Kutafuta Amani Binafsi
Ninaomba kwamba upate amani, uwasaidie wengine wengi kuipata, na kuipitisha kwa wengine.
Kaka na dada zangu wapendwa, tumebarikiwa kwa mafundisho yenye maongozi na muziki mzuri ambao umetugusa katika kikao hiki cha ufunguzi wa mkutano mkuu. Tunawashukuru kwa ushiriki wenu na kwa imani yenu.
Leo nitazungumza juu ya kile nilichojifunza kuhusu muujiza wa kupata amani binafsi, bila kujali hali zetu. Mwokozi anajua kwamba watoto wote wa Baba wa Mbinguni wanatamani amani, na Alisema kwamba Angeweza kutupatia. Unakumbuka maneno ya Yesu Kristo yaliyoandikwa katika kitabu cha Yohana: “Amani nawaachieni, amani yangu nawapa: niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”1
Anachomaanisha kwa amani na jinsi anavyoweza kuitoa vinaonekana kwenye hali za wale waliomsikia akisema maneno hayo. Sikiliza simulizi toka Yohana ya kilele cha huduma ya Kristo. Majeshi makali ya uovu yalikuwa yakimshambulia na yangewajia wanafunzi Wake punde tu.
Haya ni maneno ya Mwokozi:
“Kama wanipenda, shika amri zangu.
“Na nitamwomba Baba, naye atawapa Mfariji mwingine, ili aweze kuwa nanyi daima;
“Hata Roho wa kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu hawamwoni, wala kumjua: ila ninyi mnamjua; kwani anakaa ndani yenu, na atakuwa nanyi.”
“Sitawaacha ninyi yatima: Naja kwenu.”
“Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona: Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi pia mtakuwa hai.
“Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.
“Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye: naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda, na kujidhirihisha kwake.
“Yuda, siye Iskarioti, akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu?
“Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.
“Yeye asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; na neno hilo mnalolisikia si langu, bali ni la Baba aliyenituma.
“Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu.
“Lakini Mfariji, ambaye ni Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowambieni.
“Amani nawaachieni, amani yangu nawapa: niwapavyo mimi, sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”2
Nimejifunza angalau kweli tano kutoka kwenye mafundisho hayo ya Mwokozi.
Kwanza, zawadi ya amani inatolewa baada ya sisi kuwa na imani ya kushika amri Zake. Kwa wale ambao ni washiriki wa agano wa Kanisa la Bwana, utiifu ndio kitu ambacho tayari tumeahidi kufanya.
Pili, Roho Mtakatifu atakuja na kukaa nasi. Bwana anasema kwamba, kadiri tunavyoendelea kuwa waaminifu, Roho Mtakatifu atakaa ndani yetu. Hiyo ndiyo ahadi katika sala ya sakramenti kwamba Roho atakuwa mwenza wetu na kwamba tutahisi, katika mioyo na akili zetu, faraja Yake.
Tatu, Mwokozi anaahidi kwamba tunaposhika maagano yetu, tunaweza kuhisi upendo wa Baba na Mwana kwa kila mmoja wetu na kwa ajili yetu sisi. Tunaweza kuhisi ukaribu Wao katika maisha yetu ya duniani, kama tutakavyohisi tutakapobarikiwa kuwa nao milele.
Nne, kushika amri za Bwana kunahitaji zaidi ya utiifu. Tunapaswa kumpenda Mungu kwa mioyo yetu yote, nguvu, akili na roho zetu zote.3
Wale wasiompenda Yeye hawashiki amri Zake. Na hivyo, hawatakuwa na zawadi ya amani katika maisha haya na katika ulimwengu ujao.
Tano, ni wazi kwamba Bwana alitupenda vya kutosha kulipa gharama ya dhambi zetu ili kwamba tuweze—kupitia imani yetu Kwake na toba yetu, kwa njia ya Upatanisho Wake—tuwe na zawadi ya amani “ipitayo akili zote,”4 katika maisha haya na pamoja Naye milele.
Baadhi yenu, pengine wengi, hamhisi amani ambayo Bwana aliahidi. Huenda umesali kwa ajili ya amani binafsi na faraja ya kiroho. Hata hivyo kwenye kuishi kwako unaweza kuhisi kwamba mbingu ziko kimya kwa maombi yako ya amani.
Kuna adui wa nafsi yako ambaye hataki wewe na wale unaowapenda mpate amani. Hawezi kuifurahia. Anafanya kazi kwa bidii ili kukuzuia hata kutaka kupata hiyo amani ambayo Mwokozi na Baba yetu wa Mbinguni wanatamani uwe nayo.
Jitihada za Shetani za kupanda chuki na mabishano kila mahala zinaonekana kuongezeka. Tunaona uthibitisho wa hilo kutokea miongoni mwa mataifa na miji, katika majirani, kwenye vyombo vya habari vya kielektroniki, na kote ulimwenguni.
