Kufikia Nguvu za Mungu kupitia Maagano
Unapotembea njia ya agano, kuanzia ubatizo hadi hekaluni na maisha yako yote, ninakuahidi nguvu ya kwenda dhidi ya mtiririko wa asili wa kiulimwengu.
Novemba iliyopita, nilipata fursa ya kuweka wakfu Hekalu la Belém Brazil. Ilikuwa shangwe kuwa pamoja na waumini wa Kanisa waliojitolea katika Brazil ya kaskazini. Wakati huo, nilijifunza kwamba mji wa Belém ni lango la mkoa ambao hujumuisha mto mkuu ulimwenguni, Mto Amazon.
Licha ya nguvu ya mto, mara mbili kwa mwaka, jambo linaloonekana lisilo la asili hutokea. Wakati jua, mwezi na dunia vinapokuwa katika mpangilio fulani, mawimbi ya maji yenye nguvu hutiririka juu ya mto, dhidi ya mtiririko asilia wa maji. Mawimbi ya urefu wa mita 61 yakisafiri takribani umbali wa kilometa 502 dhidi ya mkondo yamethibitishwa. Tukio hili, kwa ujumla likijulikana kama mawimbi makubwa, hujulikana kwa lugha ya eneo kama pororoca, au “mrindimo mkubwa” kwa sababu ya kelele nyingi yanayosababisha. Tunaweza kwa usahihi kuhitimisha kwamba hata Amazon kuu lazima isalimu amri ya nguvu za mbinguni.
Kama vile Amazon, tunao mtiririko asilia kwenye maisha yetu; tunapenda kufanya kile kinachokuja kiasili. Kama vile Amazon, kwa msaada wa mbinguni, tunaweza kufanya mambo yanayoonekana yasiyo ya kiasili. Hata hivyo, si asili kwetu kuwa wanyenyekevu, wapole au radhi kuweka mapenzi yetu chini ya yale ya Mungu. Lakini ni kwa kufanya hivyo pekee tunaweza kubadilishwa, kurudi kuishi katika uwepo wa Mungu na kufikia hatma yetu ya milele.
Tofauti na Amazon, tunaweza kuchagua ikiwa tunachagua kuwa chini ya nguvu za mbingu au “tunaendelea na uasilia.”3 Kwenda kinyume na uasilia inaweza kuwa vigumu. Lakini tunapojiweka chini ya “ushawishi wa Roho Mtakatifu” na kuweka kando tabia za ubinafsi za mwanaume au mwanamke wa tabia ya asili,4 tunaweza kupokea nguvu ya kubadilisha ya Mwokozi katika maisha yetu, nguvu ya kufanya mambo magumu.
Rais Russell M. Nelson alitufundisha jinsi ya kufanya hili. Aliahidi, “Kila mtu anayefanya maagano kwenye sehemu za ubatizo na ndani ya mahekalu—na kuyashika—ana ongezeko la kufikia nguvu ya Yesu Kristo … [ya kutuinua] juu dhidi ya nguvu ivutayo ya ulimwengu huu ulioanguka.”5 Kwa maneno mengine, tunaweza kufikia nguvu za Mungu, lakini ni pale tu tunapounganika Naye kupitia maagano matakatifu.
Kabla ya dunia kuumbwa, Mungu alianzisha maagano kama utaratibu ambao kupitia huo sisi, watoto Wake, tungeweza kujiunganisha Kwake. Kulingana na sheria ya milele, isiyobadilika, Yeye amebainisha hali zisizobadilika ambapo tunabadilishwa, kuokolewa na kuinuliwa. Katika maisha haya, tunafanya maagano haya kwa kushiriki kwenye ibada za ukuhani na kuahidi kufanya kile Mungu anachotutaka tufanye, na kama malipo, Mungu anatuahidi baraka fulani.6
Agano ni ahadi ambayo tunapaswa kujiandaa kwayo, kuielewa dhahiri na kuiheshimu kikamilifu.7 Kufanya agano na Mungu ni tofauti na kufanya ahadi ya kawaida. Kwanza, mamlaka ya ukuhani yanahitajika. Pili, ahadi dhaifu haina nguvu ya kuunganisha ya kutuinua juu dhidi ya nguvu ya uvutano wa mtiririko wa asili. Tunafanya agano wakati tunapokusudia kujitoa kwa upekee kulitimiza.8 Tunakuwa watoto wa Mungu wa agano na warithi wa ufalme Wake, pale hasa tunapojitambulisha kikamilifu kwa agano.
