Mkutano Mkuu
Wamoja katika Kristo
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Wamoja katika Kristo

Ni katika na kupitia uaminifu wetu binafsi na upendo kwa Yesu Kristo kwamba tunaweza kutumaini kuwa wamoja.

Kama ambavyo Rais Dallin H. Oaks amesema, leo ni Jumapili ya Matawi, mwanzo wa wiki takatifu, ikiashiria kuingia kwa ushindi kwa Bwana huko Yerusalemu, mateso Yake Gethsemane na kifo msalabani siku chache baadaye na Ufufuko Wake wenye utukufu kwenye Jumapili ya Pasaka. Naomba tusisahau kile ambacho Kristo alivumilia ili kutukomboa.1 Na tusipoteze shangwe kuu tutakayoihisi kwa mara nyingine siku ya Pasaka wakati tunapotafakari ushindi Wake juu ya kaburi na zawadi ya ufufuko wa ulimwengu wote.

Jioni kabla ya mateso na kusulubiwa kulikokuwa kunamsubiri, Yesu alishiriki mlo wa Pasaka pamoja na Mitume Wake. Mwishoni mwa Mlo huu wa Mwisho, katika sala takatifu ya kutuombea, Yesu alimuomba Baba Yake katika maneno haya: “Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa [mitume wangu], ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.”2

Kisha, kwa ukunjufu, Mwokozi aliongezea ombi Lake kuwajumuisha wote waaminio.

“Siwaombei hao tu, bali nawaombea pia wote watakaoamini kutokana na ujumbe wao;

“Ili wote wawe kitu kimoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, ili nao waweze kuwa kitu kimoja na sisi.”3

Kuwa wamoja ni dhima inayojirudia katika injili ya Yesu Kristo na katika matendo ya Mungu kwa watoto Wake. Tukirejelea mji wa Sayuni siku za Henoko, inasemwa kwamba “walikuwa wa moyo mmoja na wazo moja.”4 Kuhusu Watakatifu wa kale wa Kanisa la mwanzo la Yesu Kristo, Agano Jipya linasema, “Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja.”5

Katika nyakati zetu, Bwana ameasa, “Ninawaambia, muwe na umoja; na kama hamna umoja ninyi siyo wangu.”6 Miongoni mwa sababu ambazo Bwana alizitoa za kwa nini Watakatifu wa Missouri walishindwa kujenga Sayuni ni kwamba “hawana ushirikiano kulingana na ushirika unaotakiwa kwa sheria ya ufalme wa selestia.”7

Mahala ambapo Mungu anashinda katika mioyo na akili, watu huelezewa kama “kitu kimoja, watoto wa Kristo.”8

Wakati Mwokozi aliyefufuka alipowatokea watu wa kale wa Kitabu cha Mormoni, alielezea kutopendezwa na kukosekana kwa maelewano miongoni mwao kuhusu ubatizo na mambo mengine. Aliwaamuru:

“Na hakutakuwa na ugomvi miongoni mwenu, kama vile ilivyo hapa sasa; wala hakutakuwa na ugomvi miongoni mwenu kuhusu nukta za mafundisho yangu, kama vile ilivyokuwa.

“Kwani amin, amin, nawaambia, yule ambaye ana roho ya ubishi siye wangu, bali ni wa ibilisi, ambaye ni baba wa ubishi.”9

Katika ulimwengu wetu wa mabishano mengi, umoja utapatikanaje, hususani ndani ya Kanisa, ambapo tunapaswa kuwa wa “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja”?10 Paulo anatupatia mwongozo:

“Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.

“Hapana Myahudi wala Myunani, hapana mtumwa wala huru, hapana mtu mume wala mtu mke: maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.”11

Sisi pia tu tofauti na wakati mwingine tusioelewana sana mpaka kukosa kuja pamoja kama wamoja kwa msingi wa lolote au kwa jina lolote lile. Ni katika Jina la Yesu Kristo pekee tunaweza kwa dhati kuwa wamoja.

Kuwa wamoja katika Kristo huanza kwa mtu mmoja mmoja—sote tunaanza na sisi wenyewe. Sisi ni wanadamu wa nyama na roho na wakati mwingine tupo katika vita ya nafsi zetu wenyewe. Kama Paulo alivyosema:

“Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani;

“Lakini viungo vyangu [vya mwili] vinapiga vita dhidi ya sheria ya akili yangu, na kunileta katika utumwa wa sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu.”12

Yesu pia alikuwa mwanadamu wa mwili na roho. Alijaribiwa; Anaelewa; Anaweza kutusaidia tufikie umoja wa ndani yetu.13 Kwa hivyo, tukitegemea nuru na rehema ya Kristo, tunajitahidi kuzipa roho zetu—na Roho Mtakatifu—utawala juu ya mwili. Na tunapoanguka, Kristo, kwa Upatanisho Wake, ametupatia zawadi ya toba na fursa ya kujaribu tena.

