Mavuno Hafifu
Mwokozi anasimama tayari kukubali matoleo yetu madogo na kuyakamilisha kupitia neema Yake. Tukiwa na Kristo, hakuna mavuno hafifu.
Kama mvulana mdogo, nilijifunza kupenda mabadiliko ya kuvutia katika misimu ya mwaka huko kusini magharibi mwa Montana, mahali nilipokulia. Msimu wangu pendwa ulikuwa ni msimu wa majani kupukutika—wakati wa mavuno. Familia yetu ilitumaini na kusali kwamba miezi yetu ya kazi ngumu ingelipwa kwa mavuno mengi. Wazazi wangu walihofia hali ya hewa, afya ya wanyama na mazao, na mambo mengine mengi ambayo kwayo wao walikuwa na udhibiti mdogo.
Kadiri nilivyokua, nilielewa zaidi kuhusu utayari uliohitajika. Maisha yetu yalitegemea mavuno. Baba yangu alinifundisha kuhusu vifaa tulivyotumia kuvuna nafaka. Nilitazama alipokuwa akiendesha mashine katika shamba, akikata fungu la nafaka na kisha akikagua nyuma ya mashine ya kuvunia kuhakikisha kwamba nafaka nyingi inaingia kwenye tangi na haikutupwa pamoja na makapi. Alirudia zoezi hili mara kadhaa, akirekebisha mashine kila wakati. Nilikimbia pembeni mwake na kupurua makapi pamoja naye na kujifanya kwamba nilikuwa najua kile nilichokuwa ninafanya.
Baada ya yeye kuridhishwa na urekebishaji wa mashine, nilipata punje za ngano ndani ya makapi mchangani na kuzipeleka kwake kwa mtazamo wa uhakiki. Sitasahau kile baba yangu alichoniambia: “Ni vyema vya kutosha na kilicho bora zaidi ambacho mashine hii inaweza kufanya.” Bila kuridhishwa na maelezo yake, nilitafakari mapungufu ya mavuno haya.
Baadaye kidogo, wakati hali ya hewa ilipogeuka kuwa baridi jioni, nilitazama maelfu ya bata maji, bata bukini, na bata wa kawaida waliokuwa wakihama wakishuka shambani kujilisha wenyewe katika safari yao ndefu ya kwenda kusini. Walikula mabaki ya nafaka kutoka kwenye mavuno yetu yaliyo na mapungufu. Mungu alikuwa ameyakamilisha. Na hakuna punje iliyopotea.
Mara nyingi ni jaribu katika ulimwengu wetu na hata katika utamaduni wa Kanisa kuwa na tamanio kuhusu ukamilifu. Mitandao ya kijamii, matarajio yasiyofikiwa na mara nyingi kujikosoa kwetu binafsi huleta hisia za kuwa na mapungufu—kwamba sisi si wazuri vya kutosha na kamwe hatutakuwa. Wengine hata hukosa kuelewa mwaliko wa Mwokozi wa “basi ninyi mtakuwa wakamilifu.”1
Kumbuka kwamba nadharia ya ukamilifu sio sawa na kuwa mkamilifu katika Kristo.2 Nadharia ya ukamilifu huhitaji yasiyowezekana, kiwango cha kujiumiza ambacho hutulinganisha sisi na wengine. Hii husababisha hatia na wasiwasi na inaweza kutufanya tutake kujiondoa na kujitenga wenyewe.
Kukamilishwa katika Kristo ni jambo lingine. Ni mchakato—unaongozwa kwa upendo na Roho Mtakatifu—wa kuwa zaidi kama Mwokozi. Viwango vinawekwa na Baba mkarimu wa Mbinguni na mwenye kujua yote na kwa uwazi vimeelezwa katika maagano tuliyoalikwa kukumbatia. Hutuondolea mzigo wa hatia na mapungufu, daima kusisitiza sisi ni kina nani mbele za Mungu. Wakati mchakato huu hutuinua na kutusukuma kuwa bora, tunapimwa kwa kujitolea kwetu binafsi kwa Mungu ambako tunaonyesha katika juhudi zetu za kumfuata Yeye kwa imani. Tunapokubali mwaliko wa Mwokozi wa kusonga Kwake, punde tunatambua kwamba ubora wetu unatosha vizuri na kwamba neema ya Mwokozi mwenye upendo hufidia tofauti katika njia tusizoweza kufikiria.
