Je, Ni Kweli Nimesamehewa?
Ahadi ya msamaha kamili na mkamilifu imefanywa kwa kila mtu—katika na kupitia Upatanisho usio na mwisho wa Yesu Kristo.
Miaka michache iliyopita, Dada Nattress na mimi tulihamia Idaho, tulipofungua biashara mpya. Kulikuwa na mchana mrefu na usiku mrefu ofisini. Cha kushukuru, tuliishi mitaa michache tu kutoka kazini. Kila wiki, Shawna na mabinti zetu watatu—wote chini ya umri wa miaka sita—walikuwa wakija ofisini kushiriki nasi chakula cha mchana.
Katika siku mojawapo kama hiyo baada ya chakula cha mchana cha familia, niligundua kwamba binti yetu wa miaka mitano, Michelle, alikuwa ameniachia ujumbe binafsi, ulioandikwa kwenye Karatasi ndogo ya ujumbe na kuwekwa kwenye simu ya ofisini kwangu.
Ulisomeka, “Baba, kumbuka kunipenda. Akupendaye, Michelle.” Huu ulikuwa ni ukumbusho wenye nguvu kwa baba kijana kuhusu mambo yale yaliyo muhimu zaidi.
Akina kaka na akina dada, nashuhudia kwamba Baba yetu wa Mbinguni daima anatukumbuka na kwamba Anatupenda kikamilifu. Swali langu ni hili: Je, sisi tunamkumbuka Yeye? Na tunampenda Yeye?
Miaka kadhaa iliyopita, nilitumikia kama kiongozi wa Kanisa katika eneo nililoishi. Kijana wetu mmoja, Danny, alikuwa ni bora katika kila kitu. Alikuwa mtiifu, mkarimu, mwema na alikuwa na moyo mkuu. Hata hivyo, alipohitimu sekondari ya juu, alianza kujihusisha na makundi mabaya. Alijiingiza kwenye madawa ya kulevya, hususani methamphetamine, na akaanza kuzama kwenye kina cha uraibu na maangamizo. Kabla ya muda mrefu, mwonekano wake ulibadilika kabisa. Ilikuwa ni ngumu kumtambua. Badiliko lake kubwa lilikuwa ni kwenye macho yake—nuru kwenye macho yake ilikuwa imefifia. Mara nyingi nilimfuata kuzungumza naye, bila mafanikio. Hakupendelea.
Ilikuwa vigumu kumuona kijana mzuri kama huyu akitaabika na kuishi maisha ambayo yalikuwa si yake! Alikuwa na uwezo wa mengi zaidi.
Ndipo siku moja, muujiza wake ulipoanza.
Alihudhuria mkutano wa sakramenti ambapo mdogo wake alishiriki ushuhuda kabla ya kwenda misheni. Wakati wa mkutano, Danny alihisi kitu ambacho hakuwahi kukihisi kwa muda mrefu. Alihisi upendo wa Bwana. Hatimaye alikuwa na tumaini.
Ingawa alikuwa na tamanio la kubadilika, ilikuwa vigumu kwa Danny. Uraibu wake na hatia iliyomwandama vilikuwa ni vitu ambavyo hangeweza kuvihimili.
Adhuhuri moja mahususi, nilipokuwa nje nakata nyasi bustanini, Danny alishuka kwenye gari lake kimya kimya. Alikuwa akipambana vikali. Nilizima mashine na tuliketi pamoja kwenye kivuli cha barazani. Ndipo hapo aliposhiriki nami hisia za moyo wake. Kwa kweli alitaka kurudi. Hata hivyo, kuachana na uraibu wake na mfumo wake wa maisha ilikuwa ni vigumu sana. Kama nyongeza kwenye hili, alijihisi mwenye hatia, na aibu kwa kuanguka mbali namna hii. Aliuliza, “Ni kweli naweza kusamehewa? Kuna njia ya hakika ya kurudi?”
Baada ya kuumimina moyo wake na wasiwasi wake, tulisoma Alma mlango wa 36 pamoja:
“Ndiyo, nilikumbuka dhambi zangu na uovu wangu. …
“Ndiyo, … wazo la kuja katika uwepo wa Mungu wangu lilizonga moyo wangu kwa machungu yasiyoelezeka” (mistari ya 13–14).
Baada ya mistari hiyo, Danny alisema, “Hivi ndivyo hasa ninavyohisi!”
Tuliendelea:
“Na ikawa kwamba wakati nilihuzunishwa na ufahamu wa dhambi zangu nyingi, tazama, nilikumbuka pia kumsikia baba yangu akitoa unabii kwa watu kuhusu kuja kwa mmoja aitwaye Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, kulipia dhambi za ulimwengu. …
“Na ee, ni shangwe gani, na ni mwangaza gani wa ajabu niliouona”(mistari ya 17, 20)
Tulipokuwa tunasoma vifungu hivi, machozi yalianza kutiririka. Shangwe ya Alma ilikuwa shangwe aliyokuwa akiitafuta!
Tulijadiliana kwamba Alma alikuwa mwovu wa kipekee. Hata hivyo, mara alipotubu, kamwe hakutazama nyuma. Akawa mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo. Alikuwa nabii! Macho ya Danny yalitanuka. “Nabii?” alisema.
Niliitikia tu, “Ndiyo, Nabii. Hakuna shinikizo kwako!”
Tulijadiliana kwamba wakati dhambi zake hazikufikia kiwango cha Alma, ahadi ile ile ya msamaha mkamilifu imefanywa kwa watu wote—na kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo usio na mwisho.
Danny sasa alielewa. Alijua nini alichotakiwa kufanya: alihitaji kuanza safari yake kwa kumwamini Bwana na kujisamehe mwenyewe!
Mabadiliko makubwa ya moyo wa Danny hayakuwa chochote ila muujiza. Baada ya muda, mwonekano wake ulibadilika na mg’aro wa macho yake ulirudi. Alikuwa mwenye kustahili kwenda hekaluni! Hatimaye alikuwa amerejea!
Baada ya miezi mingi, nilimuuliza Danny kama angependa kuwasilisha maombi yake kwenda kutumikia misheni. Jibu lake lilikuwa la kushitua na kustaajabisha.
Alisema, “ningependa kutumikia misheni, lakini unajua nilikokuwa na mambo niliyoyafanya! Nilidhani nilikuwa sistahili.”
Nilijibu, “Unaweza kuwa sahihi. Hata hivyo, hakuna kitu kinatuzuia sisi kufanya maombi. Kama hukuitwa, angalau utajua kwamba ulionyesha nia yako ya kweli ya kumtumikia Bwana.” Macho yake yalifunguka. Alifurahishwa na wazo hili. Kwake hili lilikuwa jambo la muda mrefu, lakini lilikuwa ndiyo fursa aliyotaka kuifuata.
Wiki chache baadaye, na kwa mshangao wake, muujiza mwingine ulitokea. Danny alipokea wito wa kutumikia misheni.
Miezi michache baada ya Danny kuwasili misheni, nilipokea simu. Rais wake alisema, “Kuna nini kwa mvulana huyu? Ni mmisionari wa kupendeza niliyewahi kumwona!” Unaona, rais huyu alikuwa amempokea Alma Mdogo wa nyakati hizi.
Miaka miwili baadaye, Danny alirudi nyumbani kwa heshima, akiwa amemtumikia Bwana kwa moyo wake wote, uwezo, akili na nguvu.
Kufuatia taarifa yake ya umisionari katika mkutano wa sakramenti, nilirudi nyumbani, na kusikia hodi kwenye mlango wa mbele. Hapo alisimama Danny na machozi yakilenga lenga katika macho yake. Alisema, “Tunaweza kuzungumza kwa dakika moja?” Tulienda nje kwenye ngazi zile zile za barazani.
Alisema, “Rais, je, unafikiri kweli nimesamehewa?”
Machozi yangu yaliungana na yake. Mbele yangu alisimama mfuasi wa Yesu Kristo mwaminifu ambaye alijitoa yote aliyokuwa nayo kufundisha na kumshuhudia Mwokozi. Alikuwa kiunganishi cha uponyaji na nguvu za kuimarisha za Upatanisho wa Mwokozi.
Nilisema, “Danny! Umejiangalia kwenye kioo? Umeona macho yako? Yamejawa na mwanga, na una mg’aro wa Roho wa Bwana. Bila shaka umesamehewa! Unastaajabisha! Sasa unachohitaji kufanya ni kusonga mbele na maisha yako. Usiangalie nyuma! Angalia mbele kwa imani katika ibada inayofuata.
Muujiza wa Danny unaendelea leo. Alifunga ndoa hekaluni na kurudi shule, ambapo alitunukiwa shahada ya uzamili. Anaendelea kumtumikia Bwana kwa heshima na uadilifu katika wito wake. Cha muhimu zaidi, amekuwa mume bora na baba mwaminifu. Yeye ni “mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo.
Rais Russel M. Nelson alifundisha, “Bila ya Upatanisho wa milele wa [Mwokozi] binadamu wote wangepotea wasipatikane tena.”1 Danny hakuwa amepotea, na hata sisi hatujapotea katika Bwana. Anasimama mlangoni kutuinua, kutuimarisha na kutusamehe. Yeye daima anakumbuka kutupenda sisi!
Onyesho la uhakika la upendo wa Mwokozi kwa watoto wa Mungu limerekodiwa katika Kitabu cha Mormoni: “Ikawa kwamba baada ya Yesu kusema hivyo, alielekeza macho yake tena kwa umati, na akaona kuwa wanalia, na walikuwa wanamwangalia kwa uthabiti kama wanaotaka kumwomba akae nao kwa muda mrefu zaidi” (3 Nefi 17:5).
Mwokozi alikuwa ametumia siku nzima akiwahudumia watu. Hata hivyo, alikuwa na mengi ya kufanya—Alipaswa kuwatembelea kondoo Wake wengine; Alipaswa kwenda kwa Baba Yake.
Bila kujali majukumu haya, Alitambua kwamba watu walitamani Yeye aendelee kukaa nao zaidi. Kisha, kwa moyo uliojaa huruma wa Mwokozi, moja ya miujiza mikubwa katika historia ya dunia ilitokea:
Alibaki.
Aliwabariki.
Aliwahudumia watoto wao mmoja mmoja.
Alisali kwa ajili yao; Alilia pamoja nao.
Na Aliwaponya. Ona 3 Nefi 17.)
Ahadi zake ni za milele: Atatuponya.
Kwa wale ambao wamechepuka kutoka kwenye njia ya agano, tafadhali jua kuwa daima kuna tumaini, daima kuna uponyaji, na kuna njia siku zote ya kurudi.
Ujumbe wake wa tumaini la milele ni zeri ya uponyaji kwa wote wanaoishi kwenye ulimwengu wa matatizo. Bwana alisema, “Mimi ndimi njia, na kweli na uzima.”(Yohana 14:6).
Akina kaka na akina dada, hebu tukumbuke kumtafuta Yeye, na daima kumkumbuka Yeye.
Ninashuhudia kwamba Mungu yu hai na kwamba anatupenda. Ninazidi kushuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wa ulimwengu. Yeye ndiye mponyaji mkuu. Ninajua kwamba Mkombozi Wangu yu hai! Katika Jina la Yesu Kristo, amina.