Bado iko sababu ya kuwa na matumaini: ni ile Nuru ya Kristo iliyowekwa ndani ya kila mtoto mchanga azaliwaye. Kwa zawadi hiyo kwa wote huja hisia ya kile kilicho sahihi, hamu ya kupenda na kupendwa. Kuna hisia ya haki na ukweli katika kila mtoto wa Mungu anapokuja katika maisha ya duniani.
Matumaini yetu ya amani binafsi kwa watoto hao yako katika watu wanaowajali. Ikiwa wale wanaowalea na kuwahudumia wamefanya kazi ili kupokea zawadi ya amani kutoka kwa Mwokozi, wao, kwa kielelezo binafsi na juhudi, watahimiza imani ya mtoto kustahili zawadi ya amani isiyo ya kawaida.
Hivyo ndivyo maandiko yanavyoahidi: “Mlee mtoto katika njia impasayo: Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.”5 Itamhitaji yule aliyepewa jukumu la kumtunza mtoto na kumlea kuwa mwenye kustahili zawadi ya amani.
Cha kusikitisha ni kwamba, sisi sote tumehisi uchungu wakati watoto waliolelewa na wazazi wema—wakati mwingine mzazi mmoja peke yake—kuchagua njia ya huzuni, baada ya maisha yote ya imani na amani.
Hata huzuni hiyo inapotokea, matumaini yangu hutegemea zawadi nyingine kutoka kwa Bwana. Ni kwa hili: kwamba Yeye huwainua wapatanishi wengi miongoni mwa wanafunzi Wake anaowaamini. Wamehisi amani na upendo wa Mungu. Wana Roho Mtakatifu mioyoni mwao, na Bwana anaweza kuwaongoza kuwafikia kondoo wanaotangatanga.
Nimeliona hili maishani mwangu na kote ulimwenguni. Nawe pia umeliona. Wakati fulani, unapoongozwa kwenye uokoaji, inaweza kuonekana kama tukio ambalo halikupangwa.
Wakati fulani, nilimuuliza mtu fulani niliyekutana naye kwenye safari, “Je, unaweza kuniambia kidogo kuhusu familia yako?” Mazungumzo hayo yalinifanya kuomba kuona picha ya bintiye mtu mzima ambaye alisema alikuwa anasumbuka. Nilishangazwa na wema usoni mwa msichana yule kwenye picha. Nilihisi kuvutiwa kuuliza kama ningeweza kupata anwani yake ya barua pepe. Binti wakati huo alikuwa amepotea, na akijiuliza ikiwa Mungu alikuwa na ujumbe wo wote kwa ajili yake. Mungu alikuwa nao. Ilikuwa ni huu: “Bwana anakupenda. Mara zote anakupenda. Bwana anakutaka urudi. Baraka zako ulizoahidiwa bado zipo.”
Waumini kote katika Kanisa wamehisi zawadi ya Bwana ya amani binafsi. Anahimiza kila mtu kusaidia wengine kuwa na fursa za kuja Kwake na kustahili kupata amani hiyo hiyo wao wenyewe. Wao, kwa upande wao, watachagua kutafuta maongozi ya kujua jinsi wanavyoweza kupitisha zawadi hiyo kwa wengine.
Kizazi kinachoinuka kitakuwa walezi wa kizazi kitakachofuata. Matokeo ya ongezeko la zawadi hiyo yatazalisha muujiza. Itaenea na kukua baada ya muda, na ufalme wa Bwana duniani utakuwa umeandaliwa na tayari kumpokea Yeye kwa kelele za hosana. Kutakuwa na amani duniani.
Ninatoa ushuhuda wangu wa hakika Mwokozi yu hai na kwamba Anaongoza Kanisa hili. Nimehisi upendo Wake katika maisha yangu na upendo Wake na kujali kwa ajili ya watoto wote wa Baba wa Mbinguni. Mwaliko wa Mwokozi kuja Kwake ni toleo la amani.
Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Mungu aliye hai ulimwenguni kote. Amesema, “Ninakupa uhakikisho wangu kwamba bila kujali hali ya ulimwengu na hali yako binafsi, unaweza kukabiliana na wakati ujao kwa matumaini na furaha.6
Natoa upendo wangu kwenu. Imani yenu na upendo mkuu unawafikia watu na kumruhusu Bwana kubadilisha mioyo na hivyo kupata hamu ya kuwapa wengine zawadi ya amani ipitayo ufahamu wote.
Ninaomba kwamba upate amani, uwasaidie wengine wengi kuipata, na kuipitisha kwa wengine. Kutakuwa na miaka elfu ya ajabu ya amani wakati Bwana atakapokuja tena. Ninashuhudia katika shangwe na katika jina la Yesu Kristo, amina.