Mkutano Mkuu
Bwana Yesu Kristo Anatufundisha Kuhudumu
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


11:29

Bwana Yesu Kristo Anatufundisha Kuhudumu

Kwa msaada wa Mwokozi wetu, tunaweza kuwapenda kondoo Wake wa thamani na kuwatumikia kama ambavyo Yeye angefanya.

Bwana Yesu Kristo alisema:

“Mimi ndimi mchungaji mwema: mchungaji mwema hutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. …

Kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.”1

Katika toleo la Kigiriki la andiko hili, neno mwema pia humaanisha “nzuri, tukufu.” Hivyo leo, napenda kuzungumzia kuhusu Mchungaji Mwema, Mchungaji Mzuri, Mchungaji Aliyetukuka, hata Yesu Kristo.

Katika Agano Jipya, anaitwa “mchungaji mkuu,”2 Mchungaji kiongozi,”3 na “Mchungaji na Mwangalizi wa roho [zetu].4

Katika Agano la Kale, Isaya aliandika kwamba“ Atalilisha kundi lake kama mchungaji.”5

Katika Kitabu cha Mormoni, anaitwa “mchungaji mwema”6 na “mchungaji mkuu na wa kweli.”7

Katika Mafundisho na Maagano, Alitamka, “Kwa hivyo, Mimi nipo katikati yenu, na mimi ni mchungaji mwema.”8

Katika siku yetu, Rais Russell M. Nelson ametamka: “Mchungaji Mwema kwa upendo huwajali kondoo wote wa zizi Lake, na sisi ndio wasimamizi Wake wa kweli. Jukumu letu ni kushuhudia upendo Wake na kuongezea upendo wetu wenyewe kwa marafiki na majirani—kuwalisha, kuwachunga na kuwatunza—kama ambavyo Mwokozi angetutaka tufanye.”9

Hivi karibuni, Rais Nelson amesema: “Sifa bainifu ya Kanisa la kweli na lililo hai la Bwana siku zote litakuwa lenye utaratibu, lenye juhudi zilizoelekezwa kuwahudumia watoto binafsi wa Mungu na familia zao. Kwa sababu ni Kanisa lake, sisi kama watumishi Wake tutamtumikia yule mmoja, kama Yeye alivyofanya. Tutamhudumia katika jina Lake, kwa nguvu na mamlaka Yake, na kwa ukarimu wa upendo Wake.”10

Wakati Mafarisayo na waandishi waliponung’unika dhidi ya Bwana, “wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao,”11 Alijibu kwa kutoa hadithi tatu nzuri ambazo tumekuja kuzijua kama mfano wa kondoo aliyepotea, mfano wa sarafu iliyopotea na mfano wa mwana mpotevu.

Ni vyema kutambua kwamba wakati Luka, mwandishi wa Injili, alipotambulisha hadithi tatu, alitumia neno mfano katika umoja na si wingi.12 Inaonekana kwamba Bwana anafundisha somo moja muhimu kwa hadithi tatu, hadithi ambazo hutoa namba tofauti, kondoo 100, sarafu 10, na wana 2.

Hata hivyo, namba ya muhimu katika kila moja ya hadithi hizi, hata hivyo, ni namba moja. Na somo tunaloweza kupata kutoka kwenye namba hiyo ni kwamba unaweza kuwa mtumishi wa wazee 100 na wazee watarajiwa katika akidi yako ya wazee, au mshauri kwa wasichana 10, au mwalimu kwa watoto 2 wa Msingi, lakini daima, daima utawahudumia, kuwajali na kuwapenda mmoja mmoja, binafsi. Kamwe husemi, “Kondoo mpumbavu huyu,” au “Hata hivyo, sihitaji sarafu hiyo,” au “Mwana muasi huyu.” Kama wewe na mimi tukiwa na “upendo msafi wa Kristo,”13 sisi, kama mtu katika hadithi ya kondoo aliyepotea “tutawaacha wale tisini na kenda … kwenda kumtafuta yule aliyepotea, hadi, [… hadi, … hadi sisi] tumpate.”14 Au kama mwanamke katika hadithi ya sarafu iliyopotea, “Tutawasha taa, tuifagie nyumba na kuitafuta kwa bidii [… bidii] mpaka [… mpaka, … mpaka sisi] tuipate.”15 Kama tunao “upendo msafi wa Kristo,” tutafuata mfano wa baba katika hadithi ya mwana mpotevu, ambaye wakati mwana “alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu.”16

Tunaweza kuhisi utayari wa moyo wa mtu aliyepoteza kondoo mmoja tu? Au utayari wa moyo wa mwanamke aliyepoteza sarafu moja? Au upendo mkuu na huruma katika moyo wa baba wa mwana mpotevu?