Tunaweza kuona kanuni hii ikifanya kazi wakati Mwokozi alipowalisha watu elfu tano.
“Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? …
“Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu.
“Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia,
“Yupo hapa mtoto, ambaye ana mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa?”3
Je, umewahi kujiuliza jinsi Mwokozi alivyohisi kuhusu kijana huyu mdogo, ambaye kwa imani ya mtoto alitoa kile ambacho yeye alijua hakika hakingetosha kwa ajili ya kazi iliyokuwa mbele yao?
“Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka.
“Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee chochote.”4
Mwokozi alikamilisha toleo dogo.
Muda mfupi baada ya tukio hili, Yesu aliwatuma wanafunzi Wake watangulie kwa chombo. Punde walijipata kwenye bahari yenye mawimbi makali usiku wa manane. Waliogopa walipoona kiwiliwili kikitembea na kuwaendea juu ya maji.
“Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope.
“Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.
“Akasema, Njoo. Na wakati Petro aliposhuka kutoka kwenye mtumbwi, alitembea juu ya maji, kwenda kwa Yesu.
“Lakini alipoona upepo mkali, aliogopa; na kuanza kuzama, alipiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.
“Na mara moja Yesu akanyoosha mkono wake, na akamshika, na akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?”5
Akina kaka na akina dada, hiyo inawezekana haikuwa mwisho wa mazungumzo hayo. Ninaamini kwamba Petro na Mwokozi walipokuwa wakitembea kuja chomboni wameshikana mikono, Petro ameloa na labda akijihisi mpumbavu, Mwokozi anaweza kuwa alisema kitu kama hiki: “Ee, Petro, usiogope wala usijali. Kama ungejiona vile ninavyokuona wewe, mashaka yako yangeondoka na imani yako ingeongezeka. Ninakupenda, mpendwa Petro; wewe ulitoka chomboni. Matoleo yako yamekubalika, na hata ingawa uliyumba, daima nitakuwa hapo kukuinua kutoka kwenye kina, na matoleo yako yatafanywa kuwa makamilifu.
Mzee Dieter F. Uchtdorf alifundisha:
Ninaamini Mwokozi Yesu Kristo angewataka muone, kuhisi na kujua kwamba Yeye ni nguvu yenu. Kwamba kwa msaada Wake, kusiwe na mwisho wa kile mnachoweza kutimiza. Kwamba uwezekano wenu wa kuwa ni usio na mwisho. Angewataka mjione kama vile Awaonavyo. Na hiyo ni tofauti na jinsi ulimwengu uwaonavyo. …
“Yeye huwapa nguvu waliodhoofu; na kwa wale wahisio kukosa nguvu, Huwaongezea nguvu.”6
Sisi lazima tukumbuke kwamba matoleo-yetu-bora-lakini yenye mapungufu, Mwokozi anaweza kuyakamilisha. Bila kujali jinsi juhudi zetu zinavyoweza kuonekana ndogo, hatupaswi kudharau nguvu za Mwokozi. Neno rahisi la ukarimu, matembezi ya muda mchache lakini ya dhati ya kuhudumia, au somo la Msingi lililofunzwa kwa upendo vinaweza, kwa msaada wa Mwokozi, kutoa faraja, kulainisha mioyo na kubadilisha maisha milele. Juhudi zetu dhaifu zinaweza kuongoza kwenye miujiza, na katika mchakato huu, tunaweza kushiriki katika mavuno kamili.
