Nabii Aliye Hai kwa ajili ya Siku za Mwisho
Baba aliye Mbinguni amechagua mpangilio wa kufunua kweli kwa watoto Wake kupitia nabii.
Nilipokuwa mvulana mdogo, niliipenda Jumamosi kwa sababu kila kitu nilichofanya siku hiyo kilionekana kama tukio lisilo la kawaida. Lakini licha ya kila nilichofanya, daima kilitanguliwa na kitu muhimu zaidi ya vyote—kuangalia katuni kwenye runinga. Jumamosi moja asubuhi, nilipokuwa nimesimama mbele ya runinga nikibadilisha chaneli, niligundua kwamba katuni niliyotarajia kuipata nafasi yake ilikuwa imechukuliwa na matangazo ya mkutano mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Wakati nikitazama runinga na kulalamika kwamba hakukuwa na katuni, nilimwona mwanaume mwenye mvi aliyevalia suti na tai akiwa ameketi kwenye kiti cha kupendeza.
Kulikuwa na kitu tofauti kumhusu, hivyo nilimuuliza kaka yangu, “Huyu ni nani?”
Alisema, “Huyo ni Rais David O. McKay; ni nabii.”
Nakumbuka kuhisi kitu fulani na kwa namna fulani kujua kwamba alikuwa ni nabii. Wakati huo, kwa sababu nilikuwa mvulana mpenda katuni sana, nilibadili chaneli. Lakini kamwe sijasahau kile nilichohisi wakati ule mfupi, usiotarajiwa wa ufunuo. Tukiwa na nabii, wakati mwingine inachukua dakika tu kujua.1
Kujua kupitia ufunuo kwamba kuna nabii aliye hai duniani hubadili kila kitu.2 Kunamfanya mtu kutovutiwa na malumbano kuhusu wakati gani nabii anazungumza kama nabii au kama yoyote anahesabiwa haki kwa kuchagua kutofuata ushauri wa kinabii.3 Ufahamu kama huu uliofunuliwa humwalika mtu kutumainia ushauri wa nabii aliye hai, hata ikiwa hatuuelewi kikamilifu.4 Hata hivyo, Baba wa Mbinguni aliye mkamilifu na mwenye upendo amechagua mfumo wa kufunua ukweli kwa watoto Wake kupitia nabii, mtu ambaye kamwe hatafuti wito huo mtakatifu na ambaye hahitaji msaada wetu ili kujua mapungufu yake mwenyewe.5 Nabii ni mtu ambaye Mungu mwenyewe amemtayarisha, amemwita, amemsahihisha, amempa mwongozo wa kiungu, amemrudi, amemtakasa na kumthibitisha.6 Hiyo ndiyo sababu kamwe hatuwezi kuwa hatarini kwa kufuata ushauri wa kinabii.
Iwe tunapenda au la, sote tulichaguliwa katika njia fulani kwenye maisha ya mbinguni ili tuzaliwe katika siku hizi za mwisho. Kuna kweli mbili zinazohusiana na siku za mwisho. Ukweli wa kwanza ni kwamba Kanisa la Kristo litaanzishwa tena duniani. Ukweli wa pili ni kwamba mambo yatakuwa yenye changamoto sana. Maandiko yanaweka wazi kwamba katika siku za mwisho kutakuwa na “tufani kuu itakayoletwa ili kuangamiza mazao ya duniani,”7 magonjwa,8 “vita na minong’ono ya vita, na dunia yote itakuwa katika ghasia, … na uovu utaongezeka.”9
Nilipokuwa mtoto, unabii huo wa siku za mwisho ulinitisha na kunifanya niombe kwamba Ujio wa Pili usingetokea nikiwa hai—naweza kuongeza kwamba kwa kiasi nimefanikiwa. Lakini sasa ninaomba kinyume chake, ingawa changamoto zilizotabiriwa ni za uhakika,10 kwa sababu wakati Kristo atakaporejea kutawala, viumbe Wake wote “watakalishwa salama salimini.”11