Neno njia ya agano humaanisha mtiririko wa maagano ambayo kupitia kwayo tunakuja kwa Kristo na kuunganika Naye. Kupitia muunganiko huu wa agano, tunaweza kufikia nguvu Zake za milele. Njia huanza na imani katika Yesu Kristo na toba, ikifuatiwa na ubatizo na kupokea Roho Mtakatifu.9 Yesu Kristo alituonesha jinsi ya kuingia kwenye njia hii wakati alipobatizwa.10 Kulingana na maelezo ya Injili ya Agano Jipya katika Marko na Luka, Baba wa Mbinguni alizungumza moja kwa moja na Yesu kwenye ubatizo Wake, akisema, “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; ninayependezwa naye.” Tunapojiingiza kwenye njia ya agano kupitia ubatizo, ninaweza kupata taswira ya Baba wa Mbinguni akisema jambo sawa na hilo kwa kila mmoja wetu: “Wewe ndiwe Mwanangu mpendwa ninayependezwa naye. Endelea mbele.”11
Kwenye ubatizo na wakati tunapopokea sakramenti,12 tunaahidi kwamba tuko radhi kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo.13 Katika muktadha huu, acha tukumbuke amri ya Agano la Kale, “Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako.”14 Kwenye masikio yetu ya siku za leo, hii inasikika kama zuio dhidi ya kutumia jina la Bwana isivyofaa. Amri inajumuisha hilo, lakini zuio lake ni kubwa zaidi. Neno la Kiebrania lililotafsiriwa kama “taja” humaanisha “kuinua” au “kubeba,” jinsi ambavyo mtu angebeba bendera inayomtambulisha mbebaji pamoja na mtu mwingine au kundi.15 Neno lililotafsiriwa kama “bure” humaanisha “tupu” au “uongo.”16 Amri ya kutolitaja bure jina la Bwana inaweza basi kumaanisha, “usijitambulishe kama mfuasi wa Yesu Kristo isipokuwa unakusudia kumwakilisha Yeye ipasavyo.”
Tunakuwa wafuasi Wake na kumwakilisha Yeye vyema wakati kwa makusudi na kwa hatua tunapojichukulia jina la Yesu Kristo kupitia maagano. Maagano yetu hutupatia nguvu ya kubaki kwenye njia ya agano kwa sababu uhusiano wetu na Yesu Kristo na Baba wa Mbinguni umebadilika. Tumeunganika Kwao kupitia kifungo cha agano.
Njia ya agano huongoza kwenye ibada za hekaluni, kama vile endaumenti ya hekaluni.17 Endaumenti ni zawadi ya Mungu ya maagano matakatifu ambayo hutuunganisha kikamilifu Kwake. Katika endaumenti, tunafanya agano, kwanza, kujitahidi kutii amri za Mungu; pili kutubu kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka; tatu, kuishi injili ya Yesu Kristo. Tunafanya hili kwa kuonesha imani Kwake, kufanya maagano na Mungu wakati tunapopokea ibada za wokovu na kuinuliwa, kutii maagano hayo katika maisha yetu yote na kujitahidi kuishi amri kuu mbili ya kumpenda Mungu na jirani. Tunaweka agano, nne, kutii sheria ya usafi wa kimwili na, tano, kujitoa sisi wenyewe na kila kitu Bwana anachotubariki nacho kulijenga Kanisa Lake.18
Kwa kufanya na kutii maagano ya hekaluni, tunajifunza zaidi juu ya malengo ya Bwana na kupokea utimilifu wa Roho Mtakatifu.19 Tunapokea mwongozo kwa ajili ya maisha yetu. Tunakomaa katika ufuasi wetu ili kwamba tusibakie daima kuwa watoto wasio na ufahamu.20 Badala yake, tunaishi kwa mtazamo wa milele na tuna motisha zaidi ya kumtumikia Mungu na wengine. Tunapokea ongezeko la uwezo wa kutimiza malengo yetu katika maisha ya duniani. Tunalindwa dhidi ya uovu,21 na tunapata nguvu kubwa ya kushinda majaribu na kutubu pale tunapojikwaa.22 Tunapoyumba, kumbukumbu ya maagano yetu kwa Mungu hutusaidia turudi kwenye njia. Kwa kujiunganisha na nguvu za Mungu, tunakuwa pororoca, yetu wenyewe, tukiweza kwenda kinyume na mtiririko wa ulimwengu, maisha yetu yote na kwenye umilele. Hatimaye, hatma zetu zinabadilishwa kwa sababu njia ya agano huongoza kwenye kuinuliwa na uzima wa milele.23
Kutii maagano yaliyofanywa kwenye sehemu za ubatizo na ndani ya mahekalu pia hutupatia nguvu ya kushinda majaribu na maumivu ya maisha ya duniani.24 Mafundisho yanayohusiana na maagano haya hurahisisha njia yetu na hutoa tumaini, faraja na amani.
