Mkutano Mkuu
Kutumainia Mafundisho ya Kristo
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Kutumainia Mafundisho ya Kristo

Tunapokuwa tumejenga nyumba zetu juu ya mwamba wa uhusiano wa kimaagano pamoja na Kristo, tunatumainia mafundisho ya Kristo.

Katika jicho la akili yangu, namuona nabii mzee Nefi kwenye dawati lake, mabamba ya dhahabu yametandazwa mbele yake, kalamu yake mkononi.

Nefi alikuwa kwenye mchakato wa kukamilisha mwisho wa uchongaji maandishi kwenye kumbukumbu. Aliandika, “Na sasa, ndugu zangu wapendwa, namalizia maneno yangu hapo.”1 Lakini punde baadaye, Roho alimshawishi Nefi arejee kwenye kumbukumbu yake na kuandika ujumbe wa kuhitimisha. Kwa ushawishi mkuu wa Roho Mtakatifu, nabii huyo mkuu alichukua kalamu yake tena mkononi na kuandika, “Kwa hivyo, vitu ambavyo nimeandika vimenitosha, ila tu maneno machache … lazima niyazungumze kuhusu mafundisho ya Kristo.”2

Tuna shukrani milele kwa hayo “maneno machache”3 na kwa Roho kumshawishi Nefi kuyaandika. Andiko la Nefi kwenye mafundisho ya Kristo ni hazina kwa wale wanaosherehekea kwayo. Linajumuisha ono la ubatizo wa Mwokozi4 na sauti ya Mwana, akiwaalika wote kumfuata Yeye5 na “kufanya vitu ambavyo [sisi] tumemwona [Yeye] akifanya.”6 Linajumuisha ushahidi wa Nefi kwamba wale ambao, kwa imani katika Kristo, kwa dhati hutubu dhambi zao na kumfuata Mwokozi kwenye maji ya ubatizo “watapokea Roho Mtakatifu; ndiyo, kisha huja ubatizo wa moto na Roho Mtakatifu.”7 Pia tunasikia sauti ya Baba ikishuhudia: “Ndiyo, maneno ya Mpendwa wangu ni ya kweli na maaminifu. Yule atakayevumilia hadi mwisho, huyo ataokolewa.”8

Rais Russell M. Nelson alisisitiza umuhimu pekee wa mafundisho ya Kristo wakati wa mazungumzo kwa viongozi wapya wa misheni walioitwa: “Zaidi ya kitu chochote, tunataka wamisionari wetu … kuwa na mafundisho ya Kristo yakiwa yamechongwa katika mioyo yao—yakiwa na mizizi … katika uroto wa mifupa yao.”9

Hubiri Injili Yangu hutoa kwa ufupi vitu vitano vya mafundisho ya Kristo. Inasema, “[Sisi] tunawaalika wengine kuja kwa Kristo kwa kuwasaidia wapokee injili ya urejesho kupitia imani katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake, toba, ubatizo, kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu na kuvumilia hadi mwisho.”10

Lakini umuhimu wa mafundisho ya Kristo siyo tu kwa ajili ya wamisionari. Ni wa kina zaidi kuliko marudio ya ufupisho wa vitu vitano muhimu. Hujumuisha sheria ya injili. Ni mpango mkuu kwa ajili ya uzima wa milele.

Akina kaka na akina dada, kama tutakubali mwaliko wa Rais Nelson wa kuwa na mafundisho ya Kristo yawe na mizizi katika uroto wa mifupa yetu, tunapaswa kukuza uongofu wetu kwa Bwana kwa kusoma, sala, kuishi kwa uaminifu na toba endelevu. Tunapaswa kumwalika Roho Mtakatifu kuchonga mafundisho ya Kristo katika “vibao vya nyama vya mioyo [yetu]”11 kwa kina na kwa kudumu kama yalivyochogwa na Nefi kwenye mabamba ya dhahabu.