Kama kila mtu “atamchagua Kristo,” basi kwa pamoja tunaweza kutumainia kuwa, kama Paulo alivyosema, “mwili wa Kristo.”14 “Kumchagua Kristo” hakika hujumuisha kufanya “amri Yake iliyo kuu na ya kwanza”15 kuwa dhamira yetu ya kwanza na kuu, na kama tutampenda Mungu, tutashika amri Zake.16

Umoja kwa kaka na dada zetu katika mwili wa Kristo hukua tunapotii amri ya pili—isiyoweza kutenganishwa na ya kwanza—ya kuwapenda wengine kama tunavyojipenda wenyewe.17 Na nadhani umoja mkamilifu zaidi utakuwepo miongoni mwetu kama tutafuata mtazamo wa juu na mtakatifu wa Mwokozi wa amri hii ya pili—kupendana si tu kama tunavyojipenda wenyewe lakini kama vile Yeye alivyotupenda.18 Kiujumla, ni “kila mtu kutafuta ustawi wa jirani yake, na kufanya mambo yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu.”19

Rais Marion G. Romney, mshauri wa zamani katika Urais wa Kwanza, katika kuelezea jinsi amani na umoja wa kudumu unavyopatikana, alisema:

“Kama mtu mmoja, akianguka kwa Shetani, anajawa na kazi za mwili, anapigana vita ndani yake mwenyewe. Kama wawili wakianguka, kila mmoja hupigana vita ndani yake mwenyewe na anapigana na mwenzake. Kama wengi wakianguka, jamii [huvuna] mavuno ya mfadhaiko na mfarakano. Kama viongozi wa nchi wakianguka, kunakuweko na mfarakano ulimwenguni kote.”

Rais Romney aliendelea: “Kama vile ambavyo kazi za mwili zina matumizi ulimwenguni kote, ndivyo ilivyo na injili ya amani. Kama mtu mmoja akiishi kwa amani, anayo amani ndani yake. Kama watu wawili wakiishi kwa amani, wote wanakuwa na amani ndani yao na kwa kila mmoja. Kama wananchi wakiishi kwa amani, nchi ina amani. Wakati panapokuwa na mataifa mengi yakifurahia tunda la Roho la kudhibiti mambo ya ulimwengu, ndipo, na wakati huo pekee, ngoma za vita zitakoma, na bendera za vita kushushwa. … (Ona Alfred Lord Tennyson, “Locksley Hall,” The Complete Poetical Works of Tennyson, ed. W. J. Rolfe, Boston, Houghton–Mifflin Co., 1898, p. 93, mistari 27–28.)”20

Kwa “kumchagua Kristo,” itawezekana kutatua au kuweka kando tofauti, kutoelewana na mivutano. Mfano mzuri wa kushinda mgawanyiko unapatikana katika historia yetu ya Kanisa. Mzee Brigham Henry Roberts (zaidi akijulikana kama B. H. Roberts), aliyezaliwa Uingereza mnamo 1857, alihudumu kama mshiriki wa Baraza la Kwanza la Sabini—kile tunachokiita leo kama Urais wa Sabini. Mzee Roberts alikuwa mlinzi shupavu na asiyechoka wa injili ya urejesho na wa Kanisa katika baadhi ya nyakati ngumu sana za Kanisa.

Picha
B. H. Roberts akiwa kijana

Hata hivyo, mnamo 1895, huduma ya Mzee Roberts ndani ya Kanisa ilikuwa mashakani kutokana na mfarakano. B. H. alikuwa amechaguliwa kama mwakilishi kwenye makubaliano ambayo yalipendekeza katiba kwa ajili ya Utah wakati ilipokuwa jimbo. Baadaye, aliamua kuwa mgombea wa Bunge la Marekani lakini bila kuujulisha au kutafuta ruhusa ya Urais wa Kwanza. Rais Joseph F. Smith, mshauri katika Urais wa Kwanza, alimkemea B. H. kwa kushindwa huko katika mkutano mkuu wa ukuhani. Mzee Roberts alipoteza kwenye uchaguzi na kuhisi kupoteza kwake kulichangiwa kwa sehemu kubwa na kauli za Rais Smith. Aliwakosoa viongozi wa Kanisa katika baadhi ya hotuba na mahojiano ya kisiasa. Alijiondoa kwenye kushiriki kikamilifu katika huduma ya Kanisa. Katika kikao kirefu ndani ya Hekalu la Salt Lake pamoja na washiriki wa Urais wa Kwanza na Baraza la Kumi na Wawili, B. H. alibakia mkaidi kwa kujiondolea hatia mwenyewe. Baadaye, “Rais [Wilford] Woodruff alimpatia [Mzee Roberts] wiki tatu za kutafakari msimamo wake. Kama asingetubu, wangempumzisha kutoka kwa wale Sabini.”21

