda na waliishi upande wa kusini wa Israeli ya sasa.

  15. Ona 2 Wafalme 17:23.

  16. Ona Mafundisho na Maagano 133:26; ona pia Mafundisho na Maagano 110:11.

  17. 1 Nefi 10:12. Amoni baadae alisema, “Libarikiwe jina la Mungu wangu, ambaye amewajali watu hawa, ambao ni tawi la mti wa Israeli, na limepotea kutoka kwenye shina lake kwenye nchi ngeni” (Alma 26:36).

  18. Rais Spencer W. Kimball, akizungumza kuhusu Israeli ya Walamani, alifundisha kwamba Sayuni ni Mabara yote ya Amerika. Alisema, “Tuko ndani ya Israeli na tunakusanywa” (The Teachings of Spencer W. Kimball, ed. Edward L. Kimball [1982], 439).

  19. Wakati Baba Lehi alipoelekezwa aichukue familia yake na kwenda nyikani, angalau sehemu ya sababu ilikuwa kwamba Yerusalemu ingeangamizwa (ona 1 Nefi 2). Maangamizo ya Hekalu la Sulemani, kuanguka kwa Yerusalemu, na utumwa wa kabila la Yuda vilitokea karibu na miaka 586 K.K

    “Israeli ilitekwa takriban mnamo 720 B.C.E., na makabila yake 10 kupelekwa uhamishoni. … [Katika Yerusalemu,] Hekalu la Solomoni lilihimili mashambulizi kadhaa kutoka nguvu za kigeni kabla ya hatimaye, mnamo 586 B.C.E., kuharibiwa kabisa na jeshi la Nebukadreza mfalme wa Babeli” (David B. Green, “The History of the Jewish Temple in Jerusalem,” Haaretz, Aug. 11, 2014, haaretz.com/jewish/.premium-history-of-the-temple-in-jerusalem-1.5256337). Ona pia 2 Wafalme 25:8–9.

  20. Ona Tad R. Callister, Upatanisho Usio na Mwisho (2000).

  21. Ona Russell M. Nelson, “Children of the Covenant,” Ensign, May 1995, 33; ona pia “Maagano,” Liahona, Nov. 2011, 88.2011:

  22. Ona Russell M. Nelson, katika R. Scott Lloyd, “Seminar for New Mission Presidents: ‘Swift Messengers’ to Scattered Israel,” Church News, July 13, 2013, thechurchnews.com. Rais Nelson amesema kwamba mkusanyiko “si suala la kieneo; ‘Ni suala la kujitolea kwa mtu binafsi. Watu wanaweza ‘kuletwa kwenye ufahamu wa maarifa ya Bwana’[3 Nefi 20:13] bila ya kuondoka kwenye ardhi zao za nyumbani.” (“The Gathering of Scattered Israel,” Liahona, Nov. 2006, 81). Ona pia 3 Nefi 21:1–7.

  23. Mafundisho yetu yako wazi; “Bwana alitawanya na kuwatesa makabila kumi na mawili ya Israeli kwa sababu ya uovu wao na uasi. Hata hivyo, Bwana pia alitumia huu mtawanyiko kwa watu wake waliochaguliwa miongoni mwa mataifa ya ulimwengu kubariki mataifa hayo.” (Ona Guide to the Scriptures, “Israel—The Scattering of Israel,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org.)

  24. Spencer W. Kimball, The Teachings of Spencer W. Kimball, 439.

  25. Ufupisho wa kichwa cha habari katika Spencer W. Kimball, The Teachings of Spencer W. Kimball, 438. Ona pia “All Are Alike unto God,” ed. E. Dale LeBaron (1990), a collection of 23 conversion stories by Black African Latter-day Saints. Sister Julia N. Mavimbela alisema kwamba kabla hajajiunga na Kanisa na kukutana na neno Israeli, “angerusha kitabu pembeni na kusema, ‘ni kwa ajili ya wazungu. Si kwa ajili yetu. Sisi hatujachaguliwa. Leo ninajua mimi ni sehemu ya familia ya kifalme kama ninaishi kwa haki. Mimi ni Mwisraeli na nilipokuwa nikifanya ibada hekaluni nilipata hisia kwamba sote tuko duniani kama familia moja” (in “All Are Alike unto God,” 151).

  26. Mafundisho na Maagano 1:2.

  27. Spencer W. Kimball, The Teachings of Spencer W. Kimball, 438.

  28. Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli.”

  29. Mtume Paulo alimwambia rafiki yake kijana Timotheo “awe … kielelezo kwao waaminio” (1 Timotheo 4:12).

  30. Ona 3 Nefi 18:24.

  31. Ona Mosia 18:8–13; 3 Nefi 18:25; Mafundisho na Maagano 18:10–16; 31:5; 62:3.

  32. Mafundisho na Maagano 138:57.

Chapisha