Mimi pamoja na mke wangu, Maria Isabel tulihudumu huko Amerika ya Kati, kituo chetu kikiwa Jiji la Guatemala. Huko nilipata fursa ya kukutana na Julia, muumini mwaminifu wa Kanisa. Nilipata msukumo wa kumuuliza kuhusu familia yake. Mama yake alikufa kwa saratani mnamo 2011. Baba yake alikuwa kiongozi mwaminifu katika kigingi chake, akihudumu kama askofu na kama mshauri wa rais wake wa kigingi kwa miaka kadhaa. Alikuwa mchungaji wa kweli wa Bwana. Julia alinisimulia kuhusu jitihada zake za dhati za kutembelea, kutumikia na kuhudumu. Hakika alishangilia katika kulisha na kuchunga kondoo wa thamani wa Bwana. Alioa tena na kubakia muumini hai ndani ya Kanisa.

Miaka michache baadaye, alipitia talaka na sasa ilibidi ahudhurie kanisani peke yake tena. Alihisi hakuwa sehemu ya kanisa na pia alihisi kwamba baadhi ya watu walimkosoa kwa sababu ya talaka yake. Aliacha kuhudhuria kanisani kadiri roho hasi alivyoujaza moyo wake.

Julia alimpongeza sana mchungaji wake mwema, ambaye alikuwa mwanamume mchapa kazi, mwenye upendo na mwenye huruma. Kwa dhahiri nakumbuka kwamba hisia ya utayari ilinijia alipokuwa akimwelezea. Nilihitaji kufanya kitu kwa ajili ya mtu huyo, mwanamume ambaye amefanya mengi kwa wengi kwa miaka yote hiyo.

Alinipa namba yake ya simu na nikampigia, nikitumaini kupata nafasi ya kukutana naye binafsi. Baada ya wiki kadhaa na simu nyingi, nyingi bila mafanikio, siku moja hatimaye alijibu simu yangu.

Nilimwambia kwamba nilikutana na Julia, binti yake, na kwamba nilivutiwa na jinsi yeye alivyohudumu, alivyotumikia na kuwapenda kondoo wa thamani wa Bwana kwa miaka mingi. Hakutarajia maneno kama hayo. Nilimwambia kwamba nilihitaji kukutana naye jicho kwa jicho, uso kwa uso. Aliniuliza lengo langu la kupendekeza kukutana huko. Nilijibu, “kwa dhati nahitaji kukutana na baba wa binti huyo mwema.” Kisha kwa sekunde chache kulikuwa na ukimya kwenye simu—sekunde chache ambazo kwangu ilikuwa kama milele. Akasema, “Lini na wapi?”

Siku niliyokutana naye, nilimwalika kushiriki pamoja nami baadhi ya uzoefu wa kutembelea, kutumikia na kuhudumia kondoo wa thamani wa Bwana. Alipokuwa akinisimulia baadhi ya hadithi zenye kugusa, niligundua kwamba mawimbi ya sauti yake yalibadilika na roho yule aliyemhisi mara nyingi kama mchungaji alirejea tena. Sasa macho yake yalikuwa yamejawa na machozi. Nilijua kwamba huu ulikuwa wakati sahihi kwangu, lakini niligundua kwamba sikujua la kusema. Nilisali akilini mwangu, “Baba, nisaidie.”

Ghafla, nilijisikia nikisema, “Kaka Florian, kama mtumishi wa Bwana ninaomba radhi kwa kutokuwepo kwetu kwa ajili yako. Tafadhali, tusamehe. Tupatie nafasi nyingine ya kukuonyesha kwamba tunakupenda. Kwamba tunakuhitaji. Kwamba wewe ni wa muhimu kwetu.

Jumapili iliyofuata alirejea kanisani. Alikuwa na mazungumzo marefu na askofu wake na kubakia hai kanisani. Miezi michache baadae alifariki—lakini alikuwa amerejea. Alikuwa amerejea. Ninashuhudia kwamba kwa msaada wa Mwokozi wetu, tunaweza kuwapenda kondoo Wake wa thamani na kuwatumikia kama ambavyo Yeye angefanya. Na kwa hiyo, kwamba wao katika Jiji la Guatemala Bwana Yesu Kristo alimrudisha tena kondoo mzuri kwenye kundi Lake. Na Alinifundisha mimi somo la kutumikia ambalo siwezi kusahau. Katika jina la Mchungaji Mwema, Mchungaji Mzuri, Mchungaji Aliyetukuka, hata Bwana Yesu Kristo, amina.