Katika vikao vya ndani pamoja na Mitume Heber J. Grant na Francis Lyman, B. H. mwanzoni hakukubali, lakini upendo na Roho Mtakatifu hatimaye vilitawala. Machozi yalimtiririka. Mitume hao wawili waliweza kujibu baadhi ya vinyongo na makwazo ambayo yalimsumbua B. H., na waliachana kwa ombi zuri la moyo la mapatano. Asubuhi iliyofuatia, baada ya sala ndefu, Mzee Roberts alituma ujumbe kwa Wazee Grant na Lyman kwamba alikuwa tayari kuungana tena na ndugu zake.22

Alipokutana na Urais wa Kwanza baadaye, Mzee Roberts alisema, “Nilienda kwa Bwana na nilipokea nuru na maelekezo kupitia Roho Wake ya kuheshimu mamlaka ya Mungu.”23 Akihamasishwa na upendo wake kwa Mungu, B. H. Roberts alibakia mwaminifu na kiongozi shupavu wa Kanisa mpaka mwisho wa maisha yake.24

Picha
Mzee B. H. Roberts

Sisi pia tunaweza kuona katika mfano huu kwamba umoja haumaanishi tu kukubaliana kwamba kila mmoja anapaswa afanye mambo yake au kwenda anakokutaka yeye. Hatuwezi kuwa wamoja isipokuwa sote tuweke juhudi zetu kwenye lengo moja. Inamaanisha, katika maneno ya B. H. Roberts, kujiweka chini ya mamlaka ya Mungu. Sisi ni washiriki tofauti wa mwili wa Kristo, tukitekeleza kazi tofauti katika nyakati tofauti—sikio, jicho, kichwa, mkono, mguu—na bado vyote ni vya mwili mmoja.25 Kwa hivyo, lengo letu ni “kwamba kusiwe na faraka katika mwili; bali viungo vitunzane.”26

Umoja hauhitaji usawa, lakini unahitaji mapatano. Tunaweza kuwa na mioyo yetu ikiwa imefungwa pamoja katika upendo, kuwa wamoja katika imani na mafundisho na bado tukashangilia timu tofauti, tukatofautiana kwenye masuala ya kisiasa, tukawa na mijadala kuhusu malengo na njia sahihi ya kuyafanikisha na mambo mengine mengi kama hayo. Lakini kamwe hatuwezi kutofautiana au kubishana kwa hasira au kudharauliana. Mwokozi alisema:

“Kwani amin, amin, nawaambia, yule ambaye ana roho ya ubishi siye wangu, lakini ni wa ibilisi, ambaye ni baba wa ubishi, na huchochea mioyo ya watu kubishana na hasira mmoja kwa mwingine.

“Tazama, hili sio fundisho langu, kuchochea mioyo ya wanadamu kwa hasira, mmoja dhidi ya mwingine; lakini hili ndilo fundisho langu, kwamba vitu kama hivi viondolewe mbali.”27

Mwaka mmoja uliopita, Rais Russell M. Nelson alitusihi kwa maneno haya: “Hakuna kati yetu anayeweza kudhibiti mataifa au matendo ya wengine au hata washiriki wa familia zetu wenyewe. Lakini tunaweza kujidhibiti wenyewe. Wito wangu leo, akina kaka na akina dada wapendwa, ni kumaliza migogoro inayoendelea moyoni mwako, na nyumbani kwako, na maishani mwako. Zika mwelekeo wowote wa kutaka kuwaumiza wengine—iwe ni hasira, ulimi mkali au chuki kwa mtu ambaye amekuumiza. Mwokozi alituamuru kugeuza shavu lingine [ona 3 Nefi 12:39], kuwapenda maadui zetu na kuwaombea wale wanaotutumia vibaya [ona 3 Nefi 12:44].”28

Narudia tena kwamba ni katika na kupitia uaminifu wetu binafsi na upendo kwa Yesu Kristo kwamba tunaweza kutumaini kuwa wamoja—wamoja ndani yetu, wamoja nyumbani, wamoja Kanisani, hatimaye wamoja katika Sayuni, na zaidi ya yote, wamoja na Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.

Ninarejea kwenye matukio ya Wiki Takatifu na kilele cha ushindi wa Mkombozi wetu. Ufufuko wa Yesu Kristo hutoa ushahidi wa uungu Wake na kwamba Yeye ameshinda mambo yote. Ufufuko Wake unatoa ushuhuda kwamba, tukiunganishwa Kwake kwa maagano, sisi pia tunaweza kushinda mambo yote na kuwa wamoja. Ufufuko Wake unatoa ushahidi kwamba kupitia Yeye, kutokufa na uzima wa milele ni uhalisia.

Asubuhi hii, ninatoa ushahidi wa Ufufuko Wake halisi na vyote vinavyomaanishwa kwa ufufuko huo, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha