Mkutano Mkuu
Endelea Kusonga—kwa Imani
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Endelea Kusonga—kwa Imani

Kuonesha imani katika Mwokozi wetu, Yesu Kristo, hutusaidia tushinde kukatishwa tamaa bila kujali ni vikwazo gani tunakutana navyo.

Mzee George A. Smith, Mtume, alipokea ushauri toka kwa Nabii Joseph Smith wakati wa nyakati ngumu: “Aliniambia kamwe nisikate tamaa, licha ya shida zozote zinazoweza kunizingira. Ikiwa nitazamishwa katika shimo la kina kirefu la Nova Scotia na Milima yote ya Miamba kuwekwa juu yangu, sipaswi kukata tamaa bali nivumilie, na niwe na imani, na niendelee kuwa jasiri na nitaibuka juu ya rundo hilo mwishowe.”1

Ni kwa vipi Nabii Joseph alilisema hilo—kwa mtu ambaye alikuwa akiteseka? Kwa sababu alijua ilikuwa ni kweli. Aliuishi ukweli huo. Joseph mara nyingi alipitia magumu katika maisha yake. Hata hivyo, wakati alipotumia imani katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake, na kuendelea kusonga, alishinda vikwazo ambavyo vilionekana vya kutisha.2

Leo ningependa kurudia wito wa Joseph wa kutoacha kuvunjika moyo kutuzidie wakati tunapokumbana na mambo ya kuvunja moyo, uzoefu wenye uchungu, mapungufu yetu wenyewe au changamoto zingine.

Ninaposema kuvunjika moyo, sizungumzii kuhusu changamoto ziletazo udhaifu za msongo wa mawazo, hofu au magonjwa mengine ambayo huitaji matibabu maalum.3 Ninazungumzia kuhusu kuvunjika moyo ambako huja kutokana na changamoto za kimaisha.

Ninavutiwa na mashujaa wangu ambao wao huendelea kusonga—kwa imani bila kujali chochote.4 Kwenye Kitabu cha Mormoni, tunasoma juu ya Zoramu, mtumishi wa Labani. Wakati Nefi alipopata mabamba ya shaba, Zoramu alikabiliwa na uchaguzi wa kumfuata Nefi na kaka zake nyikani au pengine kupoteza maisha yake.

Ni uchaguzi mgumu ulioje! Dhamira ya kwanza ya Zoramu ilikuwa ni kukimbia, lakini Nefi alimkamata na kufanya agano kwamba kama angeenda pamoja nao, angekuwa huru na angekuwa na sehemu kwenye familia yao. Zoramu alipata ujasiri na kwenda nao.5

Zoramu alipitia magumu mengi kwenye maisha yake mapya, lakini alisonga mbele kwa imani. Hatuna dokezo kwamba Zoramu aliendelea kushikilia hali yake ya zamani au kuwa na hisia za chuki kwa Mungu na wengine.6 Alikuwa rafiki wa kweli kwa Nefi, nabii na yeye pamoja na uzao wake waliishi kwa uhuru na mafanikio kwenye nchi ya ahadi. Kile kilichokuwa kikwazo kikubwa kwenye njia ya Zoramu hatimaye kiliongoza kwenye baraka tele, kwa sababu ya uaminifu wake na utayari wa kuendelea kusonga—kwa imani.7

Hivi karibuni nilimsikiliza dada mmoja jasiri akishiriki jinsi alivyovumilia kwenye magumu.8 Alikuwa na changamoto, na Jumapili moja alikuwa ameketi kwenye darasa la Muungano wa Usaidizi akimsikiliza mwalimu ambaye alifikiri alikuwa na mwonekano wa maisha makamilifu—tofauti kabisa na ya kwake. Alichoshwa na kukatishwa tamaa. Alihisi kama alikuwa hatoshi—au hata kufaa—hivyo alisimama na kuondoka, akipanga kamwe kutorudi tena kanisani. Akitembea kuelekea kwenye gari, alihisi hisia ya utofauti: “Nenda kwenye ukumbi wa Kanisa na msikilize mzungumzaji kwenye sakramenti.” Alitilia shaka msukumo huo lakini aliuhisi tena kwa nguvu, hivyo alikwenda kwenye mkutano.

Ujumbe ulikuwa sawasawa na alichokihitaji. Alimhisi Roho. Alijua kwamba Bwana alimtaka kubakia pamoja Naye, kuwa mfuasi Wake na kuhudhuria kanisani, basi alifanya hivyo.

Je, unajua alikuwa na shukrani kwenye kipi? Kwamba hakukata tamaa. Aliendelea kusonga—kwa imani katika Yesu Kristo, hata wakati ilipomlazimu kubadilika, na yeye na familia yake wanabarikiwa sana wakati anaposonga mbele.

Mungu wa mbingu na nchi atatusaidia tushinde kukatishwa tamaa na vikwazo vyovyote tunavyokumbana navyo kama tutamtazamia Yeye, kufuata misukumo ya Roho Mtakatifu,9 na kuendelea kusonga—kwa imani.

Kwa shukrani, tunapokuwa dhaifu au wasioweza, Bwana anaweza kuimarisha imani yetu. Yeye anaweza kuzidisha uwezo wetu kupita ule tulio nao. Nimewahi kupitia hilo. Zaidi ya miaka 20 iliyopita, bila kutegemea niliitwa kuwa Sabini wa Eneo, na nilihisi sikuwa na uwezo. Kufuatia mafunzo yangu ya majukumu, nilitakiwa kusimamia kwenye mkutano wangu wa kwanza wa kigingi.10 Rais wa kigingi pamoja nami kwa uzuri tulipanga kila kitu. Muda mfupi kabla ya mkutano, Rais Boyd K. Packer, wakati huo–kama Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alipiga simu kujua kama angeweza kunisindikiza. Nilishangaa na, bila shaka, nilikubali. Nilitaka kujua ni namna gani angetaka mkutano uwe kwa sababu angeusimamia. Alipendekeza kwamba tutengue ratiba ya mkutano na tujiandae kumfuata Roho. Kizuri ni kwamba, bado nilikuwa na siku 10 za kujifunza, kusali na kujiandaa.

Tukiwa hatuna ajenda, tulikuwa kwenye jukwaa dakika 20 kabla ya mkutano wa viongozi kuanza. Nilimuegamia rais wa kigingi na kumnong’oneza “Hiki ni kigingi kizuri.”

Rais Packer alinigusa kwa kiwiko na kusema kwa upole “Hakuna kuzungumza.”

Niliacha kuzungumza, na ujumbe wake wa mkutano mkuu kuhusu “Utulivu hualika Ufunuo”11 ulikuja mawazoni mwangu. Niliona kwamba Rais Packer alikuwa akiandika marejeleo ya maandiko. Roho alinithibitishia kwamba alikuwa akipokea ufunuo kwa ajili ya mkutano. Uzoefu wangu wa kujifunza ulikuwa ndiyo kwanza unaanza.

Rais Packer alizungumza kwa dakika 15 za mwanzo na akasisitiza umuhimu wa kuendesha mikutano yote kwa kuongozwa na Roho.15 Kisha akasema “Sasa tutasikia kutoka kwa Mzee Cook.”

Wakati nikielekea kwenye mimbari, nilimuuliza angependa nitumie muda kiasi gani na kama kulikuwa na mada ambayo angependa niizungumzie. Alisema “Tumia dakika 15 na endelea kulingana na unavyopata msukumo.” Nilitumia kama dakika 14 na kushiriki kila kitu nilichokuwa nacho mawazoni mwangu.

Rais Packer alisimama tena na kuzungumza kwa dakika 15. Alishiriki andiko hili:

“Yasemeni mawazo nitakayoyaweka mioyoni mwenu, na ninyi hamtashindwa mbele za watu;

Kwani mtapewa katika saa ile ile … katika wakati ule ule, kile mtakachosema.”13

Kisha akasema, “Sasa tutasikia kutoka kwa Mzee Cook.”

Nilishtuka. Sikuwahi kufikiria uwezekano kwamba ningeombwa kuzungumza mara mbili kwenye mkutano mmoja. Sikuwa na chochote mawazoni cha kusema. Nikisali kwa dhati na kumtegemea Bwana kwa ajili ya msaada, kwa namna fulani, nilibarikiwa kupata wazo, andiko, na niliweza kuzungumza kwa dakika 15 zingine. Niliketi nikiwa nimechoka kabisa.

Rais Packer alizungumza tena kwa dakika 15 kuhusu kumfuata Roho na kushiriki mafundisho ya Paulo kwamba tusizungumze “maneno ambayo hekima ya wanadamu hufundisha, lakini yale ambayo Roho Mtakatifu hufundisha.”14 Ambavyo ungeweza kufikiria, nilizidiwa wakati alipopata msukumo kusema kwa mara ya tatu, “Sasa tutasikia kutoka kwa Mzee Cook.”

Sikuwa na cha kusema. Sikuwa na chochote. Nilitambua kwamba ulikuwa ni wakati wa kutumia imani zaidi. Taratibu, nilielekea kwenye mimbari, nikimlilia Mungu kwa ajili ya msaada. Wakati nilipofika kwenye kinasa sauti, Bwana kimiujiza alinibariki kwa namna fulani kutoa ujumbe kwa dakika 15 zingine.15

Mkutano hatimaye ulikwisha, lakini haraka nilitambua kwamba mkutano kwa ajili ya watu wazima ungeanza baada ya saa moja. Ha, jamani! Kama Zoramu, kwa dhati nilitaka kukimbia, lakini kama Nefi alivyomkamata, nilijua Rais Packer angenikamata. Mkutano wa watu wazima ulifuata mfumo ule ule. Nilizungumza mara tatu. Siku iliyofuata wakati wa mkutano wa watu wote, nilizungumza mara moja.

Baada ya mkutano, Rais Packer alisema kwa upendo, “Acha tufanye tena kama hivi wakati mwingine.” Ninampenda Rais Boyd K. Packer na kuthamini yote ambayo nilijifunza.

Unajua nina shukrani kwa kipi? Kwamba sikukata tamaa—au kukataa. Kama ningesikiliza matamanio yangu ya kukatisha tamaa ya kutoroka mikutano ile, ningekosa fursa ya kuongeza imani yangu na kupokea mtiririko tele wa upendo na msaada kutoka kwa Baba wa Mbinguni. Nilijifunza kuhusu rehema Yake, nguvu ya kimiujiza ya kuwezesha ya Yesu Kristo na Upatanisho Wake, na ushawishi wenye nguvu wa Roho Mtakatifu. Licha ya mapungufu yangu,16 nilijifunza kwamba ninaweza kutumikia; ninaweza kuchangia wakati Bwana akiwa upande wangu, ikiwa tu nitaendelea kusonga—kwa imani.

Bila kujali ukubwa, undani, na hitaji la changamoto tunazokabiliana nazo maishani, sote tuna nyakati tunapohisi kuacha, kuondoka, kutoroka au kukata tamaa. Lakini kwa kuonesha imani katika Mwokozi wetu, Yesu Kristo, hutusaidia tushinde kukatishwa tamaa bila kujali ni vikwazo gani tunakumbana navyo.

Kama vile Mwokozi alivyokamilisha kazi Aliyotumwa kufanya, Yeye ana nguvu za kutusaidia tukamilishe kazi ambayo tumepewa.17 Tunaweza kubarikiwa kusonga mbele kwenye njia ya agano, bila kujali ni jinsi gani ina miamba, na hatimaye kupokea uzima wa milele.18

Kama Nabii Joseph Smith alivyosema, “Simameni imara, enyi Watakatifu wa Mungu, subirini ingawa kwa muda mrefu, na tufani za maisha zitapita, na mtazawadiwa na yule Mungu ambaye ninyi ni watumishi Wake.”19 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. George A. Smith, katika Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2011), 235.

  2. Ona Teachings: Joseph Smith, 227–36.

  3. Ninapozungumzia kuhusu kukata tamaa, sipendekezi kwamba “Kuendelea kusonga kwa imani katikaYesu Kristo” ni juhudi pekee inayohitajika kwa watu wanaopitia msongo wa mawazo, hisia za woga au magonjwa mengineyo. Kwa marafiki hawa, wanafamilia na wengine wanaosikiliza, ninavumisha ushauri wa viongozi wetu wa Kanisa wa kutafuta msaada wa kitaalamu, wa kisaikolojoa na kiroho wakati wakiendelea kumtumaini Bwana. Hisia za moyo wangu zi juu ya wale kati yenu ambao mnatatizwa na changamoto hizi za kipekee. Kwa dhati tunawaombea.

  4. Baadhi ya mashujaa wangu kwenye maandiko ni pamoja na Kalebu (ona Hesabu 14:6–9, 24), Ayubu (ona Ayubu 19:25–26) na Nefi (ona 1 Nefi 3:7), kama nyongeza ya mashujaa wangu wa siku zetu.

  5. Ona 1 Nefi 4:20, 30–35, 38.

  6. Ona Dale G. Renlund, “Ya Kukasirisha Yasiyo Haki,” Liahona, Mei 2021, 41–45.

  7. Ona 2 Nefi 1:30–32. “Ingawa [Zoramu] alitakiwa kuvumilia uchukuliwaji usio wa kistaha, mtego uliomkamata ulikuwa ni hali pekee ambayo Mungu alikuwa ameamua ili kumbariki. Ingawa alitakiwa kuiacha nchi yake, Mungu alikuwa anaiandaa iliyo bora zaidi.” (David B. Paxman, “Zoram and I: Getting Our Stories Straight” [Brigham Young University devotional, July 27, 2010], speeches.byu.edu).

  8. Nilisikia ushuhuda wa dada huyu kwenye kata iliyo chini ya Kigingi cha Riverdale Utah mnamo Desemba 11, 2022. Uzoefu alioushiriki ulikuwa ni kutoka kwenye kata aliyokuwepo awali.

  9. See Mafundisho na Maagano 11:12–13.

  10. Jukumu langu lilikuwa kwenye Kigingi cha Benson Utah mnamo Novemba 3–4, 2001. Rais Jerry Toombs alikuwa ni rais wa kigingi.

  11. Ona Boyd K. Packer, “Reverence Invites Revelation,” Ensign, Nov. 1991, 21–23.

  12. Ona Mafundisho na Maagano 46:2.

  13. Mafundisho na Maagano 100:5–6; ona pia mistari 7–8.

  14. 1 Wakorintho 2:13.

  15. Rais Russell M. Nelson amesema, “Wakati kiroho unapofanya zaidi ya vile ambavyo umekuwa ukifanya hapo awali, ndipo nguvu ya [Mwokozi] itatiririka kwako” (“Kuleta Nguvu ya Yesu Kristo Maishani Mwetu,” Liahona, Mei 2017, 42).

  16. Ona Etheri 12:27.

  17. Ona Yohana 17:4.

  18. Ona 2 Nefi 31:20; Mosia 2:41; Alma 36:3.

  19. Teachings: Joseph Smith, 235.

Chapisha