Hali za sasa ulimwenguni zimesababisha baadhi wapate hofu kubwa. Kama watoto wa Mungu wa agano, hatupaswi kukimbilia hili ama lile ili tujue jinsi ya kukabiliana na nyakati hizi ngumu. Hatupaswi kuogopa.12 Mafundisho na kanuni tunazopaswa kufuata ili tunusurike kiroho na kustahimili kimwili vinapatikana katika maneno ya nabii aliye hai.13 Hiyo ndiyo sababu Rais M. Russell Ballard alitangaza kwamba “si jambo dogo … kuwa na nabii wa Mungu miongoni mwetu.”14
Rais Russell M. Nelson ameshuhudia kwamba “mpangilio wa kudumu wa Mungu wa kuwafundisha watoto Wake kupitia manabii unatuhakikishia kwamba Yeye atambariki kila nabii na kwamba atawabariki wale wanaosikiliza ushauri wa nabii.”15 Hivyo cha muhimu ni kumfuata nabii aliye hai.16 Akina kaka na akina dada, tofauti na vitabu vya ucheshi vya thamani na magari mazuri, mafundisho ya kinabii hayapandi thamani kulingana na umri. Hiyo ndiyo sababu hatupaswi kutafuta kutumia maneno ya manabii waliopita kupuuza mafundisho ya manabii walio hai.17
Ninapenda mifano aliyotumia Yesu Kristo kufundisha kanuni za injili. Ningependa kushiriki nanyi mfano hai wa aina hiyo asubuhi ya leo.
Siku moja niliingia mgahawani makao makuu ya Kanisa ili kupata chakula cha mchana. Baada ya kupata trei la chakula, niliingia kwenye sehemu ya kulia chakula na niliona meza ambapo washiriki wote watatu wa Urais wa Kwanza waliketi, sambamba na kiti kimoja kitupu. Kutokujiamini kwangu kulisababisha nipite mbali na meza ile, na kisha nilisikia sauti ya nabii, Rais Russell M. Nelson, akisema, “Allen, kuna kiti kitupu hapa. Njoo uketi nasi.” Hivyo nilienda.
Karibu na mwisho wa mlo, nilishangazwa kusikia kelele za kuponda ponda, na nilipotazama, niliona kwamba Rais Nelson alisimamisha chupa yake ya maji na kisha kuiminya na kuifunika.
Rais Dallin H. Oaks kisha aliuliza swali nililotaka kuuliza, “Rais Nelson, kwa nini umeminya chupa yako ya plastiki ya maji?”
Alijibu, “inawarahisishia wale wanaokusanya takarejea kwa sababu haichukui nafasi kubwa kwenye chombo cha kubebea.”
Wakati nikitafakari jibu lile, nilisikia tena sauti ya kuponda ponda. Nilitazama kulia kwangu, na Rais Oaks alikuwa ameminya chupa yake ya plastiki ya maji kama vile Rais Nelson. Kisha nikasikia kelele upande wa kushoto, na Rais Henry B. Eyring alikuwa akiminya chupa yake ya maji, japokuwa alitumia mbinu tofauti ya kufanya hilo chupa ikiwa katika mlalo, kitu ambacho kilichukua juhudi kubwa kuliko chupa ikiwa wima. Nikishuhudia hili, Rais Nelson kwa ukarimu alimwonesha mbinu ya chupa ikiwa wima ili kuiminya kwa urahisi.
Katika hatua hiyo, niliinama kidogo kwa Rais Oaks na kumuuliza, “Je, kuminya chupa zenu za maji ni kigezo kipya cha takarejea kwenye mgahawa huu?”
Rais Oaks alijibu, kwa tabasamu usoni mwake, “Unajua, Allen, unapaswa kumfuata nabii.”
Nina hakika kwamba Rais Nelson hakuwa akitangaza mafundisho mapya ya takarejea mgahawani siku hiyo. Lakini tunaweza kujifunza kutokana na mwitikio wa haraka18 wa Rais Oaks na Rais Eyring kwenye mfano wa Rais Nelson na umakini wa Rais Nelson kusaidia kuwafundisha njia bora zaidi wale waliohusika.19
Miaka kadhaa iliyopta, Mzee Neal A. Maxwell alishiriki baadhi ya uchunguzi na ushauri ambao kinabii uko kwenye hoja kulingana na siku yetu.
“Katika miezi na miaka ya mbeleni, matukio yanaweza kuhitaji kila muumini aamue ikiwa atawafuata Urais wa Kwanza ama la. Waumini watagundua kwamba ni vigumu sana kubakia zaidi kwenye mitizamo miwili. …
“… Ngoja tuache kumbukumbu ili kwamba chaguzi ziwe wazi, tukiwaruhusu wengine watende watakavyo pale ushauri wa kinabii unapotolewa. …
“Yesu alisema kwamba mitini ikianza kuchipuka, ‘wakati wa mavuno u karibu.’ … Hivyo alionya kwamba majira ya joto yapo juu yetu, basi tusilalamike kuhusu joto!”20
Kizazi kinachoinukia kinakua katika wakati ambapo kuna majani mengi ya mtini na joto jingi. Uhalisia huo unaweka jukumu zito zaidi kwenye kizazi kinachoinukia, hasa linapokuja suala la kufuata ushauri wa nabii. Wakati wazazi wanapopuuza ushauri wa nabii aliye hai, si tu wanapoteza baraka zilizoahidiwa bali kwa huzuni zaidi wanawafundisha watoto wao kwamba kile nabii anachosema hakina umuhimu au kwamba ushauri wa nabii unaweza kuchaguliwa kwenye orodha ya fasheni bila kujali matokeo ya lishe duni kiroho.
Mzee Richard L. Evans aliwahi kusema: “Baadhi ya wazazi kimakosa wanahisi wanaweza kupumzika kidogo kwenye kuongoza na kutii viwango … kwamba wanaweza kutokuwa makini kidogo kwenye misingi bila kuathiri familia zao au wakati ujao wa familia zao. Lakini ikiwa mzazi anaenda nje kidogo ya njia, watoto wana uwezekano wa kwenda nje zaidi ya mzazi.”21
Kama kizazi ambacho kina jukumu takatifu la kukiandaa kizazi kinachoinukia kwa jukumu lake lililotabiriwa katika siku za mwisho,22 jukumu ambalo lazima litimizwe katika wakati ambao ushawishi wa adui uko kwenye kilele,23 hatuwezi kuwa chanzo cha mkanganyiko kuhusu umuhimu wa kufuata ushauri wa kinabii. Ni ushauri huo hasa utakaokiruhusu kizazi kinachoinukia wamwone “adui wakati angali bado yuko mbali; na ndipo [wao] wangejitayarisha” kukabiliana na mashambulizi ya adui.24 Kile kinachoonekana ukengeufu kidogo, kupuuza kimya kimya au ukosoaji wa kunong’ona kuhusiana na ushauri wa kinabii kinaweza tu kutuongoza kwenye kutembea hatarini pembezoni mwa njia ya agano; lakini kinapokuzwa na adui katika maisha ya kizazi kinachoinukia, matendo kama hayo yanaweza kuwashawishi waache njia kabisa. Matokeo kama hayo ni gharama kubwa sana.25
Baadhi yenu mnaweza kuhisi mmepunguka katika juhudi zenu za kufuata ushauri wa Rais Russell M. Nelson. Kama hivyo ndivyo, basi tubu, anza tena kufuata ushauri wa nabii wa Mungu aliyechaguliwa. Weka kando vivuta mawazo vya katuni za utoto na mtumaini mpakwa mafuta wa Bwana. Shangilia kwa sababu kwa mara nyingine tena “yupo Nabii katika Israeli.”26
Hata kama huna uhakika, ninatoa ushahidi kwamba tunaweza kustahimili joto la siku za mwisho na hata kuneemeka ndani yake. Sisi ni Watakatifu wa siku za mwisho, na hizi ni siku kuu. Tulikuwa na shauku ya kuja duniani kwa wakati huu, tukiwa na ujasiri kwamba hatutaachwa tuanguke pale tunapokabiliwa na ukungu wa giza na mkanganyiko mwingi unaoongezeka wa adui27 lakini badala yake kufuata ushauri na maelekezo kutoka kwake ambaye ameidhinishwa kutuambia sisi na ulimwengu mzima, “Bwana Mungu asema hivi.”28 Katika jina takatifu la nabii ambaye Mungu alimwinua, Mtakatifu wa Israeli,29 hata Yesu Kristo, amina.