Oktoba iliyopita, Rais Nelson aliuliza, “Inamaanisha nini kuushinda ulimwengu?” Miongoni mwa vitu vingine, alisema, “Inamaanisha kutumainia mafundisho ya Kristo zaidi kuliko falsafa za wanadamu.”12

Neno tumainia limefafanuliwa kama “utegemezi thabiti kwenye tabia, uwezo, nguvu, au ukweli wa mtu au kitu.”13 Mtu huyo ni Yesu Kristo, na kitu hicho ni mafundisho Yake.

Kwa hiyo, ni kwa jinsi gani tungeweza kwa makusudi kutumainia mafundisho ya Kristo kubadili jinsi tunavyoishi maisha yetu?

Kama tunatumainia mafundisho ya Kristo, tutamwamini Kristo vya kutosha kwa kuishi kwa kila neno Lake.14 Tutajifunza kuhusu Yesu Kristo maisha yetu yote,15 huduma Yake, mafundisho Yake na Upatanisho Wake usio na mwisho, ikijumuisha Ufufuko Wake mtakatifu. Tutajifunza ahadi Zake na vigezo ambavyo kwavyo ahadi Zake hutolewa.16 Tunapojifunza, tutajazwa na upendo mkuu kwa Bwana.

Kama tunatumainia mafundisho ya Kristo, tutamsihi Baba yetu wa Mbinguni kila siku katika ombi la unyenyekevu na la siri, ambapo tunaweza kutoa shukrani zetu kwa zawadi ya Mwana Wake na kwa baraka zetu zote.17 Tunaweza kuomba kwa wenza wa ufunuo wa Roho Mtakatifu,18 kuomba kuweka matakwa yetu yaendane na Yake,19 kuomba ili kutafakari kuhusu maagano yetu na kufanya upya nia zetu za kuyatunza.20 Tunaweza kuomba ili kuwakubali na kuonyesha upendo kwa manabii wetu, waonaji na wafunuzi;21 kuomba kwa ajili ya nguvu ya utakaso ya toba;22 na kuomba kwa ajili ya nguvu za kustahimili majaribu.23 Ninawaalikeni kufanya maombi kuwe kipaumbele katika maisha yenu, mkitafuta kila siku kuboresha mawasiliano yenu na Mungu.

Kama tunatumainia mafundisho ya Kristo, tutaachana na vitu ving’aavyo vya ulimwengu ili kwamba tufokasi kwa Mkombozi wa ulimwengu.24 Tutazuia au kuondoa muda tunaotumia kwenye mitandao ya kijamii, michezo ya kidijitali, burudani chafu, zilizopitiliza au zisizofaa; hila ya hazina ya ulimwengu huu na kiburi; na shughuli zozote zile ambazo huruhusu desturi za uongo na falsafa hasi za wanadamu. Ni katika Kristo pekee tunapata ukweli na utimilifu usio na mwisho.

Toba ya dhati25 itakuwa sehemu ya shangwe26 ya maisha yetu—ili tusamehewe dhambi na tubadilishwe katika taswira ya Kristo.27 Toba kwa imani katika Kristo hutupatia uwezo wa kufikia Upatanisho wa Kristo. Rais Dallin H. Oaks amefundisha kwamba wakati Mwokozi husamehe, Yeye “hufanya zaidi ya kututakasa kutoka dhambini. Pia hutupatia [sisi] nguvu mpya.”28 Kila mmoja wetu anahitaji nguvu hii ili kutii amri za Mungu na kutimiza lengo la milele la maisha yetu.

Katika Yesu na mafundisho Yake, tunapata nguvu. Yeye alisema, “Amin, amin, nawaambia, kwamba haya ni mafundisho yangu, na yeyote atakayejenga juu yake hujenga juu ya mwamba wangu, na milango ya jehanamu haitamshinda.”29

Tunaona ahadi hii ikitimizwa katika maisha ya watu waaminifu. Ni kama mwaka mmoja hivi uliopita, nilikutana na Travis na Kacie. Walikuwa wameoana kiserikali mnamo 2007. Kwa kipindi hicho, Travis hakuwa muumini wa Kanisa. Kacie, ingawa alikuwa amekuzwa kwenye nyumba ya Mtakatifu wa Siku za Mwisho anayeshiriki kikamilifu, alichepuka kutoka imani yake enzi za ujana wake na kupotea kutoka msingi wake.

Mnamo 2018, Travis alikutana na wamisionari, na kubatizwa mnamo 2019. Travis alikuwa mmisionari kwa Kacie, ambaye pia alipitia uongofu wa kubadili maisha. Waliunganishwa hekaluni mnamo Septemba, 2020. Takribani miaka miwili baada ya ubatizo wake, Travis aliitwa kutumikia katika uaskofu.

Travis ana ugonjwa adimu ambao mara kwa mara huunda mkusanyiko wa uvimbe katika ogani zake za ndani. Amefanyiwa upasuaji mwingi ili kuondoa uvimbe unaojirudia, lakini ugonjwa hautibiki. Miaka kadhaa iliyopita, Travis alipewa miaka chini ya 10 ya kuishi.

Kacie anaugua ugonjwa wa retina, ugonjwa adimu wa kurithi ambao husababisha kufifia kwa uoni mpaka kupelekea upofu.

Kacie alizungumza nami kuhusu siku zake za usoni. Alitazamia wakati, siyo mbali sana, ambapo atakuwa mjane, kipofu, bila msaada wa kifedha na akiwa peke yake katika kulea watoto wanne. Nilimuuliza Kacie jinsi atakavyoshughulikia siku za usoni zenye kiza. Alitabasamu kwa amani na kusema, “Sijapata kuwa mwenye furaha sana au mwenye tumaini katika maisha yangu kama sasa. Tumeshikilia ahadi tulizopokea hekaluni.”

Travis sasa ni askofu. Miezi miwili iliyopita alifanyiwa upasuaji mwingine mkubwa. Lakini ni mwenye tumaini na amani. Uoni wa Kacie umedhoofu. Sasa ana mbwa wa kumwongoza na hawezi kuendesha gari. Lakini ameridhika, akiwalea watoto wake na kutumikia kama mshauri katika urais wa Wasichana.

Travis na Kacie wanajenga nyumba yao juu ya mwamba. Travis na Kacie wanatumainia mafundisho ya Kristo na ahadi kwamba Mungu “atayatakasa mateso [yao] kwa faida [yao].”30 Katika mpango mkamilifu wa Mungu, mateso kwa imani katika Kristo huendana na kuwa mkamilifu katika Kristo.31 Kama vile mtu mwenye busara katika mfano ambaye alijenga nyumba yake juu ya mwamba,32 mvua iliponyesha, na mafuriko yakaja, na pepo zikavuma, na zikapiga ile nyumba ambayo Travis na Kacie wanaijenga, haikuanguka, kwani itajengwa juu ya mwamba.33

Yesu hakuzungumzia uwezekano wa mvua na mafuriko na pepo katika maisha yetu; Alizungumzia uhakika kwamba tufani zitakuja. Utofauti katika mfano huu siyo ikiwa labda tufani zitakuja au la, bali jinsi tunavyojibu mwaliko Wake wa upendo wa kusikia na kufanya kile alichofundisha.34 Hakuna njia nyingine ya kunusurika.

Tunapokuwa tumejenga nyumba zetu juu ya mwamba wa uhusiano wa kimaagano pamoja na Kristo, tunatumainia mafundisho ya Kristo, na tunaposonga Kwake, tunayo ahadi Yake ya uzima wa milele. Watu ambao hutumainia mafundisho ya Kristo husonga mbele wakiwa imara katika Kristo na kuvumilia mpaka mwisho. Hakuna njia nyingine ya kuokolewa katika ufalme wa Mungu.35

Ninatoa ushahidi wangu binafsi wa uhalisia wa maisha na ufufuko wa Yesu Kristo. Ninashuhudia kwamba Mungu Baba Yetu aliupenda ulimwengu hata akamtuma Mwana Wake atukomboe kutoka dhambini36 na kutuponya kutoka huzuni.37 Ninashuhudia kwamba amemwita nabii wa Mungu katika wakati wetu, hata Rais Russell M. Nelson, ambaye kupitia yeye huzungumza na kutuongoza.

Kwa moyo wangu wote, ninawaalikeni kutumainia mafundisho ya Kristo na kujenga maisha yenu juu ya mwamba wa Mkombozi. Kamwe Yeye hatakuangusha. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha