Mkutano Mkuu
Akili Yangu Ilifikiria Wazo Hili juu ya Yesu Kristo
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


Akili Yangu Ilifikiria Wazo Hili juu ya Yesu Kristo

Wakati kwa umakini ukiendelea kufikiria kuhusu Yesu Kristo, ninakuahidi si tu mwongozo wa kimbingu bali pia nguvu za kimbingu.

Katika msimu huu mzuri wa Pasaka, ninatoa mwangwi wa sala ya wimbo huu mzuri, “Tuongoze, Ewe Yehova Mkuu.”1

Hadithi maridadi katika Kitabu cha Mormoni hutwambia kuhusu kijana mdogo, kutoka katika familia maarufu, aitwaye Alma, ambaye maandiko yalimwelezea kama kafiri mwabudu sanamu.2 Alikuwa mtu wa maneno mengi na mwenye ushawishi, akitumia mzaha kuwashawishi watu wamfuate yeye. Cha kustaajabisha, malaika alimtokea Alma na rafiki zake. Alma alianguka chini na alikuwa dhaifu sana kwamba alibebwa na kupelekwa nyumbani kwa babaye. Alibakia kwenye hali ya kukosa fahamu kwa siku tatu.3 Baadaye, alieleza kwamba wakati akionekana kama mtu aliyepoteza fahamu kwa wale waliomzunguka, akili yake ilikuwa sawia wakati nafsi yake ikihuzunika, akifikiria kuhusu maisha yake ya kutotii amri za Mungu. Aliielezea akili yake kwamba “ilihuzunishwa na ufahamu wa dhambi [zake] nyingi”4 na “kusumbuliwa na mateso ya milele.”5

Katika kukata kwake tamaa, alikumbuka kufundishwa ujanani mwake kuhusu “kuja kwa mtu mmoja aitwaye Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, kulipia dhambi za ulimwengu.”6 Kisha alitoa kauli hii ipasayo tafakuri: “Nilipofikiria wazo hili, nililia ndani ya moyo wangu: Ee Yesu, wewe Mwana wa Mungu, nihurumie.”7 Alipokuwa akiomba kwa ajili ya nguvu ya kiungu ya Mwokozi, kitu cha kimiujiza kilitokea: “Nilipofikiri hivi,” alisema, “sikukumbuka uchungu wangu tena.”8 Ghafla alihisi amani na nuru. “Hapakuwa na kitu kizuri hivyo na kitamu vile ilivyokuwa shangwe yangu,”9 alisema.

Alma “alifikiria” ukweli kuhusu Yesu Kristo. Kama tungekuwa tunatumia neno “kushikilia” katika hali ya kawaida, tungeweza kusema, “alishikilia kingo za pembeni alipokuwa karibu kuanguka,” ikimaanisha alijishikiza kwa haraka na kwa nguvu kwenye kitu imara kilichosimikwa kwenye msingi imara.

Katika tukio la Alma, ilikuwa ni akili yake ambayo ilifikia na kuushikilia ukweli huu wenye nguvu juu ya dhabihu ya upatanisho ya Yesu Kristo. Kwa kutumia imani kwenye ukweli huo, na kwa nguvu na rehema ya Mungu, aliweza kuokolewa kutoka kuangamizwa na akajazwa na tumaini.

Wakati uzoefu wetu unaweza usiwe kama wa Alma, bado hata uzoefu huo una umuhimu wa milele. Akili zetu pia “zimefikiria wazo hili” juu ya Yesu Kristo na dhabihu Yake ya rehema, na nafsi zetu zimehisi nuru na shangwe ambayo huja.

Kulinda Wazo lihusianalo na Yesu Kristo

Ombi langu katika kipindi hiki cha Pasaka ni kwamba kwa dhati zaidi tutanoa, kuimarisha na kulinda wazo hili muhimu sana juu ya Yesu Kristo katika vyumba vya nafsi zetu,10 tukiliruhusu kutiririka kwenye akili zetu, likituongoza katika kile tufikiriacho na kufanya, na kuendelea kuleta shangwe tamu ya upendo wa Mwokozi.11

Kuzijaza akili zetu kwa nguvu ya Yesu Kristo hakumaanishi kwamba Yeye ndiye wazo pekee ambalo tunalo. Lakini humaanisha kwamba mawazo yetu yote yanafungwa ndani ya upendo Wake, maisha na mafundisho Yake na dhabihu Yake ya upatanisho na Ufufuko mtukufu. Yesu kamwe hayuko kwenye kona iliyosahaulika, kwa sababu mawazo yetu juu Yake mara zote yapo na “vyote vilivyoko ndani [yetu humwabudu] yeye!”12 Tunasali na kuendelea kukumbuka mawazoni mwetu uzoefu ambao ulituleta karibu na Yeye. Tunakaribisha mawazoni mwetu taswira takatifu, maandiko matakatifu na nyimbo zenye kulete msukumo ili kutuliza mawazo yasiyohesabika ya kila siku yajayo kwa kasi kwenye maisha yetu yenye shughuli nyingi. Upendo wetu kwake hautukingi dhidi ya huzuni na majonzi kwenye maisha haya, lakini unaturuhusu kutembea kupita changamoto tukiwa na nguvu zaidi ya uwezo wetu wa kawaida.

Yesu, Ninapokuwaza

Nafurahi moyoni;

Na nitafurahi hasa

Nikikaa kwako.13

Kumbuka, wewe ni mtoto wa kiroho wa Baba wa Mbinguni. Kama Mtume Paulo alivyoeleza, sisi “ni wazao wa Mungu.”14 Umeishi kwa utambulisho wako binafsi kitambo kabla ya kuja duniani. Baba yetu aliandaa mpango mkamilifu kwa ajili yetu wa kuja duniani, kujifunza na kurudi Kwake. Alimtuma Mwana Wake Mpendwa ili kwamba kupitia nguvu za Upatanisho Wake wa milele na Ufufuko, tuishi baada ya kifo; na tunavyokuwa tayari kutumia imani katika Yeye na kutubu dhambi zetu,15 tunasamehewa na kupokea tumaini la maisha ya milele.16

Kuzipa Akili Zetu na Roho Umakini wa Kipekee

Katika maisha haya, akili zetu na roho vinahitaji umakini wa kipekee.17 Akili zetu huturuhusu kuishi, kuchagua na kutambua zuri na baya.18 Roho zetu hupokea ushahidi wa dhati kwamba Mungu ni Baba yetu, kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, na kwamba mafundisho Yao ni mwongozo wetu kwenye furaha hapa duniani na uzima wa milele baada ya kaburi.

Akili ya Alma ilifikiria wazo hili juu ya Yesu Kristo. Wazo lilibadilisha maisha yake. Mkutano mkuu ni fursa nzuri ya kujifunza kile ambacho Bwana angependa sisi tufanye na tuwe. Pia ni muda wa kutafakari maendeleo yetu. Kadiri majukumu yangu yalivyonipeleka kote ulimwenguni, nimeona ongezeko la nguvu ya kiroho kwa waumini wema na waaminifu wa Kanisa.

Miaka mitano iliyopita, tuliombwa kumweka Mwokozi zaidi katika yote tuyafanyayo kwa kutumia jina halisi la Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.19 Tunazungumza jina Lake kwa dhati zaidi.

Miaka minne iliyopita, kwa kupunguza muda wetu wa kikao cha Sakramenti, tulikuza fokasi yetu ya kushiriki sakramenti ya Bwana. Tunafikiria zaidi kuhusu Yesu Kristo na kuwa wadhati zaidi katika ahadi yetu ya daima kumkumbuka.20

Pamoja na kujitenga kulikotokana na janga la ulimwengu na kwa msaada wa Njoo, Unifuate, mafundisho ya Mwokozi yanakuwa ya kina majumbani mwetu, yakisaidia kumwabudu kwetu Mwokozi katika kipindi cha juma.

Kwa kufuata ushauri wa Rais Russell M. Nelson wa “msikilize Yeye,”21 tunaboresha uwezo wetu wa kutambua minong’ono ya Roho Mtakatifu na kuona mkono wa Bwana katika maisha Yetu.

Kwa matangazo ya mahekalu na ukamilishwaji wa mahekalu, tunaingia kwenye nyumba ya Bwana mara kwa mara na kupokea baraka Zake zilizoahidiwa. Tunahisi kwa nguvu zaidi uzuri usio na kifani wa Mwokozi na Mkombozi wetu.

Rais Nelson alisema: “Hakuna kitu rahisi au cha kujiendesha chenyewe kuhusu kuwa [mfuasi] mwenye nguvu. Fokasi yetu lazima ikazwe kwa Mwokozi na injili Yake. Ni nidhamu kuu ya kiakili ya kujitahidi kumtazama Yeye katika kila wazo.”22

Kwa kufokasi umakini wetu kwa Yesu Kristo, vyote vinavyotuzunguka—tukiwa bado hai—huonekana kupitia upendo wetu Kwake. Vivuta mawazo visivyo vya msingi hufifia, na tunaondoa vitu vile visivyoendana na nuru Yake na sifa yake. Kwa umakini unapoendelea kufikiria wazo hili juu ya Yesu Kristo, kumwamini Yeye na kushika amri Zake, sikuahidi tu mwongozo wa kimbingu bali pia nguvu za kimbingu —nguvu iletayo uwezo kwenye maagano yako, amani kwenye magumu yako na shangwe kwenye baraka zako.

Kumkumbuka Yesu Kristo

Wiki chache zilizopita, mimi na Kathy tulitembelea makazi ya Matt na Sarah Johnson. Ukutani ilikuwa ni picha ya familia yao ya thamani, picha nzuri ya Mwokozi na picha ya hekalu.

Mabinti zao wanne, Maddy, Ruby, Claire na June walizungumza kwa furaha kuhusu jinsi wanavyompenda mama yao.

Kwa zaidi ya mwaka Sarah amekuwa akipanga familia kuhudhuria hekaluni kwa pamoja siku za Jumamosi ili kwamba mabinti wangeshiriki katika ubatizo kwa niaba ya wanafamilia walioishi kabla yao.

Mnamo Novemba ya mwaka jana, Sarah alipanga familia kwenda hekaluni katika wiki ya mwisho ya Desemba siku ya Alhamisi badala ya Jumamosi. “Nadhani uko SAWA kwenye hilo,” alimuuliza Matt.

Sarah alikuwa akisumbuliwa na saratani, lakini madaktari walikadiria kwamba angeishi miaka miwili au mitatu zaidi. Wakati wa mkutano wa sakramenti, Sarah alishiriki ushuhuda wake mzito, akisema kwamba bila kujali kitakachomtokea, alimpenda Mwokozi kwa moyo wake wote, na kwamba Mwokozi tayari “amekwisha utwaa ushindi.” Desemba ilipokuwa ikisonga, ghafla afya ya Sarah ilidhoofu, na akalazwa hospitalini. Mapema asubuhi siku ya Alhamisi, Desemba 29, kwa utulivu alikamilisha maisha yake ya duniani. Matt alikuwa pembeni ya Sarah usiku kucha.

Kwa kuvunjika kwake moyo na kukata tamaa kimwili na kihisia, alifika nyumbani, akihuzunika pamoja na mabinti zake. Matt alipotazama simu yake, alikumbuka ukumbusho wa siku ya Alhamisi ya kwenda hekaluni ambao Sarah aliupanga katika siku hiyo. Matt anasema, “Kwanza nilipoona ukumbusho huo, niliwaza, Hili haliwezi kutimia.”

Lakini kisha akili ya Matt ikafikiria wazo hili: Mwokozi yu hai. Hakuna sehemu ambayo tungeweza kuwa kama familia zaidi ya kwenye nyumba Yake takatifu.”

Picha
familia ya Johnson

Matt, Maddy, Ruby, Claire na June waliwasili hekaluni kwa ajili ya miadi ambayo Sarah aliipanga kwa ajili yao. Kwa machozi yaliyotiririka katika mashavu yake, Matt alifanya ubatizo pamoja na mabinti zake. Kwa kina walihisi upendo wao na muunganiko wa milele pamoja na Sarah, na wakahisi upendo wa kina na amani ya kufariji ya Mwokozi. Matt alishiriki kwa upendo, “Japo nahisi huzuni kuu na majonzi, ninashangilia kwa shangwe, kwa kuujua mpango mzuri wa Wokovu wa Baba yangu.

Katika kipindi hiki cha Pasaka, ninashuhudia ukweli mkamilifu na halisi wa dhabihu ya Mwokozi ya kulipia dhambi, dhabihu isiyoweza kulinganishwa na chochote na kwa Ufufuko Wake mtukufu. Kama akili zenu zitabakia imara na daima juu ya wazo kuhusu Yesu Kristo, na mnapofokasi maisha yenu zaidi kwa Mwokozi, ninawaahidi kwamba mtahisi tumaini Lake, amani Yake na upendo Wake. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. “Tuongoze Ee Yehova,” Nyimbo za Dini, na. 37.

  2. Ona Mosia 27:8.

  3. Ona Alma 36:10.

  4. Alma 36:17

  5. Alma 36:12

  6. Alma 36:17

  7. Alma 36:18 Maana nyingine ya “shikilia” inayotumika katika Kitabu cha Mormoni ni ile inayowazungumzia wale “walioshikilia mwisho wa fimbo ya chuma” (1 Nefi 8:24, 30).

  8. Alma 36:19

  9. Alma 36:21

  10. “Vita vikuu vya maisha hupiganwa ndani ya vyumba vya utulivu vya nafsi yako” (David O. McKay, katika Conference Report, Apr. 1967, 84).

  11. “[Mawazo] hudhamini matendo yote. Mawazo yetu ni ubao wa swichi, sehemu inayoongoza matendo yetu” (Boyd K. Packer, Mine Errand from the Lord [1982], 33).

    Rais Dallin H. Oaks alifundisha: “Tunaweza kupoza matamanio maovu kwa yale ya haki. Hii hujumuisha elimu na mazoezi. Rais Joseph F. Smith alifundisha kwamba ‘elimu … ya matamanio yetu ni ya umuhimu mkubwa mno’” (Pure in Heart [1988], 149).

  12. “Sifa kwa Bwana, Mwenyezi,” Nyimbo za Dini, na. 33.

  13. “Yesu Ninapokuwaza,” Nyimbo za Dini, na. 73.

  14. Matendo ya Mitume 17:29.

  15. Ona Mafundisho na Maagano 58:42–43.

  16. Ona Mafundisho na Maagano 14:7.

  17. “Hakuna yeyote ila Mungu ambaye hujua mawazo yako na dhamira ya moyo wako” (Mafundisho na Maagano 6:16).

  18. “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.” (Luka 6:45).

  19. Ona Russell M. Nelson, “Jina Sahihi la Kanisa,” LiahonaNov. 2018, 87–89.

  20. Agano letu kila wiki katika sala ya sakramenti ni kwamba “daima tumkumbuke” (Moroni 4:3; Mafundisho na Maagano 20:77). Kitabu cha Mormoni hutuhimiza kwa kutumia neno mara mbili, moja baada ya jingine: “kumbuka, kumbuka” (Mosia 2:41; Alma 37:13; Helamani 5:9). Ukumbusho wa kiroho huja kupitia nguvu za Roho Mtakatifu: “Atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”(Yohana 14:26).

  21. Russell M. Nelson, “Msikilize Yeye,” Liahona,, Mei 2020, 90.

  22. Russell M. Nelson, “Kuvuta Nguvu ya Yesu Kristo kwenye Maisha Yetu,” Liahona, Mei 2017, 41. Rais Nelson pia alisema, “Shangwe ambayo [Watakatifu wa Siku za Mwisho] huihisi inahusika kwa kiasi kidogo sana na hali za maisha yetu na inahusika kwa kila kitu na fokasi ya maisha yetu” (“Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona, Nov. 2016, 82).

Chapisha