Bibi na babu yangu Lena Sofia na Matts Leander Renlund walipokea nguvu za Mungu kupitia maagano yao ya ubatizo walipojiunga na Kanisa mnamo 1912 nchini Ufini. Walikuwa na furaha kuwa sehemu ya tawi la kwanza la Kanisa nchini Ufini.
Leander alikufa kutokana na kifua kikuu miaka mitano baadaye wakati Lena alipokuwa mjamzito wa mtoto wao wa kumi. Mtoto huyo, baba yangu, alizaliwa miezi miwili baada ya kifo cha Leander. Lena hatimaye alimzika si tu mumewe bali pia watoto wake saba kati ya kumi. Kama mjane maskini, alipambana. Kwa miaka 20, hakupata mapumziko mazuri ya usiku. Wakati wa mchana, alitaabika kupata chakula kwa ajili ya familia yake. Usiku, aliwapa uangalizi wanafamilia waliokuwa mahututi. Ni vigumu kufikiria jinsi alivyoweza.
Lena alistahimili kwa sababu alijua kwamba mumewe na watoto waliofariki wangeweza kuwa wake milele yote. Mafundisho ya baraka za hekaluni, ikijumuisha yale ya familia za milele, yalimletea amani kwa sababu alitumaini katika nguvu ya kuunganishwa. Akiwa katika maisha ya duniani, hakupokea endaumenti yake wala kuunganishwa kwa Leander, lakini Leander alibaki kuwa ushawishi mkubwa katika maisha yake na sehemu ya tumaini lake kuu kwa ajili ya wakati ujao.
Mnamo 1938, Lena aliwasilisha kumbukumbu ili kwamba ibada za hekaluni zifanywe kwa niaba ya wanafamilia wake, baadhi ya mawasilisho ya mwanzo kabisa kutoka Ufini. Baada ya kufariki, ibada za hekaluni zilifanywa na wengine kwa niaba yake, Leander na watoto wake waliofariki. Kwa niaba, alipokea endaumenti, Lena na Leander waliunganishwa na watoto wao waliofariki waliunganishwa kwao. Kama vile wengine, Lena “alikufa katika imani, bila kupokea zile ahadi, bali akiziona tokea mbali, … [na] kuzishangilia … na kukiri.”25
Lena aliishi kama vile alikuwa tayari amefanya maagano haya katika maisha yake. Alijua kwamba maagano yake ya ubatizo na sakramenti yalimuunganisha kwa Mwokozi. Aliruhusu “ile shauku ya kuja mahali patakatifu pa [Mwokozi] ilete tumaini kwenye moyo [wake] wenye majonzi.”26 Lena aliichukulia kama moja ya rehema kuu za Mungu kwamba alijifunza kuhusu familia za milele kabla ya kupitia huzuni katika maisha yake. Kupitia agano, alipokea nguvu za Mungu za kuvumilia na kuinuka juu ya mvuto wa msongo wa changamoto na magumu yake.
Unapotembea njia ya agano, kuanzia ubatizo hadi hekaluni na maisha yako yote, ninakuahidi nguvu ya kwenda dhidi ya mtiririko wa asili wa kiulimwengu—nguvu ya kujifunza, nguvu ya kutubu na kutakaswa na nguvu ya kupata tumaini, faraja na hata shangwe wakati unapopitia changamoto za maisha. Ninakuahidi wewe na familia yako ulinzi dhidi ya ushawishi wa adui, hususani wakati hekalu ni fokasi kubwa katika maisha yako.
Unapokuja kwa Kristo na umeunganishwa Kwake na kwa Baba yetu wa Mbinguni kwa agano, jambo linaloonekana lisilo la asili hutokea. Unabadilishwa na kuwa aliyekamilishwa katika Yesu Kristo.27 Unakuwa mtoto wa agano wa Mungu na mrithi katika ufalme Wake.28 Naweza kupata taswira Yake akikuambia, “Wewe ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye. Karibu nyumbani.” Katika Jina la Yesu Kristo, amina.