Kila mara, tunawekwa katika hali ambayo itatusaidia tukue. Yawezekana tusifanye jukumu ipasavyo. Yawezekana tukawatazama wale tunaotumikia nao na kuhisi kamwe hatutawafikia. Akina kaka na akina dada, kama mnahisi hivi, watazameni wanaume na wanawake wa kipekee walio nyuma yangu ambao ninatumikia nao.
Ninahisi uchungu wenu.
Nimejifunza, hata hivyo, kwamba kama vile ambavyo nadharia ya ukamilifu si sawa na kuwa mkamilifu katika Kristo, kujilinganisha si sawa na kufuata mfano. Tunapojilinganisha na wengine, kunaweza kuwa na matokeo mawili tu. Huenda tutajiona kuwa bora kuliko wengine na kuwahukumu na kuwakosoa, au tutajiona sisi wenyewe kuwa duni kuliko wengine na kuwa na wasiwasi, kujikosoa na kukata tamaa. Kujilinganisha na wengine ni nadra sana kuwa na tija, hakuinui na wakati mwingine huuzunisha kabisa. Kwa kweli, ulinganisho huu unaweza kuwa angamizi kiroho, kukatuzuia kupokea msaada wa kiroho tunaohitaji. Kwa upande mwingine, kufuata mfano wa wale tunaowaheshimu wanaoonesha sifa kama za Kristo kunaweza kutufunza, kutuinua na kutusaidia tuwe wafuasi bora wa Yesu Kristo.
Mwokozi alitupatia mfano wa kufuata kwa Yeye kufuata mfano wa Baba. “Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?”7
Na kisha Yeye alifundisha, “Amini, amini, nawaambia, mtu aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo atazifanya pia.”8
Bila kujali jinsi juhudi zetu zinavyoonekana ndogo, kama tu waaminifu, Mwokozi atatutumia sisi kutimiza kazi Yake. Kama tutafanya vyema tuwezavyo na kumtumainia Yeye kufidia upungufu, tunaweza kuwa sehemu ya miujiza ambayo inatuzunguka sisi.
Mzee Dale G. Renlund alisema: “Haupaswi kuwa mkamilifu, lakini tunakuhitaji wewe kwa sababu kila mtu aliye radhi anaweza kufanya kitu.”9
Na kama Rais Russell M. Nelson alivyofundisha: “Bwana anapenda juhudi.”10
Mwokozi anasimama tayari kukubali matoleo yetu madogo na kuyakamilisha kupitia neema Yake. Tukiwa na Kristo, hakuna mavuno hafifu. Ni sharti tuwe na ujasiri wa kuamini kwamba neema Yake ipo kwa ajili yetu—kwamba Yeye atatusaidia, kutuokoa kutoka kilindini pale tunapoyumba na kuzikamilisha juhudi zisizo kamili.
Katika mfano wa mpanzi, Mwokozi anaelezea mbegu ambazo zilipandwa kwenye udongo mzuri. Nyingine ilizaa mara mia, nyingine mara sitini na nyingine mara thelathini. Yote ni sehemu ya mavuno Yake kamili.11
Kama Moroni alivyotualika: “Mje kwa Kristo, na mkamilishwe ndani Yake, … na ikiwa mtajinyima ubaya wote, na kumpenda Mungu na mioyo yenu, akili na nguvu zenu zote, basi neema Yake inawatosha, kwamba kwa neema Yake mngekamilishwa kwa Kristo.”12
Akina kaka na akina dada, Mimi nashuhudia juu ya Kristo, ambaye ana nguvu za kukamilisha hata dhabihu yetu iliyo hafifu. Acha tufanye vyema kadiri tuwezavyo, kuleta kile tunachoweza, na, kwa imani, kuweka dhabihu yetu hafifu kwenye miguu Yake. Katika jina la Yeye ambaye ni Bwana wa mavuno kamili, hata Yesu Kristo, amina.